Mwanza
Na Paul Mabuga
Kuna makundi kadhaa ya vizazi kutokana na mazingira na matukio katika nyakati mbali mbali.
Mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia, na hasa mapinduzi ya kidijitali, yamechangia zaidi kuongezeka kwa tofauti kati ya makundi ya vizazi, hali ambayo imeathiri mahusiano, mitindo ya maisha, na makuzi.
Uhusiano wa kizazi kimoja kwenda kingine, limekuwa ni jambo lenye changamoto kulimudu. Katika muktadha huo, mwandishi wetu Paul Mabuga anaangalia uhusiano kati ya wanandoa kutoka zama za ‘baby boomer’ na ‘milenia’.
Harufu ya sangara anayekaangwa, imetanda katika nyumba moja iliyopo katika mtaa wa Nyamanoro jijini Mwanza. Kwa hakika inavutia, kwani hata kwa mwenye hisia ndogo ya kunusa, anaweza kuitambua, na kwa mwenye njaa aliye jirani, ni lazima aombe msaada.
Baba mwenye nyumba tunayemwita Adam Fungamwango, yupo sebuleni akisoma gazeti. Unamtazama, unapokewa na sura yenye mikunjo inayokutangazia kuwa Bwana huyu umri wake kwa makadirio ni miaka 64. Na wewe ni mgeni pekee sebuleni.
“Karibu, lakini kabla ya yote fanya ufanyavyo kwenye mahojiano, lakini jina langu sitaki lijulikane! Vinginevyo hakuna mahojiano hapa,” anasema bwana huyu akikukaribisha na kuendelea na mazunguzo baada ya kuhakikishiwa kuwa litatumika jina bandia ili kuficha utambulisho wake, “Mie nilikuwa dereva, na nimeendesha maafisa wengi wakubwa, na sasa ni miaka minne tangu nimestaafu.”
Anasema, mkewe ambaye naye, tunamtambulisha, kwa jina la bandia la Diana Fungamwango, bado ni mfanyakazi kama katibu muhtasis katika moja ya mashirika ya umma jijini Mwanza, na ana umri wa miaka 44 kwa sasa. Walioana miaka 23 iliyopita, na kwamba Diana anatumia muda mwingi kazini isopokuwa siku za mwisho wa juma.
Diana ambaye ndiye anayekaanga samaki, hana makuu, katopea katika simu yake ya mkononi akitaradika na yaliyomo. Pengine anaanza leo wasanii gani wamechambana kwenye mitandao, anashuka na wale wasemaji wa timu za mpira na washabiki wao, na baadaye anatambaa na darasa la sifa za mume bora, na kumalizia na hadithi. Yeye ameshika mbili na wala hazimponyoki, huku ana simu, na kule anakaanga.
Hii ni ndoa kati ya mume ambaye katika zama za vizazi, yupo kwenye kundi la ‘Baby Boomer,’ ambao wamezaliwa kati ya miaka ya 1946 na1964 na mke ambaye yupo kwenye lile linalojulikana kama ‘milenia’, ambao walizaliwa kati ya 1981 na1996. Makundi haya ya vizazi na mengine, kila moja lina sifa zake,
Kwa maana hiyo watu katika kundi la ‘baby boomer’ wana umri kati ya miaka 61 na 79 kwa mwaka huu wa 2025. Kwa idadi kulingana na taasisi mbali mbali [Shirika la Takwimu la Taifa linalosimamia Sensa ya Watu na Makazi, (National Bereau of Statistics: NBS), na Benki ya Dunia, idadi yao hapa nchini ni kama milioni tatu, ama asilimia tano, ya Watanzania .
Wale walioko kwenye kundi la milenia, wana umri kati ya miaka 29 na 44, na idadi yao kulingana na taasisi hizo, inakadiriwa kuwa kama nilioni 12 ama asilimia 20 ya Watanzania kwa kadirio. Ni sawa na kusema ni kundi lenye watu wengi, na ambalo kwa idadi, ni mara nne ya lile la ‘baby’ boomer. Licha ya changamoto kadhaa, lakini kuna ndoa baina ya makundi haya kama ilivyo katika makala haya.
“Ni kweli kuna tofauti za kimtazamo katika baadhi ya mambo kati yangu na mke wangu, mathalan, mimi najali sana mambo ya maendeleo kitaifa, nikiona mtu anaonewa siwezi kupita bila kuhakikisha haki inapatikana;
Ninajali majaliwa ya taifa letu siku za usoni, na nipo tayari kujitolea kwa ajili ya jamii yangu,” anasema Fungamwango wakati alipotakiwa kufafanua baadhi ya mambo anayopendelea katika fikra zake,
Sifa hizi anazozieleza Mfungamwango, zinaelezwa na watafiti kuwa zinatokana na ukweli kwamba, ‘baby boomers’ walizaliwa katika kipindi cha harakati za kuleta mabadiliko katika jamii, na kupambania haki za binadamu, na hii ndiyo sababu ya wao kuwa hivi,
Kwa upande mwingine, tafiti zinaonesha kizazi cha milenia, kimetekwa na teknolojia, hasa kwa sababu wamekulia katika mazingira ya kuibuka na kushamiri kwa matumizi ya ‘internet’. Wana mapokeo yenye uwanda mkubwa ikilinganishwa na baby boomer na hivyo kuwafanya wao kuwa huru. Wanapenda kuwa wajasirimali na wanafanya kazi kwa uwiano na uhuru. Wanajali sana mitindo ya mavazi na vifaa vingine