Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Moja ya Mambo muhimu na ya Msingi ambayo Baba Mtakatifu Fransisko ameyakazia na kuyasisitizia katika ziara ya Kitaifa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan na ujumbe wake aliyoifanya hivi karibuni mjini Vatican, ni malezi na makuzi ya Watoto.
Katika ziara hiyo ya Kitaifa, Mama Evaline Malisa Ntenga, ambaye ni miongoni mwa ujumbe huo wa Rais, anasema kuwa Baba Mtakatifu Fransisko amekazia umuhimu wa malezi na makuzi ya watoto, sanjari na kujikita katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia.
Dalmas G. Gregory, M/Kiti Halmashauri Walei Jimbo la Zanzibar, anasimulia yale yaliyomgusa. Leonard Mapolu, Mwenyekiti wa VIWAWA, Taifa, anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema na baraka kupitia kwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (Tanzania Episcopal Conference: TEC).
Imegota takribani miaka 12 tangu Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania alipotembelea mjini Vatican na kukutana na Baba Mtakatifu Benedikto XVI tarehe 19 Januari 2012.
Katika mazungumzo ya dakika kumi na tano, viongozi hawa wawili waligusia kuhusu: Majadiliano ya kidini, amani katika eneo la Maziwa Makuu, Afya, Ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.
Ni katika muktadha wa kujenga na kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na Vatican, tarehe 12 Februari 2024, Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania alikutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Fransisko mjini Vatican.
Aidha, Rais Samia alibahatika pia kukutana na kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu Mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu Mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa.
Katika mazungumzo yao ya faragha yaliyodumu kwa takribani dakika 25 wameridhika na uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican na Tanzania; mchango na dhamana ya Kanisa Katoliki katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Tanzania, hususan katika sekta ya: elimu, afya, ustawi wa jamii pamoja na changamoto ambazo Tanzania inapitia kwa sasa.
Mama Evaline Malisa Ntenga, Mjumbe wa Bodi Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani na Rais wa Wanawake Wakatoliki Afrika WUCWO Afrika, ambaye pia ni Mwenyekiti wa WAWATA, Taifa, nchini Tanzania, katika mahojiano maalum na Radio Vatican, alionesha furaha kwa heshima waliyopewa waamini walei kuungana na Rais Samia Suluhu Hassan katika ziara yake ya kikazi mjini Vatican.
Mama Ntenga alimpongeza Rais Samia kwa juhudi zake za kukuza: Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Kusonga mbele; mambo yanayofumbatwa katika falsafa ya “Four R.” Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu Fransisko alipokutana na kuzungumza na Mama Ntenga amekazia umuhimu malezi na makuzi ya watoto sanjari na kujikita katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia.
Amewasihi waamini walei waendelee kushikamana na kutembea pamoja kama sehemu muhimu sana ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi nchini Tanzania; ujenzi ambao kimsingi unafumbatwa katika: Umoja, Ushiriki na Utume. Ameipongeza Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, (WAWATA), kwa kuendelea kuwa mstari wa mbele kwa malezi na makuzi ya Utoto Mtakatifu nchini Tanzania.
Pamoja na mambo mengine, Rais Samia Suluhu Hassan alikazia umuhimu wa kujenga, kuendeleza pamoja na kudumisha maridhiano ili kuendeleza misingi ya haki, amani, ustawi na maendeleo ya Tanzania.

LUSAKA, Zambia
Shirika la Huduma za Vyombo vya Habari vya Kikatoliki, limeadhimisha Siku ya Redio Duniani kwa kutambua mchango mkubwa wa redio katika kueneza ujumbe wa matumaini, upendo na haki ya kijamii.
Mkurugenzi Mtendaji wa Huduma za Vyombo vya Habari Katoliki nchini Zambia, Padri Winfield Kunda alisema kuwa Siku ya Redio Duniani mwaka huu imeadhimishwa chini ya kaulimbiu “Radio - A Century Informing, Burudani, na Kuelimisha.” Inaangazia athari kubwa ya redio katika kuunda maisha kwa kutuhabarisha na kukuza elimu tangu zamani.

