Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

DAR ES SALAAM

Na Mathayo Kijazi

Wafanyakazi wa Tumaini Media wamewakumbuka wenzao waliofariki dunia kwa kufanya ziara maalumu ya kiroho walikozikwa kwenye makaburi ya Kinondoni na Pugu, jijini Dar es Salaam.
Katika Hija hiyo ya kiroho ya kuwakumbuka wenzao waliokuwa wakifanya kazi katika Vyombo vya Habari vya Tumaini Media, pamoja na mambo mengine katika Kuhitimisha Kampeni ya Mwezi wa Moyo Mtakatifu wa Yesu, ni kuwaombea marehemu hao.
Akizungumza katika ziara hiyo ya kiroho, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Tumaini Media, Arnold Kimanganu alisema kuwa yeye pamoja na wafanyakazi wote walioshiriki, wameguswa sana, kwani sala zao zina faida kubwa kwa wapendwa wao waliotangulia mbele za haki.
“Mimi kama mfanyakazi wa Tumaini Media nikiwakilisha wenzangu, nimeguswa kwa jambo hili jema la kiroho, na natamani sana lisiwe mwisho, bali tuendeleze utaratibu huu wa kuwakumbuka wale ndugu zetu waliokwisha kupumzika, kwa sababu tunafahamu kwamba wote hapa duniani tuko safarini, na mwisho wa safari yetu ni mauti,” alisema Kimanganu.
Aliwasihi kila mmoja katika ziara hiyo ya kiroho, kuiga yale mazuri yaliyowahi kutendwa na wapendwa wao enzi za uhai wao, na kuongeza kuwa watumie nafasi hiyo pia kuwaombea kwa yale mapungufu waliyokuwa nayo wapendwa wao hao, kama yanafahamika.
Naye Sista Leonora John, Mfanyakazi wa Tumaini Media alisema kuwa kila mmoja katika Dunia hii anatakiwa kuutambua mpango wa Mwenyezi Mungu, kwamba amepewa muda maalum wa kuishi hapa duniani, na akaongeza kuwa kifo kinawatenganisha kimwili tu, bali kiroho, wako pamoja.
“….Na kwa namna ya pekee kabisa, tunahitimisha ziara hii katika makaburi ya Pugu ambapo amelala Padri Paul Haule, pamoja na Mapadri wengine ambao wamelitumikia Kanisa Takatifu. Bila shaka tunajifunza kwamba sisi pia tuna safari ambayo tunatakiwa kuimaliza. Hivyo, tukiishi vizuri katika ulimwengu huu, tutayatimiza mapenzi ya Mungu Baba kama Yesu Kristo alivyosema, “Anayeishi vyema, atakuja kwangu, kwa sababu mimi ni njia, ukweli na uzima,” alisema Sista.
Kwa upande wake Mhariri Mkuu wa Gazeti Tumaini Letu, Alex Kachelewa alisema kuwa ipo haja ya kuendelea kuwaombea wapendwa wao waliolala katika Kristo, kwani kila mmoja anatakiwa kuiga uwajibikaji waliokuwa nao wapendwa wao enzi za uhai wao.
“Mama Esther Chilambo namkumbuka kama Mkurugenzi wa Pili wa Radio Tumaini, kabla haijaundwa Tumaini Media. Yeye alikuwa akiamini sana katika kazi, na hasa kuamini yale ambayo anaamini kwamba yanaweza kufanyika. Kwa hiyo, alikuwa ni mwenye misingi ya kusimamia kazi. Nakumbuka alikuwa na ‘column’ yake moja kwenye gazeti Tumaini Letu iliyoitwa ‘Dunia na Maumbile’. Lakini pia nakumbuka maneno machache aliyowahi kusema, “Ukiamua kufanya kazi, basi ifanye kwa moyo wa dhati,” alisema Kachelewa.
Kachelewa aliongeza kuwa Mama Esther Chilambo alikuwa ni mtu mwenye kujiamini katika utendaji kazi, kwani kwa mipango yake, alisaidia pia kuanzishwa kwa gazeti Tumaini Letu mwaka 2004, huku akisimamia mpango wa vyombo vya habari vya Kanisa, hasa Televisheni, iunde king’amuzi chake, ila baada ya kifo chake, mipango hiyo haikuendelea tena.
Naye Gaudence Hyera, Mratibu wa Matukio ya Kanisa wa Tumaini Media, alisema kuwa kufuatia Hija hiyo, wana imani kwamba sala zao zitafika pia Mjini Marseille, Ufaransa, alikozikwa mwanzilishi wa Tumaini Media, Padri Francois Galtier {aliyependa yeye kujiita ‘msela wa kijiweni’}, aliyefariki dunia Mei 17 mwaka 2021.
Gaudence aliongeza kwa kusema, “Kama ambavyo Kanisa linatufundisha kila siku juu ya kuwakumbuka marehemu, na tunatambua kwamba Kanisa lina makundi matatu, lina wale ambao bado wanaishi, ambalo linaitwa Kanisa linalosafiri; kuna wale waliotangulia, linaitwa Kanisa la wafu; lakini pia kuna wale washindi, linaitwa Kanisa la washindi, yaani wale Watakatifu wa Mbinguni;
“Kwa hiyo, ni jambo la muhimu sana ambalo tunalifanya kiimani na kijamii, lakini pia katika masuala mazima ya mahusiano ya kibinadamu, kwamba huyu aliishi katikati yetu. Kwa hiyo kwa namna moja ama nyingine, tunatakiwa kumkumbuka siku kwa siku,” alisema Hyera.
Kwa upande wake Editha Mayemba, Mtangazaji wa Redio Tumaini, alisema kuwa bado wanatambua mchango mkubwa uliofanywa na wapendwa wao, licha ya kwamba kwa sasa wametangulia mbele za haki, ila watayaendeleza mazuri yote yaliyoanzishwa na wapendwa hao.
Makaburi waliyoyatembelea wafanyakazi hao ni Kinondoni kwenye kaburi la aliyekuwa Mkurugenzi wa Pili wa Tumaini Media, Mama Esther Chilambo; kaburi la mtangazaji nguli wa Redio Tumaini Frederick Mosha, ali maafarufu ‘Defao’; na Pugu kwenye kaburi la aliyekuwa Mkurugenzi wa chombo hicho, Padri Paul Haule.

