Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

DAR ES SALAAM

Na Mathayo Kijazi

Waliokuwa wanafunzi katika Shule za Seminari nchini, wamekutana na kutafakari Neno la Mungu katika mafungo yaliyoandaliwa na Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, huku wakiaswa kutambua kwamba hata Mtu anapojiona ni Mtakatifu kiasi gani, lakini bado mbele za Mungu, ni mdhambi, kwani Mungu ndiye Mtakatifu pekee.
Kauli hiyo ilitolewa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi katika Mafungo ya ‘Former Seminarians’, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, yaliyofanyika katika Kituo cha Hija – Pugu, jimboni humo.
“Mbele ya Mungu hata kama uko Mtakatifu kiasi gani, mbele ya Mungu ambaye ndiye utakatifu wote, ndiye ukamilifu wote, ni lazima ujitambue kwamba uko mdhambi, kwa kuwa Mungu tu ndiye peke yake Mtakatifu, Mungu tu ndiye peke yake mwenye haki, na Mungu tu ndiye peke yake asiye na lawama yoyote. Sisi wote tumeshaguswa na dhambi,” alisema Askofu Mkuu Ruwa’ichi.
Aidha, Askofu Mkuu aliwasihi Waseminari hao kutokuona haya kumwomba Mungu toba, au kujikabidha mbele za Mungu na kuomba huruma yake, kwani yeye ndiye anayewastahilisha, anayewatakasa na kuwawezesha.
Aliwataka kutokuogopa kufuata mfano wa mtoza ushuru, ambaye kwa kujitazama mapungufu yake, alisimama mbali na kujipiga kifua, huku akiomba toba.
Aliwaonya kuacha kujitokeza mbele za Mungu na kumkumbusha kwamba wao ni wenye haki kutokana na mambo wanayoyafanya katika maisha yao.
“Yaani mtego wa kufanya mazoezi fulani ya kiroho au ya kidini, na kujidhani sasa wamemuweka Mungu sawa, na kujidhani kwamba sasa sisi ni wenye haki, ndivyo alivyofanya yule Mfarisayo aliyeenda mbele ya Altare akaanza kumkumbusha Mungu jinsi yeye Farisayo alivyo na fadhila.
“Niwakumbushe tu kidogo, alimwambia Mungu, tazama mimi nilivyo mwenye haki, nafanya kadha wa kadha. Siko mzinzi, siko mwizi, siko mwongo, siko mvivu…… Yaani ni kama Mungu anatangaziwa hizo fadhila kusudi iweje. Kusudi mategemeo ni kwamba Mungu atampigapiga mabegani, na kumwambia ‘well done’. Lakini Mungu siyo wa hivyo, Mungu harubuniwi,” alisema Askofu Ruwa’ichi.
Alisema kuwa malezi waliyoyapata Waseminari hao pindi wakiwa Seminarini, yamewaunda na kuwapa fursa ya kupambanua na kuitikia wito wa Mungu.
Askofu Mkuu alisema kuwa kijana mdogo katika kukua kwake anapojitambua, asaidiwe ili akue katika mtindo ambao unamjenga kiutu, kiroho, na unamsababisha afanye maamuzi sahihi.
Aliwataka wale walioondolewa Seminarini ambao bado wana majeraha, kuondoa majeraha hayo, ili waamue kujikabidhi kwa Mungu na kuomba neema ya kukua katika njia zake, pamoja na kusamehe.
Pia, alisema kuwa mtu asiyesamehe, anaendelea kubeba mizigo, hivyo akawataka walioondolewa Seminarini, kuacha kujibebesha mizigo ya hasira, na ya kutaka kulipiza kisasi.
Kwa upande wake Mkuu wa Majeshi Mstaafu (CDF), Venance Mabeyo, akizungumza kwa niaba ya Waseminari wa zamani, alisema kuwa hiyo ni fursa kubwa kukutana katika Adhimisho hilo, kwani wengine hawafahamiani kutokana na wingi wao.
Mabeyo aliwasihi Waseminari wenzake wa zamani kuwa watu wa kusameheana pale wanapokoseana, huku wakiepuka kuwa na jazba, akisema kwamba yeyote mwenye jazba, neno ‘msamaha’ halikai katika msamiati wake.
Alisema pia kuwa kila mmoja anatakiwa kujitafakari na kujiuliza, je, anafanya mara ngapi matendo ya huruma? Huku akisisitiza kuishi vizuri na watu wa hulka tofauti tofauti katika jamii zao.

