Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

DAR ES SALAAM

Na Arone Mpanduka

Afisa Habari wa Klabu ya soka ya Ruvu Shooting, Masau Bwire amesema kuwa timu yake imeanza maandalizi ya sherehe za ubingwa wa Ligi Kuu ya msimu huu, licha ya kwamba bado ni mapema.
Akizungumza hivi karibuni katika mahojiano maalum, Bwire alisema kwamba wanajivunia maandalizi waliyofanya kabla ya msimu kuanza na sasa wana kikosi imara.
Alisema pia kuwa wamesajili kikosi kizuri ambacho kinaweza kuhimili ushindani katika Ligi ikilinganishwa na timu zingine.
“Sisi tuna kikosi kizuri, na falsafa yetu siku zote ni kuwa na wachezaji wazawa.Hicho ndicho kitu tunachojivunia.Wanaotudharau wakija kucheza na sisi watakiona cha mtema kuni,”alisema Bwire.
Alisema kwamba hakuna timu iliyoandikiwa kupata ubingwa siku zote kwa sababu ubingwa ni haki ya kila timu inayowania, na kwamba hawapo kwenye Ligi kwa ajili ya kupoteza muda au kusindikiza tu timu zingine.
“Huwa tunasikia tu eti kuna timu zimesajili Wazungu, zingine Wabrazil, zingine Wajapan, lakini sisi hatutetereshwi na mbwembwe zao.Sisi tutawaonyesha uwanjani”       
Alisema kuwa kuna timu zinawadharau, lakini mechi inapokaribia matumbo yao yanavurugika kwa hofu ya kufungwa.

DAR ES SALAAM

Na John Kimweri

Imeelezwa kuwa kiburi cha elimu ni sababu mojawapo inayowafanya watu kuacha kumwamini Mungu, na kutegemea utashi wao na mali walizonazo, kama jawabu katika maisha.
Kauli hiyo ilitolewa na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Stephano Musomba, wakati akitoa homilia yake kwenye Adhimisho la Misa Takatifu ya Sakramenti ya Kipaimara kwa vijana 125, iliyofanyika Parokia ya Mtakatifu Martin wa Porres, Mwananyamala.
Askofu Musomba (pichani) alisema kuwa kiburi ni dhambi na ndiyo chanzo cha migogoro mingi duniani, akiwataka waamini  kuhakikisha licha ya elimu walizonazo, lakini watambue uwepo wa Mungu katika maisha yao kwa sababu bila yeye, hawawezi kufanya kitu chochote.
“Kiburi cha usomi kinaweza kusababisha mtu akaona kuwa hakuna Mungu, na eti anajiweza yeye mwenyewe bila ya msaada wa Mungu, kiburi ni dhambi kubwa sana na ndiyo chanzo cha migogoro mingi duniani,” alisema Askofu Musomba.
Askofu  Musomba, alieleza kuwa kiburi kingine ni cha maendeleo na kiroho, akiwaonya waamini wanaojiona kuwa wamekamilika kuliko wengine kuacha kufanya hivyo.
Aliwakumbusha wazazi kuhakikisha kuwa wanapowarithisha  watoto wao mali na vitu vingine vya thamani, wasisahau kuwarithisha imani, kwani hilo ni jambo lisiloharibika wala kuchakaa.     
Aidha, aliwataka waimarishwa kutambua kwamba wanapopokea Sakramenti hiyo, Roho Mtakatifu anaingia ndani mwao na kuwafanya kuwa wapya katika kila jambo, huku akiwaasa wazazi nao kuwa na desturi ya kusali pamoja, na pia kusoma Neno la Mungu na watoto wao.  
Alisema kwamba Roho Mtakatifu ni nyenzo ya utume ya kuwasaidia waamini kuinjilisha hapa duniani, na kudai kuwa utume wa kweli unatakiwa kuanzia kwenye ngazi ya familia.
Kwa mujibu wa Askofu  Musomba, utii unamfanya mtu akabidhi utashi na kuwa mtii kwa Mungu mwenyewe, na kuongeza kwamba pia utii huendana na usikivu, ambapo mwisho wake huleta unyenyekevu kwa mtu.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Walei Parokia hiyo, Jeremia Mchomvu, alisema kuwa Parokia hiyo ina jumla ya waamini 6757, kutokana na sensa iliyofanyika Januari mwaka 2020.
Alisema kuwa Parokia kwa sasa ina mpango wa kununua nyumba mbili, ili kupanua eneo la kanisa.

