Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

Waamini wa Parokia ya Mtakatifu Andrea Mtume, Bahari Beach, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, wakiwa katika Adhimisho la Misa Takatifu ya kutoa Sakramenti ya Kipaimara iliyofanyika hivi karibuni parokiani hapo.

Vijana Waimarishwa wa Sakramenti Takatifu ya Kipaimara wa Parokia ya Kung’ara kwa Yesu Kristo, Mbezi Mshikamano, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, wakiwa katika Adhimisho la Misa Takatifu ya kupokea Sakramenti hiyo, iliyokwenda sanjari na Kutabaruku Kanisa na Altare.

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi, akiweka ubani katika vyombo ili kufukiza, wakati wa Kutabaruku Kanisa na Altare katika Adhimisho la Misa Takatifu iliyofanyika Parokia ya Kung’ara kwa Yesu Kristo, Mbezi Mshikamano, jimboni humo. (Picha zote na Yohana Kasosi)

DAR ES SALAAM

Na Arone Mpanduka

Women Jazz Band ilikuwa bendi ya muziki wa dansi jijini Dar es Salaam, Tanzania. Bendi ilianzishwa mnamo 1965 ikiwa na wanawake tupu, lakini baadaye ilileta wanaume kwenye upande wa kupiga vyombo.
Mwaka 1965 kundi jipya la muziki la aina yake lilianzishwa Tanzania. Lilikuwa ni bendi ya akina mama watupu. Akina mama hawa, wengine wakiwa wafanyakazi wa Government Press, walijichagua na kuanza kuhudhuria mafunzo ya muziki chini ya yule mwanamuziki mahiri Mzee Mayagilo, aliyekuwa kiongozi wa shughuli za muziki katika Jeshi la Polisi.
Akina mama hawa wakawa chini ya kitengo cha Polisi Jazz Band, wakaanza kufanya mazoezi ya nguvu. Bendi hiyo ya akina mama ilikuwa chini ya ufadhili wa TANU Youth League.
Wakati wakianza shughuli hiyo, walikuwa hawana ujuzi wowote wa muziki. Kutokana na jitihada waliyofanya, taratibu wakaanza kufanya maonyesho yao, hasa kwenye hafla za Serikali na Chama tawala wakati huo.
Tarehe 31 Mei 1966, Women Jazz band iliingia katika studio za Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) na kurekodi nyimbo sita ambazo ni ‘Tumsifu Mheshimiwa’; ‘Leo Tunafuraha’, ‘Mwalimu Kasema’; ‘Women Jazz’; na ‘Sifa nyingi tuwasifu Viongozi na TANU yajenga nchi.’
Bendi hiyo iliundwa na Washiriki kama Mary Kilima (Mwimbaji); Juanita Mwegoha (Mwimbaji); Siwema Salum (Mwimbaji); Rukia Hassan (Mwimbaji); Kijakazi Mbegu (Solo Guitar); na Mwanjaa Ramadhan (Bass Guitar).
Wengine ni Chano Mohammed (Rhythm Guitar); Tatu Ally (Alto Sax); Mina Tumaini (Tenor Sax); Anna Stewart (Alto Sax); Rukia Mbaraka (Tenor Sax); Lea Samweli (Bongos, au Conga); Josephine James (Drums); Zainab Mbwana (Maracass); na Tale Mgongo (Timing).
Inaelezwa kuwa wazo la kuwa na bendi ya wanawake tupu lilianzia kwenye bendi ya wanawake ya Les Amazones De Guinee ya nchini Guinea kwa wakati huo.
