Dar es Salaam
Na Laura Chrispin
Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, amesema kuwa Taifa kwa sasa linapitia kipindi kigumu, kwani kimejaa vilio na wasiwasi mwingi kutokana na vitendo vya watu kutekwa na kuuawa, na miili yao kutupwa.
Kardinali Pengo alisema hayo wakati akitoa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya kutoa Sakramenti Takatifu ya Kipaimara, iliyoadhimishwa Parokia ya Ekaristi Takatifu-Keko Jimboni humo.
“Kipindi tunachopitia sasa kimejaa vilio, wasiwasi na huzuni, kwani watoto na watu wazima wanatekwa, kuteswa na kuuawa. Imefika hatua unatafuta wapi tunaokota mwli wa mtu ambapo hiyo hali hatukuwahi kiiona na hatujaizoea,”alisema Kardinali Pengo.
Akizungumza kuhusu Waimarishwa, Kardinali Pengo, alisema kwamba Wanakipaimra hao wamekubali kuimarishwa, hivyo yawapasa wawe tayari kusikia sauti ya Kinabii na nguvu ambayo inatokana na Sakramenti ya Kipaimara.
Kardinali Pengo aliendelea kusema kwamba vijana hao wanatakiwa kuwa tayari kusikia sauti ya Kinabii ndani yao, kwani Mitume wa mwanzo hawakuwa jasiri wa kutangaza habari njema kwa watu, ndiyo maana walijificha ndani kwa hofu ya Manabii, lakini baada ya kushukiwa na Roho Mtakatifu, walikuwa jasiri kwani walitoka nje na kuanza kufundisha habari njema kwa Mataifa yote Ulimwenguni.
Aidha, aliwasihi Waimarishwa hao kukabiliana na dhambi binafsi, na zile watu wanazotumia kuongozea taifa.
Kardinali Pengo alitoa wito kwa Waamini wote kuwa bega kwa bega na Waimarishwa kwenye kazi zao za kiutume.
Kwa upande wake Katibu Crinton Mushi, alimshukuru Askofu Mstaafu kwa kutoa Sakramenti hiyo, kwa Vijana 13.
Aidha, alimwomba Kardinali Pengo kuwasaidia kuzirudisha Jumuiya zilizochukuliwa na Parokia za jirani ya Kurasini na Chang’ombe.
Naye Paroko wa Parokia hiyo, Padri Meinrad Bigirwamungu Kalikawe, alimshukuru Kardinali Pengo kwa kuadhimisha Misa hiyo kwenye Parokia ya Ekaristi Takatifu.