Padri Germine Laizer akiwavisha rozari baadhi ya wanachama wapya wa Chama cha Wajane na Wagane

Dar es Salaam

Na Benedikto Agostino

Wajane na Wagane nchini wametakiwa kuendelea kuishi fadhila za Mtakatifu Monica bila kukata tamaa, na kumshukuru Mungu kwa maisha ya wenzi wao waliotangulia mbele ya haki, bila kusahau kuwaombea hao na watoto waliochwa na wazazi wao kila mara.
Hayo yalisemwa na Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Kamili, Yombo Kiwalani, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaaam, Padri Germine Laizer, wakati akihubiri katika Adhimisho la MIsa Takatifu ya Somo wa Wajane na Wagane, Mtakatifu Monica, iliyofanyika kwa ngazi ya Jimbo katika Parokia hiyo.
Katika homilia yake, Padri Laizer aliwakumbusha wajane na wagane kutambua maisha ya Mtakatifu Somo wao, Monica, kama mjane aliyeishi katika mateso na maisha mabaya ya mwanae Augustino, lakini licha ya kupitia changamoto hizo, hakukata tamaa hadi mtoto wake alipoongoka, na sasa ni Mtakatifu.
Alisema kwamba pamoja na ujane na ugane wao, ni muhimu kuishi fadhila ya unyenyekevu, kwani ni ishara ya itii mbele ya Mungu na watu, na hasa kila mmoja anapojishusha na kuwa kama mtoto mdogo.
“Maisha yetu yana maana kubwa kila tunapojinyenyekeza na kujikabidhi mbele ya Mwenyezi Mungu, kwani kila mmoja wetu anadaiwa kadri anavyokuwa mkuu kunyenyekea,” alisema Padri Laizer.
Aliongeza kusema kwamba watu wengi walioishii fadhila hiyo ya unyenyekevu wamepata kibali mbele za Mungu, na kujibiwa sala na maombi yao na kumbukumbu lao linaishi hata hivi leo.
“Tabia ya kiburi na majivuno ni kinyume cha unyenyekevu, na mara baada  ya mtu kuwa na maisha hayo, hali ya mtu hubadilika na kuharibika kabisa,” alisema Padri Laizer.
Alisema kuwa tukiongozwa na unyenyekevu ni lazima tufike mbali, kwani fadhila hiyo inalipa, na hakuna aliyeishi hali hiyo ambaye hakufanikiwa kamwe.
“Ni wazi unyenyekevu unapokosekana popote, yanatawala mafarakano, uogomvi na majigambo, hali inayotawanya kundi na kupoteza amani na mshikamano miongoni mwa familia ya Mungu,” alisema padri huyo.
Aliwataka waamini kuiga mfano mzuri wa mtu pekee aliyeishi fadhila ya unyenyekevu, ambaye ni Bikira Maria ambapo pamoja na magumu aliyoyapitia, aliyaweka mengi moyoni mwake.
Naye Mwenyekiti wa Wajane na Wagane Jimbo, Sweetbeter Mzungu alimshukuru Paroko wa Parokia hiyo, kwa utayari wake wa kupokea ujio wa sherehe hizo, na kuwapongeza wanachama wote waliojitokeza kufanikisha shughuli hiyo muhimu ambayo hufanyika mara moja kila mwaka.
Sweetbeter alisema kwamba moja ya mafanikio makubwa kwa sasa ni hatua waliopiga kutoka kutambuliwa kama kikundi na kuwa chama cha kitume ingawa bado changamoto kubwa ni mwitikio, hasa wa kupokelewa katika Parokia zote.
Alibainsha kuwa mara nyingi watu wengi hawapendi kujitambulisha kama wajane au wagane, na hali hiyo hutokana na kutokujikubali au kuipokea baada ya kuondokewa na wapendwa wao, na hasa wagane.

