Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

SINGIDA

Na Mwandishi wetu

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amewataka wananchi watakaopitiwa na mradi wa ujenzi wa barabara ya Sabasaba-Sepuka-Ndago-Kizaga mkoani Singida yenye urefu wa Kilometa 77.6, kutohujumu mradi huo kwa kutokuiba vifaa ili kufanikisha ujenzi huo kukamilika kwa wakati.
Bashungwa aliyasema hayo katika hafla ya kukabidhi mradi huo kwa Mkandarasi Henan Highway Engineering Group Ltd ya nchini China, kuanza kazi ya ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
“Serikali imetoa fedha nyingi za utekelezaji wa miradi mbalimbali kote nchini ikiwemo ya Mkoa wa Singida, hivyo niwapongeze wananchi kwa ushirikiano mnaowapa wakandarasi. Hata hivyo, nitoe tahadhari ya wizi wa mali na vifaa vitakavyotumika katika ujenzi, naomba viongozi muwasisitize wananchi wanaozunguka maeneo ya mradi kuepukana na uhalifu wa aina yoyote kwa vifaa hivyo, badala yake wavilinde,” alisema Bashungwa.
Katika hatua nyingine, Bashungwa aliwataka Wakala wa Barabara nchini (Tanzania National Roads Agency: TANROADS), kuhakikisha wanamsimamia kikamilifu mkandarasi huyo ili kukamilisha kazi hiyo kwa wakati uliopangwa na ubora.
“TANROADS nyie ndio wenye dhamana ya kusimamia ujenzi wa barabara hapa nchini, jipangeni vizuri ili ujenzi ukamilike ndani ya muda uliokusudiwa na kwa ubora, na si vinginevyo,” alisema Bashungwa.
Bashungwa alisema kwamba ujenzi wa barabara hiyo utagharimu Sh.Bilioni 88.583 bila kujumlisha kodi ya ongezeko la thamani VAT Sh. Bilioni 15.944, chini ya kampuni hiyo.
Bashungwa alitumia nafasi hiyo kumpongeza Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohammed Besta na watendaji wenzake, pamoja na viongozi wote wa Mkoa wa Singida kwa kuandaa vizuri hafla hiyo, na kueleza kuwa Singida imefungua njia, na sasa ataanza ziara ya kwenda kuwakabidhi wakandarasi miradi iliyopo katika wilaya mbalimbali, akiambatana na Wabunge wa maeneo ilipo, ambayo imekwishatengewa fedha na Serikali.
Naye Waziri wa Fedha Dk. Mwigulu Nchemba ambaye pia ni Mbunge wa Iramba Magharibi, naye alikuwa mwenyeji wa makabidhiano hayo ya barabara hiyo, pamoja na Mbunge wa Singida Magharibi, Elibariki Kingu, aliwataka Watanzania kuwa wamoja, hasa katika suala la kuinua uchumi wa nchi, kazi ambayo Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imeianza kwa kushirikisha sekta binafsi katika uwekezaji wa uchumi.
“Mimi kitaaluma ni mchumi, hakuna nchi yoyote duniani ambayo inaweza kukuza uchumi wake pasipo kuwekeza kwenye sekta binafsi, na katika jambo hili hatutarudi nyuma, kwani litaongeza mapato ya nchi na kutuwezesha kutoa ajira nyingi, ikiwa ni pamoja na za wauguzi ambao watakuwa wakifanya kazi kwenye vituo vya afya tulivyovijenga nchi nzima,” alisema Mwigulu.
Alisema kwamba kumekuwa na tofauti katika jambo hilo la uwekezaji hadi kufikia hatua ya kutaka kufarakana kati yao, ambao wapo wanaoamini kwamba kupitia uwekezaji, watapiga hatua, na wenzao ambao hawautaki, wakidai Serikali inaweza kufanya kazi hiyo peke yake.
Mwigulu alitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za ujenzi wa barabara hiyo ambayo alikuwa ameanza kuiomba tangu alipoingia bungeni kwa mara ya kwanza, barabara ambayo inakwenda kuinua uchumi wa wananchi wa Wilaya za Ikungi, Iramba, Mkoa wa Singida na nchi kwa ujumla, kutokana na kupata masoko ya mazao yao.
Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi, Elibariki Kingu, licha ya kumshukuru Rais Samia kwa kutoa fedha za ujenzi wa barabara hiyo, alitoa onyo kwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, Freeman Mbowe aache kumsakama Rais Samia kwa kumteua Mohamed Mchengerwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) si kwa sababu ni mkwe wake, bali inatokana na uchapa kazi wake uliotukuka kabla hajawa waziri, na baada ya kuwa Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, na Wizara ya Maliasili na Utalii.
Akitoa taarifa fupi ya mradi huo, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohammed Besta, alisema kwamba barabara hiyo inapita katika maeneo yenye uchumi wa kilimo, misitu, madini na rasilimali nyingi ambazo hazichangii kikamilifu kwenye Pato la Taifa, kutokana na kutopitika kiurahisi.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba akitoa taarifa fupi ya maendeleo ya mkoa huo, alisema una vijiji 441, kati ya vijiji hivyo, vijiji 341 tayari vina umeme, na vijiji 100 ambavyo havina, wakandarasi wapo kazini.
Alisema pia kwamba mambo hayo yote yanafanyika kwa ufundi na ustadi wa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amefanya mambo mengi katika miradi ya maji, sekta ya elimu na mingine mingi, ikiwemo minara ya simu na kilimo cha mazao yote ya alizeti, mpunga, mahindi, dengu, vitunguu, pamba, na kueleza kuwa anaamini sasa kwamba Mkoa wa Singida unakwenda kuwa kinara wa uzalishaji wa mafuta ya kula, na mazao yote ya chakula na biashara yanayolimwa mkoani humo.
Mkurugenzi wa kampuni hiyo iliyopewa kazi ya kujenga barabara hiyo, Huang Lele, alisema kwamba wamejipanga kukamilisha kazi hiyo kwa wakati uliopangwa, na akaomba kupewa ushirikiano kwa kuzingatia kuwa China na Tanzania ni marafiki wa muda mrefu.

