SAKA (SALA NA KAZI)
DODOMA
Na Gaudence Hyera
Miongoni mwa Parokia zinazounda Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma ni ya Parokia ya Watakatifu Wote, Nzuguni, ambayo inatarajiwa kuadhimisha miaka mitatu Novemba Mosi mwaka huu, tangu ilipozinduliwa rasmi Novemba Mosi mwaka 2020 na Askofu Mkuu wa Jimbo hilo, Mhashamu Beatus Kinyaiya.
Kwa mujibu wa Takwimu za kichungaji zinaonesha kuwa kwa sasa Jimbo hilo lina Parokia 51na Parokia Teule mbili na vigango vinavyotarajiwa kupandishwa hadhi.
Parokia ya Watakatifu Wote, Nzuguni, inaundwa na Vigango vinne vilivyozinduliwa rasmi katika kipindi cha miaka miwili na miezi sita ya Utume wa Paroko wake wa kwanza, Padri Joseph Mkonde “Kazikunema”.
“Nilifika Dodoma wakati huo ikiwa Parokia Teule na ilituchukua miezi minne na kufanikisha kufanya uzinduzi wa kuwa Parokia, ambapo Kanisa lilifanyiwa maboresho na nyumba ya Padri na baadaye tukajenga nyumba inayotarajiwa kuwa ya Masista,” alisema Padri Mkonde.
Alivitaja vigango hivyo kuwa ni Kigango cha Mtakatifu Yohane Mbatizaji, Sokoine, ambacho kilianzishwa mwaka 1967; Kigango cha Roho Mtakatifu kilichoanzishwa mwaka 2022; na Kigango cha Bikira Maria Mpalizwa Mbinguni, cha mwaka 2022.
Kigango kipya cha Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Mvwagamale, Mtaa wa Magufuli kilizinduliwa Dominika ya Juni 11, 2023 sanjari na Adhimisho la Sherehe ya Mwili na Damu Takatifu ya Bwana Yesu Kristo.
Katika mahubiri yake wakati wa Misa hiyo Takatifu, Padri Kazikunema aliwataka waamini kuishi Kauli Mbiu inayohamasisha majitoleo kwa Sakramenti Kuu ambayo ni “Yesu wa Ekaristi Takatifu; Sadaka yangu; Chakula changu na Rafiki yangu”.
Parokia hiyo ni ya Kibalozi ikiwa chini ya Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma. Kichungaji na Kiutawala iko chini ya Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, baada ya Askofu Mkuu Kinyaiya, OFMCap, kukubaliana na Askofu Mkuu Jude Thaddaeus Ruwa’Ichi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.
Vivyo hivyo kwa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Parokia ya Kibalozi ni ya Mtakatifu Yuda Thadei, Stakishari, ambayo Paroko wake wa kwanza ni Padri Laurent Lelo kutoka Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma, ikiwa chini ya utawala wa Jimbo Kuu hilo, na uchungaji wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.
Parokia ya Watakatifu Wote, Nzuguni inaundwa na Vigango vinne vilivyozinduliwa rasmi katika kipindi cha miaka miwili na miezi sita ya Utume wa Paroko wa kwanza, Padri Joseph Mkonde “Kazikunema”.
Padri Mkonde ni miongoni mwa Mapadri watatu Wakurugenzi wenza wa miito ya Upadri, Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma, na pia ni mlezi wa Utume wa Mtakatifu Rita wa Kashia wa Jimbo hilo, ambapo Makao Makuu yake yapo katika Parokia ya Nzuguni.
“Nilifika Dodoma wakati huo ikiwa Parokia Teule, na ilituchukua miezi minne tu kufanikisha kufanya uzinduzi wa kuwa Parokia, ambapo kanisa lilifanyiwa maboresho pamoja na nyumba ya Padri, na baadaye tukajenga nyumba inayotarajiwa kuwa ya Masista, ambayo timu ya Tumaini Media ikiongozwa na Gaudence Hyera, ilifikia humo kwa muda wote walipokuwa Nzuguni kuanzia Juni 8 hadi 12; 2023” alieleza Padri Mkonde.
Alivitaja Vigango hivyo kuwa ni Kigango cha Mtakatifu Yohane Mbatizaji, Sokoine, ambacho kilianzishwa mwaka 1967; Kigango cha Roho Mtakatifu, Nharawanda, kilichozinduliwa mwaka 2022; na Kigango cha Bikira Maria Mpalizwa Mbinguni-Chamelo.
Kingine ni Kigango kipya cha Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Mvwagamale, Mtaa wa Magufuli kilichozinduliwa na Padri Joseph Mkonde Kazikunema, Dominika ya Juni 11 mwaka 2023, sanjari na Sherehe ya Mwili na Damu Takatifu ya Bwana Yesu Kristo.
Katika mahubiri yake wakati wa adhimisho la Misa Takatifu, Padri Kazikunema aliwataka waamini kuishi kauli mbiu inayohamasisha majitoleo (Totus Tuus)kwa Sakramenti Kuu, ambayo ni “Yesu wa Ekaristi Takatifu; Sadaka yangu; Chakula changu na Rafiki yangu.”
Jambo ambalo si jepesi na siyo kawaida, licha ya kutokea katika baadhi ya Parokia, ni andamo la Ekaristi ambalo lilichukua umbali wa zaidi ya kilomita 15, huku Paroko Padri Mkonde aliyekuwa peke yake, alibeba Monstrance yenye Hostia Takatifu, mpaka mwisho.
