MOROGORO
Na Mwandishi wetu
Katibu wa Askofu wa Jimbo Katoliki la Morogoro, Padri Boniface Mliga amewataka Watawa wa Kike wa Shirika la Maria Imakulata (SMI), walioweka Nadhiri za Daima kuona fahari kwa kutoa maisha yao kama Sadaka ili kumtumikia Mungu.
Padri Mliga alisema hayo hivi karibuni wakati wa Adhimishi la Misa Takatifu ya Nadhiri za Daima kwa Masista wa Shirika la Maria Imakulata –SMI, iliyofanyika katika Parokia ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli –Kihonda, jimboni Morogoro.
“Ndugu zangu, inawapasa kutambua Agano ni makubaliano, kwani hata Wana Waisraeli waliweka Agano na Mungu, nanyi mnaweka Agano kati ya Mungu na Kanisa, la kumtumikia kama kiumbe chake mwenyewe, huku mkitoa maisha yenu kama zawadi na sadaka kwake,”alisema Padri Mliga.
Aidha, aliwataka Masista hao kutenda mema na kumtumikia Kristo siku zote za misha yao, akiwakumbusha kuwa kila mtu anayehitaji kumfuata Yesu, lazima aikane nafsi yake kwa kuachana na mambo ya kidunia, na kumfuata.
Padri Mliga aliendelea kusema, “Ukiikana nafsi yako, pia unatakiwa ubebe msalaba wako.”
Aliendelea kusema kwamba kama mtu amechagua kumfuata Kristo na kukubali, yampasa kujiuliza, je, ana uwezo huo wa kuacha mambo yote?
“Kwani wasije kukubali kuacha ya ulimwengu, na baadaye wakashindwa na wakakata tamaa, kwani maisha ya kumfata Kristo, si maisha ya kimasihara,”alisema Padri Mliga.
Kwa mujibu wa Padri Mliga, Kristo alichekwa na kudhihakiwa na baadhi ya watu, lakini hakukata tamaa na badala yake, aliendeleza kazi yake ya kuhubiri Injili kwa mataifa, na mwishowe aliteswa na kukubali kufa msalabani, ili atimize agano lililoandikwa hapo kale.
Alitoa wito kwa Masista wamkimbilie Mungu siku zote za maisha yao, kwa kupokea msalaba na kuubeba kwa furaha na si kwa huzuni, ili waweze kukidhi vigezo vya kuwa wafuasi wa Kristo.
Mbali na hayo, Padri Mliga aliwataka watawa hao wasitazame walipotoka wala kukata tamaa, bali watazame Msalaba wa Kristo kwa imani na matumaini makubwa, kwa kujitoa zaidi, wakiomba Mungu waendelee kuubeba Msalaba wa Kristo, kwa amani na upendo.