Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Ambosi –IPTL, Salasala, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Paul Sabuni akiwaapisha Viongozi wapya wa Parokia Teule ya Utatu Mtakatifu, Skanska -IPTL, baada ya kupandishwa hadhi Parokia hiyo.

Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu akipokea akipokea sadaka kutoka kwa Waamini na Viongozi wa  Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA), wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Sakramenti Takatifu ya Kipaimara, iliyofanyika Parokia ya Mtakatifu Clara –Magole Jimboni humo.

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi na Mapadri wakiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Kamati Tendaji ya Parokia ya Bikira Maria Mama wa Mkombozi, Sinza, jimboni humo. (Picha zote na Yohana Kasosi).

DAR ES SALAAM

Na Pd. Dkt. Clement Kihiyo (TEC)

Mwaka wa Liturujia Leo ya Wokovu
1. Utangulizi:
Ishara na matendo yanayofanywa kwa wakati huwa njia ya wokovu kwetu. Mwaka wa Liturujia ambao pia huitwa mwaka wa Kanisa ni fumbo la Kristo. Ni kwa njia ya maadhimisho ya kumbukumbu takatifu ndani ya Mwaka wa Liturujia, ndipo tunapata wokovu. Katika Mwaka wa Liturujia, Fumbo zima la Kristo linafunuliwa; yaani, kutoka Umwilisho na kuzaliwa, na kutoka Kupaa hadi Pentekoste
Mama Kanisa Takatifu huchukulia wajibu wake kuadhimisha kwa kumbukumbu takatifu kazi ya ukombozi ya Bwanaarusi wake aliye Mungu, katika siku zilizopangwa katika mwenendo wa mwaka mzima. Kila juma, Kanisa katika siku aliyoiita “Dominika”, yaani “Siku ya Bwana”, linaadhimisha kumbukumbu ya ufufuko wa Bwana. Kwa namna ya pekee, linauadhimisha ufufuko huo pamoja na mateso yake yenye heri mara moja kwa mwaka katika Sikukuu ya Pasaka, iliyo kubwa kuliko maadhimisho yoyote (SC 102).
Katika mzunguko wa mwaka mzima, Mama Kanisa analikunjua fumbo la Kristo, tangu umwilisho na kuzaliwa, hadi kupaa mbinguni, mpaka siku ya Pentekoste na kungojea kwa tumaini lenye heri kurudi kwake Bwana. Anapokumbuka namna hii mafumbo ya ukombozi, Kanisa huwafungulia waamini utajiri wa uweza na mastahili ya Bwana wake. Kwa njia hii, uwepo wa mafumbo haya unakuwapo kwa nyakati zote, ili kutoka humo waamini waweze kuchota na kujazwa neema ya wokovu.
Mwaka wa Liturujia pia unawakilisha na kueneza tena  imani, maisha ya Kikristo na uwepo wa ukombozi wa Kristo na utajiri wa wokovu (SC. 102c). Mwaka wa Liturujia ni safari ya wokovu wa Kristo Mwenyewe na Kanisa lake (Lk, 24:15). Mwaka wa Liturujia sio mfuatano wa jumla wa siku na miezi, lakini unakuwa alama/ishara ya mfuatano ambao matukio ya neema yanatokea kama matukio ya wokovu kwetu hapa leo. Mwaka wa Liturujia ni wakati wa wokovu, ‘epifania’ ‘hic et nunc’ (hapa na sasa) kwetu.

2. Baadhi ya Mambo Makuu ya Mwaka wa Liturujia
2.1 Mwaka wa Liturujia ni Maadhimisho:
Matukio ya Mwaka wa Liturujia sio tu mifano ya kutafakari au kuiga uungu, lakini ni ishara zenye ufanisi za wokovu, ambao Kristo katika Utatu Mtakatifu, wamekamilisha kwa wokovu wa wanadamu. Mambo makuu ya ukombozi ni sisi kuadhimisha na kurithisha kwa kizazi kingine. Mwaka wa Liturujia una nguvu maalum ya kisakramenti na ufanisi wa kuimarisha maisha ya Kikristo.

