Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

Dar es Salaam

Na Arone Mpanduka

Mshindi wa pili wa mbio za Boston Marathon Alphonce Felix Simbu, amesema kuwa kifo cha Baba Mtakatifu Fransisko kimeleta simanzi kubwa ulimwenguni, hasa kwa Wakatoliki.
Akizungumza na Tumaini Letu kwa njia ya simu, Simbu alisema kwamba kifo chake pia kimeleta pigo kubwa kwa wanamichezo kwa kuwa alikuwa mpenda michezo enzi za uhai wake.
“Sijapata nafasi ya kumfuatilia sana kwa upande wa michezo, lakini nimekuwa nikisikia kwamba alikuwa mdau mkubwa wa michezo mbalimbali. Mimi ninamuombea kwa Mungu apate pumziko la milele,”alisema.
Hivi karibuni Simbu aliandika historia mpya katika mbio za kilomita 42 kwa kushika nafasi ya pili, mbio za Boston Marathon zilizofanyika huko Massachusetts, Marekani.
Alimaliza mbio hizo kwa muda wa saa 2:05:04, akitanguliwa kwa sekunde chache na Mkenya John Korir aliyeibuka kidedea kwa muda wa saa 2:04:45, ikiwa ni muda wa pili kwa kasi zaidi katika historia ya mbio hizo.
Katika mbio hizo, Simbu alionesha ushindani wa hali ya juu, akiibuka kinara kutoka kwa kundi kubwa la wanariadha waliotabiriwa kufanya vizuri, akiwemo Cybrian Kotut wa Kenya aliyeshika nafasi ya tatu na Mmarekani Conner Mantz aliyemaliza wa nne.

Dar es Salaam

Na Mwandishi Wetu

Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini(TFF), limeahidi kuendelea kuwekeza kwenye teknolojia ya Msaidizi wa Video (VAR) kwa kutoa elimu kwa waamuzi wengi zaidi, na hata kuzalisha wakufunzi wazawa ili kuhakikisha usimamizi wa mechi nchini, unaendana sawa na mabadiliko kulingana na wakati kwa kufuata viwango vya kimataifa.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Sheria, Habari na Masoko wa Shirikisho hilo, Boniface Wambura ambaye pia ni Msimamizi Mkuu wa Kozi mbalimbali, zinazowezeshwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Alisema kuwa wanahitaji kuona mabadiliko chanya kwenye usimamizi wa mechi nchini, hivyo kupitia VAR wanaamini watapunguza malalamiko ya maamuzi na kuongeza ubora wa ligi na mashindano mengine wanayosimamia.
Alisema kwamba anaamini hadi kufikia muda rasmi wa kuanza matumizi ya teknolojia hiyo katika Ligi ya Tanzania, waamuzi wengi watakuwa na weledi mkubwa kuhusiana na matumizi yake.
Wambura alisema kuwa kozi hizo zitaendelea kutolewa kwa makundi mbalimbali, ili kuongeza zaidi idadi ya namba kubwa ya waamuzi wenye ujuzi wa kutumia teknolojia hiyo ya VAR.
Tayari TFF ilitangaza mpango wa kuanza kutumia baadhi ya mashine za VAR, ili kupunguza malalamiko ya kimaamuzi ingawa bado kuna uhitaji mkubwa wa mashine nyingi, ili kila uwanja uwe unatoa haki ya kimaamuzi.

