DAR ES SALAAM
Na Deus Helandogo
Raga, maarufu kama Rugby, ni mchezo ulioanzishwa mwanzoni mwa karne ya 19 katika Mataifa ya Uingereza na Marekani, na una namna nyingi ya kuchezwa, kama vile kwa kutumia mikono pamoja na miguu, huhusisha wachezaji 15 kwa kila upande wa timu shindani
Mchezo huu ni maarufu sana kwenye Mataifa ambayo yana shabihiana kiutamaduni na Taifa la Uingereza, ikiwemo Umoja wa Jumuiya ya Madola kama vile Austalia, Kenya, Afrika Kusini, Canada na Namibia, kwenye baadhi ya Mataifa mchezo huu ni mchezo ambao una sifa ya kuwa mchezo wa Kitaifa
Raga ilianza pamoja na mchezo wa mpira wa miguu, na baadae sheria za michezo hiyo miwili zikatofautiana na kuwa michezo miwili tofauti. Raga ikabaki ikichezwa kwa kutumia mikono na miguu, huku mpira wa miguu akaanza kuchezwa kwa kutumia miguu tu
Mpira unaotumika kuchezea Raga umetengenezwa kwa mfumo wa umbo mviringo, mithili ya yai unaoweza kubebeka na kukimbia nao, ukiwa mkononi, na inapotokea kuurusha haumsumbi mchezaji huurusha kwa haraka
Takwimu zinaonesha kuwa mchezo huu umezidi kukua kwa kasi ulimwenguni kwani huchezwa na kila jinsia na umri wowote. Mwaka 2023, ilithibitika kuwa zaidi ya watu milioni kumi (10) hucheza mchezo huu duniani kote.
Na katika kipindi hicho, watu milioni 8.4 walikuwa wamesajiliwa na Chama cha mchezo huo duniani ambacho kifupi chake ni (IRFB), na Mataifa 116 yana vyama vinavyoongoza mchezo wa Raga duniani kote.
Kuanzia miaka ya 1863, mchezo huu ulikuwa unachezwa kama ridhaa kwa kujifurahisha zaidi, na siyo kazi rasmi ambayo ilikuwa na maslahi, mpaka ilipofika mwaka 1995 ndipo sheria mpya zilitungwa na kuurasimisha mchezo huu ambapo ulianza kulipa wachezaji, makocha na waamuzi, hivyo watu wakaanza kunufaika na mchezo wenyewe.
Mchezo wa kwanza wa Raga wa Kimataifa ulichezwa mnamo 27 Machi, 1871 kati ya Scotland na Uingereza huko Edinburgh, Scotland ilishinda mchezo huo kwa bao moja, hadi kufikia mwaka 1881, ambapo Ireland na Wales zilikuwa na timu za uwakilishi katika mashindano ya Kimataifa
Mashindano muhimu zaidi katika mchezo wa Raga ni Kombe la Dunia la Raga, mashindano ya wanaume, ambayo yamekuwa yakifanyika kila baada ya miaka minne tangu kuzinduliwa kwa michuano hiyo mnamo mwaka 1987.
Afrika Kusini ndiyo Mabingwa watetezi baada ya kuifunga New Zealand 11-12 katika fainali ya Kombe la dunia la Raga 2023 nchini Ufaransa.
Lakini katika historia, Afrika Kusini ina idadi kubwa zaidi ya kushinda makombe, kwani imeshinda Kombe la Dunia mara nne (1995, 2007, 2019 na 2023).
New Zealand imeshinda taji hilo mara tatu (1987, 2011 na 2015); Australia imeshinda mara mbili (1991 na 1999); na Uingereza mara moja (2003).
England ndio timu pekee kutoka Kaskazini mwa Bara la Ulaya ambayo imeshinda Kombe la dunia la Raga
Kombe la Dunia la Raga limeendelea kukua tangu kuanzishwa kwake mwaka 1987 kwani mashindano ya kwanza, ambayo timu 16 zilishiriki ilionyeshwa kwa nchi 17, na jumla ya watazamaji milioni 230 wa televisheni, walishuhudia. Mauzo ya tiketi wakati wa hatua za bwawa na fainali za mashindano hayo, yalikuwa chini ya milioni Kombe la Dunia la mwaka 2007 lililoshindaniwa na nchi 94, na mauzo ya tiketi yalikuwa 3,850,000.
