Na Askofu Method Kilaini
Katika safu hii ya Chimba Chimba Historia ya Kanisa wiki iliyopita, tuliwaletea historia ya Mafanikio ya Mtaguso wa Vatikano katika Kuimarisha Kanisa Katoliki. Leo tunawaletea Historia ya Dini ilivyokuwa wakati wa Mapinduzi ya Viwanda barani Ulaya. Sasa endelea…
Rerum Novarum:
Mei 15 mwaka 1891, Papa Leo XIII (1878-1903: wa 256) alichapisha barua yake ya Kitume maarufu sana hadi nyakati zetu ya Rerum Novarum (Mambo Mapya). Papa Leo XIII katika historia alijulikana zaidi kwa barua yake hii ya Rerum Novarum, iliyoongea juu ya ustawi wa jamii na haki za binadamu na jamii.
Huu ulikuwa wakati wa Mapinduzi ya Viwanda (Industrial Revolution), kwa sababu watu walikuwa hawana uwezo wa kulima na kupata faida, hivyo walikimbilia mjini na kuajiriwa katika viwanda. Hali ya waajiriwa ilikuwa mbaya sana, kwani walidhalilishwa na kuishi maisha yasiyo na staha.
Sheria ya uchumi huru ilikuwa ya soko huria, na kwa sababu walikuwepo watu wengi bila kazi, matajiri waliweza kuwatumkisha watu kama walivyotaka, ukikataa unafukuzwa, na kupata kazi ilikuwa ni vigumu.
Masaa ya kazi yalikuwa mengi na mshahara kidogo. Matajiri wakipata faida kubwa kwa taabu ya maskini. Wafanyakazi maskini hawakupewa na heshima ya utu. Karl Marx katika kitabu chake cha “Mtaji” (Das Kapital) na baadaye katika “Manifesto”, aliwaita na kuwahamasisha waajiriwa maskini wapigane na matajiri kwa msemo wake kwamba “Piganeni hamna kitu cha kupoteza, isipokuwa minyororo yenu.”
Mawazo yake yalichochea mfarakano kati ya waajiriwa na waajiri. Huu ndio ulikuwa msingi wa Ukomunisti ambao ulitangaza vita kati ya wenye nacho na wasio nacho, ili kuunda serikali inayodhibiti kila kitu.
Umma ulishika kila kitu, na mtu binafsi hakuwa na haki ya kumiliki hasa ardhi au viwanda. Papa Leo XIII alipinga mawazo yao. Alionyesha waziwazi kwamba Ukomunisti siyo suluhu hata kidogo, bali ni mbaya zaidi kuliko hata Ubepari.
Alikataa msemo wa Wakomunisti kwamba lazima pawepo vita na mgogoro kati ya waajiri na waajiriwa, matajiri na maskini. Dhidi ya dhana ya Wakomunisti, anatambua haki ya kuwa na mali binafsi.
Kwa maneno yake, wale wanaokataa haki hizi za umiliki wa kibinafsi, hawaoni kwamba wanamlaghai mwanadamu kile ambacho kazi yake mwenyewe imekizalisha. Uwezo wa kumiliki mali binafsi, anauita haki takatifu ya asili.
Papa Leo XIII alichambua hali halisi ya wakati huo, hasa mgongano kati ya wafanyakazi na waajiri. Wakati akitambua haki za watu kuwa na mali na kupata faida kutokana na uwekezaji wao, alisisitiza juu ya haki za wafanyakazi kupata mshahara unaoweza kuwapa heshima, na uwezo wa kuzitunza vizuri familia zao.
Alihimiza pia masaa ya kazi kutokuwa mengi, kutazama na jicho la wema watoto na wanawake ili wapate ahueni katika kazi. Ingawa ni vema kwa mwajiiri na mwajiriwa kupatana, kazi ya serikali ni kuhakikisha mfanyakazi anapata haki zake za msingi kwa sababu ni mnyonge, na hivyo rahisi kupunjwa na kuonewa.