DAR ES SALAAM

Na Mathayo Kijazi

Utoaji wa huduma za Kijamii zikiwemo Elimu, Afya, na huduma zingine katika kustawisha ustawi na maendeleo ya mwanadamu, ni njia mojawapo za uinjilishaji katika kumtangaza Yesu Kristo.
Hayo yalisemwa hivi karibuni na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Dominika ya Nne ya Kwaresma, iliyokwenda sanjari na kuweka jiwe la msingi katika Shule ya Parokia ya Bikira Maria Mama wa Rozari Takatifu - Makongo Juu, jijini Dar es Salaam.
“Hamkuishia hapo, mmepania kujikita katika huduma za kijamii. Huduma za Kijamii ni namna mojawapo ya uinjilishaji. Tunainjilisha kwa kutoa elimu, tunainjilisha kwa kutoa huduma za afya, tunainjilisha kwa kutoa huduma nyingine zozote zinazochangia ustawi na maendeleo ya mwanadamu;
“Basi, kwa kuwa na mikakati hiyo, nawatambua kama Parokia hai. Muendelee kuwa na umoja, muendelee kuwa na mwamko wa kichungaji, muendelee kuinjilisha na kumtangaza Kristo kwa hali na mali. Leo mnapoweka jiwe la msingi la shule ya Parokia hii, nawaombea shughuli hii iendelee vizuri ili ipate kufikia upeo unaotakiwa,” alisema Askofu Ruwa’ichi.
Awali katika homilia yake, Askofu Mkuu Ruwa’ichi aliwataka Wakristo kusikia furaha kutambulika kama watoto wa Mungu, na kama watu waliokombolewa katika maisha yao.
Aliwasihi kuendelea kumwomba Mungu awazidshie neema yake ili wazidi kukua katika fadhila, katika imani, na katika ushuhuda wa Kikristo.
Aidha, aliwaalika Waamini kutambua kwamba wao siyo Wakristo kwa sababu ya mastahili yao wala kutokana na wema wao, bali wako Wakristo kwa sababu Mungu anawapenda na kuwahurumia.
“Mungu alilichagua Taifa la Israel liwe Taifa lake Takatifu, siyo kwa sababu walikuwa Taifa kubwa kuliko Mataifa yote, na wala siyo kwa sababu walikuwa wazuri kuliko watu wote, bali Mungu aliwateua kutokana na huruma na upendo wake,” alisema Askofu Mkuu, na kuongeza,
“Na ukweli huo unaweza kuusema pia kuhusu sisi Wakristo. Sisi tuko Wakristo, siyo kwa sababu ya mastahili yetu, tuko Wakristo, siyo kwa sababu ya wema wetu, tuko Wakristo kwa sababu Mungu anatupenda.”
Kwa upande wake Paroko wa Parokia hiyo, Padri Joseph Massenge, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Tumaini Media, alimshukuru Askofu Mkuu Ruwa’ichi kwa kufika parokiani hapo na kudhimisha Misa hiyo Takatifu, pamoja na kuweka jiwe la msingi la shule ya Parokia hiyo.
Padri Massenge alisema kuwa lengo la kujenga shule hiyo, ni kuwapunguzia changamoto wazazi na walezi ambao mara kwa mara hutumia muda wao kuwapeleka watoto wao katika shule za mbali na eneo hilo.
“Shule hii tungependa iwe na mtindo wa shule kama ile ya St. Joseph kule mjini, kwa sababu watu wengi kutoka huku Makongo wanaamka usiku usiku kuwapeleka watoto wao kule St. Joseph,” alisema Padri Massenge.
Aidha, Padri Massenge alitumia nafasi hiyo kuwaomba Waamini kuchangia ujenzi wa shule hiyo, ili baadaye wapewe kipaumbele pindi wanapokwenda kuandikisha watoto wao kujiunga na shule hiyo.
“Lakini niwakumbushe ninyi vijana mnaozaa, nawaambia tena, hata kama Baba Askofu atanihamisha, nitarudi kuja kukagua siku ya kuandikisha watoto, kama majina yako hayapo kwenye vitabu vya kuchangia shule, kupata nafasi utapata tabu sana. Kwa hiyo mjitahidi mchangie,” alisema Padri Massenge.
Vile vile, Padri huyo alithibitisha kwamba shule hiyo haitakuwa na gharama kubwa katika utoaji wa huduma ya elimu, bali itakwenda katika mfumo wa kawaida, kwani ni Waamini wenyewe ndio wamechangia ujenzi huo.