2.2 Mwaka wa Liturujia Kuanzia Ufufuko:
Tukianzia na habari ya wanafunzi wa Emao (Lk 24:25-26); Yesu alieleza kisa chote kuanzia Ufufuko hadi Manabii. Ina maana kila kitu kinamhusu Kristo. “Bila ufufuko imani yetu haina maana” (1Kor. 15:13-17). Ufufuko ni chanzo na kitovu cha Mwaka wa Liturujia. Ufufuko ni siku ya Adamu Mpya (Rum. 11:5, Efe 2:5,8).
2.3 Siku ya Kwanza ya Juma-Dominika- Siku ya Bwana
Tangazo la ufufuko lilianza siku hii kwa amri ya Bwana (Mk.16.7, Mt. 28.7, Lk. 24.9). Ndipo wale wanawake wakatangaza ufufuko siku ile ile. Kwa hiyo, Dominika ni mwendelezo wa tangazo la Ufufuko. “Tunasherehekea Dominika kwa sababu ya Ufufuko Mtukufu wa Bwana wetu Yesu Kristo, na tunafanya hivyo sio tu wakati wa Pasaka bali pia kila mzunguko wa juma, yaani kila Siku ya Kwanza ya Juma. Mtakatifu Augustino anaiita Dominika kwa usahihi kama Sakramenti ya Pasaka  (Taz . In Io. Tract . XX, 202: CCL 36,203), (SC 26, 184). Kwa Kanisa la Mashariki Dominika ni ‘Anastasimos hemera’, yaani, siku ya ufufuko.
Matendo ya kiliturujia si matendo ya kila mmoja peke yake, bali ni maadhimisho ya Kanisa, ambalo ni “sakramenti ya umoja”, yaani taifa takatifu linalokusanywa na kuratibishwa chini ya uongozi wa Maaskofu SC 26.
Kwa sababu hiyo matendo hayo ni ya mwili wote kabisa wa Kanisa, nayo huudhihirisha na kuuimarisha. Aidha, kila mmoja wa wanakanisa anahusika kwa namna tofauti, kadiri ya utofauti wa daraja, wa majukumu, na wa ushiriki kiutendaji
Matukio maalum ya kimungu siku ya Dominika pia yanaipa siku hii umaalumu wake. Maana yake:

i.    Roho Mtakatifu alitolewa kwa Wanafunzi siku ya Dominika (Pokeeni Roho Mtakatifu, wowote mtakaowaondolea dhambi wameondolewa),
ii.    Pentekoste ilikuwa siku ya Dominika,
iii.    Dominika ni siku ya Amani, siku ya Yubilei ya Roho Mtakatifu (Lk 4:18-19, Isa 61:1-3).
iv.    Kwa namna ya pekee, Dominika ni siku ya uumbaji mpya, siku ya Jua Jipya (Mal, 4:2).

2.4 Dominika ni Kitovu na Kiini cha Mwaka wa Liturujia:
Dominika ni Kitovu na Kiini cha Mwaka wa Liturujia kwa muktadha ufuatao:
Dominika ni siku ya Bwana. Wayunani wanaiita, “Kyriake Hemera”, ambapo kivumishi ‘Kyriake’ kinarejelea Kyrios, yaani Bwana aliyefufuka pamoja na Roho (1 Kor. 16:2, Mdo, 20:7, Ufu.1.10).
Dominika ni siku ya kimungu ya kumwadhimisha Bwana, siku kwa ajili ya kumega mkate na Neno, siku kwa ajili ya karamu na kwa ajili ya kukusanya sadaka kwa ajili ya maskini (2 Kor, 9:12, Rum. 15:27).
Dominika ni siku ya mwanzo wa uumbaji, ni siku ya nane baada ya ufufuko. Ni siku ya nane kwa sababu ni nje ya muda unaopimwa katika wiki. Siku ya nane ni siku ya Ekaristi. Hivyo, Dominika hugusa fumbo zima la wokovu. Inaleta pamoja na yenyewe ulimwengu wote wa mfano wa Kikristo. Inaangazia siku ya mwisho, siku ya Parousia.
Kwa hiyo, Dominika ni siku maalum na siku pekee  ya Bwana. Inaunda mwendelezo halisi wa adhimisho wa Kanisa kutoka Pentekoste hadi kurudi kwa Bwana. Maadhimisho mengine, isipokuwa kama yana umuhimu mkubwa, hayatapewa kipaumbele kuliko Dominika ambayo ndiyo msingi wa kweli na kiini cha Mwaka mzima wa Liturujia.
Kadri ya mapokeo ya Mitume, yanayopata asili yake katika siku ya ufufuko wa Kristo, Kanisa huadhimisha fumbo la Pasaka kila siku ya nane, katika siku ile iitwayo kwa haki kabisa Siku ya Bwana au Dominika. Katika siku hii Waamini wanapaswa kujumuika pamoja ili, wanaposikiliza Neno la Mungu na kushiriki Ekaristi, wafanye ukumbusho wa mateso, ufufuko na utukufu wa Bwana Yesu. Na pia watoe shukrani kwa Mungu “aliyewazaa upya katika tumaini lenye uhai kwa njia ya ufufuko wa Yesu Kristo katika wafu” (1Pet, 1:3). Kwa hiyo, siku ya Dominika ni Sikukuu ya kwanza ambayo ni lazima ielezwe vizuri na kuingizwa, kwa kadri inavyowezekana, katika maisha ya kidini ya Wakristo, ili iweze kuwa pia siku ya furaha na ya kuacha kazi. Maadhimisho mengine yasitiliwe mkazo sana, isipokuwa yale yenye umuhimu zaidi, kwa sababu siku ya Dominika ni msingi na kiini cha mwaka mzima wa Liturujia (SC. 106).