MOSHI

Na Mwandishi wetu

Mkuu wa Jeshi la Polisi (Inspector General of Police: IGP) nchini, Camillus Wambura amesema kwamba takwimu za makosa makubwa ya jinai nchini yameongezeka katika kipindi cha Januari hadi Juni mwaka 2022.
IGP Wambura aliyasema hayo wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha maofisa wa waandamizi wa Jeshi la Polisi Makao Makuu, na makamanda wa Polisi wa Mikoa na Vikosi, akisema kuwa makosa hayo yameongezeka kutoka 24,848 kipindi kama hicho mwaka 2021 hadi makosa 27,848, sawa na ongezeko la asilimia 11.2.

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Wanachama wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) wamesema wamekumbwa na mashaka kuhusu matumizi ya michango yao.
Kwa nyakati tofauti, wanachama hao  wamesema hawana imani kama michango yao bado ipo salama kutokana na hali ya namna ilivyokuwa ikiendeshwa ndani ya CWT.

DODOMA

Na Ndahani Lugunya

Wakristo nchini wametakiwa kufanya kazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo, kuchangia Pato la Taifa, na kutatua changamoto katika maeneo yao.
Hayo yalielezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, George Simbachawene, wakati akizunguma katika sherehe ya kumweka wakfu Askofu wa  tatu wa Kanisa  la Anglikana, Dayosisi ya Mpwapwa, George Chiteto, iliyofanyika Jijini Dodoma, baada ya aliyekuwa Askofu wa Kanisa hilo, Askofu Donald Mtetemela kustaafu.
Simbachawene alisema kuwa changamoto nyingi za kiuchumi katika jamii zitatatuliwa endapo wananchi watajituma kufanya kazi na kuwa wabunifu  kwa kuanzisha miradi mbalimbali, kama ambavyo Maandiko Matakatifu yanavyoagiza watu kufanya kazi.
“Lazima Wakristo wa sasa tufanye kazi, lazima tutatue changamoto kwenye maeneo yetu kwa sababu imeandikwa katika Biblia, ‘asiyefanya kazi na asile’, kwa hiyo kufanya kazi ndio uhai wako, heshima yako na ukizalisha, utaweza kuendesha maisha yako binafsi,” alisema Simbachawene.
Aliongeza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na Taasisi za Dini, kwani zimekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo, kusimamia maadili na kupambana na vitendo vya mmomonyoko wa maadili kwa baadhi ya watu wasio na hofu ya Mungu.
Aidha, alibainisha kwamba Serikali inaendelea  kuchukua hatua za kisheria kwa watu wote wanaojihusisha na vitendo vya rushwa, ufisadi, utovu wa nidhamu kwa watumishi wa umma, pamoja na jamii kwa ujumla.
Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania, Dk. Maimbo  Mndolwa, aliipongeza Serikali kwa kuwa mstari wa mbele kuziunga mkono Taasisi za Dini  katika nyanja zote, huku akimtaka Askofu Chiteto kufanya kazi kwa kumtegemea Mungu, hatimaye kufikia malengo ya Kanisa.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary  Senyamule  aliwataka wakazi wa mkoa huo kutumia fursa ya Serikali  kushusha bei ya  mbolea kwa kujikita katika kilimo.

