DAR ES SALAAM
Na Mwandishi wetu
Watawa wametakiwa kuishi viapo vyao, na kujitoa kikamilifu katika Utume wao.
Wito huo umetolewa hivi karibuni na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Stephano Musomba, wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Jubilei ya Miaka 25 na 50 ya Utawa kwa Sista Adela Chami, Sista Victoria Ligambas, Sista Mbetina Kapwaga, na Sista Lucina Escudero kwa kutimiza miaka 50 ya Utawa katika Shirika la Wateresiari Wakapuchini wa Tamilia Takatifu,-TC, iliyofanyika katika Viwanja vya Shule ya Luis Amigo Tungi, Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Askofu Musomba alisema kwamba Watawa wengi siku hizi wanapenda kutumia mitandao kutazama vitu ambavyo havina maadili mazuri.
“Muda mwingi wanachati habari za mitandaoni kupiga mapicha mitandaoni. Hii siyo sahihi. Unakuwa bize na mambo ya mitandaoni, unaacha kazi uliyoitiwa na Mungu kuwaongoza watu….Waongozeni Waamini vizuri na kuwapa maadili ya Kristo sio kuwapotosho Waamini katika mitandao,”alisema Askofu Musomba.
Askofu Musomba alisema kwamba Watawa hao wameitwa na Mungu ili muje kuwatumikia waamini na kuwaongoza, kwa kuwapatia mafundisho mazuri na yenye maadili mema.
“Watawa mnatakiwa muwe mfano mzuri katika macho ya watu, Mtawa usiwe kero kwa Waamini …. mnatakiwa kuwasikiliza Waamini na kutatua shida zao,”aliongeza kusema Askofu Musomba.
Kwa Upande wake, Askofu wa Jimbo Katoliki la Kahama Mhashamu Christopher Ndizeye Nkoronko (pichani), alisema kuwa Utawa siyo igizo, bali ni sehemu ya maisha Matakatifu.
“Umechaguliwa na Mungu uje umtumikie, mtumikie kwa uaminifu,”alisema Askofu Nkoronko, akiwapongeza Wanashirika hao na Wana Jubilei miaka 25 na 50 kwa utume wao.
Naye Mama Mkuu wa Shirika hilo, Sista Pelagie Matilde aliwashukuru Maskofu wa Jimbo Kuu Katoliki la Der es Salaam na Askofu wa Jimbo Katoliki la Kahama kwa kushiriki sherehe hiyo.
Aliwaomba Wazazi wenye watoto wa kike, wawapeleke kwenye shirika hilo, wajiunge katika kazi ya Utume.
Mama Mkuu huyo aliwashukuru Masista wote wa shirika hilo kwa kumuamini awaongoze akwiasihi wazidi kushirikiana wka kazi zote Ili shirika lizidi kusonga mbele.
Akitoa salamu za Wanajubilei hao, kwa niaba ya wenzake, Sista Lucina Escudero aliyetimiza miaka 50 ya Utawa, alisemwa wanamshukuru Mama Mkuu kwa kukubali kuwafanyia sherehe hiyo.