Katika kuadhimisha Somo wa Kanda ya Mtakatifu Raphael Malaika Mkuu, Parokia ya Mtakatifu Kamili - Yombo Kiwalani, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, waamini wamealikwa kumwomba Mungu ili wafanane na Malaika katika kumtukuza na kumtumikia Mungu.
Hayo yalisemwa na Paroko wa Parokia hiyo, Padri Kanuth Nyoni katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Somo wa Kanda hiyo, iliyoadhimishwa parokiani hapo hivi karibuni.
Aliwaasa Wanakanda hao kuendelea kuwa wamoja katika kumtukuza Mungu, huku wakiyafanya yote katika utimilifu wake.
Pia, alitoa wito kwa kila mmoja kuwa kweli watu wa Mungu, wakiwa tayari kupeleka habari njema kwa kufuata nyayo za malaika zao.
Aidha, akiwaalika kuongeza umoja na mshikamano wao katika kuhakikisha Kanda na Jumuiya zao zinazidi kuwa imara.
Padri huyo alisema kuwa Mungu anawaona katika kila wanachokiwaza, huku akiwafanyia yale aliyowaahidia katika maisha yao.
Aliwataka kutambua kwamba licha ya kutowaona Malaika hao, bali watambue kwamba wapo, huku wakiiga na kufuata nyayo za Malaika hao.
