Washington DC, USA
Mwanasiasa wa Kamanda wa Washington, Brian Robinson amefanyiwa upasuaji baada ya kupigwa risasi wakati wa jaribio la wizi wa kutumia silaha, au wizi wa gari.
Nyota huyo wa Washington Commanders, Brian Robinson alipata majeraha yasiyo ya kutishia maisha, baada ya kupigwa risasi.
Idara ya Polisi ya Washington DC ilisema kwamba Robinson alipata majeraha mawili ya risasi kwenye chini ya mguu wakati wa tukio hilo lililotekea Jumapili.
Tukio hilo lilitokea mwendo wa saa 18:00 kwa saa za huko, katika mji mkuu wa Marekani. Polisi walisema washukiwa wawili walitoroka eneo la tukio, na bunduki ilipatikana karibu.
Siku ya Jumatatu, Robinson aliandika kwenye Instagram kwamba “upasuaji ulikwenda vizuri.”
Kocha wake mkuu Ron Rivera alimtembelea Robinson Jumapili jioni, na kusema Robinson “anaendelea vyema”.

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi (mwenye Fimbo ya Kiaskofu), akiwa na Maaskofu Wasaidizi wake, Mhashamu Henry Mchamungu (mbele kulia), na Mhashamu Stephano Musomba (mbele kushoto), wakiwa katika Maandamano ya kuingia katika viwanja vya Seminari Ndogo ya Visiga, kwa Adhimisho la Misa Takatifu ya Kilele cha Miaka 50 ya Jubilei ya WAWATA, Jimboni humo. (Picha na Yohana Kasosi)

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi, akiwauliza maswali vijana wa Parokia ya Mtakatifu Dominiko Savio, Mikoroshoni, Jimboni humo kabla ya kuwapa Sakramenti Takatifu ya Kipaimara, wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya kutoa Sakramenti hiyo. (Picha na Yohana Kasosi)

