Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

DAR ES SALAAM

Na Mathayo Kijazi

Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Askofu Mstaafu wa  Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, amesema kuwa watu wanaolitangaza jina la Mungu katika mazingira yoyote, hueleweka.
Kardinali Pengo alisema hayo wakati akitoa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Sakramenti ya Kipaimara iliyofanyika Parokia ya Mtakatifu Clara wa Asizi - Chamazi, jijini Dar es Salaam.
“Watoto wa Kipaimara, jitahidini sana kulitangaza jina la Mwenyezi Mungu katika maisha yenu. Watu wanaolitangaza jina la Mungu katika mazingira yoyote yale, watu hao hueleweka,” alisema Kardinali Pengo.
Aidha, Kardinali Pengo aliwasisitiza vijana waliopokea Sakramenti hiyo kutambua kwamba, lengo kuu la kupokea Sakramenti kuja kulitangaza Neno la Mungu.
Aliongeza kuwa siku watakaposahau kwamba lengo lao kuu ni kulitangaza Neno hilo, basi watajikuta wanaingia katika vurugu.
Wakati huo huo Kardinali Pengo, aliwaasa Waimarishwa hao kuepuka kuwa waoga, badala yake watambue kwamba wanasimama kwa niaba ya kundi lililoamini kuwa Kristo alifufuka katika wafu.
Katika hatua nyingine, Kardinali Pengo aliwapongeza waamini wa Parokia hiyo, kwa kuwa na kanisa kubwa na la kisasa, akiwasihi kuongeza nguvu ili kukamilisha maboresho yaliyobaki kwa sasa.

DAR ES SALAAM

Na Mathayo Kijazi

Benki ya Biashara ya Mkombozi imepandishwa hadhi kutoka Soko la Ukuzaji Mitaji la Dar es Salaam Stoke Exchange(DSE) (EGM) na kwenda Soko Kuu la Uwekezaji (MIMS).
Akizungumza katika hafla ya kuipandisha hadhi Benki hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Chande alisema kuwa benki hiyo imepanda kutoka hatua moja kwenda nyingine ndani ya muda mfupi.
“Hongereni sana Mkombozi Bank kwa hatua hii mliyofikia, kwa sababu mmepanda hadhi kutoka hatua moja kwenda nyingine ndani ya muda mfupi sana…msiridhike na hatua hiyo mliyoifikia, kwa sababu kuna maneno yanasema ‘Mpanda patosha, huvuna pa mkwisha,”alisema Chande.
Naibu Waziri Chande aliwasihi watendaji wa Benki hiyo kutoridhika na hatua waliyofikia, badala yake waendelee kufanya uhamasishaji ili Benki iendelee kukua.
Aidha, Chande aligusia pia suala la riba kwa wanaochukua mikopo, na kusema kuwa Serikali inaendelea kulifanyia kazi suala hilo, ili riba inayochukuliwa, isiwe ya kuwaumiza wananchi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Mkombozi, Respige Kimati, alisema kuwa Benki hiyo imewekeza nguvu nyingi ili kuanza kutoa gawio kuanzia mwakani 2025.
Alisema pia kuwa Benki hiyo imekuwa mstari wa mbele kuungana na Serikali katika kuwashika mkono watu waliopatwa na majanga mbalimbali ndani ya jamii.
Kimati aliongeza kuwa Benki ya Mkombozi kwa sasa imepiga hatua kubwa ikilinganishwa na miaka 10 iliyopita, ina wakala zaidi ya 1000 kote nchini.

VATICAN CITY, Vatican

Baba Mtakatifu Fransisko ameiasa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha inaendelea, kuwapokea na kuwahifadhi wakimbizi duniani kote.
Baba Mtakatifu alitoa wito huo hivi karibuni wakati wa Siku ya Kimataifa ya wakimbizi akisema kwamba inapaswa kuwa ni fursa ya kuelekeza macho na usikivu wa kidugu kwa wale wote wanaolazimika kuyahama makazi yao kutafuta amani na usalama.
Baba Mtakatifu alisema hayo baada ya Katekesi yake katika fursa ya kuelekea kilele cha Siku hiyo inayoadhimishwa kila ifikapo Juni 20 ya kila mwaka.
Katika salamu mbali mbali baada ya katekesi, akizungumza na waamini na mahujaji waliofika katika uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican, kwa, Baba Mtakatifu Fransisko, alisema kwamba jamii inapasswa kutowanyanyasa wakimbizi na wahamiaji.
“Iwe ni fursa ya kuelekeza macho ya usikivu na ya kidugu kwa wale wote wanaolazimika kuyahama makazi yao kutafuta amani na usalama. Sote tumeitwa kuwakaribisha, kuwahamasisha, kuwasindikiza na kuwaunganisha wale wanaobisha hodi kwenye milango yetu,”alisema Baba Mtakatifu Fransisko.
”Ninaomba kwamba Mataifa yafanye kazi ili kuhakikisha hali ya kibinadamu kwa wakimbizi na kuwezesha michakato ya ujumuishaji.”
Baba Mtakatifu aliwakaribisha kwa moyo mkunjufu mahujaji wanaozungumza lugha ya Kiitaliano, kwa namna ya pekee, Chama cha Marafiki wa Kardinali Celso Costantini, wakisindikizwa na Askofu Giuseppe Pellegrini wa Jimbo la Concordia-Pordenone, katika kuadhimisha miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Concilium Sinense ya Shanghai.
Katika hatua nyingine, Baba Mtakatifu Fransisko amewaombea wagonjwa, wazee, wenye ndoa wapya na  hasa vijana.
Aidha alikubusha siku kuu ya Mwanzislihsi wa Shirika lake inayoandimishawa kila Juni 21, kila mwaka.

