DAR ES SALAAM
Na Celina Matuja
Madaktari na Wauguzi Wakatoliki nchini wametakiwa kuzingatia mambo muhimu ili waweze kutoa huduma kadri ya mwelekeo wa Bwana Yesu Kristo.
Madaktari na wauguzi hao wameaswa pia kutumia muda wao kusali ili kuomba mwongozo wa Mungu katika huduma zao kwa wagonjwa.
Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katopliki la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu ametoa maagizo hayo katika salamu kwenye Semina ya Madaktari na Wauguzi Wakatoliki, iliyoandaliwa na Jimbo hilo, iliyofanyika katika Parokia ya Kristo Mfalme, Tabata.
Semina hiyo ilikwenda sanjari na Adhimisho la Misa Takatifu, ambapo katika homilia yake aliwataka madaktari hao, kufuata mfano wa Mtakatifu Paulo aliyewaua na kuwatesa Wakristo, lakini aliongoka, hivyo wao nao wahakikishe wanaleta uponyaji kwa wagonjwa na kuihubiri Injili.
“Kutokana na Ufunuo wa Kristo mwenyewe, Mtakatrifu Paulo alifanya kazi kubwa na nyingi kufundisha habari njema za Yesu Kristo, baada ya kuongoka. Sisi pia tuongoke kama Paulo, hivyo nawapatia ‘take home’ ili mpate kuzingatia katika kazi yenu,” alisema Askofu Mchamungu.
Askofu awapa Madaktari ‘vitendea kazi’:
Moja ya mambo ambayo walitakiwa kuzingatia wanataaluma hao ni kusali na kuomba maongozi ya Mungu, kwa sababu kazi yao inagusa moja kwa moja uumbaji na uhai.
Kuwahi kazini na kuwajibika kwa wagonjwa kwa moyo wa upendo na furaha, kuwasikiliza wagonjwa kwa umakini ili kuelewa shida zao kiafya ili kutoa matibabu sahihi.
Kuepuka uzembe kazini na kuwa makini, kwa kufanya kazi kwa kujiamini ili kumpa mgonjwa tumaini la kupona ama kupata ahueni, kupenda kazi na kuitenda kwa furaha kwa kuwa ni wito wao.
Kutoa huduma bila kudai chochote kwa mgonjwa, na kutumia lugha nzuri, ikiwemo kutunza siri za mgonjwa.
Kutokuwa na mahusiano ya kimapenzi na wagonjwa wao, kuwahudumia kwa karibu wagonjwa wanaohitaji uangalizi makini, kama wanaoongezewa damu, maji mwilini, na hasa nyakati za usiku.
Aidha, Askofu Mchamungu aliwataka kusoma na kujiendeleza zaidi ili kuwa na ujuzi mkubwa kwa kusoma vitabu mbalimbili vinavyohusu taaluma yao.
Padri Mosha: Fanyeni kazi bila kinyongo:
Kwa upande wake, Padri Dakta Joseph Mosha, Paroko wa Parokia ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alikemea baadhi ya tabia za Wauguzi na Madaktari kutotoa huduma kwa moyo na ari kwa wagonjwa.
Aliwataka kutambua kwamba wao ni washirikishwa wa kazi ya utendaji wa Mwanadamu kutoka kwa Mungu, na kutokuondoa nafasi ya Mungu katika maisha ya Mwanadamu.
Padri Mosha alisema kuwa Maandiko, kitabu cha mwanzo 1:26 akinaeleza kwamba “Sisi Binadamu tumeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu,”, akiwataka Wanataaluma hao kutambua kwamba kila wanapomwona mgonjwa, watambue kuwa ni sura na mfano wa Mungu.
Alisema kwamba maisha huanza kwenye familia, hivyo hawana budi kutenda kwa misingi ya Mwenyezi Mungu pasipo kufuata ile siasa ya uhuru wa kufanya lolote, ambao una upotofu.
Padri Kessy: Tendeni kazi kwa upendo:
Naye Padri Prosper Kessy Gombera wa Kituo cha Hija cha San Damiano Msimbazi, aliwakumbusha Madaktari na Wauguzi hao, kutenda kazi zao kuzingatia huruma na upendo.
Aidha, aliongeza kuwa itamsaidia sana mgonjwa iwapo atapokea huruma na upendo, bila kusahau kumhudumia kwa hadhi njema, na hisia ya utu.
Kwamba kuna baadhi ya watu wamepoteza hisia, wanaona kila jambo ni sawa, wamezoea kifo, hata wakimwona mgonjwa yu mahututi wanaona kama ni mfu, wasikubali iwatawale, kwani Mungu amempa kila mtu hisia na huruma.
Jambo lingine la kuzingatia ni kuigeuza kazi kuwa sala,kwa maana ya kusali kabla ya kuwahudumia wagonjwa na kuifanya kazi hiyo kwa umakini, ndipo inapogeuka kuwa injili na sala.
Aliwataka pia kuvumilia kutokana na matukano mbali mbali, ila kusimama na msimamo wa kuutafuta utakatifu na uaminifu kwa kuheshimu uhai mwanzo mpaka mwisho, kwa kukemea maovu mamlaka waliyopewa wasikubali kushiriki katika dhambi.
Akinukuu Maandiko Matakatifu Matayo 28:16 – 20: Nimepewa mamlaka yote Duniani na Mbinguni enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi mkiwabatiza kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu.