VATICAN CITY
Mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Taleb Al Abdulmohsen, mwenye umri wa miaka 50, Daktari wa Afya ya Akili, aliyeingia nchini Ujerumani kunako mwaka 2006, hivi karibuni amevamia Soko la Noeli, lililoko mjini Magdeburg, nchini Ujerumani, na kusababisha vifo vya watu watano, na kujeruhi watu zaidi ya 200, na kati yao, watu 41 wako katika hali mbaya.
Kufuatia tukio hilo, Baba Mtakatifu Fransisko amesikitishwa na shambulizi hilo la kinyama, huku akionesha uwepo wake wa karibu kwa waathirika.
Alisema kwamba kwa masikitiko makubwa, anaungana na watu wenye mapenzi mema kuwaombolezea wale wote waliopoteza maisha kutokana na shambulio hilo, na kwamba, yuko karibu na wote walioguswa na kutikiswa na msiba kutokana na tukio hilo.
Aidha, Baba Mtakatifu Fransisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu Mkuu wa Vatican, aliwapongeza wale wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya kuwahudumia waathirika wa shambulio hilo.
Papa anasali pia na kuwaweka waathirika wote chini ya Kristo Yesu, tumaini la waja wake, nuru inayoangaza kwenye giza la uvuli wa mauti, akiwaombea kwa moyo wote msaada na faraja kutoka mbinguni.
Mji wa Magdeburg ni maarufu sana kwa viwanda na bandari, na upo katikati ya Ujerumani kwenye ukingo wa Mto Elbe, ambapo wachunguzi wa mambo wanasema Taleb Al Abdulmohsen amevamia Soko la Noeli kwa kutoridhishwa na jinsi ambavyo Serikali ya Ujerumani inavyowatendea wakimbizi na wahamiaji, ila yeye bado anashikiliwa na vyombo vya ulinzi na usalama kwa uchunguzi zaidi.