DAR ES SALAAM
Na Mwandishi wetu
Tumaini Televisheni nchini Tanzania kwa kushirikiana na Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Italia (Conference Episcopal of Italia: CEI), imezindua rasmi mpango maalumu wa Utunzaji Mazingira kwa kupanda miti katika Dekania, Parokia, na sehemu mbalimbali kote nchini ikiwa ni kuunga mkono Utekelezaji wa Tamko la Baba Mtakatifu Fransisko kuhusu Mazingira, ‘Laudato Si’.
Uzinduzi huo ulifanywa Machi 26 mwaka huu na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Kubariki Mafuta Matakatifu, iliyoadhimishwa katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu, jimboni humo.
Baada ya uzinduzi huo, Askofu Ruwa’ichi alikabidhi miche ya miti kwa Madekano wa Dekania zote 15 za Jimbo hilo, ili kwenda kuipanda miti hiyo katika Dekania zao na Parokia, akiwataka Madekano hao kwenda kuhamasisha utekelezaji wa mpango huo wa kutunza mazingira kwa Waamini wao.
Akizungumzia mpango huo wa kutunza mazingira, Mkurugenzi wa Tumaini Media yenye vyombo vyake Tumaini Televisheni, gazeti Tumaini Letu, na Redio Tumaini, Padri Joseph Massenge alisema kwamba zoezi la kupanda miti ni endelevu linalotekelezwa Nchi nzima.
“Yaani kazi hii haina mwisho, ni mpaka mwisho wa dunia kwa lengo la kuhakikisha mazingira yanatunzwa kwa kupanda miti katika Majimbo Katoliki yote nchini Tanzania,” alisema Padri Massenge.
Mkurugenzi huyo wa Tumaini Media alisema kuwa mpango huo unaendana na utoaji wa elimu kwa vijana na Waamini kuhusu umuhimu wa kuhifadhi na kutunza mazingira Nchi nzima.
Padri Massenge aliyataja Majimbo Katoliki Makuu ambapo mradi wa kutunza mazingira kwa kupanda miti, unaendelea kutekelezwa, kuwa ni Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Dodoma, Arusha, Mwanza, Mbeya, Tabora, na Jimbo Kuu Katoliki la Songea.
Kwa mujibu wa Padri Massenge, kazi ya upandaji miti ltasaidia kwa kiasi kikubwa kunusuru uharibifu wa mazingira nchini, unaotokana na ukataji miti ovyo.
Julai 13 mwaka 2022, Baba Mtakatifu Fransisko alitoa Waraka wake wa Kichungaji wa ‘Laudato Si,’ yaani ‘Sifa iwe kwako juu ya utunzaji wa nyumba ya wote’ unagusia kuhusu mazingira; Injili ya Kazi ya Uumbaji na Amani; Vyanzo vya mgogoro wa Ikolojia na watu; Ikolojia ya mazingira, uchumi na jamii.