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Licha ya ratiba na takwimu za msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kuonyesha kwamba Yanga imebakiza michezo minne ili kumaliza msimu huu, wenyewe wanasisitiza kwamba wamesaliwa na mechi tatu pekee.
Yanga imebakiza mechi dhidi ya Namungo FC (nyumbani), Tanzania Prisons (ugenini), Dodoma Jiji (nyumbani) na Simba SC (nyumbani).
Mbali na ratiba kuonyesha hivyo, wenyewe wamesisitiza kwamba kwa sasa anazifukuzia pointi zao tisa, ili wamalize Ligi na kushangilia ubingwa wa nne mfululizo wa Ligi Kuu.
Afisa Habari wa Klabu hiyo Ali Kamwe (Pichani) alisema kuwa wao wanachotambua kwa sasa wana kazi kubwa ya kuhakikisha wanashinda mechi tatu zilizo mbele yao.
“Tuna mechi tatu zilizobaki mbele yetu, tutajitahidi kuhakikisha tunapata ushindi mechi zetu zote ili kutangaza ubingwa, hiyo nyingine hatuifahamu na haituhusu. Mashabiki wetu tunawasihi wasianze sherehe sasa hivi, ni mapema mno kwa sababu hatujamaliza mechi zetu tatu,” alisema Kamwe.
Hadi sasa wapenzi wa soka wanasubiria siku ambayo Bodi ya Ligi itaweka wazi tarehe ya mchezo wa watani wa jadi Simba na Yanga, ambao ulipangwa kuchezwa Machi 8 mwaka huu lakini ukaahirishwa.
Bodi hiyo bado imeonekana kuwa na kigugumizi cha kupanga tarehe ya mechi hiyo, kufuatia Yanga kupeleka malalamiko katika Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo Duniani (CAS).
Tayari CAS hivi karibuni ilitoa siku 10 kwa walalamikiwa kuwasilisha utetezi wao, baada ya Yanga kupeleka rufaa yao kuhusiana na kile kilichotokea Machi 8.
Mchezo wa Simba na Yanga una umuhimu mkubwa, kuchezwa kwa sababu huenda ndio ukawa mchezo utakaompata bingwa wa Ligi Kuu msimu huu.
Hiyo itatokea endapo Simba na Yanga wote wakaendelea kushinda bila kupoteza pointi yoyote, hadi watakapokutana wenyewe kwa wenyewe.

Na Laura Chrispin

Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Petro – Oyesterbay, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Alister Makubi amewaasa wauguzi kuwa na roho ya huruma na wasiwe wa kwanza kuwakatia tamaa wengine, bali wawe mahujaji wa matumaini, huku wakitambua kuwa Yesu ndiye muuguzi wa kwanza aliyewaponya wagonjwa.
Padri Makubi aliyasema hayo hivi karibuni wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Jubilei ya Wauguzi na Wagonjwa, iliyofanyika katika Parokia ya Bikira Maria wa Fatima – Msimbazi, jimboni humo.
“Muuguzi hutakiwi kumkatia mtu tamaa, bali unatakiwa kuwa ni mtu wa matumaini kama Yesu alivyompa matumaini, yule mgonjwa aliyelala kwa miaka 38 kwa kumwambia ainuke na aende, na kuachana na maji yale yaliyokuwa kwenye birika,” alisema Padri Makubi, na kuongeza.
“Wauguzi kuweni na huruma kwa kuwatakia mema wagonjwa wenu, na kuwaambia wasimame na kuchukua magodoro yao ili waende, kwani wakati mwingine ugonjwa ni kama mradi, kwa sababu mtu anapoumwa, mwingine hufaidika.”
Padri huyo aliendelea kusema kuwa kila mtu anaumwa kimwili na kiroho, na kwamba wamepona kwa kufanya maungamo kwa kusafisha roho zao na kuwa watoto wapya wa Mungu.

Na Mathayo Kijazi

Wanaojigamba kutokana na afya, elimu, mali walizonazo, wametakiwa kuacha kufanya hivyo na kujiweka karibu zaidi na Mungu, kwani ndiye aliyewawezesha.
Wito huo ulitolewa na Askofu wa Jimbo Katoliki Teule la Bagamoyo, Mhashamu Stephano Lameck Musomba -OSA, wakati akitoa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Dominika ya 5 ya Kwaresma, katika Parokia Teule ya Mtakatifu Anthony wa Padua – Nyeburu, iliyopo chini ya Parokia ya Mtakatifu Yohane Paulo II - Buyuni, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.
“Afya, elimu, utajiri pamoja na mazuri yote uliyonayo, ni Mungu ndiye aliyekuwezesha kuvipata, ni Mungu ndiye aliyekufanya kuwa hivyo ulivyo. Na kwa sababu hiyo, kiri udhaifu wako mbele yake,” alisema Askofu Musomba.
Askofu Musomba aliwataka Waamini kuacha dhambi ya uzinzi pamoja na yale yote yasiyompendeza Mwenyezi Mungu, kwani hayo hayatoi utambulisho ulio bora mbele za Mungu.