TAFAKURI YA SOMO LA INJILI DOMINIKA YA 12 MWAKA B

Na Pd. Gaston George Mkude

Amani na Salama!
Baadhi ya miujiza inayosimuliwa katika Maandiko Matakatifu, inatuacha na mshangao mkubwa: Mti uliolaaniwa kwa kukosa kutoa matunda wakati si majira yake (Marko, 11:13), maji yanageuzwa kuwa divai (Yohane, 2:1-11), Yesu akitembea juu ya maji, na Petro akimwomba naye atembee juu ya maji (Matayo, 14:22-33), Petro analipa zaka ya hekalu kwa kupata pesa kutoka kinywa cha samaki (Matayo 17:24-27). Hivyo, ili kupata ujumbe kutoka miujiza ya namna hii, hatuna budi kuingia ndani kabisa bila kuishia katika miujiza pekee.
Muujiza wa leo pia ambapo Yesu anatuliza dhoruba ya upepo mkubwa baharini, ni moja ya miujiza inayotutaka kutafakari zaidi ili kuweza kupata ujumbe kusudiwa. Baada ya kulisoma somo la Injili ya leo, mara moja tunaweza kuwa na maswali kadhaa.
Mwinjili anatuambia kuwa ilikuwa jioni, na kama ni jioni iliwapasa kurejea nyumbani Kapernaumu, na siyo kuvuka na kwenda upande mwingine, maana bado swali kwa nini muda ule walivuka kwenda upande mwingine? Na zaidi sana, kwa nini walienda upande wa Wagerasi, watu waliokuwa wapagani na wasiochangamana na Wayahudi? Na hata tukisoma zaidi Injili ya Marko, tunaona kuwa Yesu hakupokelewa wala kufahamika vyema katika nchi ile ya Wagerasi. (Marko, 5:17)
Na hata wafuasi wake wanaomwamsha ili awaokoe katika hatari ile ya dhoruba kubwa, na wanafanya hilo, kwani waliamini katika uwezo wa Yesu, lakini Yesu anawakemea kwa kuwa hawana imani. Pia, hata baada ya Yesu kuituliza dhoruba ile kubwa, tunashangaa kuona wanafunzi wake, badala ya kufurahi, wamejawa na uoga na hofu kuu.
Ni kwa msaada wa maswali haya ndipo tunaweza sasa kuona somo la Injili la leo linatualika kwenda ndani zaidi ili kuweza kupata ujumbe kusudiwa. Si nia wala lengo la Mwinjili Marko kutupa simulizi tu la muujiza alioufanya Yesu wa kuituliza dhoruba, bali tangu mwanzo tunaona ni nia ya Mwinjili Marko kutusaidia hatua kwa hatua katika kumtambua Yesu ni nani, utambulisho wa Kimasiha unaojifunua hatua kwa hatua.
Hivyo, masimulizi na nia kuu ya Mwinjili Marko ni kumtambulisha Yesu kwetu, kwa kila mmoja anayetaka kukutana na kumjua Masiha, basi Injili ya Marko ni msaada mkubwa kwetu. Ni Injili ambayo tangu mwanzoni inajaribu kujibu swali lile la; Yesu ni nani.
Leo tunakutana na chombo kikiwa baharini pamoja na vyombo vingine, zaidi sana pia chombo hiki kikielekea katika nchi ya wapagani, yaani Wagerasi, mawimbi makali na makubwa, giza la usiku, maana ilikuwa jioni, Yesu amelala katika shetri na juu ya mto, upepo mkali, hofu na uoga uliowajaa wafuasi wa Yesu, ni moja kati ya lugha ya picha tunazokutana nazo mara nyingi katika Maandiko Matakatifu.
Injili yetu ya leo inaanza na kutuambia muda wa muujiza ndio jioni, na uelekeo wa chombo kile alimokuwemo Yesu na wanafunzi wake.
Ni jioni. Ndiyo kusema ni baada ya Yesu kumaliza utume na misheni yake ya kuusimika na kuutangaza Ufalme wa Mungu, wanafunzi wake wanaingia chomboni pamoja na Yesu na kuelekea upande mwingine, lakini wanakwenda wapi haswa?
Ni baada ya kusoma zaidi Injili ya Marko, kwamba walikuwa wanaelekea katika nchi ile ya Wagerasi, waliokuwa wapagani. (Marko 5:1) Na ndipo tunaona mara moja kuwa katika nchi ile kulikuwepo na nguruwe malishoni mlimani, ambapo Yesu baada ya kumponya mtu aliyekuwa na pepo wachafu, pepo wale wakamwomba Yesu, kutoka na kuwaingia nguruwe, na hata nguruwe wale wakaishia wote baharini. Uwepo wa nguruwe kati yao ni ishara tosha kuwa watu wale hawakuwa Wayahudi, bali wapagani, kwani Wayahudi ni marufuku kufuga au kula nyama ya nguruwe.
Chombo ndiyo ishara ya jumuiya ya Wakristo yaani Kanisa lake Yesu Kristo, ambao baada ya Yesu kukamilisha utume na misheni yake, wanaalikwa kutoka na kwenda kuitangaza Habari Njema ya Wokovu kwa watu wote. Lakini tunaona chomboni lazima pia awepo na Yesu, kwani uwepo wake ni wa lazima na wa muhimu kwa usalama wa jumuiya ya Kanisa. Tunaona leo chombo kikiwa katikati ya safari, kinakuwa katika hatari kubwa kwa upepo mkubwa na dhoruba.
Mwinjili Marko anatuambia pia kwamba kulikuwa na vyombo vingine, ndiyo kusema Mwinjili anajaribu kutuonesha kuwa hata baada ya utume wa Yesu Kristo kukamilika hapa duniani, kulikuwa na jumuiya kadhaa za Kikristo katika Kanisa lile la mwanzo.
Ilikuwa jioni, ndiyo kusema ilikuwa giza. Giza katika Maandiko ni ishara hasi, ni kukosekana utaratibu kama ilivyokuwa mwanzo kabla ya uuumbaji. (Tohuwabohu - Mwanzo, 1 :2). Fujo ni kukosekana uwepo, na hasa uweza wake Mwenyezi Mungu.
Ni hapo katika uwepo wa giza tunaona yule mwovu anatawala, na hivyo tunahitaji uwepo wake Mungu ili kututoa na kutuacha salama katika mitego ya yule mwovu. Chombo kinasafiri saa ile ya giza, saa ile ya fujo, saa isiyokuwa ya mwanga wala utulivu. Ni saa ile ambayo chombo kinakuwa katika hatari kubwa na kupigwa na kuyumbishwa na upepo mkali wa dhoruba.
Yesu anakuwepo chomboni, lakini amelala katika shetri, sehemu ambayo kwa desturi anakaa nahodha, muongoza meli au vyombo vya majini. Ni Yesu anayepaswa kuwa nahodha na rubani wa chombo kile, yaani Kanisa lake, Ni yeye ambaye tunapaswa kumkimbilia na kumlilia. “Mwalimu, si kitu kwako kuwa tunaangamia?” (Marko, 4 :38).