3. Fumbo na Mafumbo ya Kristo:
Imani ya Kikristo inaadhimisha Fumbo Kuu Moja la Pasaka, nalo ni  Fumbo la Kristo, aliyeteswa, akafa, akazikwa na kufufuka. Kanisa linaendelea kuadhimisha Fumbo hili kwa njia tofauti. Fumbo hili lilianza kufunuliwa katika Agano la Kale; na linatimizwa kihistoria katika maisha ya kidunia ya Kristo, na lipo katika mafumbo ya kisakramenti.
Fumbo la Pasaka huadhimishwa katika mwaka kwa njia tofauti, lakini katika utaratibu ule ule wa Neno, mwili na kikombe cha Yesu Kristo. Awamu tofauti za maadhimisho zinalenga kutufanya tuelewe vizuri Fumbo hilo. Katika uwezo wetu mdogo wa kibinadamu na kisaikolojia, hatuwezi kulielewa na kuliadhimisha hilo Fumbo kwa wakati mmoja na kuchota utajiri wa neema ya Fumbo hilo la Kristo”, kwa hivyo, Mwaka wa Liturujia unatupa muda wa kutosha wa kuliadhimisha na kuchota neema zake.
Kwa muktadha huu, katika kila Misa kuna Majilio, Noeli, Epifania, Alhamisi Kuu, Ijumaa Kuu, Pentekoste, Pasaka, Kupaa, na Watakatifu wote. Kwa hiyo, Mwaka mzima wa Kanisa ni Fumbo Moja, “ Sakramenti Paschale ” ambalo huadhimishwa kila Dominika.
Kutoka hili Fumbo Kubwa la Pasaka, linajigawa katika mafumbo kadhaa yanayorejelea matukio tofauti katika maisha ya Kristo, na ni ushiriki na ukuzaji wa Fumbo moja pekee la Pasaka, ambalo huanza kutoka Usiku Mtakatifu wa Ufufuo hadi wakati wa Pasaka hadi Pentekoste, Wiki Takatifu, Kwaresima, Wakati wa Kawaida, Majilio, Noeli hadi Epifania na Sikukuu mbalimbali.
Itaendelea toleo lijalo.

