DAR ES SALAAM
Na Mwandishi wetu
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi amesema kuwa Pendekoste ni mwanzo wa Kanisa, wa kuitangaza habari njema na Injli.
Aidha, amesema kuwa Injili ni mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo.
Askofu Mkuu Ruwa’ichi alisema hayo wakati akitoa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Ekaristi Takatifu, iliyofanyika katika Parokia ya Mtakatifu Maria De Mathias, Mivumoni, jimboni Dar es Salaam.
“Pentekoste ni fumbo la wokovu wetu, ambao kila mbatizwa anaitwa na anatumwa kuliishi na kulishuhudia…Kabla ya kuteswa kwake, Bwana Yesu Kristo aliwaandaa wafuasi wake, aliwafundisha, aliwatangazia kwamba ulimpasa kukataliwa na watu, kufa kifo cha aibu, lakini kwamba atafufuka.”
Alisema kuwa Yesu aliwatangazia ukweli huu wa kukataliwa kwake, kuzalilishwa kwake, kuuawa kwake na kufufuka kwake, lakini pamoja na kuambiwa jambo hilo mara tatu Mitume hawakulipokea hawakulielewa,kwa sababu vyote wanajua lakini habari ya ufufuko, si habari waliyoizoea.
Askofu Mkuu alisema: “Yesu peke yake ndiye aliyeteswa, akafa na akafufuka na kwa hayo, sisi tumekombolewa na kutambulika kama watoto wa Mungu.”
Kwa mujibu wa Askofu Ruwa’ichi, kila mmoja anapaswa kujua wajibu na jukumu lake katika utume huu, na atekeleze kwa nguvu zote.
Alibainisha kuwa Utume huo ni kumtangaza Kristo kwa ulimwengu, wamfahamu na wampokee na kupokea tunu yake Mungu.
“Kumtangza Kristo ni jukumu zito ambalo hatuwezi kufanya kwa nguvu zetu wenyewe, bali ni kwa nguvu zake Roho Mtakatifu,”alisema Askofu Mkuu Ruwa’ichi.
Naye Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Maria De Mathias, Mivumoni, Padri Edwin Kigomba, alimshukuru Askofu kwa kuadhimisha Misa hiyo na kutoa Sakramenti ya Kipaimara kwa vijana 85, akiwakumbusha waamini kutimiza wajibu wao kuieneza Injili.
“Watoto, endeleeni na maisha ya kiroho, hata baada ya kupokea sakramenti hii.
Aidha, Padri Kigomba alitumia nafasi hiyo kuwasihi Maparoko, Waamini na wote wenye mapenzi mema, kujitoa kwa hali na mali kusaidia Tumaini Media, ili iweze kuinjlisha kote nchini.
Naye Chysanthus Chenga, Mwenyekiti Parokia hiyo, alisema kuwa wanamsukuru Mungu, na kumpongeza Askofu kwa Jubilei ya Miaka 25 ya Uaskofu wake.
Aidha, alisema kwamba watakuwa bega kwa bega katika kuunga mkono juhudi za Askofu Mkuu Ruwa’ichi katika ujenzi wa Kanisa mbadala huko Gezaulole.
Kuhusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu, Chenga aliwataka wenye nia ya uongozi na nia ya kuwaendeleza watu, wajitoe na kuchukua fomu wakati utakapofika, ili kuwania nafasi hizo.