ADDIS ABABA, Ethiopia

Askofu Mwandamizi wa Jimbo Katoliki la Eparchy Emdibir Eparchy, Mhashamu Askofu Teshome Fikre, amesimikwa.
Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Ethiopia, Mwadhama Abune Kardinali Berhaneyesus, aliongoza Ibada hiyo ya kuwekwa wakfu Askofu Teshome Fikre, ambapo Askofu huyo mpya amechukua jina la ‘Askofu Luka.’
Tukio hili lilihudhuriwa na Askofu Mkuu Antoine Camilleri, Balozi wa Kitume nchini Ethiopia na Djibouti, Askofu Mussie, Askofu wa Emdibir Eparchy, Maaskofu Katoliki kutoka Ethiopia na Eritrea.
Wengine ni Padri Raphael Simbine, Katibu Mkuu wa SECAM, Padri Anthony Makunde, Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya AMECEA, kutoka Kanisa la Kiorthodoksi la Ethiopia, Askofu Mkuu Melketsedik, Askofu Mkuu wa Jimbo la Gurage Mashariki na Magharibi.
Kutoka Kanisa la Kiinjili, Mekane Yesus na Padri Yonas Yigezu; Rais wa Ethiopia akiwa na Balozi Misganu Arega; Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Shirikisho la Ethiopia; na Waamini wengine kutoka kote Ethiopia, walihudhuria.
Wakati wa Homilia, Kardinali alikumbusha kwamba moja ya majukumu ya Askofu ni kuhubiri na kueneza Injili ya Bwana, hata katika nyakati zinazofaa na zisizofaa, kama vile Mtume Paulo alivyomwambia Timotheo.
Mwadhama Abune Kardinali Berhaneyesus alimtaka Askofu mpya Lukas kusimama upande wake, na atamsaidia kwa maombi ili kutimiza wajibu huo.
Askofu Lukas katika maelezo yake, alitangaza mstari mkuu aliouchagua kwa utumishi wa Uaskofu wake, “Chunga Kondoo Wangu” Yoh 21:15.
“Siku zote Mchungaji atawaongoza kondoo mbele yao ili wasimame pamoja kwa upatano na mioyo na akili zao, bila kupoteza tumaini lao. Wakati mwingine anakuwa kati yao, akiwa mnyenyekevu na mwenye rehema,” alisema Askofu Lukas.
Kwa upande wake, uongozi wa Askofu Mussie umekuwa wa kuigwa tangu kuanzishwa kwa ‘eparchy’, ukiacha alama ya kudumu kwa jamii.
Katika moja ya utume wake, ni kuongoza ujenzi wa makanisa 15 mapya, ufunguzi wa makutaniko 12 ya kidini, na kupanua huduma za utawala.
Aidha, kujitolea kwake kunaenea zaidi ya mambo ya kiroho, kama inavyothibitishwa na mipango yake katika elimu (shule), huduma za afya (vituo vya afya, hospitali), miundombinu (maji, kilimo), na usaidizi wa kijamii (vituo vya wanawake na vijana, pia vituo vya huduma).