Mbinga

Na Mwandishi wetu

Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma imefanikisha mpango wa kumtua ndoo kichwani mama baada ya kuanzisha huduma ya maji.
Hatua hiyo imetokana na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wilayani Mbinga kukamilisha ujenzi wa mradi mkubwa wa maji utakaohudumia zaidi ya wakazi 3,600 wa kijiji hicho, na kijiji cha Mangwangala.

Songwe

Na Mwandishi wetu

Halmashauri ya Wilaya ya Songwe, mkoani Songwe imepatiwa magari matatu ya kubebea wagonjwa (Ambulances) ili kutoa huduma za dharura na kwa rufaa za matibabu kwa wananchi.
Waziri wa Afya Ummy Mwalimu (pichani) alitoa taarifa hiyo wakati akizungumza na Madaktari, Wauguzi na timu ya usimamizi wa Afya ngazi ya Halmashauri katika ziara yake mkoani Songwe.

DAR ES SALAAM

Na Esther Ngubes- TUDARCO

Wakatoliki wametakiwa kuepuka dhuluma, wizi na rushwa kwa sababu ni matendo maovu mbele ya Mungu.
Aidha, wameaswa kuacha kujihusisha na vitendo vya utoaji mimba, na wenye kushiriki vitendo hivyo vya uuaji yawapasa kufanya toba kwa Mwenyezi Mungu.
Wito huo ulitolewa hivi karibuni na Padri wa Jimbo Katoliki la Shiyanga, Padri Dunstan Sita, wakati akitoa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Dominika, iliyofanyika katika Parokia ya Bikira Maria Mama wa Mwokozi, Sinza, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.
“Tunaalikwa kuwa na moyo mkuu, moyo hodari, na hatupaswi kuwa na deni…baadhi ya familia hususan wazazi na walezi, wanawasaidia mabinti kutoa mimba, jambo hilo ni baya na watu wanatakiwa wakatubu,” alisema Padri Sita.
Padri huyo alisema kwamba waamini wanapaswa kuwa sababu ya watu wengine ili kufikia malengo na mafanikio yao, na kuwa taa kwa kuwaonya watu wanaokosea katika ngazi za familia hadi Jumuiya.
Aliendelea kusema kwamba Kanisa lina wajibu mkubwa wa kuonya na kuwasaidia watu wanaokosea na wale wenye kwenda kinyume na maadili.
Padri Sita alisema pia kuwa dhambi ni chukizo kwa Mungu, hivyo waamini wasiwe wanatakiwa kuanza kuishi kwa mazoea, na badala yake waonyeshe upendo kwa wenzao.

DAR ES SALAAM

Na Eva Paul – TUDARCO

Wananchi wa Mtaa wa Mikongeni, Manisipaa ya Ilala Jijini Dar es Salaam, wameiomba Serikali kuimarisha ulinzi na usalama ili kudhibiti vitendo vya uhalifu vilivyokithiri katika eneo hilo.
Akizungumza na gazeti la Tumaini Letu katika mahojiano maalumu, Mjumbe wa nyumba kumi katika mtaa huo, Sara Malimbwi, alisema kuwa mtaa huo unakabiliwa na makundi ya vijana wanaovamia watu majumbani, na kuwaibia mali zao.
“Ni watoto wadogo tu, ambao walipaswa wawe shule, lakini wamejiingiza kwenye makundi ya wahuni, yaani ukiwaona utasikitika, kwani ni watoto wadogo, wengine hata darasa la saba hawajamaliza, lakini tayari wameshaacha shule, kutwa wanashinda vijiweni… Sisi kama wazazi tunaumia sana kuona watoto wanaharibika kiasi hiki, lakini hatuna cha kufanya,” alisema Sara.
Aliwasihi wazazi na walezi kuwaonya na kuwadhibiti watoto wao ili waache vitendo vya wizi.
Baadhi ya wananchi hao walisema kwamba vijana hao wanaotembea kwa makundi, wamekuwa wakiwavamia wananchi, hata nyakati za mchana.
Kwa upande wao baadhi ya wakazi wa eneo hilo, walisema kuwa wanashangazwa kwa kukithiri uhalifu huo, licha ya kuwepo kwa ulinzi shirikishi unaochangiwa na malipo ya Shilingi 1000/= kwa mwezi kwa kila kaya.
“Tunalipa pesa ya ulinzi, lakini bado tunaibiwa, sasa walinzi wanafanya kazi gani?...” alihoji Hassan Selemani mkazi wa mtaa huo.
Naye Anna Lucas, mkazi wa eneo hilo alisema kuwa vitendo hivyo vimewachosha, kwani vimekithiri mtaani hapo.