Kipindi hicho, Rais wa Guinea ya Conakry, Sekou Toure alikuwa na tabia ya kuambatana na bendi yake hiyo katika ziara zake mbalimbali Barani Afrika, na nje ya Afrika.
Ndipo mwaka 1965, Rais huyo alipata fursa ya kufanya ziara nchini Tanzania na kuja na ndege iliyosheheni wasanii wengi wa kike kuliko wanasiasa, ambapo miongoni mwa bendi alizoambatana nazo kwenye msafara wake, ni ya Les Amazones.
Wakati walipowasili,baadhi ya mabinti wa TANU Youth League hapa nyumbani ndio walikuwa wenyeji wa wanamuziki hawa wa kike. Rais Sekou Toure na wasanii wake walipoondoka walikuwa wamepanda wazo la vikundi vya sanaa vya Taifa, na pia wazo la bendi ya wanawake.
Wanawake waliokuwa wakizunguka na wanamuziki wa kigeni, wengi wakiwa wanafanya kazi Government Press, waliazimia nao kuanzisha bendi ya wanawake, japo walikuwa hawana ujuzi wa chombo chochote cha muziki, lakini nia yao ilikuwa kuwa na bendi kama Les Amazones.
Women Jazz ilipata umaarufu kiasi cha kuanza kufanya safari nje ya Tanzania, na kuweza kufanya maonyesho Nairobi na Mombasa nchini Kenya, baada ya kutembelea miji kadhaa nchini Tanzania.
Wakati wa matayarisho ya kwenda China, kundi lilisambaratika. Kikubwa kilichosababisha hili ilikuwa ni wanamuziki kuona hawapati chochote kutokana na mapato yaliyotokana na muziki wanaoupiga.
Baada ya bendi kufa, TANU youth League ikachukua vyombo vyake na kuvihifadhi, hatimaye vyombo hivi vikawa ndivyo vyombo vilivyotumika kuanzisha Vijana Jazz Band chini ya Mzee John Ondolo, miaka kadhaa baadaye.
Vijana Jazz Orchestra ambayo ilikuwa inajulikana kama Vijana Jazz Band au Vijana Jazz) ilikuwa ni bendi ya muziki wa dansi ya Kitanzania iliyofikia kilele cha umaarufu katika miaka ya 1980.
Kama ilivyokuwa kwa bendi nyingi za dansi za enzi hizo, ilifadhiliwa na taasisi ya Serikali, yaani Umoja wa Vijana kupitia Tawi la Vijana la Chama Tawala cha Tanzania (TANU) kwa wakati huo.
Bendi hiyo ilianzishwa mwaka 1971 na John Ondolo Chacha. Mnamo mwaka wa 1978, serikali ya Tanzania ilipitisha sheria iliyoruhusu bendi kununua ala za kigeni (jambo ambalo hapo awali lilikuwa limekatazwa na Baraza la Muziki la Taifa (BAMUTA), baraza la serikali linalohusika na udhibiti wa biashara ya muziki).
Vijana Jazz ilikuwa mojawapo ya bendi za kwanza kuchukua fursa hii, na katika miaka ya 1980, ilipata umaarufu mkubwa kwa sababu ya sauti yake ya ubunifu iliyotumia sanisi na mashine za ngoma.
Mitindo maarufu (styles) iliyobuniwa na Vijana Jazz include sindimba, heka heka, koka koka, watoto wa nyumbani, na pamba moto. Baadhi ya wanamuziki mashuhuri waliowahi kutamba katika Vijana Jazz ni Hamza Kalala, Hemedi Maneti, Issa Chikupele na Manitu Musa.