Na Pd. Richard Mjigwa

Siku ya Kuombea Utunzaji Bora wa Mazingira kwa mwaka 2022, imebebwa na Kauli mbiu: “Sikilizeni Kilio cha Kazi ya Uumbaji.”
Baba Mtakatifu Fransisko anakazia wongofu wa kiikolojia; (COP27) utakaofanyika Misri, Novemba 2022, Umuhimu wa utunzaji bora wa mazingira na deni kubwa la kiikolojia. Wongofu wa kiikolojia ni dhana ya Mt. Yohane Paulo II wakati ambapo Mt. Paulo alikazia wongofu wa janga la kiikolijia
Siku ya Kuombea Utunzaji Bora wa Mazingira kwa upande wa Kanisa Katoliki inayoadhimishwa tarehe 1 Septemba 2022 inanogeshwa na kauli mbiu “Sikilizeni Kilio cha Kazi ya Uumbaji.” Siku hii ilianzishwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 10 Agosti 2015, kama sehemu ya mchakato endelevu na fungamani wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu, 2015-2016.
Baba Mtakatifu aliwataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha kazi ya uumbaji. Kwa kuthamini na kujali umuhimu wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, maadhimisho haya yakachukua mfumo wa kiekumene na kilele chake ni hapo tarehe 4 Oktoba ya kila mwaka.
Hii ni Sikukuu ya Mtakatifu Fransisko wa Assisi, aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya maskini, amani na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Hii ni dira na mwongozo wa maisha na utume wa Baba Mtakatifu Fransisko kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Hiki ni kipindi muafaka cha kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kazi kubwa ya uumbaji sanjari na kujibu kwa vitendo kilio cha Mama Dunia na Maskini, hawa ndio wale “Akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi.”
Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol katika maadhimisho haya anakazia umuhimu wa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote kwa kujikita katika mchakato wa uwajibikaji, ushirikiano na mshikamano wa udugu wa kibinadamu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.
Utunzaji bora wa mazingira hauna budi kwenda sanjari na huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa ajili ya Siku ya Kuombea Utunzaji Bora wa Mazingira kwa mwaka 2022 anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema akisema: “Sikilizeni Kilio cha Kazi ya Uumbaji.”
Anakazia wongofu wa kiikolojia katika maisha ya kiroho, Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP27) utakaofanyika nchini Misri, Mwezi Novemba 2022, Umuhimu wa utunzaji wa bora wa mazingira nyumba ya wote pamoja na deni kubwa la kiikolojia.
Wongofu wa kiikolojia ni changamoto iliyoyolewa na Mtakatifu Yohane Paulo II wakati ambapo wongofu wa janga la kiikolijia ni dhana iliyovaliwa njuga na Mtakatifu Paulo VI, mwaliko wa kusikiliza na kujibu kilio cha Mama Dunia na Maskini, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.
Baba Mtakatifu Fransisko anasema, ikolojia ya maisha ya kiroho iwahamasishe waamini kuwa na shauku ya kulinda mazingira, kwa kufungamanisha maisha ya kiroho na utunzaji bora wa mazingira, kwa kutambua uwepo angavu wa Mungu katika kazi ya uumbaji, kwa kuonesha moyo wa ukarimu na kujali kwa kutambua kwamba, ulimwengu ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, mwaliko wa kujitoa sadaka kwa ajili ya matendo ya huruma.
Kazi ya uumbaji na kilio cha maskini ni mambo yanayopaswa kupewa msukumo wa pekee, bila kuwasahau watu mahalia ambao kimsingi wamekuwa wahanga wa athari za mabadililo ya tabianchi kama vile: ukame wa kutisha, mafuriko, vimbunga pamoja na ongezeko kubwa la kiwango cha joto duniani. Lakini, ikumbukwe kwamba, kilio cha maskini kina nguvu kwani kinapanda hadi mbinguni.
Uchoyo na ubinafsi ni sababu kubwa ya kilio cha Mama Dunia na maskini na kwamba vijana wanawataka watu wazima, kusimama kidete kulinda ikolojia ya ulimwengu huu, kwa kuheshimu kazi ya uumbaji; kwa toba na wongofu wa ndani, kwa kujenga na kudumisha urafiki mpya na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani.
Changamoto ya utunzaji bora wa mazingira haina budi kupewa kipaumbele cha pekee kama ilivyo pia kwa sekta ya afya na vita sehemu mbalimbali za dunia, wito kwa wote ni wongofu wa kiikolijia unaosimikwa katika wongofu wa kijumuiya ili kuleta mabadiliko ya kudumu; mambo yanayopaswa pia kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa.
Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP27) utakaofanyika nchini Misri, Mwezi Novemba 2022 ni sehemu ya mchakato kwa Jumuiya ya Kimataifa kutekeleza kwa vitendo Makubaliano ya Mkataba wa Paris kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, COP21.
