DAR ES SALAAM
Na Mwandishi wetu
Baba Mtakatifu Fransisko ameridhia ombi la kung’atuka kutoka shughuli za kichungaji za Jimbo Katoliki la Iringa, lililowasilishwa na Askofu wa Jimbo hilo, Mhashamu Tarcisius Ngalalekumtwa, akimteua Padri Romanus Elamu Mihali kuwa Askofu mpya wa jimbo hilo.
Askofu Mteule Mihali ameteuliwa baada ya Askofu Ngalalekumtwa aliyekuwa akiongoza jimbo hilo, kufikisha umri wa kustaafu.
Kabla ya uteuzi huo, Askofu mteule Mihali alikuwa Makamu wa Askofu wa Jimbo Katoliki la Mafinga, na Paroko wa Parokia ya Ujewa, jimboni humo.
Askofu Mteule Mihali alizaliwa Juni 10, mwaka 1969 katika Kijiji cha Itulituli, Wilaya ya Mufindi, Mkoa wa Iringa.
Baada ya majiundo yake ya Falasafa na Taalimungu katika Seminari Kuu ya Songea, alipewa Daraja Takatifu la Upadri Julai 13 mwaka 2000 kwa ajili ya Jimbo la Iringa.
Askofu Mteule Mihali katika utume wake, alishika nyadhifa mbalimbali na kuendelea na masomo zaidi, ambapo mwaka 2000 hadi 2003, alikuwa Paroko Msaidizi wa Parokia ya Mtakatifu Paulo Mtume huko Ilula, jimboni Iringa.
Mwaka 2003 hadi mwaka 2005 alikuwa Mlezi na Mkufunzi wa Seminari Ndogo ya Mtakatifu Kizito, Jimbo Katoliki la Mafinga.
Aidha, mwaka 2005, hadi 2011, aliendelea na masomo yake ya Uzamili wa Sayansi katika Sayansi ya fani ya wanyama, na kupata Shahada yake katika Chuo Kikuu cha Kerala nchini India.
Mwaka 2012 hadi 2015 alifanya utume kama Paroko Msaidizi wa Parokia ya Bikira Maria wa Fatima huko Usomaki, jimboni Iringa.
Mwaka 2015 hadi 2024, alikuwa akifanya utume kama Paroko wa Parokia ya Bikira Maria Mpalizwa, Ujewa, Iringa.
Baada ya kuundwa kwa Jimbo Katoliki la Mafinga mwaka 2024, na kupatikana Askofu mpya wa Jimbo hilo, Padri Romanus aliteuliwa kuwa Makamu Askofu wa Jimbo hilo, na Paroko wa Parokia ya Bikira Maria Mpalizwa (Mafinga), hadi uteuzi wake.
Askofu Mstaafu Tarcisius Ngalalekumtwa ataendelea kuwa Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki la Iringa hadi Askofu Mteule Mihali atakapowekwa wakfu wa Kiaskofu kwa ajili ya Jimbo hilo hilo.