DODOMA
Na Angela Kibwana
Watu wenye ulemavu sawa na makundi mengine katika jamii, wana haki ya kunufaika na upatikanaji wa haki ya Afya ya Uzazi, kama haki ya msingi ya binadamu bila vikwazo, unyanyapaa na ubaguzi wa aina yoyote.
Haki ya Afya ya Uzazi kwa watu wenye ulemavu imetamkwa na kuelekezwa kwenye Sera, Miongozo na Sheria mbalimbali za Kimataifa, Kikanda na Kitaifa kama vile: Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watu Wenye Ulemavu (2006), kifungu cha 25 (Article 25), umesisitiza watu wenye ulemavu, wana haki ya kupata huduma za afya bila ubaguzi
Sheria ya Tanzania kwa Watu Wenye Ulemavu (2010) kifungu cha 26, Kifungu kidogo cha Kwanza hadi cha tatu limesisitiza kuhusu haki ya kupata huduma ya afya na utengamao kwa watu wenye ulemavu, bila ubaguzi,Sera ya Watu Wenye Ulemavu ya Mwaka 2004, imetambua suala la ulemavu kama haki za msingi za binadamu.
Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, imeeleza watu wenye ulemavu ni wale wote wenye changamoto za muda mrefu za kimaumbile, kiakili na katika mfumo wa fahamu (intellectual or sensory), hivyo kukosa na kushindwa kushiriki sawa na makundi mengine ya kijamii katika kuzifikia fursa mbalimbali.
Takribani asilimia 11 ya watu kuanzia umri wa miaka saba (7) na kuendelea, wanaishi na ulemavu wa aina fulani, ikiwa ni ongezeko kutoka asilimia 9.3 (Sensa Mwaka 2012).
Hata hivyo, takwimu zinaonesha kuwa idadi ya watu wenye ulemavu inatofautiana kati ya kijijini kwa asilimia 11.5 na mjini asilimia 10.6.
Mkoa wa Dodoma una idadi ya watu 299,689, sawa na asilimia 12.3 zaidi ya kiwango cha kitaifa cha asilimia 11, ukiwa ni mkoa wa sita kwa idadi kubwa ya watu wenye ulemavu (Sensa Mwaka 2022) nchini.
Pamoja na jitahada zote zilizofanyika na zinazoendelea kufanyika na serikali, asasi zisizo za kiserikali na wadau wa maendeleo, kundi la watu wenye ulemavu, wameendelea kukabiliwa na changamoto nyingi za afya ya uzazi, zikijumuisha changamoto za kimazingira na kisera zinazo athiri upatikanaji na ufikikaji wa huduma za Afya, kwa mfano miundo mbinu isiyo rafiki, umbali na gharama za huduma na kukosekana kwa teknolojia saidizi.
Pia, unyanyapaa na mtazamo hasi kutoka kwa wana familia, jamii na watoa huduma za afya dhidi ya haki ya huduma za Afya ya Uzazi kwa watu wenye ulemavu; Ujumuishaji hafifu wa watu wenye ulemavu kwenye programu na mipango mbalimbali ya afya; watoa huduma za afya kutokuwa na uelewa kuhusu masuala yanayohusu mahitaji ya watu wenye ulemavu, kama vile lugha ya alama, pamoja na namna ya kutoa huduma rafiki kwao; matumizi hafifu, pamoja na kutokuwa na takwimu sahihi za watu wenye ulemavu ili kujumuishwa kwenye mipango, bajeti na huduma za afya katika ngazi ya halmashauri, vituo vya kutolea huduma za afya, na jamii kwa ujumla.
Changamoto hizo zimeongeza uhatarishi zaidi kwa makundi ya wanawake na vijanawenye ulemavu, hali ikiwa mbaya zaidi kwa wale wanaoishi vijijini wakikabiliwa na umaskini uliokithiri, pamoja na ukatili wa kingono, kama vile Ubakaji na ndoa za kulazimishwa.
Kwa kutambua changamoto na umuhimu wa haki ya hudumu za Afya ya uzazi kwa watu wenye ulemavu kama ilivyoainishwa katika Sera, Miongozo na Sheria za Kimataifa, Kikanda na Kitaifa; Shirika la Marie Stopes Tanzania, kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Watanzania chini, ya ufadhili wa Marie Stopes International (MSI) kupitia mradi wa Investiment Fund (IF), wameligeukia kundi hili ambalo halijafikiwa ipasavyo kwa kuwekeza fedha, utaalam na miundombinu, ili kutengeneza mazingira wezeshi kwa watu wenye ulemavu kuzifikia huduma bora za Afya ya Uzazi.