VATICAN CITY, Vatican
Baba Mtakatifu Fransisko amedinzua rasmi vikundi vya mafunzo ambavyo vitaratibiwa na Sekretarieti Kuu inayoshirikisha mabaraza yenye uwezo.
Kikao cha pili cha Sinodi kitafanyika kuanzia Oktoba 2 hadi 27 maka huu na kitatanguliwa na siku mbili za mafungo.
Sekretarieti kuu ya Sinodi imetaarifu kwamba Baba Mtakatifu Fransisko ameweka tarehe za kikao cha pili cha Mkutano Mkuu wa XVI utakaofanyika kuanzia Jumatano Oktoba 2 hadi Dominika  ya Oktoba 27 maka huu ili kuendeleza kazi ya Sinodi ya Kisinodi yenye kauli mbiu: “Kwa ajili ya Kanisa la Sinodi:ushirika, ushiriki na utume.”
Wakati huo huo kama taarifa hiyo, iyoandikwa kwa mkono (chirograph) kutoka kwa Papa pia ilichapishwa, ambayo itaanzisha vikundi vya mafunzo ili kuzama zaidi katika baadhi ya mada zilizoibuka katika kipindi kilichopita.
Vitaanzishwa vikundi kati ya Mabaraza ya Kipapa ya Curia Romana vyene uwezo na Sekretarieti Kuu ya Sinodi, ambayo itaratibu.
Katika barua ya mkono wake (chirograph), iliyowekwa kwa ushirikiano kati ya mabaraza ya Curia na Sekretarieti ya Sinodi, Papa Francisko anataja katiba ya Mtaguso wa Vatican, ya  hati ya Lumen Gentium ili kukumbuka kwamba Kanisa linaonesha uwepo wake, “katika Kristo, kwa njia fulani sakramenti, ambayo ni ishara na chombo cha ‘muungano wa karibu sana na Mungu na umoja wa jamii nzima ya binadamu’ na kwamba “inajidhihirisha kwa uwazi zaidi na uaminifu kwa ulimwengu katika tamaduni mbalimbali kama fumbo la ushirika wa kimisionari, Mwili mmoja, unaoshiriki katika Roho wake anayeufanya upya na kuuongoza katika kutangaza Injili kwa watu wote.”
Katika mwanga huu, katika katiba Mpya ya  Curia Romana ya  Praedicate Evangelium, tunasoma kwamba “maisha ya ushirika hulipatia Kanisa sura ya kisinodi. Hasa kusikiliza kwa pande zote na nguvu ya usawa katika kujiweka katika huduma ya utume wa watu wa Mungu kuhitimu kazi ya usaidizi wa Curia Romana kwa huduma ya Askofu wa Roma, ya mtu binafsi, maaskofu na Baraza la Maaskofu.
Ustadi wa kichungaji unaoutekeleza hupata madhumuni na ufanisi wao katika huduma ya ushirika wa kiaskofu na ushirika wa kikanisa katika muungano na chini ya uongozi wa Askofu wa Roma.
Tayari katika hati ya maandalizi ya “Kuelekea Oktoba 2024” ya Sekretarieti Kuu ya Sinodi, iliyochapishwa  mnamo tarehe 11 Desemba 2023, ilisisitizwa jinsi mkutano ujao ungezingatia mada ya ushiriki, kuhusiana na utekelezaji wa mamlaka, kama usemi wa ushirika katika huduma ya utume. Kwa hiyo  yangechunguza jinsi ya kuishi sinodi katika ngazi zote za Kanisa.
Sasa uamuzi wa Papa unaweka wazi kwamba baadhi ya dhamira muhimu zaidi zilizoibuka kutokana na kusikiliza Makanisa zinahitaji muda mwingi kwa ajili ya mafunzo ya kitaalimungu, kanuni na kichungaji kadiri ya utaratibu wa sinodi inayohusisha wataalam kutoka mabara yote na mbaraza ya Curia Roman kulingana na uwezo wao.