DAR ES SALAAM

Na Mathayo Kijazi

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi amesema kuwa Kanisa halihitaji Mapadri wanaolaza damu katika utume wao, hivyo Padri anapopokea Daraja hilo Takatifu, anapaswa kuwa mchakarikaji katika Kanisa la Mungu.
Askofu Mkuu Ruwa’ichi alisema hayo hivi karibuni wakati akihubiri katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Daraja Takatifu la Upadri kwa Shemasi Emmanuel Mushi -P.O.C.R, iliyofanyika Parokia ya Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu – Buza, jimboni humo.
“Tunamwomba Mungu aliyekujalia wito wa kuwa Mtawa na kuwa Padri, akujaze Roho wake Mtakatifu, akujaze nguvu na neema, akupe mvuto na ari ya kuwa Padri mwema, Padri mwadilifu, Padri Mtakatifu, Padri mchakarikaji katika Kanisa la Mungu,” alisema Askofu Mkuu Ruwa’ichi, na kuongeza,
“Hatuhitaji Mapadri wanaolaza damu, na wewe ujitahidi usiwe kuwa Padri wa kulaza damu…, uwe Padri wa kujitosa, kwa sababu anayekuita anataka uwe Padri unayefurahi kuwa Padri, uliye tayari kuuishi Upadri wako kiadilifu, kuuishi Upadri wako kiheshima, kuuishi Upadri wako ukichuchumilia utakatifu.”
Aidha, Askofu Mkuu Ruwa’ichi, aliwataka waamini kumwombea Padri Emmanuel ili akue na kuimarika katika utakatifu kama Kuhani na Kasisi wa Bwana.
Wakati huo huo, Askofu Ruwa’ichi aliwasihi Wakristo kumwomba Mungu ili aendelee kuwaita vijana wengi wenye afya, akili timamu, walio watakatifu na waadilifu, ili wapokee wito wa kumtumikia Kristo ndani ya Kanisa lake kwa kuwa Mapadri.
Aliwakumbusha pia kumshukuru Mungu kwa zawadi ya Padri Emmanuel, kwani amepata wito huo si kwa mastahili yake, bali kwa mastahili ya Mungu Mwenyezi.
Padri Emmanuel ametakiwa kujibidiisha kuwakusanya waamini kuwa familia moja, ili waweze kusimama katika misingi ya kumpendeza Mungu.
Aidha, Askofu Mkuu Ruwa’ichi alilipongeza Shirika la Mapadri la Aldorin, kwa kupata Padri mpya.
Aliwashukuru wazazi wa Padri huyo kwa kumzaa, kumlea na kumtoa kwa Mungu kwa ukarimu, kwani wapo baadhi ya wazazi wasio na mtazamo sahihi, mathalani huwakataza watoto wao kutumikia miito yao.
“Kila mtoto ni mali ya Mungu… kwa hiyo kazi ya wazazi ni kuwalea watoto wao kama atakavyo Mungu, siyo kama watakavyo wao. Jifunzeni kuwalea watoto wenu ili watimize yale ambayo ni mpango wa Mungu kwa maisha yao, siyo mpango wenu kwa maisha yao,” alisema Askofu Ruwa’ichi.
Askofu Ruwa’ichi aliziasa familia zote ziwe ni kitalu cha kulea Miito Mitakatifu, kwani katika shamba la Bwana, mavuno ni mengi, ila watendakazi ni wachache.

TRIPOL, Libya

Katika telegramu kwa Balozi wa Vatican huko Rabat nchini Libya, Baba Mtakatifu Fransisko anaonesha uchungu, na kuwaombea marehemu zaidi ya 2,300 waliofariki dunia kutokana na mafuriko yaliyokumba eneo la mashariki mwa nchi na kueleza ukaribu kwa walionusurika na waokoaji.
Askofu Overend, Msimamizi wa Kitume wa Benghazi, alisema kuwa kuna hitaji kubwa la msaada wa kiutu kwa waathirika wa tukio hilo.
Kwa mujibu wa waraka wa Baba Mtakatifu, faraja, nguvu na ustahimilivu, ndiyo maombi yake kwa ajili ya watu wa Mungu walioathiriwa na uharibifu uliosababishwa na mafuriko mashariki mwa Libya.
Waraka huo wa Baba Mtakatuifu umewasilishwa kwa njia ya telegramu iliyotiwa saini na Kardinali Pietro Parolin, Katibu wa Vatican akielekezwa kwa Balozi wa Vatican, Askofu Mkuu Savio Hon Tai-Fai.
Baba Mtaklatifu alisema kuwa ameguswa ka kiasi kikubwa kuhusu hasara kubwa ya maisha na uharibifu uliosababishwa na mafuriko katika eneo la mashariki mwa Libya, na anawahakikishia maombi yake kwa ajili ya roho za marehemu na wale wote wanaoomboleza kupoteza wapendwa wao.
Baba Mtakatifu pia anaonesha ukaribu wa kina wa kiroho kwa waliojeruhiwa, kwa wale wanaoogopa wapendwa wao waliopotea na wafanyakazi wa dharura wanaotoa msaada na usaidizi. Kwa wale wote walioguswa na janga hilo, Baba Mtakatifu Fransisko kwa utashi wake mwema, anawaombea baraka za Mungu za faraja, nguvu na uvumilivu,” unasomeka Ujumbe huo uliotiwa saini na Katibu wa Vatican.
Idadi ya watu waliopotea kufuatia mafuriko yaliyosababishwa na kimbunga Daniel kilichosababisha vifo vya watu 2,300 katika eneo la mashariki mwa nchi, kulingana na idadi kubwa ya watu waliopotea ni 10,000.
Mkuu wa ujumbe wa Msalaba Mwekundu katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa uliofanyika mjini Geneva, Uswisi, aliyeunganishwa kupitia video na Tunisia alisema kuwa dhoruba kali baada ya kuzuru Ugiriki, Uturuki na Bulgaria, ilisababisha kuporomoka kwa wakati mmoja kwa mabwawa mawili ambayo yalitoa lita milioni 33 za maji. Kwa hiyo hali ni mbaya kama ile ya Morocco, ambayo inashughulikia matokeo ya tetemeko la ardhi.
Kwa upande wake Askofu Sandro Overend Rigillo, Msimamizi wa Kitume huko Benghazi, aliyefikiwa kwa njia ya simu na Vatican News, alisema kwamba mahali walipo kulikuwa kumetulia hata kama kulikuwa na dhoruba kali na mabomu ya maji, hapakuwapo na matatizo.