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini Tanzania (Tanzania Rural and Urban Roads Agency: TARURA), Mkoa wa Dar es Salaam, umeombwa kujenga kwa kiwango cha lami, barabara yenye urefu wa kilometa tatu kutoka Barabara Kuu ya Morogoro kuelekea katika Parokia ya Mtakatifu Ambrose, Tagaste, Jijini Dar es Salaam, ili kuwaondolea kero ya usafiri wakazi wa maeneo hayo.
Rai hiyo imetolewa na Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo hilo, wakati akizungumza katika Adhimisho la Misa Takatifu ya kutoa Sakramenti Takatifu ya Kipaimara iliyoadhimishwa hivi karibuni parokiani hapo.
“Mmejitahidi kufanya vizuri, ila barabara imekuwa ngumu kwangu na kwa wengine kufika hapa kanisani. Hivyo basi, Viongozi mngezungumza na Mbunge mmwombe walau atengeneze kwa kiwango cha lami,” alisema Kardinali.
Aidha, aliwaomba Viongozi wa Halmashauri ya Walei wa Parokia kuchukua jukumu hilo ili kufanikisha ujenzi wa barabara hiyo.
Awali akihubiri katika Adhimisho la Misa Takatifu ya kutoa Sakramenti Takatifu ya Kipaimara katika Parokia hiyo, Kardinali Pengo aliwataka Wakristo kuepuka kujilinganisha na Mungu, kwani wengi wanafanya mambo yao kwa kujiamulia wenyewe bila kumshirikisha Mwenyezi katika maisha yao.
“Kujaribu kujilinganisha na Mungu wakati wewe ni kiumbe wake, ndiko kulikotuponza sisi wanadamu tangu wazazi wetu wa kwanza. Hatutaki kumwachia Mwenyezi Mungu nafasi yake kwamba yeye aliyetuumba, ndiye aamue kwamba kipi ni kizuri kwetu, na kipi hakifai kwetu kutenda,” alisema Kardinali Pengo.
Alisema kuwa wanataka kujikana na Mungu, wanataka wawe sawa na Mungu, na wajiamulie wenyewe yale wanayotaka kufanya, matokeo yake, ndiyo vurugu zinazojitokeza kwa sasa.
“Tukigundua mfano wa dhati kabisa, Mwenyezi Mungu alipomuumba mtu, alimuumba mtu mume na mtu mke, na akasema ‘nendeni mkaongezeke’, leo hii unaona watu wanasema ‘mimi mwanaume siyo lazima nikae na mwanamke, mimi nakaa na mwanaume mwenzangu,” alisema Kardinali Pengo, akionya ukengeufu wa wandamu.
Kwa mujibu wa Kardinali Pengo, kitendo cha wanadamu kutompatia Mungu nafasi yake katika maisha yao, ndiko kunakowafanya waingie kwenye dhambi.
Aidha, Kardinali Pengo aliwataka Wakristo kufahamu kwamba Mungu ndiye mwenye kauli, na si vinginevyo, kwani wao kazi yao ni kujikusanya kwa pamoja ili wamwombe awaondolee hofu, na kuwapa ujasiri wa kuitangaza Habari Njema.
Awajaza Imani Waimarishwa Kardinali Pengo alitumia nafasi hiyo kuwasihi Waimarishwa wa Sakramenti Takatifu ya Kipaimara, kuhakikisha wanajikita zaidi katika imani yao, kwani wao ni Askari Hodari wa Bwana Yesu Kristo.
Kwa upande wake Paroko wa Parokia hiyo, Padri Onesmo Ngonyani alimshukuru Kardinali Pengo kwa kuadhimisha Misa hiyo Takatifu, na kumpongeza kwa Jubilei yake ya Miaka 25 ya Ukardinali.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Walei wa Parokia hiyo, Pius Maneno, akisoma risala katika Misa hiyo alisema kuwa Parokia hiyo ilizinduliwa na Kardinali Pengo, Januari 13 mwaka 2013, ikiwa ni Parokia ya 76 ya Jimbo hilo.

