DAR ES SALAAM
Na Mathayo Kijazi
Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam limepata Parokia mpya tatu, na hivyo kufikisha idadi ya Parokia 170 na kulifanya jimbo hilo kuwa na parokia nyingi ikilinganishwa na majimbo ya Kanisa Katoliki nchini.
Parokia mpya ambazo awali zilikuwa Parokia Teule, ni Parokia ya Mtakatifu Karoli Lwanga - Mwongozo, inayozaliwa kutoka Parokia ya Gezaulole, ambayo Paroko wake ni Padri Miki Mbuku, Parokia ya Mtakatifu Stephano - Makurunge, inayozaliwa kutoka Parokia ya Kiluvya, ambayo Paroko wake ni Padri Amani Shirima, na Parokia ya Bangulo, iliyozaliwa na Parokia ya Mt. Padri Pio, Ulongoni, ambayo Paroko wake ni Padri Daniel Matungwa.
Hayo yalifanywa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu hilo, Mhashamu Sana Jude Thaddaeus Ruwa’ichi OFMCap, wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya kutoa Daraja Takatifu ya Ushemasi kwa Mafrateri 11 katika Parokia ya Roho Mtakatifu – Kitunda, jimboni humo.
Mashemasi hao wapya waliopokea Daraja hiyo Takatifu, ni Shemasi Benjamin Maganga Bundala, Shemasi Francisco Benedicto Chabili, Shemasi George Arnold Mbago, Shemasi Josephat Wilson Mlacha, Shemasi Emmanuel Lazaro Mbuya, Shemasi Gabriel Victor Kihondo, Shemasi Richard Osvaldo Villar Zorilla na Shemasi Mark Clement Xavier, wote wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.
Wengine ni Shemasi Christian Leonard Mlela- MI, Shemasi Charles Msabila- MI, na Shemasi Kanuth Martin Nyoni -MI, wote wa Shirika la Wahudumu wa Wagonjwa, yaani Wakamiliani.
Askofu Mkuu Ruwa’ichi alifanya mabadiliko ya Mapadri katika baadhi ya Parokia za Jimbo Kuu hilo, ambapo Padri Charles Kayumba amekuwa Paroko wa Parokia ya Misugusugu, Padri Venance Shiganga Paroko Msaidizi wa Parokia ya Kibiti; Padri Canisius Hali, Paroko Msaidizi wa Parokia ya Muungano; na Padri Baltazar Mbwale amekuwa Paroko Msaidizi wa Parokia ya Makongo Juu.
Katika nasaha zake, Mchungaji Mkuu huyo wa Jimbo aliwahimiza Mapadri hao kuendelea kujituma na kuwajibika ipasavyo katika maeneo yao wanayofanyia kazi za kitume, ili waweze kutekeleza vyema Utume wao.
Awali, katika homilia yake Askofu Msaidizi wa Jimbo hilo, Mhashamu Stephano Musomba aliwataka Mashemasi hao wapya kutambua kwamba kwenye sehemu ya Liturujia, wana nafasi kubwa, hivyo ni wajibu wao kutangaza Habari Njema kama walivyoagizwa.
“Lakini Shemasi, kwenye sehemu ya Liturujia, una nafasi kubwa vile vile. Kuna sehemu kuu tatu zinazoongea na wewe mwenyewe unazitumia. Lakini hizo ni kwa ajili ya Tafakari la Maisha ya Kikristo katika Liturujia…
“Sehemu ya kwanza, ukiwa kwenye Misa, Shemasi wewe ni wa kutangaza Habari Njema, unapokuwa untangaza Habari Njema, furahia sasa, tangaza kwa umakini Habari Njema kwa watu, na unaposoma hivyo, usome maisha yako ya Kikristo na Ukuhani wako,” alisema Askofu Musomba.
Aliongeza kuwa hata wanapotamka juu ya kutakiana amani, wanatakiwa kuhakikisha kwamba hata wao wenyewe wanakuwa na amani hiyo ndani ya mioyo yao, kwani huo ndio Umisionari.
“Unachokitamka, ‘tutakiane amani’, au ‘mpeane amani’, basi kitoke moyoni mwako nayo amani hiyo, lakini ya tatu, nendeni na amani, unapomalizia misa, unaposema nendeni na amani, inamaanisha unatumwa kutangaza Habari Njema, unawatuma watu watangaze Habari Njema, na wewe mwenyewe unatakiwa kutangaza Habari Njema, lakini hilo lote linaonyesha Umisionari, ambalo vile vile ni dhamiri ya Kanisa, Kanisa la Kimisionari,” alisema Askofu Msaidizi Musomba.
Vile vile, Askofu Msaidizi Musomba alibainisha kwamba Waamini wanapomtangaza Yesu Kristo, hawatakiwi kuwa kama wanakwenda sokoni, bali wanatakiwa kuwashirikisha wengine yale wanayoyaishi wao.
Aliwasisitiza Mashemasi hao wapya kutimiza majukumu yao, wakifahamu kwamba sasa wamepokea Daraja Takatifu, kwani ndani ya Daraja hilo, kuna changamoto zake.