Andamo hilo lilianzia Mvwagamale, kupitia katika vigango na vituo vya sala vya Nanenane-Mtakatifu Faustina(Mtume wa Huruma ya Mungu), na Nhunduru-Mtakatifu Rita wa Kashia (muombezi wa mambo yaliyoshindikana), na kumalizikia Parokiani Nzuguni.
Akizungumzia shughuli za kichungaji, Padri Mkonde alieleza kuwa Misa Takatifu inaadhimishwa kila Dominika katika vigango vyote, akisaidiwa na mapadri na wengine wakiwemo Wamisionari wa Shirika la Ndugu Wafransisko Wakapuchin-OFMCap, na Ibada katika vituo vya Sala.
“Tunaendelea na miradi ya ujenzi parokiani na katika vigango vyote, ambapo ujenzi wa nyumba ya mapadri ya ghorofa tano, kwa matumizi mbalimbali ya kichungaji, inajengwa katika eneo la Parokia, pamoja na Grotto ya Familia Takatifu na ya Mtakatifu Rita wa Kashia,” alieleza Padri Mkonde.
Alieleza pia kuwa nyumba hiyo ya ghorofa tano kwa sasa inaonekana kama ni kubwa mno, lakini miaka ijayo itakuwa ndogo kwa kuwa wanatarajia mapadri, watawa na viongozi walei na waamini wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, watakuwa wanapata mahali pa kufikia wakiwa katika uinjilishaji Dodoma.
Aligusia pia katika Kigango cha Sokoine, ujenzi wa nyumba ya mapadri umeanza na pia mkakati wa kuongeza eneo lao kwa kununua baadhi ya nyumba za jirani, ili kufanya upanuzi wa kanisa na kujenga nyumba ya Masista.
Kigango cha Roho Mtakatifu kipo katika hatua ya kumalizia ujenzi wa kanisa na kupaka rangi, pamoja na kuanza ujenzi wa nyumba ya Mapadri, kwani wanayo matarajio makubwa ya kutangazwa kuwa Parokia Teule wakati wowote mwaka 2023 au 2024.
Akizungumza na Tumaini Letu, Mwenyekiti wa Halmashauri Walei wa Kigango hicho, Isaya Ntalugila alisema kuwa ni kigango cha pili kuzinduliwa katika Parokia ya Nzuguni, mbali na kuwa ni kigango cha pili, lakini kinasifika kwa waamini wake kujitoa kwa hali na mali katika kufanikisha maendeleo ya kiroho, kimwili na kijamii.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Kigango hicho, Jeremiah Msangi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Liturjia Kigango cha Roho Mtakatifu, alikazia kwamba hawana hofu kwamba kila jambo lililopangwa, ikiwemo miundombinu bora na taratibu za liturjia, ziko vizuri.
Msangi alieleza kuwa walipata ruhusa ya Paroko kuadhimisha Sherehe ya Mwili na Damu peke yao kutokana na utaratibu waliojipangia wa kufanya Andamo la sakramenti kuu kwa kupita katika kila nyumba ya mwamini kigangoni hapo na kuhamasisha Imani na majitoleo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kigango cha Bikira Maria Mpalizwa Mbinguni, Francis Mwakasege alisema kuwa kilizinduliwa rasmi Mei 28 mwaka 2023 na Paroko wa Parokia hiyo, Padri Joseph Mkonde Kazikunema.
Alibainisha pia kuwa matarajio ya waamini wa kigango hicho ndani ya miaka miwili, ni kuijenga ili iwe Parokia Teule.
Nao Viongozi wa Vyama vya Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA), Anecia Longino, na wa Utume wa Wanaume Katoliki (UWAKA), Acley Mushi, waliunga mkono kile ambacho alieleza Mwenyekit Mwakasege.
“Tumejipanga ili kuhakikisha tunapiga hatua za haraka kuyafikia malengo tuliyojiwekea, ikiwemo kuimarisha Utume wa Walei kuanzia ngazi ya Familia, Jumuiya na Vyama vya kitume,” walisema viongozi hao.
Nacho Kigango cha Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili kinaendelea kujiongeza kwa ujenzi wa kanisa, na kujiandaa kuanza ujenzi wa nyumba za mapadri, masista na huduma nyingine.
Parokia ya Nzuguni pia inazo Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo ambazo zinathibitisha uhai wa imani kwa waamini wake kiroho na kimwili, kutokana na kujitoa kwa moyo kushiriki kazi za uinjilishaji kuanzia mwamini binafsi, katika familia, hadi Parokiani.
Upande wa Vyama vya Kitume, Parokia hiyo inajumuisha Utoto Mtakatifu, Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA), Utume wa Wanaume Katoliki (UWAKA), Vijana Wakatoliki Wafanyakazi (VIWAWA), Utume wa Rita wa Kashia, Lejio Maria, na Utume wa Kwaya Katoliki Tanzania (UKWAKATA).
Kauli Mbiu ya Parokia ya Watakatifu Wote, Nzuguni, ni: “Watamtazama yule waliyemtoboa,” andiko linalopatikana katika Injili kama ilivyoandikwa na Mtakatifu Yohane, Sura ya 19, Aya ya 37.
Andiko hilo linasomeka chini ya msalaba kwenye Mnara wa Msalaba Mtakatifu uliosimikwa mbele ya lango kuu la Kanisa la Parokia ya Watakatifu Wote, Nzuguni.