DAR ES SALAAM
Na Mwandishi wetu
Mshambuliaji wa Yanga, Kennedy Musonda, amefunguka juu ya ukweli wa maisha yake binafsi, huku akiweka wazi kuwa malengo yake ya kwanza yalikuwa ni kuwa Mhandisi, lakini mwisho wa siku mambo hayakwenda vile ambavyo alikuwa anataka.
Nyota huyo (pichani) ambaye anamudu uwanjani kwenye nafasi ya mshambuliaji wa kati na pembeni alisema kuwa mwanzo alikuwa anataka kuwa Mhandisi kabla ya soka kummbadilishia mwelekeo na hatimaye akaacha kile alichokuwa anatamani kukifanya.
Musonda alisema kuwa alitakiwa kwenda chuo kwa ajili ya kusomea Uhandisi, lakini soka lilimbadilishia mfumo wa maisha na sasa amekuwa mfumania nyavu uwanjani.
“Mwanzo nilitakiwa kwenda chuo kusomea Usanifu wa Majengo, lakini mpira ulinipa mwelekeo mwingine wa maisha ndiyo kama hivi kwa sasa, nachezea Yanga”, alisema Musonda.
Kuhusu kazi yake na majukumu yake uwanjani kama mchezaji sasa wa Yanga, Musonda amepanga kufunga mabao zaidi na kuisaidia Yanga kushinda kila mchezo wake msimu huu.
Lakini, kwa upande mwingine Musonda alifunguka juu ya ugumu anaoupata wa namba tangu asajiliwe ndani ya Yanga huku akiweka wazi kuwa juu ya mkanganyiko wa mashabiki wake, wanaojiuliza juu ya kwa nini hafunguki akiwa na Yanga huku kwenye timu yake ya Taifa akifunga.
Musonda alisema kuwa kwenye timu yake ya Taifa, anapata nafasi sana na ndiyo maana anafunga sana, lakini kwa upande wa klabu imekuwa tofauti, kwani hapati nafasi sana. Mpaka sasa amecheza mara 20 pekee, hali inayopelekea kupata changamoto ya kupachika mabao.
DAR ES SALAAM
Na Mwandishi wetu
Wakati wa kufanyika kwa droo na hata baada ya kuanza kwa michuano ya Afrika ambayo Simba na Yanga wanashindania Ubingwa, mashabiki wengi na wadau wa soka walikuwa na maoni tofauti juu ya timu zao wakizichambua katika viwango vya juu, lakini kwa sasa hali imekuwa tofauti, kwani maji na unga vimeanza kujitenga.
Mpaka sasa bado mambo hayajaenda sawa kwa klabu za Tanzania ambazo zinashindana katika michuano hiyo ya Afrika msimu huu, tofauti na ilivyotarajiwa.
Simba inashiriki Kombe la Shirikisho kutokana na kushika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi msimu uliopita, huku watani zao klabu ya soka ya Yanga ikishiriki michuano ya Klabu Bingwa Afrika, na hii ni baada ya kuwa Mabingwa msimu iliopita katika Ligi Kuu Soka Tanzania Bara.
Mwenyekiti wa zamani wa klabu ya soka ya Simba, Ismail Aden Rage, aliweka wazi kuwa klabu ya soka ya Yanga bado hawajawa katika kiwango bora kama walivyokuwa katika misimu miwili ya nyuma na hilo limechangia kuwepo kwenye nafasi waliyopo sasa.
Rage alisema na kuweka wazi mara baada ya kufanya tathmini yake katika mchezo wao uliopita waliocheza katika dimba la Benjamini Mkapa, akidai kuwa walipata nafasi nyingi za kufunga, lakini walishindwa kuzitumia ipasavyo dhidi ya wapinzani wao TP Mazembe.
Alisema kuwa bado Yanga wana safu mbovu ya ushambuliaji ambayo inawasababisha washindwe kupata matokeo chanya kwenye mechi zake msimu huu.
Yanga ilipata ushinda wa mabao 3-1 dhidi ya TP Mazembe katika mechi ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, iliyochezwa Jumamosi, Januari 4 mwaka huu.
Kuhusu Simba, Rage alisema kuwa, bado inajitafuta, japokuwa imefanya vyema katika michezo yake mitatu kati ya minne, ambayo mpaka sasa imeshacheza katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho, wakipata ushindi huku wakifungwa mchezo mmoja.
