Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

Na Mathayo Kijazi

Imeelezwa kuwa Wachungaji wema ni wale wenye kutenga muda wao kwa ajili ya kuwafahamu kondoo wao kwa majina, ili wasisambaratike.
Hayo yalisemwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi, wakati akihubiri katika Adhimisho la Misa Takatifu ya kutoa Daraja Takatifu la Upadri kwa Mashemasi saba wa OSA, katika Parokia ya Mtakatifu Ambrosi – Tagaste, jimboni humo.
Aliwataka Mapadri hao wapya kutambua kwamba wanatakiwa kujitosa bila kujibakiza, kwani ndiyo sifa ya uchungaji mwema, kuwakusanya kondoo wanaowachunga.
“Sifa ya uchungaji mwema ni kujitosa bila kujibakiza. Wachungaji wema ni wale wenye kuwafahamu kondoo wao, tena kwa majina, ili wasisambaratike. Mumwombe Mungu awape nguvu ya kuifanya kazi yake ili muwe vyombo vya neema yake,” alisema Askofu Mkuu Ruwa’ichi.
Askofu Mkuu Ruwa’ichi alisema kuwa kila mbatizwa alizawadiwa wito wa kumtambua na kumfuata Kristo, akiwasisitizia Wakristo kuitambua fursa hiyo.
Aliwasihi Wakristo kuthubutu kumkimbilia Mungu, kwani kwa kufanya hivyo, watapata faraja na kusamehewa dhambi zao.
Askofu Mkuu Ruwa’ichi alisema kuwa Mungu ndiye chimbuko la kila jema, na pia ndiye anayetoa kila wito ulio sahihi katika maisha ya mwanadamu.
“Ndugu zangu, Mungu ndiye chimbuko la kila jema, na pia ndiye anayetoa kila wito ulio sahihi. Wapo baadhi ya watu wanaolala na kuamka, kisha kujitangaza kuwa wana wito. Mtu anaamka asubuhi anamwambia mke wake kwamba ‘usiku nimeoteshwa’. Huo siyo wito ulio sahihi, kwani wito ulio sahihi hutoka kwa Mungu Mwenyezi,” Askofu Mkuu.
Askofu Mkuu Ruwa’ichi aliongeza kuwa Mungu ni mwenye huruma, ndiyo maana licha ya mapungufu ya wanadamu juu ya dhambi zao, yeye huwahurumia.
Aliwasisitiza Mashamasi hao kuwa wakawe Mapadri wenye kujituma bila kulaza damu, bali watumie kila muda wao kwa ajili ya kuwahudumia watu wa Mungu.
Aidha, aliwataka pia Wakristo kutambua kwamba Yesu Kristo hashabikii dhambi, bali humwokoa mdhambi na kumzawadia wokovu maishani mwake.
Wakati huo huo, Askofu Mkuu Ruwa’ichi alisema kuwa kama Kanisa, wanamshukuru Mungu kwa kupata Mapadri wapya watakaosaidiana nao kufanya utume kwa ajili ya kuwatakatifuza watu wa Mungu.
Kwa upande wake Padri Laurent Temanya- OSA, mmoja wa waliopokea Daraja hilo Takatifu, alisema kwamba wao kama Mapadri, wanamshukuru Mungu kwa zawadi ya maisha ya Upadri.
Alimshukuru Askofu Mkuu Ruwa’ichi kwa kuongoza Adhimisho hilo, huku wakiwashukuru wazazi wao kwa kuwaleta duniani pamoja na kuwaruhusu kuuitikia wito huo.
Waliwashukuru walezi wao katika maeneo yote waliyopita kwa mchango mkubwa katika safari yao hiyo, huku wakiwashukuru pia wote waliowaombea, na kusema kwamba bado wanahitaji sala zao.
Aliwaasa wazazi kuendelea kuziombea familia zao, hasa zenye watoto wanaowiwa kuufuata wito, ili katika shamba la Bwana, watendakazi wawe wengi.

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Kanisa la Parokia ya Kibamba, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, limetabarukiwa, huku Waamini wakionywa kutotumia vibaya kanisa hilo, kwani linapotabarukiwa, linawekwa maalumu kwa ajili ya Mungu na mambo Matakatifu.
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi, alisema hayo wakati akihubiri katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Kutabaruku Kanisa la Parokia ya Mtakatifu Vincent wa Paulo – Kibamba, jimboni humo.
“Kanisa linatabarukiwa ili liwe tu kwa ajili ya Mungu na watu wake, pamoja na mambo yote matakatifu. Hapa si mahali pa disko, disko pelekeni ukumbini. Msipafanye hapa kuwa jalala,” alisema Askofu Ruwa’ichi.
Askofu Ruwa’ichi alisisitiza kuwa kanisani si mahali pa kupumzishia mifugo, ikiwemo mbuzi wala kondoo, kwani likifanywa hivyo, hilo litakuwa jalala, badala ya kanisa.
Aliwapongeza waamini wa Parokia ya Mtakatifu Vincent wa Paulo – Kibamba, kwa moyo wa majitoleo waliouonyesha, hadi kukamilisha ujenzi wa kanisa hilo.
“Wapendwa familia ya Mungu katika Parokia ya Kibamba, nianze kwa kuwapongeza kwa kazi nzuri na nzito mliyoifanya kwa kipindi cha miaika kumi. Kwa mshikamano wenu, imani yenu, mmemjengea Mungu kanisa zuri,” alisema Askofu Mkuu.
Aidha, Askofu Mkuu aliwakumbusha Wakristo kufahamu kwamba yeyote aliyebatizwa anatakiwa kutojiruhusu kuwa jalala, bali afahamu kwamba yeye ni ndugu yake Kristo.
Askofu Mkuu Ruwa’ichi aliwaasa waamini kutambua kwamba biashara yoyote yenye sura ya dhambi, Yesu Kristo haitaki, wala haiungi mkono biashara hiyo.
Katika hatua nyingine, Askofu Mkuu Ruwa’ichi aliwataka Waamini wa Parokia hiyo kutobadilisha mwonekano wa kanisa hilo, kwani tayari limeshatabarukiwa.
“Kwa hiyo, ninyi sitegemei kwamba mwakani mtapenda kuja kurefusha upande huu na upande ule, au mtakuja kulibadilisha liwe tena la shughuli tofauti. Hili litakuwa ni mahali pa sala, mahali pa ibada, mahali penu pa kumtukuza Mungu kwa miaka yote. Hivyo, tunalipa hati ya kutabarukiwa,” alisema Askofu Mkuu Ruwa’ichi.
Kwa upande wake Paroko wa Parokia hiyo, Padri Prijo Joseph alimshukuru Mungu kwa kuwawezesha na kuwapa nguvu katika kipindi chote, hadi kukamilisha ujenzi wa kanisa hilo.
Aidha, Padri Prijo alimshukuru Askofu Mkuu Ruwa’ichi kwa mawazo na ushauri aliowapatia hadi kuweza kukamilisha ujenzi wa kanisa hilo lililotabarukiwa.
Vile vile, Paroko aliwapongeza Wanaparokia hiyo kwa ushirikiano mkubwa waliouonyesha, kwani walikuwa bega kwa bega katika kipindi chote cha ujenzi huo wa kanisa.
Naye Padri Augustine Paikkatt, Mkuu wa Shirika la MC BS (Superior General MC BS), alisema kuwa anafurahi sana kushiriki katika Adhimisho hilo la Misa Takatifu ya Kutabaruku Kanisa.
Padri Augustine aliwapongeza waamini wa Parokia ya Kibamba, kwa michango na majitoleo yao hadi kukamilisha ujenzi wa kanisa hilo.

