Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

Mchango wa Kanisa Tanzania wateka mazungumzo ya Rais Samia na Papa

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan (kushoto), akiwa katika mazungumzo ya kidiplomasia na Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Baba Mtakatifu Fransisko mjini Vatican alipofanya ziara ya Kitaifa, hivi karibuni. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan (kushoto), akiwa katika mazungumzo ya kidiplomasia na Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Baba Mtakatifu Fransisko mjini Vatican alipofanya ziara ya Kitaifa, hivi karibuni.

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Tanzania na Vatican zimeridhika na uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili kwa mchango wa Kanisa Katoliki katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu.
Katika mazungumzo ya faragha kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan na Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Baba Mtakatifu Fransisko yaliyodumu kwa takribani dakika 25, Viongozi hao waliridhika na mchango wa Kanisa katika sekta ya elimu, afya na ustawi wa jamii, licha ya changamoto ambazo Tanzania inapitia kwa sasa.
Aidha, Viongozi hao katika mazungumzo yao walijikita zaidi katika masuala ya kijamii, Kikanda, Kimataifa na umuhimu kudumisha amani miongoni mwa jamii.
Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Vatican ulianzishwa Aprili 19 mwaka 1968 na Askofu Mkuu Pierluigi Sartorelli aliyeteuliwa kuwa Balozi wa kwanza wa Vatican nchini Tanzania, utume alioutekeleza hadi Desemba 22 mwaka 1970.
Uhusiano huo kama alivyobainisha Baba Mtakatifu Benedikto XVI (2005-2013: wa 265, aliyefariki mwaka 2023), wakati akipokea hati za utambulisho kutoka kwa Balozi Ali Abeid Aman Karume wa Tanzania mjini Vatican, unasimikwa katika tunu msingi za Amani, haki, mshikamano na uhuru, kwani haya ni mambo yanayopata asili yake kutoka katika utu, heshima na haki msingi za binadamu, daima ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, yakipewa msukumo wa pekee.
Tangu mwanzo wa mchakato wa uinjilishaji nchini Tanzania, Kanisa limekuwa mstari wa mbele katika kuchangia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi hususan katika nyanja za elimu, afya, maendeleo na ustawi wa jamii, bila kusahau huduma ya maisha ya kiroho kwa watu wa Mungu nchini Tanzania, na katika mchakato wa kudumisha amani ulimwenguni.
Takwimu zinaonesha kwamba Kanisa Katoliki nchini Tanzania linamiliki na kuendesha Shule za Awali 240, Shule za Msingi 147, Shule za Sekondari 244, Vyuo vya ufundi, vyuo vikuu vitano; taasisi za elimu ya juu 5, na vituo viwili ambavyo viko chini ya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino, (St. Augustine University of Tanzania: SAUT), Mwanza.
Vyuo vyote hivyo vina jumla ya wanafunzi 31, 000 pamoja na taasisi 473 za afya, kwa lengo la kumhudumia mtu mzima: kiroho na kimwili, kwani kuna uhusiano mkubwa kati ya shule zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki, pamoja na dhamana ya Uinjilishaji wa kina inayovaliwa njuga na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Uinjilishaji nchini Tanzania.
Shule na taasisi za elimu ya juu pamoja na vyuo vikuu vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki nchini, vimekuwa ni vituo vya majiundo makini ya vijana, kiakili, kimaadili, kiroho na kiutu, kwa kuzingatia ubora na viwango vya kitaifa na kimataifa, ukweli ambao kamwe hauwezi kufumbiwa macho nchini Tanzania.
Elimu bora inayotolewa na Kanisa, inalenga kuwajengea wahitimu uwezo wa kujiamini na kumudu ushindani wa kitaifa na Kimataifa kwa kuwapatia: elimu, ujuzi na uwezo wa kushiriki katika ujenzi wa Tanzania, katika ujumla wake.
Historia inaonesha kuwa wakati wa mkesha wa uhuru wa Tanzania mwaka 1961, Baba Mtakatifu Yohane XXIII (1958-1963: wa 261), alitunga sala maalum kwa ajili ya kuiombea Tanzania ili uhuru wake uwawezeshe Watanzania kuishi maisha mema zaidi kadri iwastahilivyo watoto wa Mungu.
Imepita takribani miaka 12 tangu Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania alipotembelea mjini Vatican na kukutana na Baba Mtakatifu Benedikto XVI, Januari 19 mwaka 2012.
Katika ziara hiyo, Rais Samia aliambatana na Mama Evaline Malisa Ntenga, Mjumbe wa Bodi ya Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani na Rais wa World Union of Catholic Women’s Organisations (WUCWO) Afrika, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) Taifa, nchini Tanzania.
Wengine ni Profesa Deogratius Rutatora, Mwenyekiti Halmashauri ya Walei, Taifa; Leonard Mapolu, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana Wakatoliki Wafanyakazi Tanzania, Taifa, VIWAWA; Dalmas Gregory, Mwenyekiti Halmashauri Walei, Jimbo Katoliki la Zanzibar, na Theresia Seda, Mwenyekiti wa Utoto Mtakatifu, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.

Rate this item
(0 votes)

Leave a comment

Make sure you enter all the required information, indicated by an asterisk (*). HTML code is not allowed.