Washington, USA
Mrusha nyundo Gwendolyn Berry amepigwa marufuku kwa miezi 16 na Wakala wa Kupambana na Dawa za Kulevya nchini Marekani, kwa kukutwa na dawa iliyopigwa marufuku.
Kusimamishwa huko kunamaanisha kwamba Mmarekani huyo mwenye umri wa miaka 34, atakosa Mashindano ya Riadha ya Dunia mwezi huu huko Budapest.
Ukiukaji wa Berry ulitokana na matumizi yake ya dawa ya juu, krimu inayotumika kutibu maumivu katika sehemu mahususi ya mwili iliyokuwa na ‘spironolactone.’
Ni marufuku ya pili ya kutumia dawa za kusisimua misuli ndani ya kipindi cha miaka 10 kwa Berry, ambaye alikuwa mwanachama wa timu za Olimpiki za 2016 na 2020 za Marekani.
Kupigwa marufuku kwake kunamaanisha kuwa atakosa pia Michezo ya Olimpiki ya Paris ya mwaka 2024, itakayoanza Julai ijayo.

LONDON, Uingereza
Mpambano wa taji la dunia la Artur Beterbiev na Callum Smith umepangwa upya mapema mwaka ujao kufuatia kuahirishwa kwa tarehe ya awali ya shindano hilo.
Bingwa wa dunia wa Unified Beterbiev alitazamiwa kumenyana na Smith Jumapili, Agosti 20, baada ya kumshinda Brit mwenzake wa Smith Anthony Yarde kwenye Wembley Arena mwezi Machi na kuhifadhi mataji yake ya IBF, WBC na WBC.
Lakini mchezaji huyo wa uzani wa light-heavy wa Kanada alilazimika kuahirisha pambano hilo kutokana na upasuaji wa meno, na wawili hao sasa wakipanga tena kukutana katika Jiji la Quebec mnamo Januari 13, 2024.
Tangu ajiunge na taaluma mwaka 2013, Beterbiev ameweka rekodi ya kutoshindwa 19-0, huku ushindi wake wote ukiwa ndani ya umbali na kumfanya kuwa bingwa pekee wa dunia wa ndondi kwa sasa na rekodi ya kutoshindwa kwa asilimia 100.
“Ni miezi michache baadaye kuliko ilivyopangwa awali, lakini nina furaha kwamba Artur Beterbiev atapata nafasi ya kutetea mataji yake mbele ya mashabiki wa ajabu wa Quebec City”, alisema Bob Arum Mwenyekiti wa promota wa Top Rank.

DAR ES SALAAM

Na Arone Mpanduka

Klabu ya soka ya Mtibwa Sugar ya mkoani Morogoro imesema kwamba haina tena mpango wa kuwa na wachezaji wa kigeni,  kwa sababu hawana tofauti na uwezo walionao wachezaji wazawa.
Akizungumza na Tumaini Letu kwa njia ya simu kutoka Turiani Morogoro, Afisa Habari wa Klabu hiyo Thobias Kifaru alisema kuwa msimu uliopita walikuwa na wachezaji wa kigeni wasiopungua watano kutoka nchi mbalimbali Barani Afrika, lakini hawakuwasaidia chochote.
Alisema kwamba hata makocha watakaowatumia msimu ujao, ni wale wazawa pekee, kwa sababu wageni nao hawakuwa na mchango katika timu hiyo.
“Zamani tulikuwa na mfumo wa kutumia wachezaji wazawa, na kwa hakika tulifanikiwa kwa kiasi kikubwa, lakini baadae tukaona tujaribu kutumia mfumo wa wachezaji wa kigeni. Lakini sasa tunaona hakuna umuhimu wowote wa kufanya hivyo. Wanatuingiza kwenye gharama kubwa za uendeshaji, ikiwemo kuwalipia vibali na mishahara mikubwa, halafu hakuna matokeo mazuri uwanjani,” alisema Kifaru.
Alisema pia kuwa wapenzi wa soka wajiandae kuiona Mtibwa isiyo na kocha wa kigeni wala mchezaji wa kigeni katika msimu ujao, na kwamba huo ndio utakuwa utaratibu wao kwa misimu mingine inayofuata.
Kuhusiana na hoja ya ukata kusababisha wachukue maamuzi hayo ya kusajili wazawa, Kifaru alikana akisema kwamba Kampuni ya Mtibwa ina pesa nyingi, isipokuwa imeamua kurejesha uzalendo kwa kutumia wazawa pekee katika timu yao.
“Kiwanda cha Mtibwa Sugar ni kikongwe sana na hakijawahi kufilisika, vivyo hivyo hata kwenye timu. Sisi tulianza kuonekana Ligi Kuu mwaka 1995 na hujasikia tukitembeza bakuli kwa watu kuomba mchango.Kama tungekuwa na maisha hayo, sasa hivi tusingekuwepo kwenye ulimwengu wa soka,” alisema.
Mtibwa kwa sasa ipo chini ya kocha Habib Kondo mara baada ya kuachana na kocha Salum Mayanga waliyekuwa nae msimu uliopita.

