VATICAN CITY, Vatican
Baba Mtakatifu Fransisko amekemea vitendo vya kuwanyanyasa watoto, ikiwemo kuwanyima haki ya kupata elimu.
Baba Mtakatifu alisema hayo hivi karibuni alipokutana na Chama cha Waalimu wa Kikatoliki cha Italia (Italian Association of Catholic Teachers: AIMC), Umoja wa Waalimu wa Kikatoliki wa Italia, Wasimamizi, Waelimishaji, Wakufunzi (UCIID), pamoja na Chama cha Wazazi wa Shule za Kikatoliki (AGESC).
Alisema kwamba ni furaha yake kuona Maadhimisho ya Mashirika yao, Miaka 80 ya Chama cha Waalimu Wakatoliki wa Italia na Umoja wa Waalimu wa Kikatoliki wa Italia, Wasimamizi, Waelimishaji, Wakufunzi, na Miaka 50 ya Umoja wa Wazazi wa Shule za Kikatoliki.
Aidha, Baba Mtakatifu alibainisha kwamba anaumia kuona watoto ambao hawajasoma na kwenda kazini, mara nyingi wanatumikishwa au kwenda kutafuta chakula au vitu vya kuuza katika mazingira yasiyoridhisha.
“Ninaumia kuona watoto ambao hawajasoma na kwenda kazini,mara nyingi wanatumikishwa au kwenda kutafuta chakula, au vitu vya kuuza mahali palipo na takataka,” alisema Baba Mtakatifu.
Sambamba na hayo, Papa aliongeza, “Ni fursa nzuri ya kusherehekea pamoja na kukumbuka historia yao na kutazama siku zijazo. Zoezi hili, harakati hii kati ya mizizi - kumbukumbu - na matunda - matokeo - ni msingi wa kujitolea katika uwanja wa elimu.”
Aliwaeleza kuwa kama mwalimu anayeingia katika ulimwengu wa wanafunzi wake, Mungu anachagua kuishi kati ya wanadamu ili kufundisha kupitia lugha ya uzima na upendo.
Aliongeza kwamba hiyo inawaita kwenye ufundishaji unaothamini mambo muhimu, na kuweka unyenyekevu, ukarimu na huruma katikati, na kwamba ualimu ulio na mbali na watu, haufai, na hausaidii.
Baba Mtakatifu alibainisha kwamba ualimu huo ni mwaliko wa kutambua utu wa kila mtu, kuanzia wale waliotupwa na walio pembezoni, jinsi wachungaji walivyotendewa miaka elfu mbili iliyopita, na kufahamu thamani ya kila awamu ya maisha, ikiwa ni pamoja na utoto.
“Matumaini yake si ya kipuuzi, yamejikita katika uhalisia, yakiungwa mkono na imani kwamba kila juhudi ya elimu ina thamani, na kwamba kila mtu ana utu na wito unaostahili kukuzwa,”alisema Baba Mtakatifu Fransisko na kuongeza,
“Matumaini ndiyo injini inayomuunga mkono mwalimu katika kujitolea kwake kila siku, hata katika shida na kushindwa. Lakini tunawezaje kupoteza tumaini na kumwilisha kila siku? Kuweka mtazamo kwa Yesu, mwalimu na msindikizaji wetu njiani. Hii inatuwezesha kuwa kweli Mahujaji wa Matumaini.”
Aliwasisitiza kwamba wasisahau kamwe walikotoka, lakini wasitembee kwa kuinamisha vichwa chini kwa majuto, wakijutia nyakati nzuri zilizopita, badala yake wafikirie juu ya sasa ya shule ambayo ni mustakabali wa jamii, ikikabiliana na mabadiliko ya nyakati.