DAR ES SALAAM

Na Mathayo Kijazi

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi amesema kuwa Wakristo wanapoadhimisha Misa Takatifu ya Jubilei, wanatakiwa kumtambua Mungu kama Baba wa Huruma, wa Hisani, na pia wa Upendo katika maisha yao.
Askofu Mkuu aliyasema hayo hivi karibuni wakati akihubiri katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Kuadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya Parokia ya Bikira Maria Consolata, Kigamboni, iliyokwenda sanjari na utoaji wa Sakramenti Takatifu ya Kipaimara, na Sakramenti ya Ndoa Takatifu.
“Leo ni siku ya shangwe na shukrani kwa Mungu kutokana na mambo makuu ambayo ametutendea, kutokana na safari ambayo ametujalia kuifanya kama Wanaparokia wa Parokia hii ya Kigamboni:
“Na tunapofanya Adhimisho hili la Shukrani na Masifu kwa Mungu, tunaangazwa na kuongozwa na Neno la Mungu. Somo letu la Kwanza ambalo limetoka katika Kitabu cha Nabii Zefania, limetufundisha kwamba uhamishoni ni mahali pa mahangaiko, ni mahali pa kunyanyasika. Lakini Mungu ni mwaminifu, hata kama wamepelekwa uhamishoni kutokana na dhambi zao, dhambi haina kauli ya mwisho. Mungu anawaahidia mwanzo mpya …. Hata sisi tunaoadhimisha Miaka 50 ya Parokia hii, tunamtambua Mungu kama Baba wa Huruma, Baba wa Hisani, Baba wa Upendo.”
Katika homilia yake, Askofu Mkuu Ruwa’ichi alisema kuwa Mungu ni mwenye huruma katika maisha ya wanadamu, kwani licha ya mapungufu mengi waliyo nayo wanadamu hao, lakini yeye hawatupi, na anawapa tena fursa ya kuanza upya.
Aidha, aliwasisitiza Waamini kuitumia vyema kila fursa waliyopewa na Mungu, ikiwemo kujikusanya na kuamua kuanza upya, wakitambua kuwa kwa kufanya hivyo, ndiko kuudhihirisha ukuu wa Mungu katika maisha yao.
Wakati huo huo, Askofu Mkuu alisema kuwa katika Misa hiyo Mama Maria wanamwadhimisha kama Consolata, Mama mwenye Huruma, Mama Msaidizi, na pia kama Kimbilio na Mwombezi wao, huku akiwapongeza Wanakigamboni kwa kuzawadiwa Bikira Maria Consolata, kama Mwombezi na Msimamizi wao.
Pia, aliwaalika Wanaparokia hao kwa kuwa tayari, kwani wanaye Msimamizi mwenye uzito. Hivyo watumie nafasi hiyo kumuiga pamoja na kumpa nafasi ili waweze kuyatimiza mapenzi ya Mungu katika maisha yao, akiwapongeza kwa miaka 50 tangu kuwa Parokia mwaka 1973.
Pia, alisema kuwa wao ni wakongwe kwa sababu walipotangazwa kuwa Parokia, Jimbo lilikuwa bado halijafikisha hata Parokia 10, hivyo akawasisitiza kuutambua uzito walio nao, kwani hadi sasa zimefika 150, na Parokia Teule 24.
Kufuatia kauli hiyo, Askofu Mkuu aliwaasa kusimama kadri ya kimo chao, huku akiwataka kuonyesha nguvu yao, uwezo wao, uimara wao, pamoja na utayari wao wa kuwa mhimili wa Kanisa katika Jimbo hilo.
Askofu Mkuu Ruwa’ichi aliwaasa Waimarishwa wa Sakramenti Takatifu ya Kipaimara kumpokea Roho Mtakatifu ili awakamilishe katika Neema ya Ubatizo, na kuwapa utayari wa kwenda kumshuhudia Kristo.
Aliwasisitiza pia kuhakikisha kwamba Roho Mtakatifu wanayempokea, hawamhuzunishi, bali wanajipanga kutenda kazi pamoja naye katika maisha yao, akisema kuwa licha ya kwamba ni wadogo kiumri, kiimani ni wakubwa, hivyo wanahitaji kuendelea kuwekewa misingi imara.
Wakati huo huo pia Askofu Mkuu aliwapongeza wanandoa kwa kuchukua uamuzi huo wa kuachana na uchumba sugu, akisema kuwa kwa kufanya hivyo, wamelipokea jukumu la kuunda Kanisa la Nyumbani, pamoja na kuwa washiriki wa kazi ya uumbaji wa Mungu kitakatifu katika maisha yao.
Aliwakumbusha kuwa wito wao huo kama wanandoa, una mihimili yake ikiwemo upendo, uaminifu, na umoja, pamoja na kufahamu kwamba ndoa ya Kikristo ni ya mke mmoja na mume mmoja, na si vinginevyo. Hivyo akawasisitiza kuizingatia mihimili hiyo.
Parokia ya Bikira Maria Consolata, Kigamboni, ilitangazwa rasmi mwaka 1973, na kabla ya hapo ilianza kama Kigango cha Parokia ya Mtakatifu Yosefu, jimboni humo.

