Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

VATICAN CITY

Hayati Baba Mtakatifu Fransisko ameacha wosia wake wa kiroho kwa Ulimwengu akisema kwamba, siku zote amekabidhi maisha na huduma yake ya Kipadri na Kiaskofu chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Bwana wetu Kristo Yesu.
Katika wosia wake huo Hayati Baba Mtakatifu Fransisko aliomba maisha yake ya kibinadamu yabaki yakipumzika, katika Kanisa Kuu la Bikira Maria Mkuu, huku akingojea Siku ya ufufuo wa wafu.
Alitamani kuona safari yake ya mwisho ya hapa duniani iishie mahali patakatifu pa Bikira Maria, mahali ambapo alienda kusali.
Mazishi ya Baba Mtakatifu yalifanyika Jumamosi tarehe 26 Aprili 2025, kwenye Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na kuongozwa na Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali.

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam amewataka Waamini kumtangaza Kristo, aliyefufuka kutoka kwa wafu.
Kardinali Pengo aliyasema hayo hivi karibuni wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Dominika ya Pasaka, iliyofanyika katika Parokia ya Mtakatifu Benedicto Abate-Wazo Hill.
“Katika kumtangaza Kristo inatakiwa uwe tofauti  na wengine kwa sababu wewe umepata Sakramenti, na uwe na msimamo wa kiimani na siyo kusema tu kwa sababu ni

maneno ambayo umeambiwa au kuhadithiwa, bali aone katika maisha yako kwamba una imani hiyo iliyo thabiti,”alisema Kardinali Pengo.
Kardinali Pengo alisema kwamba Kristo alimuita kila mmoja kudhihirisha ufufuko wake katika maisha ya kila mtu, na hiyo ndio iliwaongoza wafuasi wa Bwana tangu mwanzo wake na wote walikubali kufa kwa sababu hiyo.

Dar es Salaam

Na Laura Mwakalunde

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Sana Jude Thaddeaus Ruwa’ichi amewataka Wanakwaya kutambua kwamba wanapoimba muziki Mtakatifu,  wazo sio kutumbuiza bali ni kuinjilisha.
Rai hiyo aliitoa hivi karibuni katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Utume wa Kwaya Katoliki Tanzania (UKWAKATA), Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, iliyofanyika katika Parokia ya Mtakatifu Petro-Oysterbay, jimboni humo.
“Wanakwaya siyo watumbuizaji na kama unataka kutumbuiza, basi ni vyema kwenda kwenye mahall ya disco… lakini ukitaka kuinjilisha kwa kuishi ukristo wako na katika kanisa lako, huku ukimshukuru Mungu kwa zawadi ya kipaji alichokujalia cha kuinjilisha kwa njia ya kuimba, salia Kanisani,”alisema Askofu Mkuu Ruwa’ichi.
Aidha, alisema kuwa kila mbatizwa anaitwa kuwa shahidi wa Kristo kwa kutumia Kipaji alichojaliwa na Mungu, akiwaasa Wanaukwakata hao, kutumia vyema vipawa vyao.

Dar es Salaam

Na Mwandishi wetu

Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Rita wa Kashia-Goba Mwisho, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Musa Kihoo, amewataka Waamini kufuata mafundisho ya Bwana Yesu Kristo, kwa sababu  yeye ni njia ya ukweli ya kwenda Mbinguni.
Padri Kihoo alisema hayo wakati wa Ibada ya Ijumaa Kuu, Kuabudu Msalaba Mtakatifu iliyofanyika parokiani hapo.
Padri Kihoo alisema kwamba Waamini wengi wanamchukiza Bwana Yesu Kristo kwa kutenda dhambi, ikiwemo kusema uwongo, umbeya, kusengenya wenzao, kunyanyasa wapangaji na ujambazi.

VATICAN CITY-Vatican
Maadhimisho ya kumtangaza Mwenyeheri Carlo Acutis kuwa Mtakatifu yamesitishwa kufuatia kifo cha Papa Fransisko.
Maadhimisho hayo yaliyokuwa yafanyike Dominika ya Aprili 27, mwaka huu yamesitishwa kusubiria kupatikana kwa Baba Mtakatifu mpya.
Kijana huyo aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 15, kwa sababu ya ugonjwa wa saratani ya damu Oktoba 12, mwaka 2006 tayari ametangazwa Mwenyeheri huko Assisi Oktoba 10, mwaka 2020.
Mwili wake umekuwa ukipumzika tangu 2019, katika Kanisa la Mtakatifu Maria Mkuu (Maria maggiore), Assisi.
Kwa njia hiyo Ofisi ya Waandishi wa Habari ya Vatican imefahamisha kwamba, Adhimisho la Ekaristi Takatifu na ibada ya kutangazwa kuwa Mtakatifu iliyopangwa kufanyika katika Maadhimisho ya Jubilei ya Vijana, imesitishwa.