DAR ES SALAAM

Na Alone Mpanduka

Jina lake halisi ni Anna Mae Bullock, japo tunamfahamu zaidi kama Tina Turner. Pamoja na kufahamika kama mtunzi na mwimbaji wa muziki, pia alifanya vyema kama mwigizaji wa filamu na mwandishi wa vitabu.
Alizaliwa Marekani mwaka 1939 ambapo alikua na dada zake wawili.Kwakuzaliwa ni raia wa Marekani lakini mwaka 2013 alibadili nyaraka zake na kuwa raia wa Uswisi.
Alizaliwa Anna Mae Bullock tarehe 26 mwezi Novemba mwaka 1939, katika jamii ya vijijini ya Tennessee ya Nutbush, ambayo alielezea katika wimbo wake wa 1973 “Nutbush City Limits,” kama “jamii ya zamani tulivu, na mji wa farasi mmoja.”
Akiwa binti mdogo alikua akiimba katika kwaya ya kanisani kwenye Kanisa la Kibabtisti huko Nutbush Marekani
Aliishi na bibi yake ambaye alikuwa ameshika sana dini, na katika moja ya Makala ya maisha yake inayofahamika kama I, Tina alinukuliwa akisema kuwa wazazi wake hawakumpenda na hawakumhitaji.
Katika maisha yake ya ujana na kabla ya kuwa Tina Turner alishawahi kufanya kazi za vibarua kama vile nesi msaidizi na mfanyakazi wa kazi za ndani.
Katika harakati za kimuziki, safari yake ilianza baada ya kuvutiwa na mwimbaji Ike Turner, ambaye alikuwa akiimba na bendi ya ‘Kings of rythim’. Sikumoja alipata fursa ya kushika kipaza sauti mbele ya mwimbaji huyo, akapewa fursa ya kuimba zaidi, na siku hiyo alibaki akiimba usiku mzima.
Tangu siku hiyo, aliendelea kumfunza namna ya kuimba na kutoa burudani.Hivyo, wimbo wake wa kwanza kurekodi ilikuwa ni 1958 uliitwa ‘Boxtop’ na wakati huo jina lake la stejini alitumia ‘Little Ann’.
Aliandika wimbo wake wa ‘a fool in love’ kwa ajili ya msanii Art Lassiter lengo, ikiwa yeye mwenyewe aimbe kama msaidizi, lakini bahati mbaya au nzuri, msanii huyo aliyelengwa hakufika. Ikamlazimu Little Anna kurekodi mwenyewe, kwani tayari alikuwa amelipia muda wa studio.
Hapo ndipo maisha yake yalipobadilika. Wimbo huo ulinunuliwa kwa dola $25,000 kama malipo ya awali tu. Hii ikapelekea Ike Tuner kumbatiza jina la stejini “TINA”. Baadae Ike Turner alimuongezea jina lake la mwisho ‘turner’ kisha akamsajili kisheria ili kulinda haki zake endapo mwanamuziki huyo angetaka kujiondoa chini ya menejimenti yake.
Endapo Bullock angeondoka, basi jina la Tina Turner bado lingebaki kuwa hakimiliki ya Ike, na angemuweka msanii mwingine yeyote kwa jina hilo hilo.
Hivyo, kuanzia hapo Anna Mae Bullock akatambulika rasmi katika jukwaa la muziki kimataifa kama Tina Turner.
Baadae, Tina aliolewa na Ike Turner mumewe ambaye walikuwa wakifanya muziki pamoja. Na baada ya takriban miongo miwili ya kufanya kazi na mume wake aliyemshutumu kwa unyanyasaji waliachana, ambapo Tina alibaki na magari mawili tu, pamoja na jina lake.
Baada ya kuachana, Tina aliibuka kama msanii wa kujitegemea na akawa mmoja wa wasanii wa pop wakubwa wa miaka ya 1980 na albamu yake ya ‘Private Dancer’.
Taarifa za kifo cha Tina Turner zilitikisa ulimwengu mwezi Mei mwaka jana, ambapo vyombo mbalimbali vya habari kimataifa vilitangaza taarifa za mwanamuziki huyo kuaga dunia akiwa nchini Uswisi katika umri wa miaka 83
Iliripotiwa kuwa msanii huyo alikuwa na afya dhoofu katika miaka ya hivi karibuni, kwani aligunduliwa na saratani ya utumbo mnamo 2016, na kupandikizwa figo mwaka 2017.
Taarifa za kifo chake zilitangazwa kupitia mtandao wake wa Instagram, ambapo iliandikwa:
“Ni kwa huzuni kubwa kwamba tunatangaza kufariki kwa Tina Turner. Kwa muziki wake na shauku yake isiyo na kikomo ya maisha, alivutia mamilioni ya mashabiki ulimwenguni kote na kuwatia moyo nyota wa kesho. Leo tunasema kwaheri kwa rafiki mpendwa ambaye anatuachia kazi yake kuu zaidi: muziki wake. Huruma zetu zote za dhati ziende kwa familia yake. Tina, tutakukumbuka sana”.
Wafuasi wake kutoka maeneo mbali mbali duniani walimiminika katika mitandao ya kijamii kutuma salamu za rambi rambi, huku vituo vya redio na televisheni vikicheza nyimbo zake kwa bidii kubwa kumuenzi.
Tina Turner, ambaye amefariki akiwa na umri wa miaka 83, aliunda rekodi nyingi za R&B, funk, rock na pop, zote zikiwa na uwezo wake wa kipekee wa sauti.
Nyimbo hizo zinafuatilia hadithi yake kutoka kwa ushirikiano wake usio na furaha na mumewe wa kwanza Ike, hadi miaka ya 1980 kurudi kwa hisani ya kikundi cha pop cha synth cha Uingereza.
Miaka ya 80, ilishuhudia nyimbo zake kadhaa zikiingia kwenye Top 40, zikiwemo “Typical Male,” “The Best,” “Private Dancer” na “Better Be Good To Me.”
Tamasha lake la 1988 mjini Rio de Janeiro, Brazil, lilivutia watu 180,000, ambalo linasalia kuwa moja ya hadhira kubwa zaidi ya tamasha kwa msanii yeyote.