MWANZA

Na Paul Mabuga

Tunapaswa tujiulize tumekosea wapii, kama tunaona mkoloni aliweza hata mwalimu wenye ‘denge’ ni wetu. Ungana na Mwandishi Wetu, PAUL MABUGA, katika makala haya.
Uamuzi wa serikali wa kuwafanyisha mtihani walimu waliohitimu mafunzo ya taaluma hiyo kabla ya ajira kama ulivyotangazwa na Profesa wa Uchumi na Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Fautine Mkenda ni jambo linalofikirisha na hata kufukarisha.
Inafikirisha na kufukarisha hisia kwa sababu, Walimu wanaofanyishwa mtihani ni wale ambao walipewa mafunzo na kufaulu na kisha kupata hadhi hiyo adhimu.
Ni lazima akili zifubae kwa sabau ukiwakuta walimu katika shule zetu katika nyakati hizi unakoma ubishi.
Unakuta mwalimu katika shule naye kanyoa nywele pembeni ya kichwa na kuziacha zikichanua kwa juu, hata zamani mnyoo wa aina hiyo ulikuwepo na ulikuwa maarufu kwa jina la denge.
Yaani kichwa kinakuwa ndege anayejulikana kama shole kibwenzi, ila walimu walikuwa hawawezi kunyoa hivi kwa ajili ya staha na haiba.
Profesa Mkenda amekakaririwa akisema Utaratibu huo, unalenga kurudisha hadhi ya taaluma ya ualimu, isitazamwe kuwa chaguo la mwisho baada ya kukosa nyingine na pengine katika mtazamo huo inategenewa kujibu baadhi ya malalamiko ambayo yamekuwa yakitolewa.
Yaani kile Waziri huyu alichokuwa akikiona kwa walimu wake wakati akiwa mtoto wa shule katika miaka ya sitini kule Rombo, sasa hakipo na kwamba hadhi ya taaluma hiyo imeshuka.
Kwamba mwalimu wa wakati huo alikuwa na hadhi  ikilinganishwa na vijana wa kisasa.
Kwamba walimu wa kizazi cha elimu mkoloni na mchanganyiko kidogo wa Tanganyika huru walikuwa bora na wenye hadhi na wakifanya kazi yao barabara.
Wengi wao wakiwa wamevuka ile hali ya kuvaa kamptura safi na sasa wanavaa suruali lakini wamechana ‘way’ kwenye nywele kama wazungu. ‘Way’ ni kule kuchana nywele na kuachia ki njia upande wa kushoto.
Kwamba kutokea hapo, tukaja na kizazi cha walimu katika miaka ya 1980 na mwanzono mwa 1990, hapa kulikuwa na walimu kutoka vyuoni lakini pia na wale wa  Azimio la Musoma ambao walikuwa wahitimu wa kidato cha sita na kulazimika kufanya kazi miaka miwili ikiwa ni pamoja na kufundisha kabla kwenda Chuo Kikuu.
Lakini pia kulikuwa na walimu ambao baada ya kuhitimu elimu ya msingi walisajiliwa kuwa walimu, huku wakiendelea kupata mafunzo nje ya vyuo kwa miaka mitatu, walijulikana kama UPE, kwa sababu walikuwa chini ya mpango wa Elimu kwa wote, [Universal Primary Education.
Hawa na wengine wote walikuwa na hadhi kuliko hali ilivyo sasa kama ilivyo dhania ya Profesa Mkenda kupitia utaratibu wa mtihani kabla ya ajira ya ualimu Je ni kweli hadhi ya Ualimu imeshuka?