DAR ES SALAAM

Na Arone Mpanduka

Imeelezwa kwamba mshambuliaji mpya wa Yanga kutoka nchini Ghana, Hafiz Konkoni, ni mwalimu kitaaluma.
Hayo yalisemwa na mwandishi wa habari za michezo nchini Ghana, Evans Gyamera, wakati akizungumza na Tumaini Letu kwa njia ya simu kutoka jijini Accra.
Gyamera ambaye pia ni miongoni mwa wadau wakubwa wa soka nchini humo, alisema kuwa Konkoni, licha ya kulijua kandanda, pia ana taaluma ya ualimu aliyoipata katika Chuo cha Ualimu cha Tumu (Tumu Teachers Training College) kilichopo Upper West nchini humo.
Mwanahabari huyo alisema kuwa kwa sasa Konkoni ana Diploma ya Ualimu wa Shule, ingawa mwenyewe anapenda zaidi kucheza soka.
Alisema kwamba taaluma aliyopata inamsaidia kuwa na weledi wa kufahamu lugha mbalimbali na kuzungumza kwa ufasaha, kitu ambacho kinamfanya aelewe vyema maelekezo ya makocha mbalimbali wanaomfundisha uwanjani.
“Ni kijana mwenye nidhamu na anajua kucheza soka, ikiwemo kutunza mpira kwenye miguu yake usipotee kirahisi kwa kupokonywa na wapinzani.Yanga wamepata mchezaji mzuri ambaye ninaamini atawasaidia,”alisema Gyamera.
Alisema Konkoni ni mchezaji ambaye amepata bahati ya kuaminiwa na kocha wa timu ya taifa ya Ghana Chris Hughton ambaye alimuita kwenye kikosi cha timu ya taifa na kumuacha kinara wa mabao Abednego Tettey.
Ikumbukwe kwamba msimu uliopita wa Ligi kuu ya Ghana, Konkoni alimaliza akiwa na magoli 15 na pasi za mwisho za usaidizi kabla ya kufunga magoli (assists) 3, akiwa katika nafasi ya pili, goli moja nyuma ya mfungaji bora Abednego Tettey, wa klabu ya Bibiani Gold Stars.
Hafiz kabla ya kujiunga na Bechem ya Ghana, aliwahi kucheza soka la kulipwa katika timu za Alsancak Ye ilova na Baf Ülkü Yurdu, za Kaskazini mwa Cyprus.

KONDOA

Na Bruno Bomola

Kongamano la Utoto Mtakatifu mwaka huu limefanyika kwa ustadi katika utume na hatimaye kukonga Waamini wa Jimbo Katoliki la Kondoa ambalo limepokea Msalaba kutoka Jimbo  Kuu  Katokiki la Tabora.
Kongamano hilo ambalo limekutanisha Majimbo 34, na Washiriki wa Mashirika 5515 ya Kipapa limekuwa fursa katika kuwaimarisha kiroho Waamini wa Majimbo hayo kwa njia ya semina, warsha na mafundisho ya Imani Katoliki na kuhitimishwa kwa Misa Takatifu.
Hii ni kwa mara ya kwanza kuwakutanisha watoto wa Majimbo yote kwa pamoja katika Kongamano la Kitaifa la Utoto Mtakatifu kwa mwaka huu 2023, likiwa limebeba kauli mbiu, ‘Ushirika na Utunzaji wa Mazingira’, ikiwa na mwendelezo wa Waraka wa Baba Mtakatifu Fransisko, ‘Laudato Si’, juu ya utunzaji wa mazingira.
Wamisionari hawa waliweka kambi tangu Juni 22 hadi 23 mwaka huu.
Kongamano lilifunguliwa kwa Adhimisho la Misa Takatifu na Askofu mwenyeji wa Jimbo Katoliki la Kondoa, Mhashamu Bernardin Mfumbusa, akishirikiana na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Songea, Mhashamu Damian Dallu, na Askofu wa Jimbo Katoliki la Tunduru Masasi, Mhashamu Filbert Mhasi.