Hayo ni kama vile, Uzazi wa Mpango, Huduma wakati wa Ujauazito, Kujifungua, baada ya kujifungua, Ukatili wa Kijinsia na Ukatili dhidi ya watoto, elimu na taarifa sahihi kuhusu Afya ya Uzazi na Ujinsia, pamoja na ushiriki wa watu wenye ulemavu katika masuala yanayo athiri maisha yao, ikiwepo Afya Uzazi na Ujinsia kama ilivyoelezwa na Ndugu Goryo Moris Kitege, mtoa huduma za afya ya uzazi wa mpango kutoka Marie Stopes Tanzania
Pia, Ndugu Goryo alisema kuwa Shirika la Marie Stopes Tanzania kwa kushirikiana na Serikali, wanaendelea kuona namna watakavyowajengea uwezo watoa huduma za afya namna kuwahudumia watu wenye ulemavu, pamoja na kufanya ulaghabishi (advocacy), kuhusu uboreshaji wa mazingira wezeshi ili kufikia kundi kubwa la watu wenye ulemavu wa aina mbali mbali nchini.
Kwa mujibu wa Ndugu Amina Issa anayeishi na ulemavu wa kusikia kutoka Chama cha Viziwi Dodoma, anasema, “Mara nyingi hatupati huduma stahiki kutoka kwa watoa huduma za afya kwa kuwa watoa huduma hawajui Lugha ya Alama”
Pia, Amina anatoa mfano wa unyanyapaa wanaokutana nao watu wenye ulemavu, akisema, “Kuna wakati unakutana na kauli za kudhalilisha, kama vile ‘Hata wewe mtu mwenye ulemavu umeweza kupata ujauzito?’ Kauli hizi zina tuumiza sana,” kwani na sisi tunahisia na tuna haki ya kuwa na familia, pamoja na kufurahia maisha ya mahusiano na ujinsia kama watu wengine” hali hii inakatisha tamaa kwenda kupata huduma.
Vile vile katika kuendeleza jitahada za kuwafikia watu wenye ulemavu katika masuala ya Afya Uzazi; Marie Stopes Tanzania kwa kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu (SHIVYAWATA), wameendelea kutoa elimu na huduma bora za Afya ya Uzazi ambapo watu zaidi ya 300 wenye ulemavuwamepatiwa huduma na elimu kuhusu afya ya uzazi.
Justus Ngwantalima, Katibu wa SHIVYAWATA, anasisitiza kwamba ni muhimu kwa jamii kuwa na mtazamo chanya dhidi ya watu wenye ulemavu, ili kufanikisha lengo la usawa katika jamii kwa mujibu wa sera na sheria za nchi.
Kwa mujibu wa Omary Lubuva, Mwenyekiti wa SHIVYAWATA Dodoma,kuna haja ya kuboresha mfumo wa mawasiliano ili kuimarisha upatikanaji wa huduma bora kwa watu wenye ulemavu.
Pia, wataalamu wa afya wanapaswa kupewa mafunzo maalum ya kushughulikia mahitaji ya kundi hili.
Aidha, watu wenye ulemavu wanapaswa kushirikishwa katika kupanga, kutekeleza na kutathmini mipango na bajeti za afya kama ilivyoelekezwa kwenye sera na miongozo mbalimbali ya kimataifa, na ya nchi kwa ujumla.
Hata hivyo, aliwashukuru Marie Stopes Tanzania pamoja na serikali kwa jitahada zao katika kuwashirikisha kushughulikia mahitaji yao; kwani si jambo jepesi kulifikia kundi kubwa kama hili la watu wenye mahitaji maalumu kwa wakati mmoja, hivyo nguvu ielekezwe pia kwa watu wenye ulemavu walio vijijini kwa njia shirikishi na endelevu.
Katika mahojiano ya mwandishi wetu na Mratibu wa Huduma za Afya ya Uzazi na Mtoto wa Wilaya ya Bahi, Ndugu Agnes Mwabungulu, anasema kuwa vituo vingi vya afya havina miundombinu rafiki kwa watu wenye ulemavu.
Pia, anabainisha ukosefu wa wataalamu wenye ujuzi wa Lugha ya Alama kama changamoto kubwa.
Hata hivyo, amesema kuwa serikali kwa kutumia rasilimali chache zilizopo, pamoja na kupitia ushirikiano na wadau, wamekuwa wakikabiliana na changamoto mbalimbali zinazo athiri utoaji, upatikanaji na utumiaji wa huduma za afya uzazi kwa watu wenye ulemavu, kulingana na sera na miongozo ya nchi.
Aliongeza kwa kusema kuwa jitahada za kuwafikia watu wenye ulemavu, hazilengi tu kuwafikia katika hali yao ya uhitaji, bali kuzuia ulemavu kwa watoto wanaowazaa, unaoweza kuchangiwa na kukosekana kwa huduma bora kabla, wakati wa ujauzito, kujifungua na baada ya kujifungua. Hivyo kuongeza changamoto zaidi kwao, serikali, jamii na watoto watakaozaliwa na ulemavu wa aina mbalimbali.
Mwisho, amewashukuru Marie Stopes Tanzania na wadau wa maendeleo kwa ushirikiano wa, na kazi nzuri wanayoifanya katika Halmashauri ya Bahi, ili kuimarisha upatikanaji wa huduma za Afya ya Uzazi kwa mtoto na vijana.
Pia, wanawakaribisha kwa ushirikiano zaidi pamoja na wadau wengine, ili kuwakufikia watu wenye ulemavu, pamoja na makundi mengine yenye changamoto katika jamii.