Watanzania wengi bado hawana matumaini ya dhati juu ya klabu hizo kutokana na nafasi walizokuwa nazo kwenye misimamo ya makundi yao, huku kwa sasa ni mahesabu ya vidole tu ndiyo yaliyobaki.
Yanga kwa kuchechemea katika michezo minne, ameshinda mchezo mmoja, akipata sare mchezo mmoja huku akifungwa michezo miwili, na amekusanya alama nne, akishika nafasi ya tatu katika msimamo wa kundi lake michuano ya Klabu Bingwa Afrika, hatua ya makundi.
Simba nayo ni kama wanaingia wanatoka, kwani katika michezo minne, ameshinda michezo mitatu, akifungwa mchezo mmoja, akijikusanyia alama tisa, akishika nafasi ya pili kwenye hatua ya makundi katika michuano ya Kombe la Shirikisho.
Timu zote hizo zinatarajiwa kutupa karata zao nyingine katika viwanja vya ugenini January 12 ambapo klabu ya Simba watawafuata Bravos ya Angola huku klabu ya soka ya Yanga ikiwafuata Al Hillal ya kutokea kule Sudan.
Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu akiwa katika picha ya pamoja na Kamati Tendaji ya Parokia ya Mtakatifu Cesilia, Kisarawe II, jimboni humo. Kulia kwa Askofu ni Paroko wa Parokia hiyo, Padri Roger Kamuzinzi, na kushoto ni Paroko Msaidizi. (Picha na Yohana Kasosi)
Waamini wa Parokia ya Bikira Mama wa Kanisa, Goba, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam wakiwa kanisani wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Sikukuu ya Krismas iliyoadhimishwa hapo hivi karibuni.
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Sana Jude Thaddaeus Ruwa’ichi, akibariki matoleo wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Noeli katika Parokia ya Mtakatifu Agustino – Salasala. Kushoto ni Paroko wa Parokia hiyo, Padri Peter Assenga. (Picha na Mathayo Kijazi)
Padri Denis Kunambi, Paroko wa Parokia ya Roho Mtakatifu Segerea, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam akikabidhi vitendea kazi kwa Kamati Tendaji ya Kigango cha Kuzaliwa Bikira Maria, Kisukuru, Parokia ya Roho Mtakatifu, Segerea, wakati wa Misa Takatifu ya Uzinduzi wa Kigango hicho.
Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Stephano Musomba -OSA, akimbatiza mtoto Kiernani James katika Parokia ya Mtakatifu Boniventura, Kinyerezi jimboni humo wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ambapo watoto 93 walibatizwa, na Watoto 43 walipata Sakramenti ya Ekaristi Takatifu. (Picha na Yohana Kasosi)
Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu akiumwagia maji mti baada ya kuupanda katika Parokia ya Mtakatifu Cesilia, Kisarawe II, Kigamboni jimboni humo. Wengine ni Mapadri, Viongozi wa Halmashauri ya Walei, na baadhi ya Waamini. (Picha na Yohana Kasosi)
Baadhi ya Waamini wa Parokia ya Mtakatifu Yakobo Mkuu-Mtume, Kijitonyama, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, wakitoa sadaka kwa Mtoto Yesu katika Pango alimolazwa, wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Mkesha wa Krismas parokiani hapo. (Picha na Yohana Kasosi)
DAR ES SALAAM
Na Mathayo Kijazi
Utume wa Wanaume Katoliki (UWAKA) wametakiwa kujadiliana na kupambanua kuhusu mambo msingi, ili waendelee kuwa nguzo imara katika Kanisa.
Wito huo ulitolewa hivi karibuni na Padri Vincent Sabiit –SDS, wakati wa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Siku ya UWAKA (UWAKA Day) Parokia ya Mtakatifu Polycarp Askofu na Shahidi – Kilamba, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.
“Ipo haja ya UWAKA kujadiliana na kupambanua juu ya mambo mbalimbali yenye tija, ili muendelee kuwa nguzo imara katika Kanisa...
“Katika kujadiliana huko, ipo haja ya kujadiliana pia kuhusu mambo yanayomhusu Mungu, ikiwemo kuwatia moyo wale wote wanaochechemea kiimani,” alisema Padri Vincent.
Padri huyo aliwasihi UWAKA kutenga muda na kuamua kujadili mambo yenye tija, huku wakiepuka kuwa na mijadala inayosababisha mipasuko na huzuni katika maisha ya watu.
