ADDIS ABABA, Ethiopia
Askofu Mwandamizi wa Jimbo Katoliki la Eparchy Emdibir Eparchy, Mhashamu Askofu Teshome Fikre, amesimikwa.
Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Ethiopia, Mwadhama Abune Kardinali Berhaneyesus, aliongoza Ibada hiyo ya kuwekwa wakfu Askofu Teshome Fikre, ambapo Askofu huyo mpya amechukua jina la ‘Askofu Luka.’
Tukio hili lilihudhuriwa na Askofu Mkuu Antoine Camilleri, Balozi wa Kitume nchini Ethiopia na Djibouti, Askofu Mussie, Askofu wa Emdibir Eparchy, Maaskofu Katoliki kutoka Ethiopia na Eritrea.
Wengine ni Padri Raphael Simbine, Katibu Mkuu wa SECAM, Padri Anthony Makunde, Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya AMECEA, kutoka Kanisa la Kiorthodoksi la Ethiopia, Askofu Mkuu Melketsedik, Askofu Mkuu wa Jimbo la Gurage Mashariki na Magharibi.
Kutoka Kanisa la Kiinjili, Mekane Yesus na Padri Yonas Yigezu; Rais wa Ethiopia akiwa na Balozi Misganu Arega; Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Shirikisho la Ethiopia; na Waamini wengine kutoka kote Ethiopia, walihudhuria.
Wakati wa Homilia, Kardinali alikumbusha kwamba moja ya majukumu ya Askofu ni kuhubiri na kueneza Injili ya Bwana, hata katika nyakati zinazofaa na zisizofaa, kama vile Mtume Paulo alivyomwambia Timotheo.
Mwadhama Abune Kardinali Berhaneyesus alimtaka Askofu mpya Lukas kusimama upande wake, na atamsaidia kwa maombi ili kutimiza wajibu huo.
Askofu Lukas katika maelezo yake, alitangaza mstari mkuu aliouchagua kwa utumishi wa Uaskofu wake, “Chunga Kondoo Wangu” Yoh 21:15.
“Siku zote Mchungaji atawaongoza kondoo mbele yao ili wasimame pamoja kwa upatano na mioyo na akili zao, bila kupoteza tumaini lao. Wakati mwingine anakuwa kati yao, akiwa mnyenyekevu na mwenye rehema,” alisema Askofu Lukas.
Kwa upande wake, uongozi wa Askofu Mussie umekuwa wa kuigwa tangu kuanzishwa kwa ‘eparchy’, ukiacha alama ya kudumu kwa jamii.
Katika moja ya utume wake, ni kuongoza ujenzi wa makanisa 15 mapya, ufunguzi wa makutaniko 12 ya kidini, na kupanua huduma za utawala.
Aidha, kujitolea kwake kunaenea zaidi ya mambo ya kiroho, kama inavyothibitishwa na mipango yake katika elimu (shule), huduma za afya (vituo vya afya, hospitali), miundombinu (maji, kilimo), na usaidizi wa kijamii (vituo vya wanawake na vijana, pia vituo vya huduma).