Kwa kumalizia Tafakuri hii nunua TumainiLetu

Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu, akibaliki matoleo ya waamini wakati wa Adhimisho la Takatifu la Misa ya Kipaimara, iliyofanyika Parokia ya Mtakatifu Clara-Magole, Jimboni humo. Kulia ni Paroko wa Parokia hiyo, Padri Christian Singano.

Viongozi na waamini wa Parokia ya Bikira Maria Mama wa Mwokozi, Sinza Jimbo Kuu Katoliki la Dar es  Salaam, wakiwa kanisani wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Kipaimara iliyofanyika hivi kalibuni parokiani hapo.

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi  akiwapatia vijana vyeti baada ya kupokea Sakramenti Takatifu ya Kipaimara, katika Adhimisho la Misa Takatifu iliyofanyika Parokia ya Bikira Maria Mama wa Mwokozi, Sinza jijini Dar es Salaam.

Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Clara –Magole, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Christian Singano [katikati mwenye kanzu] akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Kamati Tendaji ya parokia hiyo, baada ya Adhimisho la Misa Takatifu ya Kipaimara.

Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Ambrosi –IPTL, Salasala, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Paul Sabuni akimkabidhi Mwenyekiti mpya wa Parokia Teule ya Utatu Mtakatifu-IPTL, Restituta Mingo, bahasha  za kutegemeza Tumaini Media, wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Dominika iliyokwenda sanjali na kuapishwa Viongozi wapya wa Parokia hiyo. (Picha zote na Yohana Kasosi).

Maskofu kutoka Majimbo mbalimbali ya Kanisa Katoliki nchini na Wakuu wa Mashirika ya Kitawa, wakiwa katika Mkutano Mkuu wa Maaskofu, uliofanyika katika Ukumbi wa AMECEA, Baraza la Maskofu Kurasini (TEC), jijini Dar es Salaam. (Picha na Yohana Kasosi)