MWANZA
Na Paul Mabuga
Zamani ukitaka kuijua jamii tunayoisha hapa Bongoland, ilikuwa unatakiwa kutafuta kile kilichomo ndani ya vyombo vya habari, lakini kwa sasa siyo tena kwani huko yamejaa maisha ya kuigiza, bali unatakiwa kupanda daladala na hutanyimwa tafsiri ya namna tunayoishi.
Ndani ya daladala utasikia hapendwi mtu kwa kuwa huko mitaani ndiyo mtindo wa maisha uliopo kwami kinachotawala upendo ni pesa.
Utajua jamii inahalalisha udhalimu kwa kuwa kitanda hakizai haramu na tukiandaa vikao vya harusi vinaendelea mwaka mzima, lakini mafunzo ya wanandoa tunatamani hata yawe wiki mbili!
Ukizama kwenye vyombo vya habari utaona kila mtu anajua, anakosoa na hata anajadili masuala ambayo yapo juu ya upeo wake, ni kama vile wote wa shahada.
Kila mtu anaonesha maisha ya kuigiza kuliko hali halisi na ukiwatathmini watu kwa yale unayosoma, kusikia na kutazama unaweza kushindia matango pori na kupata uwelewa usio sahihi.
Unapanda daladala kutoka Buswelu kwenda Kemondo katika Jiji la Mwanza, dereva ndiye DJ, na anaweka muziki anaoutaka huku sauti ikiwa juu, abiria wanasikilizana kwa shida, hasa kwa kuwa kila viti viwili, vitatu ni kama Bunge kamili kwani kila seti ina mada ya mjadala inayoendelea nao.
Wimbo ulioingia zamu ya kupigwa unashusha kutokana na aina ya beti zake ambazo hazina staha kwa waungwana, abiria wanalalamika kwa sauti kubwa na maneno ya beti na wanaomba dereva apunguze sauti, na mzee mmoja anatasema, “angalieni [dereva] alivyonyoa kiduku, kichwa kimekuwa kama mjusi wa rangi!” Dereva anazima kabisa muziki kwa hasira, ni kama abiria wanaifurahia hali ile.
Kiti cha nyuma ni kama mama na wenzake walikuwa wakisubiri muda huo, kwa maneno yake anaonekana kama ni mjasiriamali mdogo na anawaambia wenzake juu ya mumewe ambaye ameondoka kwake na kwenda kukaa kimada kwa mama ntilie.
“Yaani alianza kuwa anachukua nguo moja moja anakwenda na anarudi, na nikaja kugundua hilo na wakati nafikiri nini cha kufanya akaja ananiambia ana safari na anataka kuchukua begi ambalo nilinunua mimi, nikamwambia we nenda ulikotamani na vitu vyangu pamoja na nguo nilizokununulia acha,’’ anasema Mama yule.
Wenzake wawili katika mjadala huo, wanaonekana kumuunga mkono na wanasema wa namna hiyo hafai!
Inabidi kushangaa, yaani inaonekana kama vile kuachana ni kama kwenda kununua parachichi Manzese na unajihoji hivi hawa huwa hawangalii “Nyumba Amninifu” ya Tumaini TV! Kwa hakika wakiangalia wanaweza kubadili fikra.
“Asikubabaishe huyo, kwa mama ntilie kafuata mapochopocho, akichoka aende zake akafie mbali, hawa ndiyo wale tunaosema wana tabia kama kipepeo, wanatoka ua moja hadi jingine!” kwa lugha ya mjini wanasema walikuwa wanamjaza.
Ni wazi huyu mama hakutayarisha kumtambua mwenza wake, ikiwa ni pamoja na kufahamu wasifu wake wa ndani na nje na kuvitawala vichocheo vinavyomuongoza, [male instincts].
Angepata mafundisho ya ndoa yanayoakisi hali halisi [Biological response] na siyo nadharia za kufikirika bila shaka angeweza kuimudu hali hiyo na ndoa ingeokolewa na hasa kama ingekuwa Takatifu.
Lakini pia ni tatizo hata kwa mwanaume! kwani inaonekana ameingia katika taasisi hiyo takatifu kama vile alikuwa anakwenda disco. Tena diisco toto lile linalopigwa mchana na saa 12 jioni mwisho ili watoto warudi nyumbani.
Kwa bahati mbaya kamati za sherehe za harusi ambazo hudumu hata kwa maandalizi ya mwaka mzima, huwa hazioni kama mafunzo kwa wanandoa ni jambo muhimu na hata halipangiwi bajeti.
Ukienda kwa kile kinachoiwa kitchen party huko mitaani kwetu, na ukasikia wanachokisema ‘masomo’, kama hujapata kiu kwenye baridi kali basi wewe ni mtu tofauti.
Tunaigiza maisha kwa sababu, vijana hawatayarishwi vilivyo katika kuishi kwenye taasisi ya ndoa. Kuna jamaa wameoana miaka mingi na bahati nzuri baada ya kulia kwa kipindi kirefu sasa wamepata mtoto!
Kuoneshwa hawjatayarishwa vya kutosha, hata jina walilompa mtoto wamelitoa kwenye filamu ya katuni. Na kanisani hawakosi kila Dominika.
Mama hajui hata kunyonyesha anategemea aangalie kwenye mitandao, matokeo yake mtoto alimaliza siku kadhaa bila kushiba kwa kuwa alikuwa hawekwi mkao wa kunyonya.
Mtoto alikaribia kupata ulemavu kwa kuwa kwenye mitandao wanakataza kumrusha mtoto atakuwa taahira na alikuwa hata hanyooshwi viungo. Ni hatari!
Yaani vijana wanaojitayarishwa kwa ajili ya ndoa wanataka waishi kama wanayoyaona kwenye runinga, bila kujua kwamba sehemu kubwa wa yale wanayotazama ni maigizo.
Matokeo yake wanakosa kujitambua na umakini na hivyo wanakutana na mazingira yanayowataka kuishi maisha halisi matokeo yake wanakwama.
Wanataka waishi kama wasanii wa muziki ambao nao pia hawaishi maisha yao halisi, kwani kilichopo kwenye vyombo vya habari ni tofauti na yale yaliyopo kwenye familia zao.
Wanapata taarifa ambazo zimepakwa rangi za kupendeza kuliko hali halisi.
Na kimsingi hata wabunge na viongozi wengine wangekuwa wanapanda daladala wangetuwakilisha vilivyo.