Mtwara

Na Mwandishi wetu

Paroko wa Parokia ya Yesu Kristo Mkombozi - Magomeni, Jimbo Katoliki la Mtwara, Padri Silvanus Chikuyu, amesema kuwa mtu yeyote anapouona Msalaba, anatakiwa asipite bila kutafakari upendo wa Yesu Kristo kwa wanadamu.
Padri Chikuyu alisema hayo wakati akitoa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Sikukuu ya Somo wa Kutukuka kwa Msalaba, Kigango cha Lyenje, Parokia ya Bikira Maria Mpalizwa Mbinguni – Luagala, Jimbo Katoliki la Mtwara.
“Na naomba kila mmoja anapouona Msalaba, asiishie tu kuuona na kupita zate, bali atafakari. Katika msalaba tuone mambo mawili makuu, kwanza kabisa tuone upendo wa Mungu kwetu sisi wanadamu….hakuna upendo ulio mkuu kama wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya wengine.
“Yesu Kristo ametupenda, akatoa uhai wake kwa ajili yetu sisi, ili sisi tuwe nao tele. Hilo ni jambo kubwa sana, usiupite tu Msalaba hivi hivi bila kutafakari upendo wa Mungu kwa wanadamu wote. Jambo la pili ni utii na unyenyekevu wa Yesu Kristo, ambaye alikubali kuachilia hali yake ya Kimungu, akajinyenyekesha akatwaa hali yetu ya kibinadamu,” alisema Padri Chikuyu ambaye pia alikuwa mgeni rasmi.
Aidha, Padri Chikuyu aliongeza kuwa ni haki kwa kila Mkristo kuwa na msalaba nyumbani kwake, kwani kwa kufanya hivyo, milango ya baraka na mafanikio itapatikana katika maisha yao.
Padri huyo alisema kuwa wapo baadhi ya Wakristo ambao wanaishi na wenza wao katika familia, lakini wamekuwa wagumu kufunga ndoa, akisema kuwa ni vyema wakawa na misalaba majumbani mwao, ili baraka ziwafikie, na waweze kufunga ndoa.
Kwa upande wake Paroko wa Parokia ya Bikira Maria Mpalizwa Mbinguni – Luagala, jimboni humo, Padri Andrew Chitanda alisema kuwa amefurahi kuona maadhimisho hayo yamekwenda vizuri.
“Maadhimisho haya yatie hamasa kwa ndugu wengine wote kutoka Parokia zote, Wakristo kutoka Vigango mbalimbali, kutoka Jumuiya mbaimbali, ili waweze kuthamini na kuadhimisha siku maalumu za Somo wa Kigango, au wa Parokia. Kwa hiyo, nawahisi Vigango vingine waweze kuiga mfano huu,” alisema Padri Chitanda.
Kwa Upande wake, Sista Elvira Lilungulu wa Shirika la Masista wa Mkombozi, Jimbo Katoliki la Mtwara, aliwaomba wazazi kuwaruhusu watoto wao wa kike na wa kiume wajiunge katika Mashirika mbalimbali ya Kitawa ili wamtumikie Mungu, kwani Mungu ndiye anayewaita kwa ajili ya kumjua na kumtumikia.
Naye Mwenyekiti wa Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) wa Kigango cha Kutukuka kwa Msalaba - Lyenje, Regina Mtanda, aliwaasa akinamama kuwalea watoto katika maadili mema ili wale wenye wito waweze kuikimbilia miito hiyo.