BERLIN, Ujerumani

Baba Mtakatifu Fransisko ametuma salam zake katika Mkutano wa Kimataifa wa Sala ya Amani wa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, huko Berlin, Ujerumani, akisema kuwa vita bado vinaendelea kuitesa dunia.
Katika salamu zake hizo Baba Mtakatifu alisema, “Hatuwezi kujikabidhi…inahitaji kufanya kitu zaidi, inahitaji shauku ya amani ambayo iko kwenye kitovu cha mkutano wenu.”
Alisema kuwa bado haitoshi kuona mazingatio ya kisiasa kwani vipengele vya kimkakati vinavyotekelezwa hadi sasa havijaleta matokeo chanya katika kuleta utulivu duniani.
Baba Mtakatifu Fransisko  katika ujumbe huo, aliwaeleza kuwa wanakusanyika pamoja mjini Berlin katika Mlango  wa Brandeburg, ambako Wakuu wa Makanisa na Viongozi wa Dini za kidunia, na Mamlaka ya kiraia walioalikwa na Jumuiya ya Mtakatifu Egidio ambao kwa uaminifu wanaendelea na hija ya sala na mazungumzo yaliyoanzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II huko Assisi, mwaka 1986.
Eneo wanalofanyia mkutano kwa namna ya pekee, linakumbusha hasa jambo la kihistoria; kuanguka kwa ukuta ambao ulikuwa unatengenisha Ujerumani mbili, ukuta huo ulikuwa unagawanya hata dunia mbili za Mashariki na Magharibi mwa Ulaya.
Kuanguka kwake ukuta huo, kulitokana na mchakato wa matukio mbali mbali, ujasiri wa wengi na sala za wengi, zilizofungua njia mpya za uhuru kwa ajili ya watu, kuunganisha familia lakini hata matumaini ya amani mpya ya ulimwengu, baada ya vita vya baridi.
Baba Mtakatifu Fransisko alisema kuwa kwa bahati mbaya kadri miaka inavyokwenda, hapakujengeka matumaini haya ya pamoja, lakini juu ya mafao maalum na juu ya kutokuaminiana kwa mtazamo wa wengine. Kwa njia hiyo, badala ya kuvunja kuta, zimesimikwa nyingine.
Na kuanza kutengeneza mitaro ambayo kwa bahati mbaya na mara nyingi ni fupi. Leo hii vita vimetapakaa sana katika sehemu mbali mbali za dunia. Papa amekumbuka sehemu za Afrika na Nchi za Mashariki ya Kati, lakini pia hata katika kanda nyingi za sayari; na Ulaya, ambayo inafahamika kwa vita vya kwa mgogoro wa Ukraine usiosemekana ambao hauoni mwisho, na umesababisha vifo, majeruhi, uchungi, kuhama na uharibifu.
“Mwaka jana nilikuwa nanyi huko Roma, katikka uwanja wa Masalia ya Kale (Koloseo), kuombea amani.”