Vile vile Papa anatambua wafanyakazi kuwa na haki ya kuwa na vyama vyao vya kujitetea (Vyama vya Wafanyakazi).
Kwa wakati wake, mawazo hayo yalikuwa ya kimapinduzi sana, na alikuwa ameona mbali. Kwa wakati huo, wengi hawakumwelewa, hasa Mabepari walimwita Mkomunisti. Kwa muda mrefu Mabepari hawakupenda au kukubali barua hii.
Wengi waliiona kama ya Kikomunisti mno, na hata kumwita Papa mwekundu yaani Mkomunisti. Labda ni kwa sababu aliifungua barua yake kwa maneno haya, “Lazima itafutwe haraka suluhu kwa ajili ya kuondoa taabu na unyonge usio wa haki unaowaelemea wengi wa wafanyakazi, ambao idadi ndogo ya matajiri imewawekea nira umma wa watu, inayofanana karibu na ile ya utumwa.”
Ni Papa Pio XI (1922 – 1939: wa 259) baada ya miaka 40 aliyeitambua na kuthamini ujumbe wa Papa Leo XIII wakati wa kuadhimisha miaka 40 ya barua hiyo. Kama kumbukumbu ya barua ya kitume ya Reruma Novarum mwaka 1931, alichapisha barua yake ya Kitume ‘Quadragesmo Anno’.
Katiba barua hiyo alirudia na kusifu mawazo ya Papa Leo XIII. Anaanza kwa kusisitiza kwamba Kanisa lina haki na wajibu wa kuongea juu ya mambo yanayohusu maadili, iwe katika siasa au katika uchumi.
Baada ya hapo, Papa wengine walitoa barua za kuadhimisha barua hiyo iliyolitoa Kanisa katika makucha ya mabwanyenye na matajiri, na kuliwaweka kati ya watetezi wa wanyonge.
Tangu wakati wa Mfalme Kostantino mwaka 313 hadi Napoleoni, na hasa Waitaliani walipovamia tawala za Papa, Kanisa lilikuwa sambamba na watawala hasa Wafalme na lenyewe kikiwa linatawala kama wao. Sasa likiwa limenyang’anywa ardhi na mali zao, liliweza kuelewa na kutetea maskini na wanyonge.
Kwa namna ya pekee mwaka 1961 Papa Yohana XXIII (1958-1963: wa 261) alitangaza barua kuu ya jamii “Mater et Magistra” yaani Kanisa kama “Mama na Mwalimu”. Katika barua hii licha ya kutetea wafanyakazi, alitetea Nchi maskini dhidi ya unyonyaji wa Nchi tajiri, na vile vile kutetea wakulima.
Papa Yohana XXIII akiwa bado Padri katika kutekeleza Rerum Novarum mwaka 1909, aliunga mkono wafanyakazi wa Bergamo walipogoma katika mgogoro wa pamba huko Bergamo, Italia. Aprili 11 mwaka 1963, aliandika barua nyingine “Pacem in Terris”, maana yake “Amani Duniani”.
Katika barua hii, aliwazungumzia kwa mara ya kwanza siyo tu Wakatoliki, bali watu wote wenye mapenzi mema, akionyesha kwamba amani ya kweli inatokana na kuheshimu haki za binadamu.
Aliwataka vile vile Waamini Wakatoliki wasipuuzie siasa, bali washiriki kikamilifu. Mawazo ya Papa Yohana XXIII yalikamilishwa na Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatikano (1963 -1965) katika hati yake ya “Gaudium et spes”, yaani ‘Hati ya Kichungaji juu ya Kanisa katika Ulimwengu wa Sasa’.
Maneno yaliyofungua hati hiyo, yalielezea lengo lake “FURAHA NA MATUMAINI (Gaudium et Spes), uchungu na fadhaa ya wanadamu wa nyakati zetu, hasa ya maskini na ya wale wote wanaoteswa, yote ni furaha na matumaini, uchungu na fadhaa ya wafuasi wa Kristo pia.”