LIRA, Uganda

Uamuzi wa kujenga Parokia nyingi katika Jimbo la Lira nchini Uganda, umetajwa kuleta msisimko na shangwe miongoni mwa Wakristo ndani na nje ya nchi hiyo.
Wazo la kufungua Parokia zaidi chini ya uongozi wa Askofu Sanctus Lino Wanok wa jimbo hilo, unalenga kuleta Sakramenti karibu na watu wa Mungu katika maeneo yao.
Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, Parokia nyingine tano zilijengwa kwenye jimbo hilo.
Parokia hizo ni Parokia ya Mtakatifu Francis wa Assisi ya Abuli katika Wilaya ya Kwania; St. Peter Clever Ober katika mji wa Lira; St. Mary’s Catholic Parish, Loro, katika wilaya ya Oyam; St. Luke Mwinjilisti, Parokia ya Kikatoliki Aputi, katika wilaya ya Amolatar; na Parokia ya Mama Yetu wa Rozari Takatifu, ya Anyeke.
Kabla ya kujengwa kwa parokia hizo, Parokia zingine mbili za Mtakatifu Joseph Agweng, na Mama Yetu Malkia wa Amani katika Wilaya za Lira na Otuke, zilijengwa rasmi mwaka 2018.
Maendeleo haya yanaleta jumla ya parokia 27 za Jimbo laLira, na ndogo zaidi, yaani Parokia zinazolelewa na kuwa parokia siku zijazo.
Ndani ya jiji la Lira pekee, Parokia tatu Ndogo za St. Peter Anai; St. Leo the Great Boroboro; na St. Philip Neri Erute; mtawalia, zinatayarishwa kuwa Parokia katika siku zijazo.
Parokia nyingine Ndogo ni; Parokia ya Adyeda All Saints, itajengwa nje ya Parokia ya Bala Katoliki; Parokia Ndogo ya Gomi; Parokia ya Onek Gwok-Ngai; Parokia Ndogo ya Abakuli huko Dokolo; Parokia Ndogo ya Etam huko Amolatar; na Parokia ya Mtakatifu Francis wa Assisi, Ayago, inajengwa nje ya Alenga Katoliki.
Kujenga Parokia Ndogo kama hizo hapo juu kumezua shangwe na msisimko zaidi miongoni mwa Wakristo katika Dayosisi ya Lira.
Hivi majuzi katika Parokia Ndogo ya Assisi, Ayago, katika wilaya ya Apac, jumuiya ya Kikristo haikuweza kuficha furaha yao katika hafla ya mapokezi rasmi ya kasisi wao, Mchungaji Denis Okello Odyek, Msimamizi mpya wa Parokia Ndogo ya Ayago, akisaidiwa na Mchungaji Deacon Moses Opio.
Tarehe 2 Septemba 2023 katika ufunguzi rasmi wa Parokia Ndogo ya Ayago, Wakristo waliwajumuisha viongozi wa mitaa, kiraia na kisiasa, na viongozi wa kitamaduni walitoa shukrani zao kwa Askofu wa Jimbo la Lira kwa uongozi wake wa maono unaowezesha kujengwa kwa Parokia nyingi. ili kuwezesha ustawi wa kiroho wa watu wa Mungu.
Jovino Akaki Ayumu, Waziri wa zamani wa Jimbo la Utalii kwa Wanyamapori na Mambo ya Kale ni makamu mwenyekiti Baraza la wachungaji la parokia hiyo, Ayago alifichua kuwa kama Wakristo wamepokea wachungaji kwa furaha na kuahidi kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuendelea na kuendeleza Parokia hiyo.
Kutoka mji wa Lira hadi Parokia Ndogo ya Ayago katika mwelekeo wa Kusini-Magharibi kupitia Manispaa ya Apac, inachukua takriban muda wa saa mbili, ikiwa na umbali wa kilometa 91, kuwa na makanisa 35 yaliyoenea ndani ya Kanda Saba chini ya Parokia Ndogo ya Ayago.

LIRA, Uganda
Askofu wa Jimbo Katoliki la Lira Kaskazini mwa Uganda, Mhashamu Sanctus Lino Wanok, ameonya dhidi ya unywaji pombe kupita kiasi unaofanywa na Makatekista na maajenti wengine wa wachungaji.
Akizungumza katika hafla ya uzionduzi wa Parokia ya Kanisa Katoliki ya Mama Yetu wa Rozari Takatifu, Anyeke wilayani Oyam, Askofu Wanok alibainisha kuwa unywaji wa pombe kupita kiasi unasababisha madhara kwa huduma ya kichungaji katika Kanisa hilo.

VATICAN CITY, Vatican

Baba Mtakatifu Fransisko amesema kwamba wakimbizi na wahamiaji wanapaswa kuombewa na kupewa hifadhi wanapoomba hifadhi.
Kauli hiyo ya Baba Mtakatifu imo katika tafakari yake kwa waamini waliofurika kwenye Uwanja wa Mtakatifu Petro, wakati Baba Mtakatifu akikumbushia Siku ya Wahamiaji na Wakimbizi, mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana.
Alisema kwamba kuna umuhimu wa kuwa na uhuru wa kukaa au kuondoka katika nchi, pamoja na ule wa kukaribishwa popote mtu anapokwenda.
Baba Mtakatifu akiwageukia waamini na mahujaji kutoka pande zote za Dunia waliounganika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro akisema, “Leo (Jumalipi ya Septemba 24) ni Siku ya Wahamiaji na Wakimbizi Duniani, yenye kaulimbiu: ‘Huru kuchagua kuhama au kubaki,’ ili kukumbusha kwamba kuhama kunapaswa kuwa chaguo huru, na kamwe, si jambo pekee lisilowezekana.
Alisema kuwa haki ya kuhama sasa imekuwa wajibu kwa wengi, na hasa mahali ambapo panapaswa kuwepo haki ya kutohama, ni kubaki katika nchi ya mtu mwenyewe.
Baba Mtakatifu alisema kuwa ni lazima kwa kila mwanaume na mwanamke kuhakikishiwa haki ya kuishi maisha yenye heshima katika jamii anamojikuta.
Aliongeza kusema kuwa kwa bahati mbaya, umaskini, vita na mgogoro wa tabianchi, huwalazimisha watu wengi kukimbia nchi zao.
“Sote tunatakiwa kuunda jumuiya ambazo ziko tayari na wazi kukaribisha, kukuza, kusindikiza na kuunganisha wale wanaobisha hodi kwenye milango yetu,” alisema Baba Mtakatifu Fransisko.
Baba Mtakatifu aliikumbuka ziara iliyompeleka Kusini mwa Ufaransa ambapo alisema, “Changamoto hii ilikuwa katikati ya Rencontres Méditerranéennes, yaani Mikutano ya Mediteranea ambayo ilifanyika katika siku za hivi karibuni huko Marsiglia, na katika kikao chake cha kuhitimisha, nilishiriki jana, nikisafiri hadi jiji, njia panda ya watu na tamaduni.”