DAR ES SALAAM

Na Dk. Deoscorous B. Ndoloi

Mpendwa msomaji, karibu tena katika makala hii ya kuzungumza katika hadhara. Kwa wasomaji ambao watakuwa wageni katika safu hii, mada juu ya kuzungumza katika hadhara tuliianza katika makala ya 13 ya mwezi Novemba 2023. Baadaye, katika makala ya 17, ya mwanzo wa mwezi Desemba 2023, tuliona jinsi ya ‘kukabili na kumiliki jukwaa’. Kwa hiyo tumedumu katika mada hii ya namna ya kuzungumza katika hadhara, kwa takriban miezi mitatu. Ni matumaini yangu kwamba umefaidika na maarifa tunayoshirikishana, ili kujijengea stadi na weledi katika mawasiliano ya kibinadamu.
Leo, katika makala hii ya 28, tujadiliane namna ya ‘kuaga jukwaa’. Natumaini msomaji wangu ungetegemea niseme ‘kuaga hadhira au wasikilizaji’ lakini nimependa kuiita stadi hii ni ‘kuaga jukwaa’ kwa sababu zitakazokuwa wazi kwako baada ya kusoma na kuielewa mada hii. Yapo mambo muhimu ya kuzingatia unapofikia tamati ya mazungumzo. Nitayajadili kwa nambari ili yawe rahisi kukumbuka, na hasa kwa wale walioniambia kwamba huwa wanajadili mada hizi kama sehemu ya mafunzo yao chuoni, juu ya mawasiliano kwa umma (mass communication).
Kwanza, nikukumbushe – tulishauriana kwamba mwisho mzuri unaandaliwa toka mwanzo kabla ya wasilisho. Hivyo utakuwa umejipanga vizuri, kiratiba, iwapo utaacha dakika walao tano za kuhitimisha wasilisho lako. Ukijipanga vibaya utamaliza wasilisho ukiwa wamebakiza muda mrefu, hivyo kuanza kutafuta namna ya kujazilizia muda uliobaki. Kwa namna hii, unaweza kushawishika kuingiza masuala ambayo hayaendani na kusudio la mada husika. Unaharibu kazi nzuri uliyokwishafanya toka awali, unawavuruga au kuwachosha wasikilizaji. Afadhali ukimaliza yale uliyopanga, aga na uondoke. Kuna hata msemo kwamba, “mgeni mzuri ni yule anayefahamu muda wa kuaga”. Wakati mwingine ukijipanga vibaya unatindikiwa na muda, huku ukiwa umebakisha masuala muhimu ya kuwasilisha. Kwa namna hii, unaanza kuongeza kasi ya ajabu kuzungumza, kiasi kwamba hueleweki tena. Unaharibu ulichokwishasema. Jifunze kutumia muda.
Pili, wakati unatoa wasilisho, inawezekana wapo waliochelewa wasiweze kusikia usuli wa mada yako. Inawezekana wapo waliolazimika kutoka nje ya ukumbi kwa dharura wakati unatoa wasilisho. Pengine wengine walikosa utulivu, au wewe mwenyewe uliharibu mtiririko wa mawazo, hivyo ukawapoteza wasikilizaji, kwa muda. Wakati wa kuaga jukwaa, ndiyo muda wa fidia. Wakumbushe tena wasikilizaji, kwa kifupi sana, lengo la wasilisho lako; kwa maneno yaleyale uliyotumia mwanzoni. Kisha, tafuta walao mambo matatu au manne ambayo, ikiwa wamesahau mengi waliyosikia, basi haya waondoke nayo. Yape msisitizo wa kutosha.
Tatu, usiombe msamaha, labda kwa vile unahisi kuhufanya vizuri au hukuitendea haki mada husika. Kuomba msamaha, hasa ukiwa umefanya vizuri, ni kujifanya kuonesha unyenyekevu ambao unaweza kutafsiriwa kama unafiki. Wewe washukuru na waambie wasikilizaji kwamba una matumaini makubwa wote wamefaidika na wasilisho lako, na kwamba waliyoyasikia watayafanyia kazi na kuwashirikisha wengine.
Nne, usipoteze muda kuwashukuru waliokualika na waandaaji wa semina au kongamano. Hawa watashukuriwa mwishoni, na wenyeji wao kwa niaba ya kila mmoja aliyealikwa na aliyehudhurisha mada. Itoshe kusema, “Nawashukuru wote kwa usikivu wenu”. Hawa ‘wote’ ni pamoja na waandaaji wa kongamano. Hapo awali, katika makala ya 23, tuliona ‘aina za hadhira’; moja tuliita hadhira chuki (hostile audience) na nyingine hadhira mateka (captive audience). Tuliona kwamba hizi aina mbili za hadhira zinaweza kuwa na watu ambao wana mwamko wa chini sana, hivyo wasikupe ushirikiano wa kutosha wakati unatoa mada. Hata kama unahisi walikuwepo watu wa namna hii, usigusie jambo hili. Washukuru wote kwa ujumla kwa ‘usikivu mkubwa’ waliokuwa nao. Kumbuka – aga jukwaa na uso uleule ulioingia nao, wa kujiamini na kuwathamini wasikilizaji.
Tano, chukua na panga vifaa vyako kwa uangalifu (karatasi, kalamu, magazeti, matini, simu, kompyuta, nk), na teremka jukwaani huku umejiamini. ‘Usikumbe’ kila ulichokuwa nacho katika rundo, na kuondoka kama umebeba taka. Tena, wakati wa kuondoka, usioneshe dalili zozote za ‘kutoroka’ ama ‘kukimbia’. Haya tumewahi kuyaona kwa wawasilishaji fulani, ambao kuondoka kwao jukwaani kuliashiria kwamba walikuwa wanasubiri kundoka katika mateso waliyokuwa wanapitia. Kule kujiamini ulikokuwa nako wakati unakabili jukwaa (self-credibility), kuwe kulekule wakati wa kushuka toka kwenye jukwaa.
Sita, kumbuka semina au kongamano linaendelea, hata baada ya wasilisho lako. Wakati unaelekea kwenye sehemu ya kuketi, kwepa kumpa kila mtu mkono kwa nia ya kupongezana. Hayo yafanyike nje ya ukumbi baada ya shughuli rasmi kumalizika. Ikiwa hadhira iliamua kukupigia makofi ulipomaliza wasilisho lako, inatosha; teremka toka jukwaani, tembea kwa kujiamini, nenda kakae. Ikiwa unahitaji kwenda maliwato, usitoke kwenye jukwaa na kupitiliza. Nenda kwanza kwenye sehemu yako, kaa kwa muda, halafu simama tena.
Wiki ijayo tutaona kanuni za kuandaa na kutumia zana (presentation aids). Tumsifu Yesu Kristu!
Itaendelea wiki ijayo.

