VATICAN CITY, Vatican
Baba Mtakatifu Fransisko amesema kwamba Wakatoliki wanapaswa kuitangaza na kuishuhudia Injili kwa Matendo ya Huruma, kiroho na kimwili.
Baba Mtakatifu alitoa rai hiyo katika salamu zake, akisema kuwa Bwana Yesu Kristo anayewachagua na kuwatuma Mitume wake 12 ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa kuonesha uwepo wa karibu wa Mungu, waamini wanatakiwa kujifunza kuwa Mitume bora, ili kutangaza na kushuhudia upendo na matumaini kwa njia ya huduma makini, kwa sala, tafakari ya Neno la Mungu, na maisha ya Kisakramenti.
Baba Mtakatifu Fransisko alisema kuwa Injili inapaswa kutangazwa na kushuhudiwa kwa matendo, na si vinginevyo.
“Kutangaza na kushuhudia Injili ni dhamana na utume ambao Kristo Yesu amewakabidhi Mitume wake. Huu ni utume wa kwanza unaopaswa kutekelezwa na Mama Kanisa kwa kila mtu na kwa ulimwengu mzima,” alisema Baba Mtakatifu.
Alibainisha kuwa Utume huu unatekelezwa kikamilifu na Mama Kanisa anapotangaza na kushuhudia Injili ya upendo inayomwilishwa katika huduma makini kwa binadamu wote, kiroho na kimwili.
Papa aliongeza kusema kwamba upendeleo wa pekee ni kwa maskini, wagonjwa na wadhaifu ndani ya jamii.
Alisema kuwa Kanisa linapaswa kujikita katika wongofu wa kimisionari, kwa kuwa ni chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu, lijitambulishe na kueleweka kuwa ni Fumbo la Ushirika unaomwilishwa katika dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa.
Baba Mtakatifu alisema kuwa Kristo Yesu aliwachagua na kuwatuma Mitume wake kutangaza na kushuhudia kwamba Ufalme wa Mungu umekaribia, yaani huruma na upendo wa Mungu umemkaribia na kumwandama mwanadamu kiasi cha kukaa kati yake.
Aliendelea kwa kusema kuwa huu ndio uhalisia wa maisha, changamoto na mwaliko kwa waamini kukuza imani na matumaini kwa Mwenyezi Mungu anayewapenda sana waja wake, na anataka kuwashika mkono na kuwaongoza taratibu, anataka kuwapenda, na hivyo kuhisi uwepo wake wenye nguvu, tayari kuwaongoza waja wake.
Baba Mtakatifu Fransisko alikazia kwa kusema kwamba ili kuwa Mitume wazuri, kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na kifani, kuna haja ya kupiga magoti na kujifunza, na hatimaye kushuhudia kwamba kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Baba anayeweza kugeuza nyoyo za watoto wake, na kuwakirimia furaha na amani ambayo kwa nguvu na jitihada zao binafsi, hawawezi kuipata.