Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

DAR ES SALAAM

Na John Kimweri

Imeelezwa kuwa kiburi cha elimu ni sababu mojawapo inayowafanya watu kuacha kumwamini Mungu, na kutegemea utashi wao na mali walizonazo, kama jawabu katika maisha.
Kauli hiyo ilitolewa na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Stephano Musomba, wakati akitoa homilia yake kwenye Adhimisho la Misa Takatifu ya Sakramenti ya Kipaimara kwa vijana 125, iliyofanyika Parokia ya Mtakatifu Martin wa Porres, Mwananyamala.
Askofu Musomba (pichani) alisema kuwa kiburi ni dhambi na ndiyo chanzo cha migogoro mingi duniani, akiwataka waamini  kuhakikisha licha ya elimu walizonazo, lakini watambue uwepo wa Mungu katika maisha yao kwa sababu bila yeye, hawawezi kufanya kitu chochote.
“Kiburi cha usomi kinaweza kusababisha mtu akaona kuwa hakuna Mungu, na eti anajiweza yeye mwenyewe bila ya msaada wa Mungu, kiburi ni dhambi kubwa sana na ndiyo chanzo cha migogoro mingi duniani,” alisema Askofu Musomba.
Askofu  Musomba, alieleza kuwa kiburi kingine ni cha maendeleo na kiroho, akiwaonya waamini wanaojiona kuwa wamekamilika kuliko wengine kuacha kufanya hivyo.
Aliwakumbusha wazazi kuhakikisha kuwa wanapowarithisha  watoto wao mali na vitu vingine vya thamani, wasisahau kuwarithisha imani, kwani hilo ni jambo lisiloharibika wala kuchakaa.     
Aidha, aliwataka waimarishwa kutambua kwamba wanapopokea Sakramenti hiyo, Roho Mtakatifu anaingia ndani mwao na kuwafanya kuwa wapya katika kila jambo, huku akiwaasa wazazi nao kuwa na desturi ya kusali pamoja, na pia kusoma Neno la Mungu na watoto wao.  
Alisema kwamba Roho Mtakatifu ni nyenzo ya utume ya kuwasaidia waamini kuinjilisha hapa duniani, na kudai kuwa utume wa kweli unatakiwa kuanzia kwenye ngazi ya familia.
Kwa mujibu wa Askofu  Musomba, utii unamfanya mtu akabidhi utashi na kuwa mtii kwa Mungu mwenyewe, na kuongeza kwamba pia utii huendana na usikivu, ambapo mwisho wake huleta unyenyekevu kwa mtu.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Walei Parokia hiyo, Jeremia Mchomvu, alisema kuwa Parokia hiyo ina jumla ya waamini 6757, kutokana na sensa iliyofanyika Januari mwaka 2020.
Alisema kuwa Parokia kwa sasa ina mpango wa kununua nyumba mbili, ili kupanua eneo la kanisa.

Padri Germine Laizer akiwavisha rozari baadhi ya wanachama wapya wa Chama cha Wajane na Wagane

Dar es Salaam

Na Benedikto Agostino

Wajane na Wagane nchini wametakiwa kuendelea kuishi fadhila za Mtakatifu Monica bila kukata tamaa, na kumshukuru Mungu kwa maisha ya wenzi wao waliotangulia mbele ya haki, bila kusahau kuwaombea hao na watoto waliochwa na wazazi wao kila mara.
Hayo yalisemwa na Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Kamili, Yombo Kiwalani, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaaam, Padri Germine Laizer, wakati akihubiri katika Adhimisho la MIsa Takatifu ya Somo wa Wajane na Wagane, Mtakatifu Monica, iliyofanyika kwa ngazi ya Jimbo katika Parokia hiyo.
Katika homilia yake, Padri Laizer aliwakumbusha wajane na wagane kutambua maisha ya Mtakatifu Somo wao, Monica, kama mjane aliyeishi katika mateso na maisha mabaya ya mwanae Augustino, lakini licha ya kupitia changamoto hizo, hakukata tamaa hadi mtoto wake alipoongoka, na sasa ni Mtakatifu.
Alisema kwamba pamoja na ujane na ugane wao, ni muhimu kuishi fadhila ya unyenyekevu, kwani ni ishara ya itii mbele ya Mungu na watu, na hasa kila mmoja anapojishusha na kuwa kama mtoto mdogo.
“Maisha yetu yana maana kubwa kila tunapojinyenyekeza na kujikabidhi mbele ya Mwenyezi Mungu, kwani kila mmoja wetu anadaiwa kadri anavyokuwa mkuu kunyenyekea,” alisema Padri Laizer.
Aliongeza kusema kwamba watu wengi walioishii fadhila hiyo ya unyenyekevu wamepata kibali mbele za Mungu, na kujibiwa sala na maombi yao na kumbukumbu lao linaishi hata hivi leo.
“Tabia ya kiburi na majivuno ni kinyume cha unyenyekevu, na mara baada  ya mtu kuwa na maisha hayo, hali ya mtu hubadilika na kuharibika kabisa,” alisema Padri Laizer.
Alisema kuwa tukiongozwa na unyenyekevu ni lazima tufike mbali, kwani fadhila hiyo inalipa, na hakuna aliyeishi hali hiyo ambaye hakufanikiwa kamwe.
“Ni wazi unyenyekevu unapokosekana popote, yanatawala mafarakano, uogomvi na majigambo, hali inayotawanya kundi na kupoteza amani na mshikamano miongoni mwa familia ya Mungu,” alisema padri huyo.
Aliwataka waamini kuiga mfano mzuri wa mtu pekee aliyeishi fadhila ya unyenyekevu, ambaye ni Bikira Maria ambapo pamoja na magumu aliyoyapitia, aliyaweka mengi moyoni mwake.
Naye Mwenyekiti wa Wajane na Wagane Jimbo, Sweetbeter Mzungu alimshukuru Paroko wa Parokia hiyo, kwa utayari wake wa kupokea ujio wa sherehe hizo, na kuwapongeza wanachama wote waliojitokeza kufanikisha shughuli hiyo muhimu ambayo hufanyika mara moja kila mwaka.
Sweetbeter alisema kwamba moja ya mafanikio makubwa kwa sasa ni hatua waliopiga kutoka kutambuliwa kama kikundi na kuwa chama cha kitume ingawa bado changamoto kubwa ni mwitikio, hasa wa kupokelewa katika Parokia zote.
Alibainsha kuwa mara nyingi watu wengi hawapendi kujitambulisha kama wajane au wagane, na hali hiyo hutokana na kutokujikubali au kuipokea baada ya kuondokewa na wapendwa wao, na hasa wagane.

Page 3 of 3