Lakini kuna mtazamo mwingine! Inatokea tu, unapita katika mitaa ya mji Kahama, Mkoani Shinyanga, sehemu ambayo awali ilikuwa ikijulikana kama Uhindini, unaingia katika familia moja ya watanzania wenye asili ya India na unakaribishwa kwenye chai ya maziwa kwenye kikombe cha udongo.
Kisha anaitwa Bibi wa familia na unatambulishwa kwamba huyu ni mtoto wa mwalimu wetu. Unapata heshima hii kwa sababu  ya baba yako na unamkumbuka alikuwa akipiga ‘way’ wakati huo.
Je kuna familia ngapi leo, zinawahusudu walimu kiasi cha kuwapa heshima inayodumu? Utawapaje heshima wakati visanga vya walimu vinatikisa taarifa kwenye vyombo vya habari!
Pale Mwalimu kazichapa ngumi na mwanafunzi, kule mwalimu kampa ujauzito mwanafunzi na walimu wamegoma kwa kucheleweshewa posho, huku wakiimba, ‘’ tunataka haki zetu.’’
Unaongea na mwalimu mmoja katika Shule ya Sekondari ya binafsi iliyopo katika Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga na anakuambia, “hawa walimu vijana waliomaliza Chuo Kikuu kwa siku hizi, tunawalipa mshahara wa Shilingi 200,000/-, kwa sababu uwezo wao mdogo na hawana ufanisi, ila wenye Diploma za zamani tunawalipa hadi Shilingi 800,000/-.”
Lakini waulize pia wanafunzi wa Sekondari waliopo ilikizo wakati huu kwamba, Walimu wanawafundisha masomo kwa lugha ipi, watakuambia masomo karibu yote yanafunddishwa kwa Kiswahili, iwe ni Biilojia, Basic Mathematics ama History, yote hayafundiswi kwa Kiingereza kama inavyitakiwa.
Mkuu mmoja wa Shule ya Sekondari anasema tunaletewa vijana ambao hawawezi hata kuongea Kiingereza katika mikuanyiko ya wanafunzi asubuhi sembuse kuandika barua ya kuomba ruhusa kwa Kiingereza.
Je mtihani ni suluhisho
Ni wazi kuwa kuna tatizo katika kuwatayarisha walimu na yote yanayolalamikiwa mchanganyiko wa mambo ambayo kwa bahati mbaya, jawabu lake siyo walimu kuwafanyisha mtihani kabla ya ajira.
Hii ni dawa isiyo na uwezo wa kutibu hata kama inaleta ahueni, [placebo]. Ni kwa sababu hailengi matatizo yaliyopo katika kuwatayarisha walimu.
Profesa Mkenda ajiulize, ni kwa nini kila Mwalimu anakuwa na jitihada na kusoma ili aweze kubadili kazi? Ajiulize ni kwa nini vyuo vyetu vinashindwa kutayarisha walimu wenye ubora na hata wanafaulu bila ya kuwa na viwango vinavyotakiwa? na kwa namna gani uwezo wa akili ya darasani unalingana na uwezo wa kufanya kazi yenyewe?
HIi ni kwa sababu hata wahuni wanaweza kufaulu mtihani huo wa ajira!Na wamejipangaje kutibu gonjwa lenyewe badala ya kuhangaika na dalili?
Wenzetu mwalimu akifuzu na kusajiliwa kuwa mwalimu, [staatsexament kwa ujeumani] kunakuwa hakuna shaka juu ya ubora wake.
Uaalimu ni taaluma nyeti, na ndiyo maana kunahitajika mfumo bora wa kuwatayarisha walimu, ikiwa tangu wakati wa kuchagua wanaingia chuoni!
Haiwezekani ukawa na mfumo wa kizembe na utegemee kupata walimu bora. Tujenge mazingira ya vijana waipende kazi na kuwa chaguo la kwanza.