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu amesema kuwa dhambi ni hali inayoleta maafa na mateso makubwa kwa watu, kwani ni chukizo kwa Mungu.
Askofu Mchamungu alisema hayo wakati akitoa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu iliyofanyika katika Kigango cha Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu-Salasala, Parokia ya Mtakatifu Agostino, Salasalaa.
“Dhambi, ndugu zangu ni chukuzi kwa Mungu, kwani dhambi inaleta maafa hata ukiangalia katika Biblia, Mungu aliruhusu watu wake wapelekwe utumwani Babeli…
Ni kwa sabababu ya matokeo ya dhambi, watu hawakumsikiliza Mungu, na matokeo yake ni kupata maafa, na hivyo nasi tujiepushe na dhambi,”alisema Askofu Mchamungu.
Askofu Mchamungu alibainisha kuwa dhambi inaleta madhara kwake mtu binafsi, kwani hata mtu anayeiba anakamatwa, anafungwa, na huko atateseka na kuwa na mahangaiko makubwa kutokana na dhambi aliyotenda.
Askofu huyo aliendelea kufafanua kwamba hata mtu aliyetoa uhai wa mtu mwenzake, anafungwa, na tena kifungo ambacho ni cha maisha, ama kupokea hukumu ya kifo kwa kunyongwa. Hiyo yote ni matokeo ya dhambi, hivyo akiwasihi waamini kukaa mbali na dhambi.
Aonya kuhusu nyumba ndogo:
Kwa mujibu wa Askofu Mchamungu, tabia ya baadhi ya watu kuwa na nyumba ndogo ni dhambi ambayo inatesa wengi, hasa kwa kushindwa kuheshimu ndoa zao, na hivyo kupata mahangaiko ya kutunza familia mbili, ikiwemo isiyo halali, akiwataka waamini kuacha kufanya hivyo.
“Na sisi dhambi tunazozitenda zinatuletea mahangaiko makubwa na mateso, na ukitaka kuishi kwa amani bila mahangaiko mengi, fuata mpango wa Mungu. Endeeleeni kumuamini Kristo, kwani kwa kufanya hivyo, mtapata uzima wa milele,” alisema Askofu Mchamungu.
Kwa upande wake Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Agostino, Salasala, Padri Peter Assenga, alisema kuwa uongozi wake kwa kushirikiana na Kamati Tendaji wamefanya jitihada mbalimbali, ikiwemo za kuwahamasisha waamini kushikamana ili kukusanya fedha za kutekeleza ujenzi wa kanisa la Kigango.
Padri Assenga aliitaka Kamati Tendaji kuhakikisha inatekeleza vyema wajibu wake ili kufanikisha mipango waliyojiwekeza ya kukamilisha ujenzi wa kanisa hilo.
Naye Boniface Ngowi, Mwenyekiti Parokia ya Mtakatifu Augustino, Salasala, alimshukuru Askofu Mchamungu kwa kusali nao katika Misa hiyo na kushuhudia maendeleo ya Kigango hicho chenye historia ya kuwa Parokia hivi karibuni.
Alisema kuwa tangu mwaka 2015 Padri Assenga alipoingia Parokia ya Salasala, alifanya kazi kubwa ya kuanzisha Vigago vya Mtakatifu Sesilia, Kinzudi, na Mtakatifu Dominiko, Mbezi Juu, ambavyo sasa ni Parokia, na Vigango vya IPTL na vingine vingi, kwani ni kazi iliyotukuka.
Ngowi alibainisha kuwa mambo yote yanayoonekana kwa sasa ni matunda ya utendaji mzuri wa Padri Assenga kwa kushikamana na Kamati Tendaji ya Parokia, kwani amefanya mambo mengi parokiani hapo, ikiwemo ujenzi wa kanisa jipya kubwa na zuri.
Aidha, aliwataka waamini wa Parokia ya Salasala kuendelea kushikamana, kwani mafanikio yote yanaletwa na wao waamini wenyewe.