Pia, aliwasisitiza kusaidiana wao kwa wao, huku wakihakikisha pia wanawasaidia vijana, hasa wale wanaosumbuliwa zaidi na malimwengu katika maisha yao.
“Sisi kama UWAKA tunaposherehekea leo, tunapaswa kujiuliza kwamba, je, kweli sisi ni nguzo imara? Je, sisi ni nguzo iliyosimama sawasawa au imeelemea upande mmoja na inataka kuanguka?
“Tukumbuke kwamba tunalo jukumu kubwa la kuendelea kujadiliana juu ya mambo yaliyo mema, ili tuzidi kuwa nguzo imara katika Kanisa letu na katika familia zetu, na pia kuweza kuwa na vijana bora watakaolisaidia Kanisa letu siku zijazo,” alisema Padri huyo.
Kwa upande wake Paroko wa Parokia hiyo ya Kilamba, Padri Timothy Nyasulu Maganga alimshukuru Padri Vincent kwa homilia yake aliyoitoa katika Adhimisho hilo la Misa Takatifu.
Padri Nyasulu aliwashukuru UWAKA kwa kufika kwa wingi katika Adhimisho hilo la Misa Takatifu, akiwasihi kuendeleza umoja na mshikamano wao, ili kuendelea kukuza chama hicho cha kitume parokiani hapo.
Naye Mwenyekiti wa UWAKA Taifa, Cassian Njowoka, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika siku hiyo ya UWAKA Parokiani hapo, aliwapongeza wana UWAKA wa Parokia hiyo kwa kuandaa Adhimisho hilo la Misa Takatifu ya Siku yao.
Njowoka aliwashauri wanaume kujiunga na chama hicho cha kitume cha UWAKA, kwani kuna faida kubwa watakazozipata ndani ya chama hicho, ikiwemo kusaidiana wakati wa magonjwa na matatizo mengine.
Vile vile, alitumia nafasi hiyo kuwaasa Wanaume Wakatoliki na Waamini wengine, kushiriki katika suala zima la Uchaguzi Mkuu mwaka ujao 2025, ikiwemo kujiandikisha na kupiga kura ili kuwachagua viongozi watakaowaongoza.
Aliwasisitiza pia kuwaunga mkono Waamini wenzao pale wanapohitaji kugombea nafasi wanazozihitaji, kwani kwa kupitia viongozi hao, watampeleka Kristo katika nafasi watakazozipata.
“Kwa hiyo, tunaaswa na Mababa tujitokeze, tujiandikishe kwa wingi, tupige kura, na kama una sifa ya kupigiwa kura, jitokeze ugombee. Na kama tunaona mwenzetu amejitokeza anataka kugombea nafasi fulani, ‘tum-support’ tusianze kupambana naye, ili ampeleke Kristu katika nafasi ambayo yeye atakuwa ameipata,” alisema Mwenyekiti huyo wa UWAKA Taifa.
Aliongeza kwamba Mungu Mwenyezi amewapa Wakristo Wakatoliki uwezo mkubwa wa kutambua mambo mbalimbali, hivyo yeyote atakayejitokeza, awe mwanaume au mwanamke, ana haki ya kuungwa mkono katika nafasi anayowania.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa UWAKA Parokia ya Kilamba, Venance Kavishe, ambaye pia ni Mwenyekiti UWAKA Dekania ya Mbagala, alimshukuru Padri Timothy Nyasulu Maganga kwa kuendelea kuwaunga mkono katika kila wanalolifanya wana UWAKA parokiani hapo.
DAR ES SALAAM
Na Mwandishi wetu
Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Stephano Musomba- OSA, amewataka Waamini kuachana na tabia na mazoea ya kushiriki na kupokea Sakramenti ya Ekaristi Takatifu bila kujiandaa.
Wito huo aliutoa hivi karibuni wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Uzinduzi wa Kigango kipya cha Kuzaliwa Bikira Maria – Kisukuru, Parokia ya Roho Mtakatifu - Segerea, jimboni humo.