Marsiglia, Ufaransa

Kikundi cha Wananchi walio katika hali ngumu ya maisha wenye kupokea msaada kutoka kwa Watawa wa Shirika la Masista wa Mama Teresa wa Kalkuta, wamepata faraja baada ya kutembelewa na Baba Mtakatifu.
Akiwa huko Marsiglia, Baba Mtakatifu alitembelea kwa faragha Nyumba ya Masista wa Mama Teresa wa Kalkuta huko Mtakatifu Mauront, ambako kikundi cha watu walio katika hali ngumu ya kiuchumi, wanasaidiwa na watawa hao.
Katika ushuhuda wake Sista Crosvita alibainisha kuwa kwa kila mtu wanayemwona, ni kama Kristo.
Akizungumza na wanakikundi hao, Baba Mtakatifu alisema kuwa kuishi kama ndugu ni unabii.
Akiwa mjini Marsiglia, Baba Mtakatifu alifanya mkutano wa faragha na baadhi ya watu walio katika hali ngumu ya kiuchumi uliofanyika katika Nyumba ya Wamisionari wa Upendo, watawa wa Mama Teresa wa Calkutta, huko Mtakatifu Mauront, moja ya vitongoji kati ya watu maskini zaidi nchini Ufaransa.
“Asante kwa makaribisho yenu, kwani sisi sote ni ndugu, hii ni muhimu, mara nyingi ustaarabu wetu unatuongoza kuishi kama maadui au wageni… ishara ya kinabii ni kuishi kama ndugu na huu ni unabii, ule wa udugu unaokwenda zaidi wa mawazo ya kisiasa na kidini,” alisema Baba Mtakatifu Fransisko.
Kwa upande wa Sista Crosvita, alimmsimulia  Baba Mtakatifu kwa hisia kali kwamba, kwani kwa miaka miwili akiwa mjini Marsiglia yeye na Masista wenzake, wamekuwa wakiendesha jiko la kupika supu kwa ajili ya maskini, ambalo linakaribisha watu 50 kwa wakati mmoja, mara tatu hadi nne kwa siku, kuanzia saa 3. 30 hadi 5.30, na katika siku moja inaweza kuwafikia watu 250.
Alisema kuwa watu hao ni maskini zaidi wengine wanaishi mitaani, ambao hivi karibuni kundi la watu wamefika kutoka Sudan, hawana pa kukaa, wanalala mitaani, na wengine hawana chakula.

