Mwanza
Na Paul Mabuga
Anna Nicodemus, mmoja wa wahariri katika kituo cha runinga cha Shirika la Utangazaji la Namibia (Namibia Broadcasting Corporation: NBC), yeye na timu yake wamepanga kufanya filamu halisi (factual film) kama sehemu ya mafunzo ya chuo kimoja katika jiji la Berlin nchini Ujerumani, na wameamua kuifanya kazi hii katika nchi yao.
Kwa hiyo, wanapanga kutengeneza maudhui ambayo yataonesha tofauti kati ya maisha ya kijijini na ya mjini, wakirejea hali ilivyo katika mji mkuu wa nchi yao- Windhoek. Lakini katika mazungumzo nao kama wanafunzi wenzao, inabainika kuwa walichodhamiria sicho walichokikuta huko walikokwenda kutengeneza filamu hiyo.
Walianza na kumchukua Mhandisi wa Mwanga katika kituo hicho, aliyetambulishwa kwa jina la Zuma ambaye anatoka katika kabila la Wa -Himba (omu himba akiwa mmoja na wakiwa wengi ni Ova himba), ambalo linatoka Kaskazini mwa nchi hiyo.Wa-himba kwa kiasi ni wafugaji, na wanasifika kwa kujipaka tope jekundu na kwa idadi wanakadiriwa kufikia watu elfu 25.
Katika filamu hiyo, Zuma ambaye ameacha mchumba wake katika jiji la Windhoek, anasafiri hadi katika kijiji chao kwa lengo la kusalimia mwishoni mwa juma. Anapofika huko, kitu cha kwanza ni kuelekezwa avue mavazi ya mjini, na kisha kuvaa lubega baada ya kujiisiliba udongo mwekundu uliochanganywa na mafuta ya ng’ombe. Hapa ndipo anapofanana na watu wa jamii yake.
Pengine tofauti na mazoea, safari hii mjomba wake anatangaza katika kadamnasi kwamba ameamua kijana wake Zuma aoe, na mwanamke yupo amemchagulia, ni mama wa ki-hinba ambaye kwa umri ni mkubwa kuliko muoaji. Kwa Wahimba mjomba ndiye mwenye mamlaka kwa kijana, na hata kwa kumtafutia mchumba. Jukumu hili hufanyika kwa umakini kwa sababu kwao mwanamke ndiye mkuu wa familia.
Mke ambaye ana watoto wanne aliozaa na wanaume wengine, sasa amepata kijana wa jijini Windhoek, na kwa taratibu Zuma hawezi hata kuleta fyoko na yule mchumba wake aliyemuacha mjini ambaye hatambuliki, kwani hana mamlaka ya kujichagulia, na lazima idhini itoke kwa mjomba.
Mke anatinga kwenye ndoa akiwa kifua wazi. Wanawake wa Kihimba ndivyo walivyo kijiji kizima, siku zote hawafichi matiti. Hakuna cha hereni za English Gold wala jeans, unafanya mchezo nini! Wametinga viurembo vya kujitengenezea wenyewe, na vijimavazi kuziba kiuno. Wamejisiliba udongo mwekundu na kujipaka mafuta ya ng’ombe. Kutoka hapo anapatikana Bi. harusi, mengine kama shela na saloon, ishia nayo huko huko.
Filamu hii ilipewa jina la Maisha Pacha ya Zuma (Double Lives of Zuma!), yaana Zuma wa jijini Windhoek anayeoongea Kireno na Kiingereza, na mwingine wa kijijini Kaokoland, anayeongea Kiherelo na Kiafricana.
Kimoja cha kuchukua ni kwamba, familia inaonesha mamlaka na wajibu katika suala la ndoa, na kimsingi huu ndio uliokuwa utaratibu mzuri katika jamii zetu. Mathalan, mjomba anamwendea kijana wake na kumwambia kule kanisani ameona msichana mrembo ambaye anamfaa kuwa mke wake. Labda hana mkorogo, na nywele kazisuka vyema, siyo kama zile zilizosambaa mithili ya brashi bovu la shetani.