DAR ES SALAAM

Na Joseph Mihangwa

Mzungu hajakubali kuwa bin-Adam wote ni sawa, wala kwamba wote ni wa baba mmoja, Adam. Pamoja na kwamba alituletea Msahafu wa Dini, yaani Biblia wenye kusisitiza “upendo”, hiyo ni ghiliba tupu kwa sababu inawabagua wana-Adam kati ya walio wana wa Taifa teule la Mungu [Israeli] na wana wa Mataifa yasiyo teule. Huko ni kukweza ngozi nyeupe.
Kwa kutumia Mungu wa kujiundia [Yahweh] na Msahafu wa kibeberu, wanaidhinishwa kutugeuza watumwa wao, eti kwamba: “Na wageni watakuwa watumwa wa kulisha mifugo yenu; na wana wa Mataifa watawalimia na kutunza mashamba ya mizabibu yenu”. Huo ndio ubaguzi wa ubeberu wa kimataifa ambao umedumu hadi leo.
Ubaguzi huo kwa misingi ya rangi ulioasisiwa, kusimikwa na kukomazwa Kimataifa na Mjerumani Johann Friedrich Blumenbach [1752 – 1840], unawagawa bin-Adam kwa viwango vya ubora katika makundi sita ya Watu weupe [Coucassians] kama daraja la kwanza; Wamongolia [Mongoloid] daraja la pili; Watu weusi [Ethiopoid]; Wamarekani wenye asili ya Kihindi [Red Indians] na Wahimalaya [Malayans] kama daraja la mwisho kwa ubora.
Wamefika mbali kwa kudai kuwa Mwafrika si Mwana-Adam, yaani hakuzaliwa na Adam. Dhana hiyo mpya inayoitwa ‘Pre-Adamisma’, inadai kuwa Mwafrika alikuwepo kabla ya kuumbwa Adam, na alikuwa kiumbe asiye na roho.
Mwasisi na Mwenezi wa dhana hiyo inayoshika kasi kipindi hiki cha utandawazi, ni Mfaransa Isaac La Peyrere [1596 – 1676]. Dhana hiyo inapinga usahihi wa Biblia juu ya uumbaji, ikidai kuwa kulikuwa na watu kabla ya kuumbwa kwa Adam na Hawa.
Anadai kwamba kulikuwa na uumbaji mbili za watu: uumbaji wa kwanza ulikuwa wa dunia nzima na Mwafrika kama mtu wa kwanza; na uumbaji wa pili ulihusu Wayahudi kama Taifa ambalo Adam alikuwa mkuu wake.
Anadai kuwa, Mataifa yote hayatokani na Nuhu, kwamba watu wa Mataifa [wasio wa Taifa teule] hawakutenda wala hawahusiki na dhambi ya asili kwa sababu walikuwepo kabla ya Adam, na hivyo hawakupokea “Sheria” au Maagizo ya Mungu, bali ni Adam na uzao wake pekee. Chini ya dhana hiyo, Wazungu ni Wana-Adam, na Mwafrika, siye.
Dhana hii ina watetezi wengi miongoni mwa Mataifa ya Ulaya: Mathew Fleming Stephenson, katika kitabu chake “Adamic Race” anasema, “Mungu alitumia mamilioni ya miaka kuumba mtu duni [Mwafrika] kabla ya kuumba mtu bora aina ya Mzungu [Caucasian] juu yake”. Wengine, kwa kutaja wanataaluma wachache tu, ni pamoja na John Harris [The Pre-Adamite Race], Isabelle Duncan [Adamites and Pre-Adamites], na wengine.
Iwe ni kwa mtizamo wa dhana ya “Pre-Adamite”, “Uumbaji” au “Mageuko” [evolution], hakuna ubishi mpaka sasa, kwamba binadamu [mtu] wa kwanza aliishi Loliondo/Ngorongoro zaidi kabla ya mwaka 10,000, Kabla ya Vizazi [KV], ambao ndio mwaka unaosemekana Adam aliumbwa.
Ustaarabu wa mtu huyu ulianza na shughuli za kilimo, ufugaji, ibada na makazi, eneo ambalo sasa linajulikana kama Nubia, au Sudan Kaskazini. Utawala wa kwanza ulianzia Ta-Seti, eneo hilo watu hawa walijulikana kama “Anu”.
Nchi waliyokalia ilijulikana kwa majina mengi, kama vile, Nubia, Kermet, Kush, Ethiopia au Egypt [Misri], na Mji Mkuu ulikuwa Kerma. Nubia imetajwa kwenye Biblia, Kitabu cha Mwanzo 2:11 kama nchi ya Havillah.
Ni Ufalme ulioundwa na watu weusi kutoka eneo la Maziwa Makuu [ANU] miaka ya 5900 Kabla ya Vizazi [KV], na maelfu ya miaka kabla ya Kisto [KK]. Hapa ndipo Gharika [la Nuhu] lilipowakuta watu hawa, wakaangamia, isipokuwa mtu mmoja – Nuhu na wanae watatu – Yafeti, Shem na Hamu. Hiyo ilikuwa Mwaka 5000 KK.
Wakati ardhi ilipoonekana kutotosheleza familia za ukoo huu ulioendelea kupanuka, Nuhu akawagawia wanawe maeneo ya kutawala: Yafeti alipewa eneo lote la nchi ya Kaskazini ya Dunia, yaani Ulaya yote; Shem maeneo yote ya Mashariki ya Kati na Asia, wakati Ham aligawiwa eneo lote la Bara la Afrika na Marekani Kusini. Ifahamike kuwa wote hawa walikuwa watu weusi kipindi hicho kabla ya koo zao kubadilika rangi maelfu ya miaka baada ya kuhamia nchi mpya.
Ham na ukoo wake alijijengea himaya ya Kikemeti yenye nguvu kiuchumi, Kijeshi na Kitheolojia kwa imani ya Kikemeti iliyotambua uwepo wa Mungu mmoja [Baba].
Mkanganyiko wa kidini na kitheolojia kati ya Mwafrika na Mzungu, unaanza na mtu mmoja aliyeitwa Abraham kutoka Mesopotamia [Ur], aliyeoteshwa ndoto na Mungu wake akielekezwa kwenda [kutafuta makazi] Kanaani, nchi ya Mwafrika aliyeitwa Kanaani, mwana wa Ham na mjukuu wa Nuhu.
Kutoka Kanaani, akaenda Misri Mwaka 1871 KK wakati mtu mweusi alikuwa mtawala na kurejea tena Kanaani, akanunua shamba kutoka [Ephron] ukoo wa Hiti [Wahiti], mwana wa pili wa Kanaani, na kufanya makazi [Mwanzo 23:1-20; 25: 7-10].