MANCHESTER, Uingereza
Meneja wa Manchester United Erik ten Hag ameweka wazi kuwa  likizo yake ya majira ya kiangazi iliingiliwa na klabu hiyo mara baada ya kumfuata kwake na kumwomba aendelee kubaki ndani ya klabu yao.
Mustakabali wa Ten Hag ulikuwa mashakani kabla ya kuiongoza United kupata ushindi katika fainali ya Kombe la FA, lakini klabu hiyo imeamua kumweka Mholanzi huyo mahali pazuri.
United walimaliza katika nafasi ya nane msimu uliopita - nafasi yao ya chini kabisa katika enzi ya Premier League.
Mmiliki mwenza mpya wa United Sir Jim Ratcliffe inadhaniwa alizungumza na kocha wa zamani wa Bayern Munich Thomas Tuchel lakini Mashetani Wekundu hatimaye wakaamua kumbakisha Ten Hag.
“Wasimamizi wa klabu walikuja kwangu nikiwa likizoni, ghafla walijitokeza kwenye mlango wangu na kuniambia wanataka kuendelea nami.”
“Manchester United wameniambia kwamba walizungumza na Tuchel, lakini hatimaye walifikia hitimisho kwamba tayari wana meneja bora,” aliongeza.
Katika msimu wake wa kwanza, Mholanzi huyo aliiongoza klabu hiyo hadi nafasi ya tatu kwenye Ligi Kuu, pamoja na fainali za Kombe la Carabao na Kombe la FA na Kisha akawaongoza kwa ushindi wa Kombe la EFL mnamo 2023.

BOSTON, Marekani
Boston Celtics walipata ubingwa wa 18 wa rekodi kwa kuwafunga Dallas Mavericks 106-88 na kukamilisha ushindi wa 4-1 katika Fainali za NBA.
Dallas walikuwa wameweka hai matumaini yao ya ubingwa kwa ushindi wa 122-84 siku ya Ijumaa na kuwanyima Celtics ushindi mnono katika msururu wa michuano yao bora kati ya saba.
Lakini mbele ya mashabiki wao wa nyumbani huko Boston, mbegu bora zilichochewa na ushindi wa Jayson Tatum wa alama 31.
Ushindi huo wa ubingwa ulikuwa wa kwanza kwa Celtics katika kipindi cha miaka 16, na unawafanya kuwa mbele zaidi ya Los Angeles Lakers, ambao wameshinda 17, kwenye vitabu vya rekodi.
Celtics walikuwa na nguvu tangu mwanzo na kuongoza kwa 67-46 katikati, huku Irving na Doncic wakizuiliwa kwa pointi 14 pekee kati yao katika robo ya kwanza.
Dallas walijizatiti kidogo katika hatua za mwisho za robo ya tatu, lakini bado hawakuweza kuwapita Celtics, ambao walichukua faida ya pointi 19 hadi robo ya mwisho.