DAR ES SALAAM

Na Dkt. Felician Kilahama

Ni vema na haki kumshukuru Mungu Mwenyezi kwa kutuwezesha kuendelea kuishi, tukipumua bila ya athari zozote. Hayo ni mapenzi yake, siyo kwa ridhaa au nguvu zetu wenyewe, bali ni kwa rehema zake kuu, hivyo, jina lake lihimidiwe.
Katika sehemu ya kwanza, Makala iliishia kwenye kipengele kilichozungumzia kuhusu vijana kupenda kupata fedha kirahisi, mfano, kupitia masuala ya ‘kubeti’.
Hatinaye, kueleza ‘ipo michezo mingine mingi inayochezwa kupitia mitandao na vyombo mbalimbali vinavyohimiza Watanzania kucheza ili kujipatia fedha kirahisi.’ Haya yote yanafanyika kwa mwelekeo wa kamari (gambling au gaming), na vijana wengi wamevutwa.
Kimsingi, masuala yanayohusiana na kucheza kamari siyo mazuri, maana yanapelekea mhusika kupotoka na kujikuta akitenda maovu. Kwanza, kuna kutekwa kifikra/kiakili na kupoteza maarifa ya kufanya uamuzi sahihi.
Kila wakati mhusika anabaki akijiweka kwenye nafasi ya kushinda, huku akitumia fedha ambazo harudishiwi iwapo hatashinda. Pili, michezo ya aina hiyo inajenga lango la kutenda uovu, ikiwemo wizi na, au udanganyifu.
Mhusika iwapo hana fedha za kumfanya acheze, atafanya kila linalowezekana apate fedha kihalali au vinginevyo, ili mradi afanikishe lengo.
Kihalali anaweza akauza vitu vyake, mfano, nguo, viatu, simu kiganjani au akahangaika akapata kibarua na kupata fedha akacheze kwa mtazamo kuwa atashinda na kupata fedha atajirike.
Vinginevyo, kuna uwezekano mkubwa wa kujenga tabia ya kudokoa mali za wengine, au kuiba fedha na vitu vingine nyumbani, mitaani na hata kupora, ili mradi afanikishe lengo lake.
Kwa bahati mbaya, mtazamo huu usiofaa kwa vijana ambao ndiyo nguvukazi kubwa ya taifa letu, unachochewa na baadhi ya matangazo yanayofanyika kupitia vyombo mbalimbali vya matangazo.
Mathalani, luninga, redio, magazeti na hata simu janja au za kawaida, kwamba kuna wakati ninapofungua sehemu ya ujumbe kwenye simu; mara kwa mara huwa nakuta ujumbe kutoka namba fulani wakitangaza, ‘wewe umekaribia kushinda kiasi fulani cha fedha, mathalani, milioni mbili, tuma neno fulani ushinde.’
Kadhalika, unaambiwa ‘weka Tshs 500 ujipatie hadi Tshs milioni tatu na bonasi ya Tshs 200,000 papo hapo,’ au ‘wewe ni milionea mpya, chagua namba 1 hadi 6 uweze kushinda hadi milioni mbili na ‘Jackpot’ ya Tshs 300,000 kila siku.’ Vile vile maneno “funua pesa mkwanja tele maisha mapya …”
Wakati mwingine unakuta kwenye gazeti, kumewekwa, mathalani, “Supa Jackpot” (TZS 1,150,172,000 kwa TZS 1,000 tu). Kijana akiangalia tarakimu hizo na kwa lugha ya mitaani: kwa buku tu, anahamasika kucheza. Lakini ili aweze kushinda na kupata hizo fedha, atacheza mara ngapi? Yote haya ni katika kukengeuza akili za wengi na hasa vijana ambao ndiyo kundi kubwa linaloathirika zaidi.
Wakati mwingine yanaletwa maswali kadha wa kadha, na mengi ni ya kimichezo, hasa soka na, au kuigiza. Pia, nyimbo hasa ‘bongo fleva’ na waimbaji wake. Nia ni watu wengi wajibu ili wakwapue hela kutoka kwenye bando kupitia mitandao husika. Katika uhalisia wa michezo kama hiyo, wengi wanaangamia, na wataangamia kwa kukosa maarifa.
Kimsingi, michezo (gaming/gambling) ni aina ya kamari hata kama tukisema imeboreshwa, lakini ni pata potea. Inafanya wengi wapoteze fedha zao kwa matumaini ya kupata/kushinda, wakati wanaoshinda ni wachache sana kulingana na idadi ya wanaocheza.
Kabla mhusika hajacheza mchezo wowote wa kubahatisha, ni lazima kujua asilimia ya kushinda, au uwezekano wa kushinda (probability rating); na hilo ni jambo la msingi, mathalani, kuna wachezaji milioni moja kwa mchezo mmoja, na pengine anatakiwa apatikane mshindi mmoja, washindi kumi, au washindi mia moja. Kinachotakiwa kukifahamu ni kujua kwa kiasi gani unaweza kushinda.
Kwa kundi la kwanza zitatolewa milioni moja; kundi la pili milioni kumi (washindi 10) na kundi la tatu milioni miamoja (washindi 100). Kiwango cha ushindi ni asilimia 0.0001; 001 na 0.01 kwa makundi hayo matatu mtawalia. Hali hiyo inaonyesha kuwa ni asilimia ndogo sana ya mhusika kuweza kuibuka mshindi, ndiyo maana ikaitwa ‘bahati nasibu’.
Kadhalika, baadhi ya vijana hutembeza barabarani baadhi ya bidhaa mbalimbali mikononi wakitafuta wateja.
Wengine wanatumia muda mrefu kutoka eneo moja kwenda jingine wakitafuta wanunuzi.
Jioni inapoingia, mhusika anapoona hana kitu mfukoni na njaa inamuuma, analazimika auze kwa bei mnunuzi anayotaka, ili mradi apate kiasi cha kumsaidia aweze kujikimu. Baadhi wana familia hivyo hujikuta katika changamoto hatarishi kiasi cha kulazimika kutenda uovu kwa kigezo cha hakuna jinsi, bora nusu shari, kuliko shari kamili, anaitelekeza familia yake.
Tujiulize kwa mustabali wa taifa letu, je, vijana kutaka kupata fedha haraka haraka kupitia michezo mbalimbali ya kifedha kama ‘kubeti’ na mingineyo, kitaifa ni jambo jema? Je, vijana na watu wengine tunatumia muda vizuri kwa manufaa yetu, familia na taifa kwa ujumla?
Kimsingi, matumizi halisi ya ‘muda’ kwa nyakati hizi ni suala la kuwekewa mkazo. Kila siku tunapoamka tunafanya nini? Maana unakuta makundi ya watu wa rika mbalimbali wakiongelea masuala ya michezo, mfano, kusajili wachezaji, hususani timu za Tanzania na za Uingereza.
Kadhalika, unaona vijana wanatumia muda mwingi kwenye mitandao ya kijamii ‘wakichati’ kupitia simu za kiganjani. Je, ni matumizi halisi ya muda? Siku ina saa 24 na wiki ina siku saba au saa 168.
Kawaida binadamu anatakiwa kulala usingizi (angalau saa 8 kwa siku), kwa wiki atatumia saa 56 kitandani. Kwa wiki, ukiondoa siku moja ya kuabudu/kusali, kuna siku sita za kufanya kazi. Hii inamaanisha kuwa tukiondoa saa za kusinzia, kwa siku tuna saa 16 za kufanya kazi, na ndani ya siku sita, ni takribani saa 96 za kufanya kazi.
Muda huu ukitumiwa kwa kiwango cha kufikia asilimia 75 (takriban saa 12 kwa siku, sawa na saa 72 kwa wiki), ukatumika kuzalisha mali na huduma ili kujipatia kipato, hakika tutajikwamua kimaendeleo (muda uliobaki, takriban saa 4 kwa siku au saa 24 kwa siku sita za kazi; ukatumika kwenda na kutoka mahali pa kazi, pengine kupata mapumziko mafupi wakati mhusika akiwa kazini).
Uzoefu unaonyesha kuwa wengi wetu, wakiwemo vijana, hatuzingatii matumizi mazuri ya muda, iwe ofisini, viwandani au kwingineko, kwani bado kuna kusuasua bila maelezo toshelezi. Hivyo, vijana tujiepushe kufuata mkumbo kwa masuala yasiyotuletea maendeleo ya kweli kimaisha.
Serikali iweke Sera thabiti kuinua maisha ya Watanzania hususan vijana. Tuliporuhusu matumizi ya ‘bodaboda’ na ‘bajaji’ kutoa huduma za usafiri na usafirishaji, jambo hilo limekuwa faraja kwa vijana wengi kujiajiri au kuajiriwa. Wanaoitumia fursa hiyo kwa umakini baada ya miaka miwili au mitatu, wanasonga mbele ipasavyo.
Mkakati wa Serikali wa kuinua zaidi shughuli za kilimo kwa lengo la kuwapatia vijana ajira na kuimarisha au kuendeleza uchumi wa taifa, upewe msukumo zaidi ili kuhusisha sekta mbalimbali za umma na binafsi. Kupanuliwe wigo ili vijana wengi waweze kujipanga vizuri kulingana na uwezo waliopewa na Mwenyezi Mungu.
Wenye ari ya kufuga wafanye hivyo kitaaluma na kibiashara; wenye kumudu masuala ya uvuvi, misitu na nyuki na utalii, pamoja na biashara, wafanye hivyo bila shida. Shughuli za ugani ziimarishwe ili kuhakikisha mafanikio tarajiwa yanapatikana.
Tukiongeza tija kwa bidhaa nyingi kuzalishwa hapa nchini, tutajenga uwezo wetu wa kujitegemea. Wakati huo huo, tutasaidia idadi kubwa ya vijana kuachana na ‘michezo potofu’, hivyo kuimarisha ‘nguvukazi’ ya taifa letu kwa faida ya wengi.
Halmashauri zote nchini na Mamlaka za Mikoa na Wilaya, zihakikishe kuna mazingira mazuri ya kuwezesha vijana kutumia rasilimali ardhi kwa faida na weledi mkubwa, mathalani, Halmashauri zianzishe mifumo thabiti ya kuunganisha ‘nguvukazi-vijana’ kwenye maeneo yao.
Kuweka fursa za ‘mitaji’ kuwakopesha vijana; tukizingatia masharti nafuu na kuweka ‘kanzidata’ kuhusu vijana kuhusiana na taaluma au uwezo wao.
Katika kuyatekeleza hayo, uwazi na uadilifu vizingatiwe ipasavyo. Vijana wajengewe mazingira ya kuwa waaminifu katika kutumia muda vizuri na kutimiza wajibu wao ipasavyo. Viongozi na wenye madaraka kwa ngazi zote, tuwe waadilifu, siyo kwa maneno tu, bali kimatendo.
Tuchukie ‘udanganyifu, wizi, kutoa au kupokea rushwa, au kukwapua’ mali za umma. Hayo yawe mwiko mkubwa katika sifa za kiongozi mzuri anayetumainiwa na wengi.
Tamaa za kujitajirisha ‘chapuchapu’ (yaani haraka haraka) kwa kutumia njia haramu na zisizofaa, vikomeshwe, na watakobainika wachukuliwe hatua kali za kiutawala na kisheria. Tafakari kwa kina, chukua hatua madhubuti.