Wakati Abraham akiondoka Ur [kwa kukosana na mtawala wa eneo lake] Mesopotamia, ilikuwa chini ya himaya ya utawala wa Mwafrika aliyeitwa Nimrodi, mwana wa Kush na mjukuu wa Ham. Dini na theolojia iliyoongoza huko ilikuwa ya Kikemeti/Kiafrika kutoka Nubia/Afrika. Abraham alikuwa wa uzao wa Nmrod, kwa hiyo alikuwa Mwafrika na alikimbilia Kanaani na Misri kwa watu weusi wenzake.
Musa alikuwa mtu mweusi, la sivyo asingelelewa kwa Farao mweusi, na hatimaye kupewa madaraka ya kitawala kabla ya kukimbilia Nubia/Ethiopia kwa tuhuma za kuua raia. Huko alioa mke wa Kikushi aliyeitwa Tharbis, mweusi tii, wakapata watoto.
Kutoka ukimbizini Nubia/Ethiopia akaenda Midiani, akafikia kwa Kingozi wa eneo hilo, Mzee Yethro aliyepata kuwa Mshauri wa Farao miaka ya nyuma. Akamuoa Ziporah, binti wa Yethro, mweusi tii kama alivyokuwa Tharbis wa Nubia. Akawa na wake wawili wakiishi mbali mbali. Hawa aliwakusanya na kwenda nao Kanaani.
Yethro alikuwa mtu mweusi wa ukoo wa Abraham kwa mke wa mjomba wake, Keturah. Na Musa angekuwa Mwisraeli [wa Taifa teule] asingeoa wake wa Kiafrika – Tharbis na Ziporah.
Wanaofikiriwa kuwa “Waisraeli” aliwaongoza kutoka Misri kwenda kuvamia Kanaani ya Wakanaani, hawakuwa Waisraeli kwa maana halisia, wengi walikuwa weusi hasa wale wa uzao wa wake za Yakobo, Leah, Raheli, Zilpha na Bilha ambao walikuwa Wakush/Wanubia kwa asili.
Na hii inajieleza wazi kuwa walioongoza maasi jangwani dhidi ya Musa walikuwa wenye asili ya Nubia/Afrika, akiwamo On [Anu] mwana wa Paleth na mmoja wa Wakuu wa kabila la Reuben, mtoto wa kwanza wa Yakobo kwa Leah.
Wengine walikuwa ni Korah [mtoto wa tatu wa Esau kwa mke wa Kikanaani, Aholibamah]; Dathan na Abiram, wote wana wa Eliab, waliendesha mgomo kupinga uvamizi wa Kanaani uliokusudiwa na Musa na washirika wao wachache wenye nia ovu.
Mazungumzo ya Musa na Mungu wa jamii ya Kiyuda yenye lengo la kujikweza ambapo inadaiwa alipewa amri kumi, ndicho chanzo cha ubaguzi wa kikabila na kitheolojia uliojenga ubeberu wa Taifa moja dhidi ya mengine. Ni nani mwenye uhakika juu ya usahihi wa dhana ya “Mungu wa Israeli” dhidi ya Mataifa mengine sawa tu na dhana ya “Pre-Adamism?”
Wanaakeolojia wanatuambia kuwa, dunia iliumbwa miaka bilioni 13 iliyopita; Adamu aliumbwa Mwaka 10,000 KV, na Wanahistoria wanasema mwaka huo [10,000], tayari Mwafrika alikuwa ameenea sehemu zote za Ulaya, Asia, Australia na Marekani Kusini.
Waafrika hao walisambaa kutoka Loliondo/Ngorongoro hadi Nubia na kuenea duniani kama ifuatavyo: Miaka 100,000 iliyopita, walijaza Palestina, Israeli na Yemen; Miaka 65,000 iliyopita wengine walitumia mkondo wa Bahari ya Atlantiki, wakaingia Amerika ya Kusini.
Miaka 50,000 iliyopita, wengine walitokea Kusini Mashariki ya Bara la Asia wakawasili Australia, wakajaza Visiwa vya Pasifiki mpaka Hawaii. Na Miaka 40,000 iliyopita wakaingia nchi za Skandinavia na Uingereza.
Wanahistoria na Wanafalsafa nguli wa kale, Flavius Josephus [37 – 86 BK], Lucius Plutarchus [46 – 119 BK], Publius Tacitus [56 – 120 BK], Eusebius Pamphilus [260 – 339 BK] na Diodurus Siculus [90 – 20 KK] walioishi kabla ya Torati [Diodurus] na Kabla ya Biblia ya Agano Jipya kuandikwa [78 BK], wanakiri kuwa Waebrania asilia walikuwa ni kikundi cha Wanubi/Wakush waliolazimika kuhama Nubia/Kush/Ethiopia kwa miguu kwenda nchi ya Kanaani, aliyotawala Kanaan, mwana wa Ham na mjukuu wa Nuhu. Ilikuwa nchi ya Waafrika eneo la Afrika Kaskazini Mashariki.
Hii ndiyo nchi ambayo Abraham aliishi kwa miaka 100 na kumuoa Hajir, Mkushi [Mwanzo 15:3]. Mipaka ya nchi hiyo Kanaani na ukoo wake waliishi na kutawala, kwa mujibu wa Mwanzo 10:19] ilikuwa “kutoka Sidoni hadi Gerari hata Gaza; Sodoma na Gomora, na Adma, na Seboimu hadi Lasha na Afrika Mashariki yote.”
Ham ni Mwafrika kwa mujibu wa Biblia. Mwanae [Kanaani] hawezi kuwa mtu mweupe. Kush, mwana mwingine wa Ham, alitawala Sudani ambayo imo Afrika – ikijulikana wakati huo kama nchi ya Kush.
Misraim, mwana mwingine wa Ham, alitawala Misri ambayo imo Afrika [Zaburi 105:23 – 27]. Uzao wake ni wa Waafrika, si wa watu weupe.
Phut, mwana mwingine wa Ham, alitawala nchi yote inayoitwa leo Libya. Kwa hiyo, ni wazi kuwa nchi na Mataifa yote yanayotajwa katika Biblia ni mali ya Afrika na Waafrika, na si ya Ulaya na Wazungu.
Mungu aliwekeza Loliondo/Ngorongoro siri na madhumuni ya uumbaji kwa utukufu wake. Uwekezaji mwingine hapo kwa uchu wa mali na wenye kufifisha kazi yake ni kufuru kubwa kwa wakfu.