Waamini wa Parokia ya Bikira Maria Consolata, Kigamboni, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, wakiwa katika Sherehe ya Adhimisho la Misa Takatifu ya Jubilei ya Miaka 50 ya Parokia hiyo iliyoanzishwa mwaka 1973. (Picha zote na Yohana Kasosi)

Wafanyakazi wa Tumaini Media wakifanya Ibada fupi  kwenye Kaburi la aliyekuwa Mkurugenzi wa Tumaini Media, Padri Paul Peter Haule, katika eneo la Makaburi ya Mapadri yaliyoko kwenye Kituo cha Hija Pugu, wakati wa ziara yao ya kiroho ya kutembelea makaburi ya waliokuwa wafanyakazi wenzao.

MWANZA

Na Paul Mabuga

Zamani ukitaka kuijua jamii tunayoisha hapa Bongoland, ilikuwa unatakiwa kutafuta kile kilichomo ndani ya vyombo vya habari, lakini kwa sasa siyo tena kwani huko yamejaa maisha ya kuigiza, bali unatakiwa kupanda daladala na hutanyimwa tafsiri ya namna tunayoishi.
Ndani ya daladala utasikia hapendwi mtu kwa kuwa huko mitaani ndiyo mtindo wa maisha uliopo kwami kinachotawala upendo ni pesa.
Utajua jamii inahalalisha udhalimu kwa kuwa kitanda hakizai haramu na tukiandaa vikao vya harusi vinaendelea mwaka mzima, lakini mafunzo ya wanandoa  tunatamani hata yawe wiki mbili!
Ukizama kwenye vyombo vya habari utaona kila mtu anajua, anakosoa na hata anajadili masuala ambayo yapo juu ya upeo wake, ni kama vile wote wa shahada.
Kila mtu anaonesha maisha ya kuigiza kuliko hali halisi na ukiwatathmini watu kwa yale unayosoma, kusikia na kutazama unaweza kushindia matango pori na kupata uwelewa usio sahihi.
Unapanda daladala kutoka Buswelu kwenda Kemondo katika Jiji la Mwanza, dereva ndiye DJ, na anaweka muziki anaoutaka huku sauti ikiwa juu, abiria wanasikilizana kwa shida, hasa kwa kuwa kila viti viwili, vitatu ni kama Bunge kamili kwani kila seti ina mada ya mjadala  inayoendelea nao.
Wimbo ulioingia zamu ya kupigwa unashusha kutokana na aina ya beti zake ambazo hazina staha kwa waungwana, abiria wanalalamika kwa sauti kubwa na maneno ya beti na wanaomba dereva apunguze sauti, na mzee mmoja anatasema, “angalieni [dereva] alivyonyoa kiduku, kichwa kimekuwa kama mjusi wa rangi!” Dereva anazima kabisa muziki kwa hasira, ni kama abiria wanaifurahia hali ile.
Kiti cha nyuma ni kama mama na wenzake walikuwa wakisubiri muda huo, kwa maneno yake anaonekana kama ni mjasiriamali mdogo na anawaambia wenzake juu ya mumewe ambaye ameondoka kwake na kwenda kukaa kimada kwa mama ntilie.
“Yaani alianza kuwa anachukua nguo moja moja anakwenda na anarudi, na nikaja kugundua hilo na wakati nafikiri nini cha kufanya akaja   ananiambia ana safari na anataka kuchukua begi ambalo nilinunua mimi, nikamwambia we nenda ulikotamani na vitu vyangu pamoja na nguo nilizokununulia acha,’’ anasema Mama yule.