Wiki iliyopita tuliwaletea kazi alizozifanya Papa Yohana XXIII katika kipindi kifupi cha uongozi wake. Leo tunawaletea historia ya uongozi wa Mrithi wake Papa Paulo VI na kuendeleza yale ya mtangulizi wake. Sasa endelea

Papa Yohana XXIII (1958 - 1963: wa 261) alipofariki Juni 3 1963, mambo yote ya Mtaguso yalisitishwa kumsubiri Papa mpya ambaye angeliamua kama Mtaguso uendelee au uishie hapo. Tarehe 21 Juni 1963 alichaguliwa Kardinali Yohana Baptista Montini, Askofu Mkuu wa Milano.

Montini alikuwa mmoja wa Makardinali wenye msimamo wa kati. Siku moja baada ya kuchaguliwa, alitangaza kwamba Mtaguso utaendelea na kwamba atajaribu kutimiza malengo yaliyowekwa na Papa Yohana XXIII. Alisisitiza kuwa  Mtaguso ndio utakuwa kipaumbele chake cha kwanza.

Kardinali Montini alizaliwa tarehe 26 Septemba 1897 huko Concesio Italia. Alipadrishwa mwaka 1920 na kutumwa Roma kwa masomo, ambako baadaye aliingizwa katika Idara ya Mambo ya Nje na kutumwa Ubalozini Warsaw, Poland, mwaka 1923 na baadaye kurudi ofisini katika idara hiyo Roma.

Mwaka 1954 Papa Pius XII (1939 - 1958: wa 260) alimteua Montini kuwa Askofu Mkuu wa Milano, na Papa Yohana XXIII akamfanya Kardinali mwaka 1958. Tarehe 21 Juni 1963, akachaguliwa kuwa Papa na kuchukua jina la Paulo VI.

Papa Paulo VI (1963 - 1978: wa 262) aliamini katika muendelezo wa mapokeo ya Kanisa bila kuyachakachua, lakini pia aliamini mapokeo yasiyokuwa ya msingi na yanayokinzana na alama za nyakati yanapaswa kuhuishwa na kufanywa upya.

Mara moja aliimarisha Tume alizoziweka Papa Yohana XXIII na kuongezea sura mpya. Kati ya Wenyeviti wa Mikutano, jumla aliweka mchanganyiko wa wanamapinduzi kama Kardinali Suenens wa Ubelgiji, Kardinali Doepfner wa Ujerumani, na Kardinali Lercaro wa Bologna, Italia, na wale wenye msimamo wa wastani kama Kardinali Agagianian. Makardinali hawa wanne ndio walikuwa mpini wa mwenendo wa Mtaguso.
 
Papa Paulo VI aliwaalika Walei kuhudhuria vikao vya jumla bila kusema au kipiga kura. Aliruhusu vile vile habari za mwenendo wa Mtaguso kutolewa mara kwa mara kwa Waandishi wa Habari.

Kikao cha Pili, Septemba 29 hadi Desemba 4, 1963:
Papa Paulo VI aliitisha kikao cha pili kuanzia tarehe 29 Septemba hadi Desemba 4 mwaka 1963. Katika ufunguzi wa kikao hicho, alirudia nia yake ya kufuata nyayo za mtangulizi wake. Wakati wa ufunguzi, alitoa madhumuni manne ya msingi kwa Mtaguso huo:

1.    Kanisa lijitambulishe kwa Ulimwengu kwa tamko rasmi, likijielezea kwa kujielewa.

2.    Aggiornamento, yaani kufanya upya, lazima iendelee, si kwa kuvunja mila na mapokeo msingi, bali kwa kuondoa kile ambacho kina kasoro.

3.    Kanisa lazima lifanye kazi kuelekea kwa umoja kati ya Wakristo wote. Wakati wa ufunguzi akisema hivyo, aliwageukia waangalizi wasio Wakatoliki na kuomba msamaha kwa jeraha lolote ambalo Kanisa Katoliki lingekuwa limewasababishia Wakristo wengine.

4.    Kanisa lazima lijihusishe na mazungumzo na Ulimwengu: “siyo kushinda na kuuteka, bali kutumikia, si kudharau bali kuthamini, si kuhukumu bali kufariji na kuokoa”.

Kikao cha Tatu, Septemba 14 hadi 21 Novemba 1964:
Katika kikao cha tatu, kutokana na manung’uniko ya Kardinali Suenens kwamba kulikosekana Wanawake Walei Waangalizi kwa sababu kulikuwepo Masista tu, Papa aliwateua Wanawake 15 Walei Waangalizi kuungana na Masista 10.
 