Wiki iliyopita tuliwaletea historia ya mchango wa Kanisa wakati wa kupambana na athari ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia (1939-1945). Leo tunawaletea mrithi wa Papa Pio X11 (1939-1958: wa 260) ambaye ni Papa Yohana XX111, aliyepigiwa kura mara 12 kumpata. Sasa endelea.

Papa Yohana XXIII (1958 - 1963: wa 261), zilipigwa kura mara 12 kabla ya kumpata. Uchaguzi wa Papa wa kumrithi Papa Pio XII, haukuwa rahisi kama uchaguzi wake. Inasemekana kwamba kura zilipigwa mara 12 ili kumpata. Kulikuwepo na wengi ambao walidhaniwa wangemrithi, lakini sasa dunia ilihitaji zaidi Mchungaji kuliko Mtawala.
Papa Pio XII alikuwa labda Papa wa mwisho wa mapokeo ya kifalme. Katika hali ngumu ya kumpata mtu wa kukidhi mategemeo ya wote, walimchagua mtu wa mpito wakiwa wanajipanga vizuri.
Walimchagua mtu ambaye hisia zake zilikuwa za mkulima, mtu rahisi kuongea naye na kufikiwa. Umri wake, miaka 76, ulikuwa umekwenda, hivyo hakutegemewa kukaa muda mrefu.
Alichaguliwa Kardinali Angelo Ronccali ambaye alichukua jina la Papa Yohana XXIII. Kardinali Ronccali alikuwa na uzoefu wa kukutana na watu wa aina mbalimbali wa kutoka nchi mbalimbali.
Ni vema na haki kujua vizuri maisha ya Papa huyu aliyebadili mwelekeo wa Kanisa katika Ulimwengu wa sasa. Kinyume na mategemeo ya wote, alifanya kazi ambayo ilikuwa haijafanyika tangu Mtaguso Mkuu wa Trento katika karne ya 16.
Angelo Giuseppe Roncalli, mtoto wa tatu kati ya watoto kumi na watatu, alizaliwa tarehe 25 Novemba 1881 huko Sotto il Monte (Bergamo), kwenye familia ya wakulima. Alipadrishwa mwaka 1904, na akaendelea na masomo na kupata Shahada ya Uzamivu katika Sheria za Kanisa.
Akiwa Katibu wa Askofu mpya wa Bergamo, Giacomo Radini –Tedeschi, Angelo alipigania haki za jamii, na baadaye alifundisha Seminarini Historia ya Kanisa, na masomo mengine. Wakati wa Vita Kuu vya Kwanza (1914-1918), mwaka 1915 alijitolea kama mhudumu wa kiroho (Chaplain) wa wanajeshi. Baada ya vita, alikuwa mlezi wa kiroho wa Seminari.
Mwaka 1921 aliitwa Roma na Papa Benedikto XV (1914-1922: wa 258) kusaidia kupanga upya Idara ya Uinjilishaji (Propaganda Fide). Mwaka 1925 alitumwa Bulgaria kama Mwakilishi wa Papa, na huko alijishughulisha na Makanisa ya Mashariki (Waortodosi). Mwaka 1934 alitumwa Uturuki na Ugriki, makao yake yakiwa Istanbul (Konstantinople ya zamani).
Huko, licha ya Wakristu Waortodosi, alikutana kwa karibu na Waislamu. Mwaka 1944 alitumwa kumwakilisha Papa huko Paris, Ufaransa, ili kusaidia Kanisa hilo kubwa kujiunda upya baada ya vita.
Hii haikuwa kazi rahisi kwa sababu Balozi aliyetangulia alishirikiana na Wajerumani. Hivyo serikali ya Rais De Gaule na Wafaransa, walimchukia pamoja na Maaskofu waliofuta, nyayo zake. Sasa Askofu Mkuu Roncalli, ilibidi afanye kazi ya ziada kutuliza hali.
Wakati huo alikuwa vile vile Mwakilishi wa Papa katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Kushughulikia Watoto (United Nations International Children’s Emergency Fund: UNICEF). Baada ya kazi nzuri akiwa na umri wa miaka 71, mwaka 1953 aliteuliwa kuwa Kardinali na Patriarka wa Venezia.
Papa Pio XII alipofariki (Oktoba 1958), Makardinali walikuwa na wakati mgumu kukubaliana juu ya nani amrithi. Ilikuwa vigumu kupata theluthi mbili za kura kwa mtu mmoja. Hivyo, baada ya kupiga kura mara 11, waliona wampate Papa wa mpito atakayekubalika kwa wote wakati hali inaendela kuwa shwari.
Tarehe 9 Oktoba 1958 katika kura ya 12, walimchagua Kardinali Angelo Roncalli, mwenye umri wa miaka 76, mtu asiyekuwa na misimamo mikali, lakini mtu wa watu na Mwanadiplomasia mzuri katika kuleta mahusiano na watu.
Alichagua jina la Yohana XXIII. Mfano wa maisha yake na mtu ambaye alitaka kufuata nyayo zake alikuwa Mtakatifu Papa Pio X (1903-1914: wa 257) ambaye alizaliwa akiwa maskini, na kufa akiwa maskini. Naye kabla ya kuchaguliwa kuwa Papa, alikuwa Patriarka wa Venezia.
Katika hotuba zake za mwanzo, mara moja Papa Yohana XXIII aligusia mambo makuu mawili ambayo alitamani kuyatekeleza. Kwanza kuhuisha Kanisa ili lioane na nyakati, yaani kusoma alama za nyakati kama alivyoiita (Aggionamento).
Alitaka kulihuisha Kanisa kiroho. Pili aligusia kuita Mtaguso Mkuu wa Kanisa kufanya kazi hiyo muhimu. Papa Yohana XXIII alihisi kwamba amevuviwa na Roho Mtakatifu kutengeneza Kanisa na kulihuisha.
Wakati akiamini juu ya Neno la Mungu na Mapokeo rasmi ya Kanisa ambayo ni msingi wa Imani na hayawezi kugeuka, aliona mazoea mengine yaliyoingia kufuatana na utamaduni na mwenendo wa watu wa mahali, au wakati fulani yanaweza na mara nyingine yanapashwa kugeuka kukidhi mahitaji ya wakati na mahali.