Wenzake wawili katika mjadala huo, wanaonekana kumuunga mkono na wanasema wa namna hiyo hafai!
Inabidi kushangaa, yaani inaonekana kama vile kuachana ni kama kwenda kununua parachichi Manzese na unajihoji hivi hawa huwa hawangalii “Nyumba Amninifu” ya Tumaini TV! Kwa hakika wakiangalia wanaweza kubadili fikra.
“Asikubabaishe huyo, kwa mama ntilie kafuata mapochopocho, akichoka aende zake akafie mbali, hawa ndiyo wale tunaosema wana tabia kama kipepeo, wanatoka ua moja hadi jingine!” kwa lugha ya mjini wanasema walikuwa wanamjaza.
Ni wazi huyu mama hakutayarisha kumtambua mwenza wake, ikiwa ni pamoja na kufahamu wasifu wake wa ndani na nje na kuvitawala vichocheo vinavyomuongoza, [male instincts].
Angepata mafundisho ya ndoa yanayoakisi hali halisi [Biological response] na siyo nadharia za kufikirika bila shaka angeweza kuimudu hali hiyo na ndoa ingeokolewa na hasa kama ingekuwa Takatifu.
Lakini pia ni tatizo hata kwa mwanaume! kwani inaonekana ameingia katika taasisi hiyo takatifu kama vile alikuwa anakwenda disco. Tena diisco toto lile linalopigwa mchana na saa 12 jioni mwisho ili watoto warudi nyumbani.
Kwa bahati mbaya kamati za sherehe za harusi ambazo hudumu hata kwa maandalizi ya mwaka mzima, huwa hazioni kama mafunzo kwa wanandoa ni jambo muhimu na hata halipangiwi bajeti.
Ukienda kwa kile kinachoiwa kitchen party huko mitaani kwetu, na ukasikia wanachokisema ‘masomo’, kama hujapata kiu kwenye baridi kali basi wewe ni mtu tofauti.
Tunaigiza maisha kwa sababu, vijana hawatayarishwi vilivyo katika kuishi kwenye taasisi ya ndoa. Kuna jamaa wameoana miaka mingi na bahati nzuri baada ya kulia kwa kipindi kirefu sasa wamepata mtoto!
Kuoneshwa hawjatayarishwa vya kutosha, hata jina walilompa mtoto wamelitoa kwenye filamu ya katuni. Na kanisani hawakosi kila Dominika.
Mama hajui hata kunyonyesha anategemea aangalie kwenye mitandao, matokeo yake mtoto alimaliza siku kadhaa bila kushiba kwa kuwa alikuwa hawekwi mkao wa kunyonya.
Mtoto alikaribia kupata ulemavu kwa kuwa kwenye mitandao wanakataza kumrusha mtoto atakuwa taahira na alikuwa hata hanyooshwi viungo. Ni hatari!
Yaani vijana wanaojitayarishwa kwa ajili ya ndoa wanataka waishi kama wanayoyaona kwenye runinga, bila kujua kwamba sehemu kubwa wa yale wanayotazama ni maigizo.
Matokeo yake wanakosa kujitambua na umakini na hivyo wanakutana na mazingira yanayowataka kuishi maisha halisi matokeo yake wanakwama.
Wanataka waishi kama wasanii wa muziki ambao nao pia hawaishi maisha yao halisi, kwani kilichopo kwenye vyombo vya habari ni tofauti na yale yaliyopo kwenye familia zao.
Wanapata taarifa ambazo zimepakwa rangi za kupendeza kuliko hali halisi.
Na kimsingi hata wabunge na viongozi wengine wangekuwa wanapanda daladala wangetuwakilisha vilivyo.