DAR ES SALAAM

Na Alone Mpanduka

Mbio rasmi za kwanza za baiskeli zilifanyika mnamo 1868 huko Ufaransa. Mnamo mwaka 1885, baiskeli za usalama zilitengenezwa huko Coventry, Uingereza, binamu wa karibu wa baiskeli ya leo. Uendeshaji baiskeli ulianzishwa katika Olimpiki ya kwanza ya kisasa mwaka wa 1896. Mnamo 1903, Maurice Garin alishinda Tour de France ya kwanza, ambayo ilijumuisha maili 1,450 katika hatua sita. 1 Mei 2024.
Kulingana na rekodi za kihistoria, asili ya baiskeli ina mizizi yake katika bustani ya Palais Royal huko Paris, Ufaransa. Mnamo mwaka wa 1791, mtu mmoja aitwaye Comte de Sivrac alionekana akiwa amepanda kitu chenye magurudumu mawili kilichofahamika kama ‘celerifere’.Ikumbukwe kuwa usafiri mkuu wa miaka hiyo ulikuwa ni farasi.
Lakini, ikumbukwe pia kwamba mashindano ya kwanza kabisa ya baiskeli yenye mvuto duniani yalianzia nchini Ufaransa, yakifahamika kama Tour de France.
Ilikuwa ni Novemba mwaka 1902, ambapo Mkurugenzi wa gazeti la michezo la L’Auto, Henri Desgrange, alikuwa akitafuta njia ya kulishinda gazeti la Le Vélo kwa mauzo. Géo Lefèvre, mwandishi chipukizi wa gazeti la L’Auto alitoa pendekezo hili: “Kwa nini tusianzishe mashindano ya baiskeli kote nchini Ufaransa?”
Mwanzoni, wazo hilo lilionekana kuwa lisilowezekana. Hata hivyo, punde si punde likaanza kupamba moto. Alasiri ya Julai 1, 1903, saa 9:16 kamili, jijini Paris, waendeshaji 60 stadi na wengine, wakaanza mashindano yanayoitwa Tour de France ya majuma matatu yenye umbali wa kilometa 2,428.
Mara moja mashindano hayo yakawavutia watu wengi. Mashabiki wengi walikuja kutoka sehemu zote za Ufaransa ili kuwatazama na kuwashangilia washindanaji hao ambao Albert Londres, mwandishi wa habari wa Ufaransa, aliwaita “watumwa wa barabara.” Kwa kweli, katika miaka michache ya kwanza, mashindano hayo hayakuwa rahisi kwa sababu vifaa vilikuwa duni, barabara zilikuwa na mashimo, mikondo ilikuwa mirefu sana, na mara nyingi mikondo hiyo ilianza usiku.
Hatua kubwa ilipigwa kufikia mwaka wa 1919, wakati ambapo mshindi wa jumla wa kila siku alitunukiwa jezi la pekee la rangi ile ile ya kurasa za manjano za gazeti la L’Auto, yaani lile jezi la manjano ambalo hupendwa sana.
Mnamo mwaka wa 1931, Desgrange alibuni gari la matangazo ambalo liliwatangulia washindanaji kwa saa moja likiwachochea mashabiki barabarani, ili kulipia gharama za mashindano hayo.
Mauzo ya Gazeti la L’Auto, ambalo sasa linaitwa L’Équipe, yakapanda. Mwaka wa 1903, nakala 130,000 za toleo la pekee lililochapishwa dakika saba baada ya kufika kwa Maurice Garin, mshindi wa mashindano ya kwanza ya baiskeli nchini Ufaransa, zilinunuliwa mara moja kutoka kwenye vibanda vya kuuzia magazeti.
Siku hizi, kwa sababu mashindano hayo huonyeshwa kwenye televisheni katika nchi zaidi ya 150, mashindano hayo ya Ufaransa yanashikilia nafasi ya tatu kati ya mashindano ya michezo, ambayo husambazwa sana na vyombo vya habari, nafasi za kwanza mbili zikichukuliwa na Michezo ya Olimpiki, na Kombe la Dunia la Soka.
Mashindano hayo yamewavutia watu wengi sana hivi kwamba mwaka wa 1987 wabunge wa Hispania walikatiza mjadala wao ili kutazama ushindi wa mwananchi mwenzao Pedro Delgado akipiga zile kona kali 21 katika mkondo mgumu wa kupanda milima ya Alpe d’Huez.

