DAR ES SALAAM
Na Mathayo Kijazi
Imeelezwa kuwa kazi ya Msimamizi katika Sakramenti Takatifu ya Kipaimara, ni kuwasaidia wazazi wa mtoto anayemsimamia, ikiwemo kujua maendeleo ya kiroho ya mtoto huyo, na kwamba siyo tu kumuwekea mkono begani wakati wa kupokea.
Ufafanuzi huo ulibainishwa na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu wakati wa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya kutoa Sakramenti ya Kipaimara kwa Vijana 49 katika Parokia ya Mtakatifu Simon Stock – Mbezi Mageti, jimboni humo.
“Pengine watu wanaweza kujiuliza kwamba nini majukumu ya msimamizi wa mtoto wakati wa kupokea Sakramenti Takatifu ya Kipaimara. Msimamizi ni mzazi wa mtoto huyo kiroho, na anatakiwa kujua maisha ya mtoto huyo baada ya kupokea Kipaimara.”
“Kwa hiyo, wewe msimamizi jitahidi kuulizia maendeleo ya mtoto uliyemsimamia. Tambueni kwamba mna kazi ya kuwalea watoto hawa, siyo tu kuwabandikia mikono begani wakati wa kupokea Sakramenti hii ya Kipaimara,” alisema Askofu Mchamungu.
Askofu huyo aliwasihi Waamini kuchangia katika shughuli za kimungu, ikiwemo ujenzi wa kanisa, kwani kufanya hivyo si kama kuchangia katika sherehe za harusi, bali ni kufanya jambo litakalowapatia baraka.
Hata hivyo Askofu Mchamungu aliwaasa Waamini kutokuoneana wivu katika maisha yao, bali waweke kipaumbele suala la kusaidiana, huku wakiwa katika misingi ya kumpendeza Mungu.
‘Kwa hiyo ndugu zangu, hakuna sababu ya kuoneana wivu. Tunaona katika maeneo mbalimbali watu wanaoneana sana wivu. Kwa Mkristu, hiyo siyo tabia nzuri kabisa,” alisema Askofu Mchamungu.
Vile vile, Askofu Mchamungu aliwapongeza Wanaparokia hiyo kwa hatua nzuri waliyofikia ya ujenzi wa kanisa, akiwaomba kuongeza umoja na mshikamano ili waweze kukamilisha.
Kwa upande wake Paroko wa Parokia hiyo, Padri Nelson Osmond alimshukuru Askofu Mchamungu kwa kufika parokiani hapo, na kuwaimarisha Vijana 49 kwa Sakramenti Takatifu ya Kipaimara.
Padri Nelson aliwapongeza Waimarishwa kwa kupokea Sakramenti hiyo, akiwasihi kuendelea kuyaishi yale yote waliyofundishwa ili yaendelee kuwasaidia katika maisha yao.
Akizungumza kwa niaba ya Halmashauri ya Walei Parokia, Mwenyekiti wa Parokia hiyo, Dk. Felix Sukuma alimshukuru Askofu Mchamungu, akisema kwamba wamefarijika kutembelewa na Askofu aliyewaongoza katika Adhimisho hilo la Misa Takatifu.