Watawa wawili wa Shirika la Dada Wadogo wa Mtakatifu Teresa waliokuwa wakifanya kazi katika shule moja huko Mirebalais, nchini Haiti, wameuawa na magenge yenye silaha kali walipokuwa wamejificha katika nyumba na msichana mmoja wakati wa mashambulizi ya silaha.
Aidha, magenge hayo yenye silaha kali yaliingia ndani ya nyumba hiyo na kuwaua watawa hao pamoja na watu wengine wote waliokuwapo.
Katika ujumbe wake Baba Mtakatifu Fransisko baada ya sala ya Malaika wa Bwana Dominika ya 5 ya Kwaresima, pamoja na mambo mengine, alitoa wito wake katika maeneo yanayojihusisha na matumizi ya silaha, kuachana na ghasia zilizopo.
Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Port-au-Prince, nchini Haiti, Mhashamu Max Leroy Mésidor, alivithibitishia Vyombo vya Habari vya ndani kuhusu kutokea kwa tukio hilo, na kuongeza “Ni hasara kubwa kwa jumuiya.”
Watawa hao ni Sista Evanette Onezaire na Sista Jeanne Voltaire waliuawa hivi karibuni, huku Jiji la Mirebalais likikabiliwa na mashambulizi ya silaha na muungano wa wahalifu Viv Ansanm, ambapo ghasia hizo pia zilichukua sura ya mashambulizi dhidi ya wafanyabiashara, vituo vya polisi na hata gereza, na kwamba zaidi ya wafungwa 500 waliripotiwa kutoroka.

Na Paul Mabuga

Jua la adhuhuri liliwaka eneo kuu la biashara na lenye shughuli nyingi katikati ya Jiji la Mwanza. Nilimpa muuza magazeti, makala ya toleo la gazeti moja la kila siku la Kiswahili, kwa mwaliko wa kimya kimya wa kumshirikisha kwa habari zinazovutia siku hiyo.
Dakika zilipita, kisha nikauliza: “Ni nini kinakuvutia?” Alionesha tangazo la EWURA, mwanga wa matumaini mbele ya matatizo ya maji yasiyoisha.
“Ni kuhusu suluhisho,” alisema.  Nilisubiri zaidi, lakini kurasa alizipita na baadaye anasema hakuna cha ziada.
Baadaye, kwenye vurugu za soko la Mlango Mmoja. Muuzaji, macho yakimtoka, alilishika gazeti kana kwamba lilikuwa adimu, lakini kumbe kwake ni la gharama kubwa. “Shilingi 1000?” alisema kwa mshangao.
“Hiyo ni chakula cha mchana cha ugali na fulu!” Gharama, sio maudhui, pengine ndio ingeuwa kichwa cha habari kwake kuliko yaliyomo kwenye gazeti.
Kisha katika safari ya kurejea maskani nikiwa nimebanwa kwenye daladala, mazungumzo na jirani yangu, kijana aliyejitambulisha kuwa msomi, yalifunua mtazamo tofauti.
 “Mitandao ya kijamii,” alisema kwa dharau, akipitia kurasa. “Matukio ya moja kwa moja kwenye TV tunaona yote kwa haraka zaidi.” Kwa hiyo Gazeti, mikononi mwake, lilionekana kama halina cha maana, maana mengi alishayapata kabla. ZAIDI KWENYE TUMAINI LETU.

Na Joseph Mihangwa

Katika mkutano wa nchi tajiri duniani (G.8), uliofanyika Gleneagles, mwaka 2005, chini ya kauli mbiu ya “Ufanye Umaskini Uwe Historia”, nchi hizo ziliahidi kuipatia Afrika  dola za Kimarekani bilioni 50 ili zijikwamue kutoka kwenye umaskini.