“Mkristo lazima ujitakase ukiwa msafi wa roho ili ushiriki chakula cha Bwana. Huyu ni Mungu, lazima ujinyenyekeze kwake ukiwa mkamilifu. Wakristo muwe watu wa kujitakasa muda wote kwa sababu, isipojiandaa mkiwa wenye usafi wa Roho na wenye Imani Moja Takatifu ya Kristo, lazima mjichunguze kwanza mnaishije hapa Duniani kwa imani hii ya Ukristo wenu. Ndugu zangu Waamini, huu Ukristo tuutumie vizuri, maana ndiyo njia yenye ukweli wa kutuongoza katika maisha yetu,” alisema Askofu Musomba.
Aidha, Askofu huyo aliwasihi Waamini wenye tabia ya kutoa mimba au kuzuia ili wasipate mimba, watambue kwamba wametenda dhambi mbele za Mungu.
“Waamini wenye kutoa mimba au kuzuia wasipate mimba wajue kwamba wametenda dhambi kubwa, wameua. Kwa hiyo msifanye hivyo. Wale wenye tabia hiyo, Mungu amewaleta ninyi hapa duniani ili mumtumikie na umtambue, kwa nini ninyi leo mnamzuia mwenzenu wasizaliwe? Acheni kabisa kufanya hivyo,” alisema Askofu Musomba.
Vile vile, aliwaasa Waamini kujiandaa vyema kwa ajili ya kumpokea Masiha, wakitambua kwamba Masiha anazaliwa kwa ajili yao, hivyo wawe tayari kwa ajili ya mapokezi yake, huku wakiwa wasafi wa mioyo, pamoja na kuachana na tabia ya kuwa watu wa chuki.
“Mama Bikira Maria alipopewa taarifa kuwa ni mjamzito, utazaa mtoto mwanaume ingawa alishangaa pia alishtuka, lakini alipokea kwa imani moja kubwa, je, wewe mama leo ungeambiwa hivi ungesema nini? Tuwe watu wa imani kupokea kitu kwa unyenyekevu na furaha, huku tukiwa watu wa imani na unyenyekevu mkubwa,” alisema Askofu huyo.
Askofu Musomba aliwaasa Wanakigango hicho kuwa watu wa kupendana na kuheshimiana, kwani wakifanya hivyo, watafika mbali kimaendeleo katika Kigango chao.
“Mkifanya hivyo, mtafika mbali katika Kigango hiki, ili mje mfikie kuwa Parokia kamili. Mtambue kwamba hakuna Kigango kinachozinduliwa na Askofu, Kigango huwa kinazinduliwa na Paroko tu, lakini ninyi leo mmepata bahati kubwa sana kuzinduliwa na mimi Askofu, msiniangushe, mjitahidi kukua haraka, mjenge kanisa kubwa pia mjenge nyumba ya Mapadri haraka sana...
“Nimefurahishwa sana na makubaliano yenu ninyi Maparoko wawili katika Parokia hizi mbili, Parokia ya Makoka na Parokia ya Segerea, mmetoa Jumuiya zenu na kuunda Kigango, mmefanya vizuri sana, huu ndio Ukristo unaotakiwa, siyo kuwa na malumbano,” alisema Askofu.
Askofu Msaidizi, Mhashamu Stephano Musomba alitangaza kuwa Kigango hicho kitahudumiwa na Mapadri wa Parokia ya Roho Mtakatifu, Segerea.
Kwa upande wake Paroko wa Parokia hiyo ya Segerea, Padri Denis Kunambi aliwaomba Waamini wa Kigango kipya wampe ushirikiano ili waweze kufikia maendeleo zaidi katika Kigango hicho.
Padri Kunambi alisema kuwa Kigango hicho kimezaliwa kwa baraka kubwa, kwa sababu eneo hilo lilinunuliwa na Parokia ya Segerea kwa lengo la kujenga shule kama mradi wa Parokia, lakini sasa wazo hilo limegeuka kuwa Kigango.
Naye Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Gaudence – Makoka, Padri Amaladoss Chinnappan aliwaasa Waamini waliotoka katika Parokia ya Makoka na kujumuika katika Parokia ya Segerea, kupitia Kigango hicho, wasichukie wala kusikitika, bali wafurahi kwa sababu wote ni Waamini Wakatoliki.
Padri Chinnappan alimshukuru Askofu kwa kuwaweka pamoja, kuwapatanisha na kuwapatia Kigango ambacho amekizindua, akiwasihi Waamini kufahamu kwamba huo ndio Ukristo wanaotakiwa kuuishi katika maisha yao ya kila siku.
DAR ES SALAAM
Na Mwandishi wetu
Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu amewataka Waamini kutokubali kuyumbishwa kiimani.