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Mlezi wa Shirika la Wazee na Wastaafu Katoliki, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, ambaye pia ni Paroko wa Parokia ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, Manzese, jimboni humo, Padri Benedict Shayo, amesema kuwa safari ya utakaso inahitaji uvumilivu.
Padri Shayo alisema hayo wakati akizungumza na Tumaini Letu katika mahojiano maalumu baada ya Shirika hilo kufanya matendo ya huruma katika Kituo cha Kulelea Watoto Wadogo, na Kijiji cha Wazee katika Kituo cha Msimbazi, jijini Dar es Salaam.
Alisema kuwa wazee wastaafu wameamua kujitoa kwa kile kidogo walichonacho kusaidia wahitaji, hasa katika kipindi hiki cha Kwaresma, kwani ni kipindi cha kujikatalia, kujinyima na kujitoa kwa ajili ya wengine.
Alisema kuwa hatua hiyo imefikiwa katika kutimiza nia ya Misa yao ya Shukrani iliyofanyika parokiani Manzese.
Alsiema kuwa wanapotambua na kutathmini upendo wa Mungu wa kuwafikisha tena katika nyakati hizi, ni vyema wakatoa majitoleo yao, kwa kutoa vipawa walivyonavyo ili waweze kutimiza nia hiyo.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Shirika la Wazee na Wastaafu Wakatoliki, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Profesa Alphonce Kyessi, alisema kuwa hatua hiyo ni katika kutimiza azma yao ya kufanya matendo ya huruma kwa kutoa sukari, mchele na mafuta kwa Wazee wa Kijiji cha Wazee, Msimbazi, ili nao waweze kujikimu.
“Tumewaona wazee wa hapa na tumetoa majitoleo yetu na tutaendelea kutekeleza wajibu huu …ni utaratibu wetu wa kila mwaka lakini mwaka huu tumeonelea vema tuje hapa Kijiji cha Wazee lakini pia tumetoa kwa Kituo cha kulelewa Watoto wadogo hapa Msimbazi,” alisema Proresa Kessy.
Aidha, Profesa Kessy amewasihi waamini na wote wenye mapenzi mema vijana UWAKA, WAWATa wanaendelea kufanya matendo ya huruma, si kwa wazee tu, lakini pia hata katika Hospitali kwa wagonjwa.
Naye Sista Rosina Isaya Ngukuyawene, Mlezi Mkuu wa Kijiji cha Wazee, Msimbazi, alisema kuwa changamoto kubwa ni bima ya afya, kwani waliyopewa na Ustawi wa Jamii ni ndogo na haiwasaidii sana wazee, na hivyo kulazimika kutoa fedha za ziada ili watibiwe.
Alisema kuwa changamoto nyingine ni uchakavu wa majengo ya nyumba za kuishi wazee hao, kwani nyingi hali yake ni mbaya na zinahitaji kufanyiwa ukarabati mkubwa kusudi wazee waishi katika mazingira bora zaidi.