Kanisa Kuu la Roho Mtakatifu, Jimbo Katoliki la Kondoa limetimiza miaka 11, huku jimbo hilo likiundwa na wilaya za Chemba na Kondoa, na wakazi wake ni Warangi, Wasandawe, Waburunge, Wagogo, Wamburu, Wabarbaigi na Watanzania wengine wanaoishi Kondoa.
Wamisionari kutoka Majimbo yote wakiongozwa na kauli mbiu ya Utunzaji wa Mazingira, wamepata nafasi ya kupitishwa kwenye semina mbalimbali juu ya umuhimu wa ikolojia na utunzaji wa mazingira, ili kuutiisha ulimwengu kama ulivyo mpango wa Mungu.
Aidha, katika kuhakikisha Watoto wanakuwa na ustawi bora wa malezi, walipata nafasi ya kupewa mafunzo ya malezi kutoka kwa Paschal Maziku na Melania Maziku juu ya haki na wajibu wa mtoto, na kukemea matumizi ya vidhibiti mimba na unyanyasaji wa kijinsia.
Katika kuhakikisha Watoto wanaendelea kupata mafunzo endelevu, Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Mhashamu Gervas Nyaisonga alizindua kitabu cha Malezi ya Mtoto, kilichoandaliwa na Sista Annagladnes Mruma.
Akitoa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu siku ya pili ya Kongamano hilo, Askofu wa Jimbo Katoliki la Tunduru Masasi, Mhashamu Filbert Mhasi aliwataka Wamisionari hao kufikiri na kuwa na hekima ya kuhubiri katika utunzaji wa mazingira.
“Tunapowaona Watoto, tunakuwa na matumaini makubwa sana na ninyi mtaenda kuinjilisha, na tena mtakuwa wainjilishaji wazuri juu ya utunzaji wa mazingira ambayo ni nyumba yetu nzuri sana, na nyumba yetu pendwa sana,” alisema Askofu Mhasi.
Juni 25 mwaka huu, Kongamano la Utoto Mtakatifu Kitaifa lilihitimishwa kwa Adhimisho la Misa Takatifu iliyoongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Songea, Mhashamu Damian Dallu, na Homilia ilitolewa na Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania, Mhashamu Garvas Nyaisonga.
Katika homilia yake, Askofu Nyaisonga aliwataka Wamisionari hao kutokuwa na hofu wala ubinafsi, badala yake wawe na fadhila ya ushirika kwa kuwatendea wengine matendo mema, bila kujali hali zao.
Aidha, Nyaisonga alisema kuwa Dunia kuna wakati inakosa usikivu kwa sababu ya kuambiwa mengi na kushindwa kuyapokea kwa usikivu, na akawataka Watoto wamisionari kuwa wasikivu kwa wazazi, walezi, waalimu na Viongozi wa Dini.
Ni kama Yesu alivyopokelewa Yerusalemu, ndivyo ambavyo maandamano yalivyopokelewa na wenyeji wa Kondoa. Waamini Wakristu na wasio Wakristu waliungana katika maandamano wakizunguka Mji wa Kondoa kumtangaza Kristu, na huu ndio Umisionari.
Hivyo ndivyo watoto 5515 wa Shirika la Kipapa wakisindikizwa na walezi wao kutoka Majimbo 34 ya Kanisa Katoliki Tanzania, walivyofanya uinjilishaji katika Jimbo Katoliki la Kondoa, huku tukisubiri tena kutangaziwa Jimbo litakaloandaa Kongamano lijalo la Kitaifa.

