ROMBO
Na Mathayo Kijazi
Watawa wa Kike wametakiwa kuendeleza karama walizojaliwa nazo, ili kila mmoja aweze kupokea baraka zaidi kupitia karama alizo nazo maishani mwake.
Hayo yalisemwa hivi karibuni na Askofu wa Jimbo Katoliki la Zanzibar, Mhashamu Agustine Shao, alipokuwa akitoa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Jubilei ya Masista 39 wa Shirika la Bibi Yetu wa Kilimanjaro (CDNK Sisters), iliyoadhimishwa katika Kanisa la Nyumba ya Asili - Huruma Convent, Rombo, Jimbo Katoliki la Moshi.
Wakati huo huo, Askofu Shao aliwataka Masista wale ambao ni waalimu, waepuke kuwachapa watoto viboko kupitiliza, bali wawafundishe kwa upole na kwa unyenyekevu, kwani kuwaelimisha siyo lazima kutumia viboko.
“Kwa hiyo, jitahidini sana kuziendeleza karama zenu mlizojaliwa nazo, ili kupitia karama hizo, kila mmoja aweze kupokea baraka zaidi katika maisha yake,” alisema Askofu Shao, na kuongeza…
“Masista waalimu, msiwatandike watoto kupitiliza, waelekezeni kwa upole na kwa unyenyekevu, kwa sababu kuwaelimisha siyo lazima mtumie viboko.”
Aidha, aliwataka Masista hao kufahamu kwamba Jubilei haiwezi kuwa Jubilei kama hawataingia ndani sana, ikiwa ni pamoja na kuwasaidia wengine, na kuwasamehe wale waliowakosea.
Pia, aliwasisitiza kulichukua jukumu la kuishi kama wawekwa wakfu, ikiwa ni pamoja na kuishi maisha yanayompendeza Mungu, kwani hilo ndilo jukumu lao baada ya kuweka Nadhiri zao za Daima.
Vile vile, alilipongeza Jimbo Katoliki la Moshi kwa kuendelea kuzalisha Watawa wengi, akiwasihi wazazi na walezi kuendeleza malezi kuendelea kuwapata Watawa wengi zaidi.
Kwa upande wake Mama Mkuu wa Shirika hilo la Bibi Yetu wa Kilimanjaro (CDNK Sisters), Sista Theresia Buretta aliwashukuru wazazi wa Masista hao, kwani wazazi ndio waliwalea katika malezi ya kumpendeza Mungu tangu wakiwa wadogo.
Aliongeza kwamba uwepo wa Masista waliomshukuru Mungu kwa Miaka 25, 50 na 60 ya Utawa, kwao ni jambo la furaha, huku akimshukuru Askofu Shao kwa kusafiri kutoka Zanzibar hadi jimboni Moshi kuadhimisha Misa hiyo Takatifu.