Kipya kingine katika ufunguzi wa kikao hicho, Papa aliadhimisha Misa na Maaskofu 24 kutoka nchi 19. Hii ilikuwa mara ya kwanza katika Kanisa la Kirumi, kwa sababu kabla ya hapo kila Padre aliadhimisha peke yake. Mapinduzi ambayo sasa ni jambo la kawaida yalikuwa yameanza.

Kikao cha Nne, Septemba 14 hadi Desema 8, 1965:
Kikao cha nne na cha mwisho kilikuwa tarehe 14 Septemba hadi 8 Desemba mwaka 1965. Kikao hiki kilikuwa kirefu zaidi ya kingine chochote kilichotangulia  kwa wiki mbili, kwani hiki kilikuwa cha wiki 12.

Katika ufunguzi wa kikao hiki, alitangaza kwamba kutakuwepo na Sinodi za Maaskofu pamoja na Baba Mtakatifu katika ngazi ya Kimataifa ili kumshauri Papa. Hii iliwafurahisha wengi. Hadi sasa, Sinodi hizi zinafanyika.

Mwishoni mwa kikao cha nne ambacho ndicho kilikuwa kikao cha mwisho, kuna matukio muhimu yalifanyika. Kitu kipya kabisa Papa alisali pamoja na Wakristu wa madhehebu mengine waliokuwa katika Mtaguso.

Tarehe 6 Desemba 1965, alitangaza Mwaka wa Jubilee kuanzia tarehe 8 Desemba 1956 hadi tarehe 8 Desemba 1966, kwa ajili ya kutangaza na kueneza Mafundisho ya Mtaguso wa Vatikani II (1962 - 1965).

Tarehe 7 Desemba akiwa pamoja na Patriarka Athenegoras wa Konstantinople, ambaye alikuwa Mkuu wa Kanisa la Kiortodosi, walilaani utengano, chuki na kuhukumiana (Excommunications) zilizofanyika mwaka 1054, zilizotenganisha Kanisa la Kiortodosi na Kanisa Katoliki.

Wote walisameheana rasmi, na kuahidi kufanya wawezavyo ili kurudisha umoja. Tarehe 8 Desemba 1965, Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatikano ulifungwa kwa Misa Takatifu iliyoadhimishwa na Papa katika Uwanja wa Basilica ya Mtakatifu Petro, huko Vatikano.

Matokeo ya Mtaguso wa Pili wa Vatikano ni kwamba kwanza uligeuza muono wa Kanisa Katoliki na kulileta katika mtazamo wa nyakati zake, bila kugeuza Mafundisho na Mapokeo Msingi ya Kanisa.