DAR ES SALAAM

Na Mathayo Kijazi

Wafanyakazi wa Tumaini Media wamewakumbuka wenzao waliofariki dunia kwa kufanya ziara maalumu ya kiroho walikozikwa kwenye makaburi ya Kinondoni na Pugu, jijini Dar es Salaam.
Katika Hija hiyo ya kiroho ya kuwakumbuka wenzao waliokuwa wakifanya kazi katika Vyombo vya Habari vya Tumaini Media, pamoja na mambo mengine katika Kuhitimisha Kampeni ya Mwezi wa Moyo Mtakatifu wa Yesu, ni kuwaombea marehemu hao.
Akizungumza katika ziara hiyo ya kiroho, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Tumaini Media, Arnold Kimanganu alisema kuwa yeye pamoja na wafanyakazi wote walioshiriki, wameguswa sana, kwani sala zao zina faida kubwa kwa wapendwa wao waliotangulia mbele za haki.
“Mimi kama mfanyakazi wa Tumaini Media nikiwakilisha wenzangu, nimeguswa kwa jambo hili jema la kiroho, na natamani sana lisiwe mwisho, bali tuendeleze utaratibu huu wa kuwakumbuka wale ndugu zetu waliokwisha kupumzika, kwa sababu tunafahamu kwamba wote hapa duniani tuko safarini, na mwisho wa safari yetu ni mauti,” alisema Kimanganu.
Aliwasihi kila mmoja katika ziara hiyo ya kiroho, kuiga yale mazuri yaliyowahi kutendwa na wapendwa wao enzi za uhai wao, na kuongeza kuwa watumie nafasi hiyo pia kuwaombea kwa yale mapungufu waliyokuwa nayo wapendwa wao hao, kama yanafahamika.
Naye Sista Leonora John, Mfanyakazi wa Tumaini Media alisema kuwa kila mmoja katika Dunia hii anatakiwa kuutambua mpango wa Mwenyezi Mungu, kwamba amepewa muda maalum wa kuishi hapa duniani, na akaongeza kuwa kifo kinawatenganisha kimwili tu, bali kiroho, wako pamoja.
“….Na kwa namna ya pekee kabisa, tunahitimisha ziara hii katika makaburi ya Pugu ambapo amelala Padri Paul Haule, pamoja na Mapadri wengine ambao wamelitumikia Kanisa Takatifu. Bila shaka tunajifunza kwamba sisi pia tuna safari ambayo tunatakiwa kuimaliza. Hivyo, tukiishi vizuri katika ulimwengu huu, tutayatimiza mapenzi ya Mungu Baba kama Yesu Kristo alivyosema, “Anayeishi vyema, atakuja kwangu, kwa sababu mimi ni njia, ukweli na uzima,” alisema Sista.
Kwa upande wake Mhariri Mkuu wa Gazeti Tumaini Letu, Alex Kachelewa alisema kuwa ipo haja ya kuendelea kuwaombea wapendwa wao waliolala katika Kristo, kwani kila mmoja anatakiwa kuiga uwajibikaji waliokuwa nao wapendwa wao enzi za uhai wao.
“Mama Esther Chilambo namkumbuka kama Mkurugenzi wa Pili wa Radio Tumaini, kabla haijaundwa Tumaini Media. Yeye alikuwa akiamini sana katika kazi, na hasa kuamini yale ambayo anaamini kwamba yanaweza kufanyika. Kwa hiyo, alikuwa ni mwenye misingi ya kusimamia kazi. Nakumbuka alikuwa na ‘column’ yake moja kwenye gazeti Tumaini Letu iliyoitwa ‘Dunia na Maumbile’. Lakini pia nakumbuka maneno machache aliyowahi kusema, “Ukiamua kufanya kazi, basi ifanye kwa moyo wa dhati,” alisema Kachelewa.
Kachelewa aliongeza kuwa Mama Esther Chilambo alikuwa ni mtu mwenye kujiamini katika utendaji kazi, kwani kwa mipango yake, alisaidia pia kuanzishwa kwa gazeti Tumaini Letu mwaka 2004, huku akisimamia mpango wa vyombo vya habari vya Kanisa, hasa Televisheni, iunde king’amuzi chake, ila baada ya kifo chake, mipango hiyo haikuendelea tena.
Naye Gaudence Hyera, Mratibu wa Matukio ya Kanisa wa Tumaini Media, alisema kuwa kufuatia Hija hiyo, wana imani kwamba sala zao zitafika pia Mjini Marseille, Ufaransa, alikozikwa mwanzilishi wa Tumaini Media, Padri Francois Galtier {aliyependa yeye kujiita ‘msela wa kijiweni’}, aliyefariki dunia Mei 17 mwaka 2021.
Gaudence aliongeza kwa kusema, “Kama ambavyo Kanisa linatufundisha kila siku juu ya kuwakumbuka marehemu, na tunatambua kwamba Kanisa lina makundi matatu, lina wale ambao bado wanaishi, ambalo linaitwa Kanisa linalosafiri; kuna wale waliotangulia, linaitwa Kanisa la wafu; lakini pia kuna wale washindi, linaitwa Kanisa la washindi, yaani wale Watakatifu wa Mbinguni;
“Kwa hiyo, ni jambo la muhimu sana ambalo tunalifanya kiimani na kijamii, lakini pia katika masuala mazima ya mahusiano ya kibinadamu, kwamba huyu aliishi katikati yetu. Kwa hiyo kwa namna moja ama nyingine, tunatakiwa kumkumbuka siku kwa siku,” alisema Hyera.
Kwa upande wake Editha Mayemba, Mtangazaji wa Redio Tumaini, alisema kuwa bado wanatambua mchango mkubwa uliofanywa na wapendwa wao, licha ya kwamba kwa sasa wametangulia mbele za haki, ila watayaendeleza mazuri yote yaliyoanzishwa na wapendwa hao.
Makaburi waliyoyatembelea wafanyakazi hao ni Kinondoni kwenye kaburi la aliyekuwa Mkurugenzi wa Pili wa Tumaini Media, Mama Esther Chilambo; kaburi la mtangazaji nguli wa Redio Tumaini Frederick Mosha, ali maafarufu ‘Defao’; na Pugu kwenye kaburi la aliyekuwa Mkurugenzi wa chombo hicho, Padri Paul Haule.