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Benchi la Ufundi la Timu ya Soka ya Simba Queens kupitia kwa kocha msaidizi Mussa Mgosi, ametamba kuwa atahakikisha klabu hiyo inabeba ubingwa mpaka pale yeye atakapoondoka.
Mgosi (pichani) ametamba kuwa kutokana na uwezo waliokuwa nao wachezaji wake, watahakikisha wengine kombe hilo wanaishia kuliona wakati likiwa linatangazwa tu mwanzoni mwa msimu, lakini kulichukua itakuw ni story za Abunuasi.
Alisema pia kuwa umakini wa wachezaji wake, hasa wanapokuwa mazoezini kabla ya mechi, ndiyo sababu kuu ya kuwafanya wafanikiwe kuchukua ubingwa kwa mara nyingine tena.
Mgosi alisema kuwa lengo lao ni kuhakikisha wanapoenda kushiriki michuano ya Kimataifa waweze kufanya vizuri, na hili litawezekana tu mara baada ya kufanyika kwa usajili mkubwa ndani ya klabu yao kwa kuchukua wachezaji wenye uwezo.
“Tunataka kuuvunja utawala wa Mamelods na tutajitahidi kufanya usajili mzuri ili kubeba ubingwa wa Cecafa, na kisha tutafanya tena usajili kwa ajili ya Klabu bingwa ambayo ina timu zenye wachezaji wazuri wa kiushindani”, alisema Mgosi.
Alisema pia kuwa wachezaji wao wamekuwa chachu ya kufanikiwa klabu hiyo kwenye ligi yao kutokana na usikivu waliokuwa nao mara baada ya kumalizika kwa mechi na kuandaa maandalizi ya mechi nyingine.
Klabu hiyo kwa sasa inajiandaa na michuano ya Afrika kwa wanawake, ambapo msimu uliopita hawakufanikiwa kushiriki michuano hiyo kutokana na kuukosa ubingwa wa Ligi uliobebwa na klabu ya JKT Queens.

DAR ES SALAAM

Na Nicholaus Kilowoko

Kocha Jamhuri Kihwelo amesema haoni mchezaji yeyote mzawa wa kumfananisha na mshambuliaji John Bocco, hasa kwenye nidhamu ya ndani na nje ya uwanja.
Bocco ambaye alistaafu rasmi kuichezea timu ya Simba SC na kugeukia ukocha wa timu za vijana za Simba SC, hivi karibuni alipewa shukrani za dhati na kheri katika maisha yake mapya na uongozi wa wekundu hao.
Akimzungumzia mkongwe huyo, Kocha huyo mwenye jina maarufu kama Julio alisema anaufahamu vyema uwezo wake uwanjani, pamoja na nidhamu aliyonayo ambayo imemfikisha mahali pazuri kwenye soka lake, licha ya kutocheza soka nje ya nchi.
Alisema kuwa Tanzania ina wachezaji wengi wenye uwezo mkubwa wa soka lakini nidhamu yao si nzuri, na hivyo kuwafanya washindwe kufika mbali na kujikuta wanastaafu soka wakiwa na umri mdogo.
“Mimi nimefundisha wachezaji wengi waliojaaliwa vipaji vizuri na vikubwa, lakini hawana nidhamu ikilinganishwa na Bocco.Unaweza kuwaambia wachezaji waingie kambini siku fulani, lakini cha kushangaza wanachelewa kuripoti. Bocco alipojiunga na Simba akitokea Azam FC, aliibadilisha kwa kiasi kikubwa katika eneo la nidhamu,”alisema Julio.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Habari cha Klabu ya Soka ya Azam FC Thabit Zacharia maarufu kama Zaka Zakazi, alisema kwamba Bocco ataendelea kubaki katika mioyo ya mashabiki na viongozi wa Azam FC kutokana na nidhamu yake.
Alisema pia kuwa Bocco hakuwa mtu wa kupigana uwanjani ama kucheza rafu zisizo na msingi ama kuwa mtu wa starehe nje ya uwanja.
“Nakumbuka Bocco wakati yupo Azam FC, ikitokea Ligi imesimama kwa wiki moja ama mbili kupisha ratiba zingine, wachezaji wenzake wote walikuwa wanaondoka kwenye hosteli, yeye anabaki peke yake na kufanya mazoezi binafsi.Anaweza kuchukua mpira akawa anaukokota goli hadi goli. Hakuwa anaijua pombe wala starehe nyingine yoyote.”
Alisema kuwa Bocco ndiye aliyefunga mabao yaliyoiwezesha timu hiyo kutinga Ligi Kuu kwa mara ya kwanza mwaka 2008 na kisha kuchangia katika ubingwa iliyopata msimu wa 2013/14 na kukata tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa kwa mara ya kwanza katika historia yake.