Kwa hakika kizazi cha Karne ya 21 kitakumbukwa kwa kubeba dhamana na wajibu wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Kiwango cha wastani wa nyuzi joto 1.5C ndicho kinachotakiwa vinginevyo, Jumuiya ya Kimataifa itakuwa inakabiliana na janga kubwa la uchafuzi wa mazingira nyumba ya wote.
Kumbe, changamoto ya kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa kwa asilimia 45% ifikapo mwaka 2030 ni muhimu sana. Umoja wa Mataifa unabainisha kwamba, kuna haja ya kutekeleza kwa vitendo upunguzaji wa nyuzi joto 1.5C kama ilivyobainishwa kwenye Makubaliano ya Paris chini ya mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi.
Kila nchi itaamua kiwango cha mchango wake katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Kiwango hicho kitategemea uchumi wa nchi husika na pia kiasi cha uzalishaji wa gesijoto. Kuongeza uwekezaji wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa angalau asilimia 50% ya fedha za jumla za ufadhili wa umma wa mabadiliko ya tabianchi.
Yote haya yanahitaji wongofu wa kiikolijia, unaojikita katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; maendeleo fungamani ya binadamu, mshikamano wa udugu wa kibinadamu sanjari na upendo.
Wongofu wa kiikolojia unahitaji haki jamii hasa kwa watu maskini ambao wanaathirika vibaya kutokana na mabadiliko ya tabianchi. Mkutano wa 15 wa Umoja wa Mataifa wa Bioanuwai (COP-15) utafanyika kuanzia tarehe 7 – 19 Desemba 2022 huko Montreal, Canada.
“UN Biodiversity Conference (COP 15) 7 - 19 December 2022 Montreal, Canada.” Huku zaidi ya spishi milioni moja za wanyama na mimea zikitishiwa kutoweka na robo tatu ya mfumo wa ikolojia wa Dunia kubadilishwa na shughuli za binadamu, COP-15 lazima ianzishe mfumo mpya wa kimataifa ili kukomesha mmomonyoko wa bayoanuwai ifikapo mwaka 2030.
Baba Mtakatifu Fransisko anakaza kusema, mintarafu hekima ya kale, maadhimisho ya Jubilei ni muda muafaka wa: “kukumbuka, kurudi, kupumzika na kurejesha.” Lengo ni kudhibiti kuporomoka zaidi kwa bayoanuwai, inayojenga “mtandao wa maisha” ambao mwanadamu amekirimiwa na Mwenyezi Mungu.
Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kufikia makubaliano juu ya Kanuni Nne Muhimu: 1. kujenga msingi wa kimaadili wazi kwa ajili ya mabadiliko yanayohitajika ili kuokoa viumbe hai; 2. Kupambana na upotevu wa viumbe hai, kusaidia uhifadhi na ushirikiano, na kukidhi mahitaji ya watu kwa njia endelevu; 3.
Kukuza mshikamano wa kimataifa kwa kuzingatia ukweli kwamba, bayoanuwai ni mafao ya pamoja ya Kimataifa yanayodai dhamira ya pamoja; na 4. Kutoa kipaumbele cha kwanza kwa watu walio katika mazingira magumu, ikiwa ni pamoja na wale walioathirika zaidi na upotevu wa viumbe hai, kama vile watu asilia, wazee na vijana.
Baba Mtakatifu Francisko anarudia kusema: “Kwa jina la Mwenyezi Mungu, naomba makampuni makubwa ya uchimbaji madini na mafuta; uvunaji misitu, mali isiyohamishika, pamoja na biashara ya kilimo kuacha kuharibu misitu, ardhi oevu na milima; kuacha kuchafua mito na bahari, kuacha kutia sumu kwenye chakula sanjari na kujali watu na mazingira.
Je, tunawezaje kushindwa kukiri kuwepo kwa “deni la kiikolojia” (Laudato si’, 51) lililofanywa na nchi tajiri kiuchumi, ambazo zimechafua zaidi katika karne mbili zilizopita; hii inadai kwamba wachukue hatua kabambe zaidi katika COP27 na COP15.
Mbali na hatua zilizoamuliwa ndani ya mipaka yao, hii ina maana ya kuweka ahadi zao za msaada wa kifedha na kiufundi kwa Nchi maskini zaidi kiuchumi, ambazo tayari zinakabiliwa na mzigo mkubwa wa mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi.
Inafaa pia kuzingatia kwa haraka msaada zaidi wa rasilimali fedha kwa ajili ya uhifadhi wa bayoanuwai. Hata zile nchi tajiri kidogo kiuchumi zina majukumu makubwa japokuwa zinatofautiana katika suala hili; kuchelewa kwa upande wa wengine kamwe hakuwezi kuhalalisha kushindwa kwetu sisi wenyewe kuchukua hatua. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kufanya maamuzi magumu kwani hali ni tete sana.
Kipindi hiki cha Sala kwa ajili ya kuombea Kazi ya Uumbaji, waamini wamwombe Mwenyezi Mungu, ili kwamba, Mikutano ya COP27 na COP15 iweze kutumika kuunganisha familia ya binadamu katika kukabiliana barabara na athari za mabadiliko ya tabia nchi sanjari na kupunguza bayoanuwai.
 Jumuiya ya Kimataifa ikumbuke himizo la Mtakatifu Paulo, Mwalimu na Mtume wa Mataifa: la kufurahi pamoja na wale wanaofurahi na kulia pamoja na wale wanaolia (Rej. Rum 12:15), watu waguswe na sala ya uchungu kuhusu kazi ya uumbaji na kutikia sala hii kwa vitendo, ili kizazi hiki na vizazi vijavyo viendelee kumshangilia na kumtukuza Mwenyezi Mungu kwa wimbo mtamu wa Kazi ya Uumbaji, Uhai na Matumaini.