MANGOCHI, Malawi

Timu ya wadau wa Kanisa na jumuiya, walitembelea nyumba iliyoonekana kutengwa na kuezekwa kwa nyasi ili kutathmini uwezekano wa kuunganishwa tena watoto wa kaya hiyo katika Taasisi ya malezi.
Nyumba hiyo ipo katika Kijiji cha Philipo Mbewe, Parokia ya Kankao, Jimbo Katoliki la Mangochi, nchini Malawi, Kusini mwa nchi hiyo.
Zaidi ya watu 20 walipofika nyumbani kwa Viola (si jina lake halisi), mtu aliweza kuhisi hali tulivu wakati mwanamke huyo wa makamo, alipokuwa akiandaa chakula cha mchana kwenye veranda ya nyumba kwa ajili ya watoto wake wa shule.
Timu hiyo ilijumuisha Askofu wa Jimbo hilo, Mhashamu Montfort Stima, Machifu wa eneo hilo wakiongozwa na mwakilishi wa Mamlaka ya Kimila (TA) Chanthunya, mwakilishi wa Ustawi wa Jamii wa Serikali, Poverelle Sisters, wanaofanya kazi katika nyumba ya watoto ya Chimwemwe.
Wengine ni Paroko wa Parokia ya Kankao na Makasisi wengine kutoka Jimbo Katoliki la Magochi, wawakilishi kutoka Chama cha Mabaraza ya Maaskofu Wanachama Afrika Mashariki (Association of Member Episcopal Conferences in Eastern Africa: AMECEA), Chama cha Masista nchini Kenya, (Association of Sisterhoods of Kenya: AOSK), na Chama cha Wanawake katika Taasisi za Kidini za Malawi (Association of Women in Religious Institutes of Malawi: AWRIM).
Kwa upande wake Paroko wa Parokia hiyo, Padri Edwin Kankao alisema kuwa kikundi kilichochaguliwa kutoka katika timu inayozungumza lugha ya Chichewa, kilimhoji Viola, shangazi ya mtoto huyo ili kuunganishwa tena, juu ya kujiandaa kwake kupokea chakula cha ziada cha mdomo, hadi cha watoto wake wanne.
Baadhi ya wanakikundi walikaa na waliotawanyika ndani ya kiwanja wakijadili umuhimu wa mageuzi ya malezi ya mtoto, wakati wakijadiliana juu ya njia ya mtoto kuunganishwa tena kutoka kwenye nyumba ya watoto ya Chimwemwe.
Alipokuwa akihutubia kundi zima baada ya mchakato wa kuhojiwa, Mtawa wa Jimbo Katoliki la Magochi Askofu Stima, alishukuru mpango wa mageuzi ya malezi na kuihakikishia familia ya Viola kuwa hawakuwa peke yao katika safari hii.
Mwakilishi wa Mamlaka ya Kijadi (TA) Moses Skello ambaye alikuwa sehemu ya kikundi kilichotembelea familia ya Viola, alitoa shukrani zake kwa timu hiyo na kuahidi kuendelea kushirikiana na kuunga mkono ili kuhakikisha kuwa mageuzi ya utunzaji yanafanyika nchini Malawi.
Ingawa hali ya uchumi katika nyumba ya Viola iliyokuwa na nyumba mbili ndogo za nyasi na rasilimali kidogo haikuonekana kuwa sawa kwa kuunganishwa tena kwa mtoto, nia ya shangazi na ushirikiano na msaada uliohakikishwa kutoka kwa wadau, ni hatua kubwa ambayo changamoto za umaskini ambazo zingeweza kuonekana wazi, mtoto kwa muda mrefu ataweza kupata mahali pa kutambua kama nyumba.

LILONGWE, Malawi
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Malawi (Catholic University of Malawi: CUNIMA), Mshiriki Profesa Ruth Ngeyi Kanyongolo, amejitolea kufanya kazi pamoja kama njia ya kufikia maono na dhamira ya chuo hicho.
Akizungumza baada ya kutambulishwa kwa wafanyakazi na wanafunzi wa chuo hicho na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho, Askofu Mkuu Thomas Luke Msusa, Makamu Mkuu huyo mpya alieleza haja ya kuwepo kwa ushirikiano kati ya wafanyakazi na wanafunzi.