Kwanza alianza na desturi za maisha ya Papa. Tofauti na watangulizi wake waliokaa ndani Vatikano, yeye alitoka nje mjini Rona na kwenda kuwatembelea watoto wagonjwa hospitalini, na hata wafungwa.
Alisisitiza kuwaona hata wafungwa sugu na hatari. Aliwaambia wafungwa: “Kwa sababu ninyi hamuwezi kuja kunitembelea, imebidi mimi nije kwenu.” Vile vile alikutana na watu ambao kabla haikufikirika kukutana na Papa kama mpwa wa Rais wa Urusi Nikta Khrushchev, Askofu Mkuu wa Kantebury, yaani Mkuu wa Kanisa la Anglikana, kasisi mkuu wa dini ya Shinto kutoka Japan, na wengine.
Kwa mara ya kwanza katika karne moja, alisafiri nje ya Roma na kwenda Asizi. Alipokutana na watu, hakujiona au kujionyesha kama Kiongozi Mkuu wa Vatikano, bali kama mchungaji au kama alivyosema “Mtumishi wa watumishi” (Servus Servorum), akiwa na sura ya Mchungaji kuliko ya Mtawala.
Papa Yohana XXIII aliliona Kanisa kama chombo cha kiroho kilicho juu ya madaraka yote ya siasa, na chenye jukumu la kuwapatanisha, mathalani wakati wa mzozo wa silaha za nuklia wa Cuba mwaka 1962, ambapo ilikuwepo hatari ya vita vikuu vya mabomu ya nuklia kati ya Urusi na Marekani kutokea.
Papa Yohana XXIII aliingilia kati baina ya John Kennedy wa Marekani na Khrushchev wa Urusi kwa kuzungumza nao, na hivyo akapunguza munkari. Mambo yalipotulia, wote wawili walimshukuru.
Papa Yohana XXIII aliongeza Jopo la Makardinali kiasi kwamba kufikia mwaka 1962, lilikuwa na Makardiali 89, ikiwa 19 zaidi ya wale 70 wa Kanuni iliyowekwa na Papa Sisto IV (1471-1484: wa 212) katika karne ya 15.
Kati ya Makardinali hao, aliwateua wengine kutoka Afrika, Filipino na Japan, licha ya Marekani na nchi nyingine. Kati ya Makardinali alimteua Mwafrika wa kwanza na mtu mweusi wa kwanza kuwa katika jopo hili, Mwadhama Laurean Kardinali Rugambwa, Mtanzania kutoka Jimbo la Rutabo, Bukoba, Kagera, Tanganyika wakati huo, mwaka 1959.
Kuna watu ambao hawakuamini kwamba mtu mweusi angelikuwa Kardinali. Ikumbukwe kwamba wakati huo karibu nchi zote za Afrika zilikuwa bado koloni na Marekani mtu mweusi hakuweza kupiga kura na hata kukaa sehemu moja na wazungu, kwani alitengwa kama mkoma. Katika uongozi wake, aliwateua Makardinali 54.
Kama Baba Watakatifu waliomtangulia, naye alitoa barua mbalimbali za kichungaji. Tofauti na wengine, barua zake hazikuwa za kulaumu, au za kutoa fasili ngumu za teolojia, bali mambo ya kawaida yenye ladha ya kichungaji yaliyowahusu na kuwagusa watu, bila ubaguzi.
Papa Yohana XXIII aliandika barua nane za kichungaji, na kati ya barua hizo  alizoziandika, mbili zilikuwa na msukumo mkubwa. Mater et Magistra (Kanisa kama Mama na Mwalimu), hii ilikuwa barua ya tano iliyotolewa tarehe 15 Mei 1961 ikiwa ni miaka 70 tangu barua ya Papa Leo XIII (1878-1903: wa 256) Rerum Novarum, na miaka 30 tangu barua ya Papa Pio XI (1922-1939: wa 259) “Quadragesimo Anno.”
Katika barua hiyo iliyosifiwa na kukubalika Ulimwengu mzima, ilijadili masuala ya jamii kama walivyofanya watangulizi wake kwa mtazamo chanya, huria na wa kujenga. Barua maarufu kuliko zote ni ile ya “Pacem in Terris“ (Amani Ulimwenguni) aliyoiandika tarehe 11 Aprili 1963, miezi miwili kabla ya kifo chake Papa Yohana XXIII.
Tofauti na barua nyingine za Baba Watakatifu wengine, Papa Yohanne XX111, aliwaadikia watu wote wenye mapenzi mema. Kweli ilikuwa inawafundisha na kuwaasa watu wa Ulimwengu mzima. Ulikuwa kama wosia wake wa mwisho kwa Ulimwengu.
Barua hii imechambua hali halisi ya kijamii Duniani. Papa Yohana XXIII anatutaka kuheshimu utu wa watu, na anadai kwamba kuheshimu haki za binadamu wote, ndio msingi wa haki na amani ya kweli.
Anaandika “Mwanadamu ana haki ya kuishi. Ana haki ya uadilifu wa mwili na njia zinazohitajika kwa maendeleo sahihi ya maisha, haswa chakula, mavazi, malazi, matibabu, mapumziko na, mwishowe, huduma muhimu za kijamii. Ana haki ya kutunzwa katika hali mbaya ya afya; ulemavu unaotokana na kazi yake; mjane, uzee; kulazimishwa kukosa kazi; au wakati wowote bila kosa lake mwenyewe, ananyimwa njia ya kujikimu.”
Licha ya kusisitiza juu ya utu na usawa wa binadamu, anaasa juu ya haki za wanawake, anawasihi kutoenezwa kwa silaha za nyuklia. Anafundisha juu ya umuhimu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kuwaleta watu wote pamoja, kujadili na kuleta muafaka juu ya kutatua mafarakano na kuleta maendeleo ya kweli kwa watu wote.
Bahati nzuri, tafsiri ya barua hii iko katika Kiswhili, na inapatikana kwenye mtandao wa Vatikano.