Pengine shangazi anamfuata binti yake na kumwambia kule kanisani amemuona kijana anayefaa kuwa mume wake, kwani kavaa vyema na hajaacha chupi nje, hajasuka wala kuvaa hereni hivyo hata wakioana na kukaa kwenye nyumba yao, atajulikana nani ni mwanamke na nani ni mwanaume. Yaani kijana mchumba mtarajiwa hajajitindua bongo na kuweka boga kichwani badala yake! Anajisimamia na hana mwelekeo wa kulelewa.
Siku hizi vijana wameachiwa demokrasia, wanaamua watakavyo! Waoe au kuolewa sawa, na wasiolewa au kutooa nayo ni burudani tu kwao. Hili la mwisho ndilo limekuwa fasheni, na ushahidi ni takwimu kwamba asilimia 61 ya Watanzania walio mijini na asilimia 55 ya walio vijijini, hawajoa wala kuolewa. Hizi ni takwimu rasmi ambazo zimekuwa gumzo mitandaoni, huku Viongozi wa Dini wakiombwa kuingilia kati.
Takwimu hizi naana yake ni kwamba karibu watu wawili katika kila watatu, ambao bila shaka wanapaswa kuwa kwenye ndoa unaokutana nao mjini, hawajaoa au hawajaolewa, huku katika kila watu wawili unaowaona kule kijijini, basi ujue mmoja kati yao hajaoa au hajaolewa. Hali hii pengine inakuja baada ya vijana kuanza kuona kwamba hakuna umuhimu wa kuoa ama kuolewa, na kwao hiyo ni fasheni.
Pengine ni kweli kwamba kuoa au kuolewa na uamuzi unaohitaji umakini, kama mwanafalsafa mmoja anayenukuliwa mara kadhaa bila kutajwa, alivyowahi kusema kuwa, kati ya kuoa na kutooa, au kuolewa ama kutoolewa, lolote kati haya utakalochagua, utajuta! Lakini ni ukweli usiopingika kwamba kuoa ama kuolewa, ni wito wa lazima, labda kuwe na sababu inayokubalika.
Mjadala wa takwimu hizi la lundo la Watanzania wasio katika ndoa, unapohamia katika daladala moja jijini Mwanza inayosafirisha abiria kutoka jijini kati kwenda Buswelu ambako unamkuta msafiri ambaye ni mwenyeji jamii moja kutoka kaskazini mwa Tanzania, na anasema, “Tatizo ni wasichana hawapendi kuzaa, wanapenda kudondosha (kutoa mimba), lakini vijana wa kiume wakilazimishwa, wataoa, wao hawana shida.”
Yeye analiona tatizo ni kwa mabinti kutotaka kuolewa wakikwepa majukumu yao ya asili ya kuwa wake, kuzaa na kulea. Wakati huyu muungwana akisema hivi, Mwenyekiti wa mtaa mmoja jijini humo, anakuja na shauri la ajabu kidogo. Linahusu mama mmoja mwenye umri wa kati ya miaka 40 na 50 ambaye anadai kwamba kuna kijana mpenzi wake amempa ujauzito na kumwibia pesa. Aliingia katika mahusiano na kijana huyo baada ya kufiwa na mumewe.
Unaposikia juu ya shauri hili, unamwangalia kijana mhusika na kugundua kuwa ana umri wa miaka kati 20 hadi 25. Lakini kabla mambo hayajaenda mbali, Mama mlalamikaji na mlalamikiwa, ambaye ni kama mwanae, wanaonekana wakiwa pamoja, wakipata kinywaji, na labda kulea mimba yao. Mwenyekiti ashauriwe, kwamba, hawawezi vijana wa kileo kwani wamenogewa kulelewa na kuwa “ndugu wakigombana, kamata jembe ukalime!”