DAR ES SALAAM
Na Mathayo Kijazi
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Sana Jude Thaddaeus Ruwa’ichi amewataka Wakristo kuliombea Taifa la Tanzania ambalo ndani yake lina changamoto, ili zisiwapeleke wasikostahili.
Aliyasema hayo hivi karibuni wakati wa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Waseminari wa Zamani, iliyokwenda sanjari na Sikukuu ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, katika Parokia ya Bikira Maria wa Fatima – Msimbazi, jimboni humo.
“Tunapokutana leo kama ‘Former Seminarians’, basi kwa niaba ya Kanisa lote nchini Tanzania, na Taifa lote la Tanzania, tumwombe Mungu ili aibariki Nchi yetu, aihurumie Nchi yetu ambayo inazo changamoto zake ambazo siyo haba. Atusaidie, kusudi hizo changamoto tunazozikabili, zisije zikatupeleka tusikostahili,” alisema Askofu Mkuu Ruwa’ichi.
Sambamba na hayo, Waseminari hao wa Zamani (maarufu Former Seminarians), walitakiwa kufahamu kwamba wao siyo tu Waseminari wa Zamani, bali wanasimama pia kama Mapadri wa uraiani, kwani wana jukumu zito la kusimamia imani na maadili katika jamii.
“Tumezoea kuwaita Waseminari wa Zamani, lakini mimi leo naomba niboreshe kidogo, ninyi ni Mapadri wa Uraiani, na hawa wengine ni Mapadri wa Altareni,” alisema Askofu Mkuu.
Aliwasihi kumshukuru Mungu kwa zawadi ya Mama wa Mwokozi, ambaye ni Mwombezi, na pia Mtetezi wa maisha yao.
Pia, aliwasisitiza kufahamu kwamba Mungu ni wa huruma, wa hisani, na ni Mungu Baba mwema, kwani hakuruhusu dhambi ya mwanadamu iwe na kauli ya mwisho, bali kauli ya mwisho ni huruma ya Mungu, na zawadi ya ukombozi.
Pamoja na mambo mengine, Askofu Mkuu aliwapongeza kwa ukarimu wao, pamoja na kukubali kutekeleza jukumu lao kama Waseminari wa Zamani.
Aliwataka Waamini kuendelea kuishi maisha ya unyenyekevu na yenye kumpendeza Mungu, kwani yeyote anayetenda dhambi, amekubali kuwa mtupu na galasha katika maisha yake.
“Mwanadamu ambaye ameshajichanganya, anapoulizwa na Mungu uko wapi, akasema ‘nimejificha, maana niko uchi. Sasa tutambue kwamba mwanadamu anaposema niko uchi, ni zaidi ya utupu wa kutokuwa na nguo, ni utupu unaomgusa katika undani wake zaidi, ni utupu wa kukosa neema…
“Kwa wale wanaocheza karata, tunasema ni galasha. Kwa hiyo ni utupu wa kuwa galasha. Na kila mwanadamu anapotenda dhambi, anakubali kuwa galasha ambalo haliwezi kula mchezo. Na kama galasha, Adamu ni kigeugeu, kwa sababu anapoulizwa kwamba umejuaje kuwa uko mtupu, badala ya kunyenyekea na kusema, eeh Mungu nisamehe, anatafuta kichaka cha kujificha, anatafuta wa kumlaumu,” alisema Askofu Mkuu Ruwa’ichi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Waseminari wa Zamani, Jaji Mstaafu Bernard Luanda, alimshukuru Askofu Mkuu Ruwa’ichi kwa kuadhimisha Misa hiyo Takatifu.
Aidha, Mwenyekiti huyo aliwashukuru Waseminari wenzake wote wa Zamani walioshiriki kwa wingi katika Adhimisho hilo la Misa Takatifu.
Kwa mujibu wa Mhazini wa Waseminari wa Zamani (Former Seminarians), CPA Julius Rutabanja, mwaka huu wamefanikiwa kutoa ahadi ya kiasi cha fedha Shilingi 223,310,000/=, kwa ajili ya kumpatia Askofu Mkuu wa Jimbo hilo, ili kusaidia kuwasomesha Mafrateri waliopo katika Seminari Kuu.