DAR ES SALAAM
Na Mwandishi wetu
Maadhimisho ya Jubilei Kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo, yananogeshwa na kauli mbiu “Mahujaji wa Matumaini.
Matumaini ya Waamini yako katika Msalaba, yaani katika Kristo Yesu, chemchemi ya wokovu wa mwanadamu aliyezaliwa katika Familia Takatifu iliyopata baraka ya kuwa na Mungu, yaani Emanueli, kati yake.
Maadhimisho ya Sikukuu ya Familia Takatifu Desemba 29, mwaka 2024, imekuwa ni fursa kwa Majimbo kufungua lango la Maadhimisho ya Jubilei Kuu.
Baba Mtakatifu Francisko, katika mkesha wa Noeli tarehe 24 Desemba 2024, amefungua Lango Kuu la Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, mwanzo wa maadhimisho ya Jubilei Kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo. Hili ni Lango la matumaini, chemchemi ya watu wote wa Mungu.
Maadhimisho ya Jubilei ni kwa ajili ya watu wote, ili kuwaonjesha tena matumaini ya Injili, matumaini ya mapendo na matumaini ya msamaha wa kweli. Pango la Noeli ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu; chemchemi ya matumaini; upendo wa Mungu unaovunjilia mbali ukaidi wa mwanadamu pamoja na hofu yake, tayari kutafakari ukuu wa matumaini yaliyo mbele ya mwanadamu. Mwelekeo huu, uwe ni mwangaza wa mapito ya kila siku ya mwanadamu.
Ni katika muktadha wa usiku huu ambapo “Lango Takatifu” la Moyo wa Mungu limefunguliwa. Kristo Yesu, Mungu pamoja nasi, anazaliwa kwa ajili ya binadamu wote.
Kumbe, pamoja naye, furaha ya dunia inachanua kama “maua ya kondeni.” Pamoja na Kristo Yesu, maisha yanabadilika na pamoja na Kristo Yesu “Spes non confundit” yaani “Tumaini halitahayarishi.” Rum, 5:5.
Maadhimisho ya Jubilei Kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo yananogeshwa na kauli mbiu “Mahujaji katika Matumaini.” Matumaini ya Waamini yako katika Msalaba, yaani katika Kristo Yesu, chemchemi ya wokovu wa mwanadamu aliyezaliwa katika Familia Takatifu iliyopata baraka ya kuwa na Mungu, yaani Emanueli kati yake. Maadhimisho ya Sikukuu ya Familia Takatifu Desemba 29, 2024 imekuwa ni fursa kwa Majimbo mbalimbali duniani kufungua lango la Maadhimisho ya Jubilei Kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo.
Januari Mosi mwaka 2025 itakuwa ni fursa kwa Parokia kufungua maadhimisho haya. Huu ni wito wa kutangaza na kushuhudia Imani yao kwa Kristo Yesu, Mlango wa uzima wa milele, na hivyo Wakristo wote wanaalikwa kuwa ni Mahujaji wa Matumaini yasiyo danganya; umoja unaopaswa kuimarishwa; kukuza na kujenga haki, amani na furaha ya kweli katika Kristo Yesu.
Kristo Yesu ndiye Lango la maisha ya uzima wa milele, anayewashirikisha waja wake Fumbo la upendo na huruma ya Mungu isiyokuwa na mipaka; huruma inayowakumbatia binadamu wote pasi na ubaguzi, changamoto na mwaliko wa kuambata toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha.
Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, katika Ibada ya kufungua Maadhimisho ya Mwaka wa Jubilei Kuu ya Mwaka 2025 ya Ukristo, amewataka watu wa Mungu kuzingatia mambo makuu manne, Kuzama zaidi katika kusoma, kutafakari na kuyaishi Maandiko Matakatifu.
Waamini wajitanabaishe kwa maisha yao ya Kikatoliki na hivyo kuachana na tabia ya kuwayawaya, kwani kwenye Kanisa Moja, Takatifu, Katoliki na la Mitume, kuna kila kitu Waamini wanachohitaji katika maisha yao ya kiroho, sanjari na wokovu. Zaidi soma Tumaini Letu