VATICAN City

Mkutano Mkuu wa kwanza wa Makardinali umeanza Aprili 22 mwaka huu, ikiwa ni siku moja baada ya kifo cha Baba Mtakatifu Fransisko.
Mkutano huo ulidumu kwa muda wa saa moja na nusu, ambapo Makardinali waliokuwepo katika Ukumbi wa Sinodi mpya walikuwa 90, walioanza kikao hicho kwa muda wa sala kwa ajili ya Papa Fransisko.
Makardinali hao waliapa kwa kuzingatia na kwa uaminifu kanuni za Katiba ya Kitume (Universi Dominici Gregis), kuhusu nafasi ya Kiti kilicho wazi cha Kitume na kuchaguliwa kwa Papa wa Roma, kasha wakaimba (Adsumus Sancte Spiritus), wimbo wa kumuomba Roho Mtakatifu awaangazie.

VATICAN CITY, Vatican

Miongoni mwa maneno ya mwisho ya Baba Mtakatifu Fransisko yalikuwa ni shukrani zake kwa msaidizi wake wa afya binafsi, Massimiliano Strappetti, kwa kumtia moyo kufanya safari yake ya mwisho katika kigari kidogo cha “Popemobile Dominika Aprili 20.
“Asante kwa kunirudisha kwenye Uwanja. Kupumzika alasiri, chakula cha jioni na utulivu, kisha alfajiri hisia za ugonjwa, kukosa fahamu na kifo, baada ya siku yake ya kusalimia, na kubariki Ulimwengu baada ya muda mrefu.
Miongoni mwa maneno ya mwisho ya Papa Fransisko ambayo aliyasema ni asante kwa wale ambao walimuhudumia katika wakati huu wa ugonjwa.
Lakini hata muda mrefu uliopita, walimwangalia bila kuchoka, kama vile Massimiliano Strappetti, muuguzi ambaye - kama alivyowahi kusema - aliokoa maisha yake kwa kupendekeza afanyiwe upasuaji wa tumbo, na ambaye Papa alimteua kuwa kama msaidizi wake wa afya tangu mwaka 2022.

Dar es Salaam

Na Pd. Gaston George Mkude

Kristo amefufuka kwelikweli, Aleluia, Aleluia!
Somo la Injili Takatifu ya leo imegawanyika katika sehemu kuu mbili. Kwanza ni Yesu anawavuvia Roho Mtakatifu wafuasi wake, na hivyo kuwapa uwezo dhidi ya uovu na yule mwovu, na ndio kuwaondolea watu dhambi zao. Hivyo Pasaka ni sherehe ya kuonja upendo na huruma ya Mungu, na ndio leo Mama Kanisa anatualika katika Dominika hii ya pili ya Pasaka kutafakari Huruma ya Mungu kwetu. Sehemu ya pili ni ile ya mtume asiyeamini bila kuona na kugusa madonda yake Yesu, ndiye Tomaso aliyejulikana pia kama Pacha.
Kabla ya mateso, kifo na ufufuko wake, Bwana wetu Yesu Kristo anawafundisha wanafunzi wake kuwa Yeye ndio Uzima na Ufufuo. Hivyo baada ya ufufuko wake anapowatokea wanafunzi wake siku ile ya kwanza ya Juma anawadhihirishia waziwazi mitume wake kuwa kweli ni mzima, na kuwasalimu kwa kuwatakia amani nafsini mwao baada ya kujawa na hofu na mahangaiko mengi baada ya kushuhudia mateso na kifo cha Bwana na Mwalimu wao. Ni kweli yeye mzima, amefufuka na mauti hayana tena nguvu dhidi yake! Ufufuko ni ushindi dhidi ya mauti na dhambi, ni ushindi wa upendo na huruma ya Mungu dhidi ya uovu na muovu. Pasaka ni tangazo la upendo na huruma ya Mungu kwa ulimwengu mzima. Pasaka ni Habari Njema kwetu tunaokimbilia huruma na upendo wa Mungu!

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Sana Jude Thaddaeus Ruwa’ichi akiwa na Mapadri na Viongozi wa UKWAKATA wa Jimbo baada ya Adhimisho la Misa Takatifu ya Jumatatu ya Pasaka iliyofanyika katika Parokia ya Mtakatifu Petro-Oyesterbay, Jimboni humo.

Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Agostino Salasala, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Peter Assenga, akiwa katika picha ya pamoja na Watawa wa Kike, Viongozi wa Kamati Tendaji na Wakatekumeni baada ya Adhimisho la Misa Takatifu ya Kesha la Pasaka, iliyofanyika parokiani hapo. (Picha zote na Yohana Kasosi)

Page 1 of 50