Waamini wa Parokia ya Mtakatifu Ambrose, IPTL Salasala, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, wakibadilishana mawazo baada ya Adhimisho la Misa Takatifu iliyoadhimishwa parokiani hapo.

Viongozi wa Kamati Tendaji ya Parokia ya Mtakatifu Yohane Mtume na Mwinjili, Tegeta Kibaoni, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, na waamini wakiwa katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Dominika ya Kwanza ya Kwaresma, iliyoadhimishwa parokiani hapo.

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi, na Mapadri wakiwa katika picha ya pamoja na Watoto wa Shirika la Kipapa la Utoto Mtakatifu wa Parokia ya Mtakatifu Josephina Bakhita, Mtoni-Mtongani, baada ya Adhimisho la Misa Takatifu ya Dominika ya Kwanza ya Kwaresma iliyokwenda sanjari na utoaji wa Sakramenti Takatifu ya Kipaimara.

Wanachama wa Moyo Mtakatifu wa Yesu kutoka Parokia mbalimbali za Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, wakisali kumshukuru Mungu baada ya Mkutano wao Mkuu wa Jimbo uliofanyika katika Ukumbi wa Kristo Mfalme, Parokia ya Kristo Mfalme, Tabata, jimboni humo.

Paroko wa Parokia ya Bikira Maria Malkia wa Amani, Chamugasa - Busega, Jimbo Katoliki la Shinyanga, Padri Dustan Sitta, akibariki vipaji wakati wa Adhimisho ya Misa Takatifu ya Dominika ya Kwanza ya Kwaresma iliyoadhimishwa katika Parokia ya Mtakatifu Yohane Mtume na Mwinjili, Tegeta Kibaoni, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.