Mpaka sasa nchi hizo hazijatekeleza ahadi yake, badala yake Afrika inaendelea kupata fedha za mzunguko wa mikopo kwa  masharti magumu.

Masharti hayo ni pamoja na kuuza/kubinafsisha Rasilimali za Taifa, kama tulivyofanya kwa Mashirika muhimu kama Benki ya NBC, NMB na mashinikizo mengine, kama vile kuruhusu vituo vya kijeshi vya Marekani nchini [AFRICOM], kutunga sheria dhidi ya “Ugaidi”, ambacho hiki kinachoitwa “Ugaidi” kusema kweli ni harakati za wanyonge dhidi ya ubabe, ubeberu na ukoloni mamboleo wa nchi za Magharibi.

Si hivyo tu, hata ahadi na misaada inayotolewa siku zote ni chini ya kiwango/kiasi kinachotamkwa. Na kwa mujibu wa taarifa ya Shirika  moja lisilo la Kiserikali barani Ulaya, CONCORD, iliyopewa jina, “Hold the Applause” [Usishangilie], ni kwamba, zaidi ya asilimia 30 ya sehemu ya misaada inayotolewa au kuahidiwa na nchi fadhili, si misaada halisi bali ni misaada iliyobinywa na urejeshaji kubebwa na Serikali inayofadhiliwa. INAENDELEA KWENYE GAZETI TUMAINI LETU.

HISTORIA YA KANISA

Na Askofu Mstaafu Method Kilaini

Mitume na wafuasi wa Kristo toka mwanzo kilele na kitovu cha Imani yao kilikuwa kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Injili zote zinasimulia juu ya wiki ya mwisho ya maisha ya Bwana wetu Yesu Kristo ulimenguni au kwa naneno mengine tunachoadhimisha kama Juma Kuu ikiwa ni matukio ya  kuwaaga mitume, kushikwa, kufa na kufufuka kwa Bwana wetu Yesu Kristo.
Hiki ndicho kilikuwa kilele cha simulizi zote. Kwa namna ya pekee tunayakuta katika Injili ya Mt. Yohana sura ya 12 hadi 20, ambayo inasimulia kwa kinaganaga juma hilo kuu. Mtakatifu Yohana alikuwa shuhuha wa matukio haya yote na hadi kifo chake aliyakumbuka kwa uwazi, yalimwachia alama kubwa katika maisha yake.
Yesu Kristo alikufa na kufufuka wakati wa maadhimisho ya Pasaka ya Wayahudi. Katika siku hizo Wayahudi humkumbuka Musa na kukombolewa kwao kutoka utumwani Misri. Huadhimisha mapatano kati ya Mungu na taifa lao la  Israel.
Pasaka, yalikuwa ni maadhimisho ya juma zima, wakikumbuka na kusimilia historia yao kuanzia baba zao walipokula chakula cha mwisho huko Misri, ikiwa ni mkate bila kutiwa chachu na mboga chungu na nyama ya kondoo, ambaye damu yake  waliipaka milango yao.

SOMA ZAIDI KATIKA TUMAINI LETU.

1. Utangulizi
Kipindi cha Kwaresima kinahusika na liturujia ya kubariki mafuta na kuweka wakfu Krisma. Askofu hana budi kuwa kuhani mkuu wa kundi lake. Maisha ya Waamini wake katika Kristo, kwa namna fulani yanatokana naye na kumtegemea yeye.
Askofu huadhimisha Misa ya Krisma, pamoja na Mapadri waliotoka sehemu mbalimbali za Jimbo Lake. Katika Misa hiyo huweka wakfu Krisma na kubariki mafuta mengine. Misa hii ya Krisma ni njia mojawapo kubwa ya kuonyesha ukamilifu wa Ukuhani wa Askofu, na ni ishara ya muungano mkubwa uliopo kati ya Askofu na Mapadri wake.
Misa ya Kubariki mafuta ya Krisma, hufanyika kabla ya Misa ya Karamu ya Mwisho ya Bwana. Misa haiadhimishwi bila mkusanyiko wa Waamini. soma kwenye Tumaini Letu