DAR ES SALAAM
Na Mathayo Kijazi
Waamini wa Parokia ya Mtakatifu Yohane Maria Muzeey – Tegeta ‘A’, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, wameadhimisha siku ya Somo wa Parokia hiyo, huku wakitakiwa kupendana katika kila hali walizo nazo, kwani hakuna aliyeumbwa kuwa mtumwa kwa wengine.
Hayo yalisemwa na Padri Prosper Kessy, Gombera wa Kituo cha Hija cha Mtakatifu Padri Pio, San Damiano – Msimbazi, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, wakati wa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Somo wa Parokia ya Mtakatifu Yohane Maria Muzeey – Tegeta ‘A’, jimboni humo.
“Kwa hiyo ndugu, tupendane katika hali zozote tulizo nazo, kwa sababu hakuna aliyeumbwa kwa ajili ya kuwa mtumwa kwa watu wengine, yaani hata ukijiona una pesa kiasi kwamba ukaamua kutafuta wafanyakazi wa nyumbani kwako, lakini tambua kwamba wale hawakuumbwa kwa ajili ya kuja kuwa watumwa wako,” alisema Padri Kessy.
Aidha, Padri huyo aliwasihi Waamini kufahamu kwamba Neno la Mungu ni tofauti na maneno mengine, kwani Neno hilo huwabadilisha hata majambazi na kuamua kuishi maisha yanayofaa katika jamii.
Padri huyo aliwasisitiza Wakristu kuliruhusu Neno la Mungu lifanye kazi katika maisha yao ili liwabadilishe, na kuwa watu wema.
Alitoa wito kwa Waamini kuliruhusu Neno hilo lifanye kazi katika biashara zao, akiwataka kuepuka udanganyifu katika biashara hizo, ikiwemo kujipangia viwango vya bei za bidhaa, tofauti na bei halali za bidhaa hizo.
“Liruhusuni Neno la Mungu liingie katika biashara zenu, ili liwasaidie kuwa waaminifu. Wapo wafanyabiashara ambao ukifika wanakudanganya kwamba ‘nguo hii imetokea Uturuki,’ ili akuuzie kwa bei ya juu zaidi, huku ukiamini kwamba kwa sababu imetoka Uturuki, basi itakuwa ni nzuri na imara zaidi…
“Yaani mtu anaamua kuuza bidhaa kwa bei mara tatu zaidi ya aliyonunulia, huo ni udanganyifu wa juu sana katika biashara. Halafu baadaye anatoka mbele za watu anasema, ‘Mungu amenitendea mambo makuu sana katika biashara yangu,’ huyo aliyekutendea siyo Mungu, bali ni shetani kupitia udanganyifu wako,” alisema Padri Kessy.
Padri Kessy alitoa wito kwa wazazi kuwapa watoto wao malezi yaliyo bora, na si ya kuwanyenyekea, kwani wakiwadekeza kupitiliza, watawatengenezea mazingira magumu pale watakapokuwa wakubwa.
Aidha, aliwashukuru Waamini wa Tegeta ‘A’ kwa kumwalika kusali naye katika Adhimisho hilo la Misa Takatifu ya Somo wa Parokia, akiwaasa kuendelea kushikamana na kuwa wamoja ili waweze kupiga hatua kimaendeleo parokiani hapo.
Kwa upande wake Paroko wa Parokia hiyo, Padri Urbanus Riziki alimshukuru Padri Kessy kwa kukubali mwaliko wa kwenda kuungana na Waamini wa Tegeta ‘A’, akimshukuru pia kwa kuongoza Misa hiyo Takatifu.
Padri Riziki aliwaasa Waamini parokiani hapo kuongeza nguvu katika kuchangia ujenzi wa kanisa jipya linaloendelea kujengwa, ili waweze kuukamilisha kwa haraka ujenzi huo.
Kwa mujibu wa Katibu wa Parokia hiyo, Prisila Clemence, Parokia ya Mtakatifu Yohane Maria Muzeey - Tegeta ‘A’ ilianzishwa kama Kigango cha Mtakatifu Yohane Maria Muzeey, Julai 6 mwaka 2007.
Kigango hicho kilianzishwa kutoka Parokia ya Bikira Maria Mama wa Huruma - Mbezi Beach (BMMH) iliyokuwa chini ya Paroko wa Mbezi Beach wa wakati huo, Padri Romuald Mukandara.
Baadaye Kigango hicho kilihamishiwa Parokia ya Bikira Maria Consolatha – Makabe, chini ya Mapadri wa Missionaries of Mary Immaculate (MMI), baadaye tena kikahamishwa na kuwa chini ya Parokia ya Benedicta wa Msalaba – Msumi.
Julai 7 mwaka 2018, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam kwa wakati huo, alikipandisha hadhi kuwa Parokia Teule.
Julai 7 mwaka 2020, Mtakatifu Yohane Maria Muzeey - Tegeta ‘A’ ilitangazwa rasmi kuwa Parokia Kamili na Askofu Mkuu wa Jimbo hilo, Mhashamu Sana Jude Thaddaeus Ruwa’ichi, na kuwekwa chini ya Mapadri wa Jimbo hilo, ambapo Padri Urbanus Riziki Ngowi alitangazwa kuwa Paroko wa Parokia hiyo.