DAR ES SALAAM
Na Happiness Mthathia-TUDARCO
Serikali imesema kwamba imejipanga kupunguza kero ya usafiri kwa wanafunzi jijini Dar es Salaam, kwa kutekeleza mikakati iliyojiwekea, ikiwemo kutumia usafiri wa mabasi yaendayo haraka (Dar es Salaam Rapid Transit: DART) na Treni.
Hayo yalisemwa na Alhaji Maulidi, Afisa Elimu wa Mkoa wa Dar es Salaam wakati akizungumza na gazeti Tumaini Letu katika mahojiano maalum yaliyofanyika ofisini kwake jijini Dar es Salaam, kuhusu kero ya usafiri kwa wanafunzi.
“Serikali inaendeleza ujenzi wa barabara za mabasi yaendayo haraka, ikiwemo barabara iendayo Gongo la Mboto kutoka mwanzo wa Barabara ya Nyerere, Msimbazi, Kariakoo. Pia, ina mkakati wa kujenga barabara kutoka Morocco (Kinondoni) kwenda Tegeta, na itafika mpaka Bunju ili kuwasaidia wanafunzi,” alisema Maulidi.
Alisema pia kuwa mpango wao ni kushirikisha sekta binafsi katika kutatua changamoto ya usafiri kwa wanafunzi jijini Dar es Salaam, kwani kwa sasa hali ni nzuri ikilinganishwa na ilivyokuwa katika miaka ya nyuma.
Maulidi alisema kuwa jukumu la Serikali kwa wanafunzi ni kuwapatia elimu bora, na kuongeza kuwa wazazi wana jukumu la kuhakikisha watoto wanafika shuleni na kurudi nyumbani kwa kuwapatia nauli kwa ajili ya usafiri.
Afisa huyo aliwataka makondakta kuwahudumia wanafunzi waweze kusafiri kwa wakati ili kupunguza changamoto wanayokumbana nayo, na kuwakanya wanafunzi nao ili wajiheshimu.
Baadhi ya wanafunzi wameliambia gazeti hili kwamba wamekuwa wakikabiliwa na changamoto kubwa ya usafiri nyakati za asubuhi na jioni kwa kukataliwa na makondakta wa daladala, na hivyo kuchelewa kwenda shule na kurejea nyumbani.
Mmmoja wa wanafunzi hao, John Elias wa Shule ya Sekondari Kawe Ukwamani jijini Dar es Salaam, alisema kuwa wanakumbana na changamoto hiyo mara kwa mara.
“Tumekua tukikataliwa na makonda kuingia kwenye daladala kitu ambacho kinasababisha tuchelewe kufika shule pia kurudi nyumbani nyakati za jioni,’’ alisema John.
Kwa upande wao baadhi ya wazazi akiwemo Mama Jordan, Mkazi wa Mtaa wa Goba jijini Dar es Salaam, alithibitisha kuwepo kwa changamoto hiyo kwa wanafunzi, akisema kuwa sababu ya makondakta kuwakwepa wanafunzi ni kiasi cha nauli wanacholipa cha Shilingi 200/=, hivyo wanaona bora wanafunzi waachwe.