Askofu Mchamungu alitoa wito huo hivi karibuni katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Sakramenti Takatifu ya Kipaimara iliyofanyika Parokia ya Mtakatifu Cesilia -Kisarawe ll, Kigamboni.
Askofu Mchamungu alisema waamini wanatakiwa kuitangaza Injili kwa watu wote ili wamjue Mungu wa kweli.
“Ndugu zangu, tushike Maandiko Matakatifu… hayo ndio yatatusaidia kuona utukufu wa Mungu,”alisema Askofu Mchamungu.
Kwa upande wa Waimarishwa wa sakramenti hiyo, aliwataka kutambua majukumu yao sis i kuwasimamia watoto hao, bali hata kuwasaidia na kuwaongoza katika misingi thabiti ya kimaadili.
Askofu Mchamungu aliwataka waamini wa parokia hiyo wajenge Kanisa kwa sababu kanisa la sasa ni dogo.
Naye Paroko wa parokia hiyo,Padri Roger Kamuzinzi, aliwaomba waamini kumpa ushirikiano ili aweze kutekeeleza vyema majukumu yake ya kitume.
Padri Kamuzinzi alimshukuru Askofu Mchamungu kwa kuwapatia vijana 31 Sakramenti ya kipaimara.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Parokia hiyo, Geofrey Lyungu alisema parokia hiyo bado changa kwani ina muda wa miezi sita tu tangu ilipotangazwa na Askofu Mkuu Mhashamu Sana Jude Thaddaeus Ruwa’ichi, kuwa Parokia Kamili.
MOROGORO
Na Mwandishi wetu
Katibu wa Askofu wa Jimbo Katoliki la Morogoro, Padri Boniface Mliga amewataka Watawa wa Kike wa Shirika la Maria Imakulata (SMI), walioweka Nadhiri za Daima kuona fahari kwa kutoa maisha yao kama Sadaka ili kumtumikia Mungu.
Padri Mliga alisema hayo hivi karibuni wakati wa Adhimishi la Misa Takatifu ya Nadhiri za Daima kwa Masista wa Shirika la Maria Imakulata –SMI, iliyofanyika katika Parokia ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli –Kihonda, jimboni Morogoro.
“Ndugu zangu, inawapasa kutambua Agano ni makubaliano, kwani hata Wana Waisraeli waliweka Agano na Mungu, nanyi mnaweka Agano kati ya Mungu na Kanisa, la kumtumikia kama kiumbe chake mwenyewe, huku mkitoa maisha yenu kama zawadi na sadaka kwake,”alisema Padri Mliga.
Aidha, aliwataka Masista hao kutenda mema na kumtumikia Kristo siku zote za misha yao, akiwakumbusha kuwa kila mtu anayehitaji kumfuata Yesu, lazima aikane nafsi yake kwa kuachana na mambo ya kidunia, na kumfuata.
Padri Mliga aliendelea kusema, “Ukiikana nafsi yako, pia unatakiwa ubebe msalaba wako.”
Aliendelea kusema kwamba kama mtu amechagua kumfuata Kristo na kukubali, yampasa kujiuliza, je, ana uwezo huo wa kuacha mambo yote?
“Kwani wasije kukubali kuacha ya ulimwengu, na baadaye wakashindwa na wakakata tamaa, kwani maisha ya kumfata Kristo, si maisha ya kimasihara,”alisema Padri Mliga.
Kwa mujibu wa Padri Mliga, Kristo alichekwa na kudhihakiwa na baadhi ya watu, lakini hakukata tamaa na badala yake, aliendeleza kazi yake ya kuhubiri Injili kwa mataifa, na mwishowe aliteswa na kukubali kufa msalabani, ili atimize agano lililoandikwa hapo kale.
Alitoa wito kwa Masista wamkimbilie Mungu siku zote za maisha yao, kwa kupokea msalaba na kuubeba kwa furaha na si kwa huzuni, ili waweze kukidhi vigezo vya kuwa wafuasi wa Kristo.
Mbali na hayo, Padri Mliga aliwataka watawa hao wasitazame walipotoka wala kukata tamaa, bali watazame Msalaba wa Kristo kwa imani na matumaini makubwa, kwa kujitoa zaidi, wakiomba Mungu waendelee kuubeba Msalaba wa Kristo, kwa amani na upendo.