VATICAN CITY

Baba Mtakatifu Fransisko amesema Serikali ya Ukraine inapaswa kukubali na kuwa jasiri katika majadiliano ya kusaka amani ya kudumu.
Alisema kuwa Ukraine haina budi kuonesha ujasiri na kuanza kujikita katika majadiliano ili kusitisha vita hiyo ambayo inaendelea kusababisha athari kubwa kwa maisha ya watu na mali zao.
Vita ya Ukraine, kuna baadhi ya nchi ambazo zimejitolea kuongoza majadiliano kati ya Urusi na Ukraine na kati ya nchi hizi na Uturuki, kabla ya mambo hayajawa mabaya zaidi. Lengo la majadiliano ni kuokoa maisha ya watu. Ukraine imeteseka tangu utawala wa Stalin.
Vita kati ya Urusi na Ukraine, Israeli na Palestina pamoja na athari zake kwenye Ukanda wa Gaza, ni kati ya tema zilizojadiliwa na Baba Mtakatifu Fransisko kwenye mahojiano maalum kati yake na Lorenzo Buccella wa Kituo cha Radio Na Televisheni cha Uswis, “Radiotelevisione Svizzera, RSI.” Mahojiano haya yatachapishwa rasmi tarehe 20 Machi mwaka 2024.
Katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, Kanisa limetumia silaha zifuatazo; Kufunga na kusali; Ibada ya Misa Takatifu; Tafakari ya Neno la Mungu; Matendo ya huruma; kiroho na kimwili pamoja na Rozari Takatifu, ili kuwajengea watu imani, matumaini na mapendo katika kipindi hiki kigumu cha historia, sanjari na kukimbilia faraja na wokovu kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Machi 13 mwaka 2013 Baba Mtakatifu Fransiko alichaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki (Papa wa 266), kielelezo cha huduma na mwaliko wa kuchuchumilia utakatifu wa maisha, aligusia madhara ya vita, na kwamba Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujikita katika kutafuta na kudumisha amani duniani, ili kuondoa giza la maisha linalomsonga mwanadamu sanjari na kuondokana na unafiki katika maisha, ili kutangaza na kushuhudia ukweli.
Baba Mtakatifu Fransisko alisema, Vita kati ya Urusi na Ukraine, Israeli na Palestina pamoja na athari zake kwenye Ukanda wa Gaza ni mambo yanayofifisha matumaini ya watu wa Mungu, na kwamba hili ni jambo baya sana na kwamba vita mara nyingi inahitimishwa kwa pande husika kuwekeana mkataba.
Baba Mtakatifu alitumia sura ya bendera nyeupe iliyopendekezwa wakati wa mahojiano ili kuonesha umuhimu wa kusitisha chuki na uhasama, ili hatimaye, kufikia maridhiano yanayopaswa kufikiwa kwa ujasiri katika mazungumzo, na kwamba matumaini yake ni suluhisho la kidiplomasia kwa haki na amani ya kudumu.
Baba Mtakatifu alikaza kusema kwamba Ukraine haina budi kuonesha ujasiri na kuanza kujikita katika majadiliano ili kusitisha vita hii ambayo inaendelea kusababisha athari kubwa kwa maisha ya watu na mali zao.
Kuna baadhi ya nchi ambazo zimejitolea kuongoza majadiliano kati ya Urusi na Ukraine, na kati ya nchi hizi na Uturuki, kabla ya mambo hayajawa mabaya zaidi. Lengo la majadiliano ni kuokoa maisha ya watu.
Ukraine ni taifa lililoteseka tangu utawala wa Joseph Stalin, kiongozi wa Sovieti ya Urusi.
Kwa mara ya kwanza katika historia ya Kanisa kwa miaka ya hivi karibuni, Baba Mtakatifu Fransisko aliadhimisha Ibada ya Liturujia ya Neno la Mungu, iliyoambatana na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu pamoja na kutoa baraka kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, maarufu kama “Urbi et Orbi” kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican.
Baba Mtakatifu alibainisha Vita nchini Slovakia kuwa imewafuta wazee wengi, na kwamba hakuna picha kubwa zaidi ya madhara ya vita kama hii, kwani watu wengi wanafariki dunia, na kwamba Njiwa ni alama ya amani.
Vita kati ya Ukraine na Urusi vimesababisha madhara makubwa.
Baba Mtakatifu alisema kwamba watoto wengi anaokutana nao kutoka kwenye maeneno ya vita hawana furaha, amani na utulivu wa ndani; ni watu ambao kesho yao imepokwa. Vita daima ni kielelezo cha kushindwa ubinadamu.
Hakuna vita ya haki, bali vita ni matokeo ya biashara haramu ya silaha duniani, kielelzo cha watu wachache kujichumia utajiri wa haraka haraka kwa damu ya watu wasiokuwa na hatia. Hiki ni kielelezo cha giza katika maisha ya mwanadamu, ubinafsi unaoteketeza maisha ya watu kimaadili.
Kwa bahati mbaya mwanadamu katika maisha yake, anayo pia sehemu ya giza, kielelezo cha dhambi inayomwandama mwanadamu. Giza katika maisha ya mwanadamu linaweza kudumu kwa kitambo kirefu.

Walezi wa Shirika la Kipapa la Utoto Mtakatifu Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam wakiwa katika viwanja vya Hospitali ya Kardinali Rugambwa iliyopo Ukonga, jijini Dar es Salaam, walipokwenda kufanya matendo ya upendo katika Hospitali hiyo. (Picha na Mathayo Kijazi)

Mlezi wa Shirika la Wazee na Wastaafu Katoliki wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Padri Benedict Shayo, akibariki majitoleo ya Wazee na Wastaafu hao wakati wa Sala iliyofanyika katika Parokia ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, Manzese jimboni humo, kabla ya kuyapeleka kwa wahitaji katika Kituo cha kulelea wazee na watoto yatima kilichopo Msimbazi Centre, Dar es Salaam. (Picha zote na Yohana Kasosi)

Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu (wa tatu kushoto), akikagua ujenzi wa kanisa lawa Mtoto Kigango cha Mtakatifu Theresia Yesu katika Parokia ya Mtakatifu Augustino, Salasala jimboni humo, baada ya Adhimisho la Misa Takatifu ya Dominika ya Nne ya Kwaresma. Wa nne kulia ni Paroko wa Parokia hiyo, Padri Peter Assenga.