DAR ES SALAAM
Na Mwandishi wetu
Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, ameonya tabia ya unyanyasaji na ukatili unaofanyika dhidi ya watu wenye ualbino, kwani hali hiyo inaleta hofu kubwa katika jamii.
Kardinali Pengo alitoa onyo hilo katika Adhmisho la Misa Takatifu ya Sakramenti ya Kipaimara kwa vijana 35, wa Parokia ya Utatu Mtakatifu – Changanyikeni, jimboni Dar es Salaam.
“Unaposikia kuna mtoto anauawa, eti kisa ni albino, na moja kati ya watu waliohusika, ni baba yake mzazi, unaanza kupata hofu ya ajabu. Mtoto bila kosa lake amezaliwa vile,” alisema Kardinali Pengo.
Alisema kuwa Waimarishwa hao, moja ya mambo wanayotakiwa kuyafanya, ni kuleta utofauti, ikiwemo kuhakikisha kwamba kila wanapokwenda, wanapeleka mwanga wa Injili.
Aidha, aliongeza kuwa wasiruhusu popote walipo pakose mwanga wa Injili, badala yake watekeleze wajibu huo kwa matendo, na si kwa maneno pekee.
Katika homilia yake, Kardinali Pengo aliwataka Waimarishwa hao kutambua ukuu wa jukumu walilopewa kwa mfano wa maisha, na si vinginevyo.
Aliwashauri Wanachanganyikeni kwamba kama wataweza, wajenge shule ya Chekechea itakayohudumiwa na Watawa katika eneo la Parokia yao.
Kwa upande wake, Rita Mzava, mmoja wa Waimarishwa, akisoma risala yao kwa niaba ya vijana wenzake, aliuomba Uongozi wa Jimbo hilo kuwawekea utaratibu wa kuendelea kupatiwa Mafundisho ya Imani, ili waendelee kuiishi imani yao.
Kwa mujibu wa risala iliyosomwa, Parokia ya Utatu Mtakatifu – Changanyikeni, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, ina jumla ya Waamini wapatao 1,500.