DAR ES SALAAM

Na Alex Kachelewa

Magonjwa yasiyoambukiza (MYA), ni maradhi ambayo hayaambukizi na wala hayawezi kusambazwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine au mnyama, ndege, kwani mara nyingi huwa ni ya muda mrefu.
Mfano wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza ni kisukari, shinikizo la juu la damu, saratani, mfumo wa upumuaji, ajali, afya ya akili, na selimundu.
Taarifa ya hali ya MYA duniani zilionesha kuwa watu milioni 42 (sawa na asilimia 71 ya vifo vyote), walifariki dunia katika matimba mbalimbali duniani kote kutokana na magonjwa haya.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani, Nchini Tanzania 33% ya vifo vyote vinachangiwa na magonjwa hayo ambayo huchangia kwa 75% ya vifo vyote vinavyohusu watu wenye umri wa miaka 30-70.
Viashiria vya Magonjwa Yasiyoambukiza:
Viashiria hatarishi vya magonjwa yasiyoambukiza vimegawanyika katika sehemu tatu; viashiria vya awali; utandawazi, ukuaji wa miji, ongezeko la watu wenye umri mkubwa.
Viashiria vinavyowezekana kubadilika; Ulaji-matunda na mbogamboga- 2.7%, matumizi ya pombe- 29.4%, Tumbaku-15.9%, tabia bwete na uzito uliozidi- na Kiribatumbo- 26%.
Mwaka 2021 jumla ya wagonjwa 3,440,708 wenye magonjwa yasiyoambukiza walitibiwa (OPD) ikilinganishwa na wagonjwa 3,852,973 waliotibiwa mwaka 2022 (ongezeko likiwa ni 412,265, sawa na 12%). Magonjwa ambayo yanaongoza ni pamoja na shinikizo la juu la damu, ugonjwa wa kisukari.
Taarifa ya vifo inaonesha kuwa katika kila vifo vitatu vinavyotokea nchini, kifo kimoja kinatokana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
Na katika magonjwa 10 yanayoongoza kusababisha vifo nchini, kuna magonjwa manne yasiyoambukiza (Magonjwa ya Moyo (4.5%) yanashika nafasi ya Pili; Shinikizo la Damu (3.8%) nafasi ya tatu; pamoja na ugonjwa wa Kisukari (2.5%), nafasi ya 9.
Hali ya magonjwa ya saratani kila mwaka inaonyesha kuwa wagonjwa wapya 40,464 wa saratani wanagundulika, ambapo sehemu kubwa ya wagonjwa hao huwa na saratani zifuatazo:-
Saratani ya Mlango wa Kizazi (25.3%); Saratani ya Matiti (9.9%); saratani ya tezi dume (8.8%). Kila mwaka saratani husababisha vifo vya watu 26,945, wengi wao wakiwa ni kina mama wenye tatizo la saratani ya mlango wa kizazi.
Hali ya magonjwa ya selimundu nchini Tanzania ni miongoni mwa nchi tano zinazoongoza kwa ugonjwa wa selimundu duniani, ambapo mtoto mmoja katika kila watoto 100 huzaliwa na ugonjwa huu, na asilimia 15 ya Watanzania, wanaishi na vinasaba vya selimundu.
Hata hivyo, watoto 70 - 90 hufariki dunia kutokana na ugonjwa huu kabla ya kufikia umri wa miaka mitano, wengi hushindwa kupata elimu kutokana na kuumwa mara kwa mara.
Tanzania imeanza huduma za kupima watoto wachanga ili kubaini mapema kama wana ugonjwa. Huduma ya upandikizaji uloto imeanza Hospitali ya Benjamin Mkapa kama tiba pekee ya tatizo hili kwa sasa.
Hali ya Magonjwa ya Akili:
Jumla ya wagonjwa 260,894 walipatiwa huduma za afya ya akili katika mwaka 2022, wagonjwa wengi ni wale wenye kifafa, sonona, na wanaotumia dawa za kulevya.
Tanzania pia ni miongoni mwa nchi ambazo kuna hali ya juu ya kujiua, ambapo kwa ujumla katika kila watu 100,000, watu wanane wamepata tatizo hilo (MNH data 2020).
Kwa vijana kati ya, miaka 13 – 17, tafiti zinaonesha kwamba katika kila vijana 100, kuna vijana 12 ambao wanapata hisia za kutaka kujiua, na kati yao 10 kwa kila 100, wameshajaribu kufanya hivyo.
Athari zitokanazo na Magonjwa Yasiyoambukiza:
Ongezeko la vifo vinavyoweza kuepukika katika ongezeko la watu wanaoishi na ulemavu au changamoto zinazoweza kuzuilika:
Kisukari huchangia asilimia 27 ya upofu unaotokana na mtoto wa jicho. Takribani asilimia 10 ya wagonjwa wa kisukari hupata matatizo ya miguu, ikiwemo kukatwa miguu kwa zaidi ya asilimia 10 ambao huanza kupata matatizo ya figo.
Shinikizo la juu la damu na kisukari, huchangia matatizo ya kiharusi (stroke), pamoja na tatizo la figo kwa zaidi ya asilimia 25 ya wagonjwa wote.
Magonjwa hayo yana athari za kiuchumi na kijamii, madhara kwenye rasilimali watu na hasara kwa Pato la Taifa  kupungua uzalishaji kwa wafanyakazi kushindwa kuhudhuria. Kushindwa kuwa na ufanisi gharama za kuajiri watumishi wapya, kupungua kwa rasilimali watu wenye ujuzi, Serikali kutumia fedha nyingi kwenye matibabu. Sekta Binafsi zinawekeza pia katika huduma za Afya (NCDs accounts for 20% of NHIF Budget).
Madhara kwa mtu na familia ni ongezeko la matumizi ya Serikali na Sekta Binafsi, husababisha kifo kupoteza kipato cha familia kuwa na ufukara kutokana na gharama za matibabu kupanda, pamoja na kupoteza muda kutokana na kuwahudumia wagonjwa, na pia familia kuachwa na yatima.
Mikakati mitano ya Serikali katika kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza ni kuimarisha huduma za Afya ya Akili, huduma za saratani pamoja na Bankable Document. Mkakati wa huduma za macho na mkakati wa (sickle cell) selimundu imeandaliwa kuongoza utekelezaji, na mwongozo wa mazoezi.
Kuongeza upatikanaji wa huduma za uchunguzi wa awali (newborn Screening), upatikanaji wa dawa ya Hydroxyurea na upandikizaji uloto kwa wagonjwa wa selimundu – ambapo tayari Bunge liliidhinisha kaisi cha Shilingi bilioni tano kwa huduma hizo.
Upanuzi wa huduma za saratani kwa ajili ya kutoa huduma za mionzi kwenye Hospitali zote za Kanda na Ujenzi wa Kituo cha Umahiri Mloganzila na Dodoma pamoja na kuimarisha huduma katika Mkoa wa Mbeya, Hospitali ya KCMC, Moshi, Mkoani Kilimanjaro, na Bugando mkoani Mwanza, ambazo tayari ujenzi wake umeanza.
Kuimarisha upatikanaji wa huduma za Elimu kwa Umma, uchunguzi na matibabu kuanzia ngazi ya Msingi, Wizara imewezesha Mafunzo kwa watendaji 2890 kwenye vituo 702 vya afya nchi nzima, vifaa vya kuwekeza katika utafiti, na tathmini ili kubaini viashiria vya magonjwa yasiyoambuza, utafiti kwenye hali na madhara ya kiuchumi yatokanayo na Tumbaku, hali ya ufanyaji mazoezi, na hali ya Lishe nchini.
Kuanzishwa kwa mpango wa Taifa (TaNCDP) – 2019, ni kwa sababu ya uhitaji wa Serikali na Wadau kuwekeza zaidi kwa kuhutubia Taifa ili Kuzindua Mpango wa Taifa.
Maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya NCD kwa Kuzindua Miongozo na Initiatives mbalimbali (National Lifeystyle Reform Campaign).
Hatua ya Serikali kuandaa Mkakati wa III wa Magonjwa Yasiyoambukiza umetokana na HSSP – v na One Plan III kuwekeza katika maeneo yanayoainishwa, na mkakati wa ugharamiaji wa huduma za Afya kwa Wote (UHC).
Uwekezaji kwenye Afya ya msingi kwa kubuni njia za upatikanaji wa rasilimali kwa ajili ya magonjwa yasiyoambukiza, kuimarisha matumizi ya takwimu na tafiti, na kadhalika.
Aidha, mikakati harakishi ni kuimarisha uratibu kwa kuhusisha sekta 12 muhimu katika kusimamia afua kinga na udhibiti wa magonjwa yasiyoambuikiza.
Kubainisha na kuandaa kampeni maalum kwa makundi yaliyo kwenye uhatarishi mkubwa Wafanyakazi mahali pa kazi ili kuhakikisha walau 75% ya watu wote wanafikiwa na elimu hiyo, na 50% ya wenye umri wa miaka 40 na kuendelea, wanapimwa afya zao.
Pia kuhakikisha 50% ya shule zinafikiwa na elimu ya magonjwa yasiyoambukiza, 75% ya wanafunzi kwenye shule hizo wanafikiwa, pamoja na watu wenye umri mkubwa (zaidi ya miaka 60) wanafikiwa.
Kufanya tafiti za hali ya magonjwa yasiyoambukiza- STEPS 2023; Utafiti kwenye hali na madhara ya kiuchumi yatokanayo na Tumbaku; Hali ya Ufanyaji wa Mazoezi, pamoja na Hali ya Lishe nchini, ni Kampeni za Uhamasishaji katika Jamii.