SAKA (SALA NA KAZI)

DODOMA

Na Gaudence Hyera

Miongoni mwa Parokia zinazounda Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma ni ya Parokia ya Watakatifu Wote, Nzuguni, ambayo inatarajiwa kuadhimisha miaka mitatu Novemba Mosi mwaka huu, tangu ilipozinduliwa rasmi Novemba Mosi mwaka 2020 na Askofu Mkuu wa Jimbo hilo, Mhashamu Beatus Kinyaiya.
Kwa mujibu wa Takwimu za kichungaji zinaonesha kuwa kwa sasa Jimbo hilo lina Parokia 51na Parokia Teule mbili na vigango vinavyotarajiwa kupandishwa hadhi.
Parokia ya Watakatifu Wote, Nzuguni, inaundwa na Vigango vinne vilivyozinduliwa rasmi katika kipindi cha miaka miwili na miezi sita ya Utume wa Paroko wake wa kwanza, Padri Joseph Mkonde “Kazikunema”.
“Nilifika Dodoma wakati huo ikiwa Parokia Teule na ilituchukua miezi minne na kufanikisha kufanya uzinduzi wa kuwa Parokia, ambapo Kanisa lilifanyiwa maboresho na nyumba ya Padri na baadaye tukajenga nyumba inayotarajiwa kuwa ya Masista,” alisema Padri Mkonde.
Alivitaja vigango hivyo kuwa ni Kigango cha Mtakatifu Yohane Mbatizaji, Sokoine, ambacho kilianzishwa mwaka 1967; Kigango cha Roho Mtakatifu kilichoanzishwa mwaka 2022; na Kigango cha Bikira Maria Mpalizwa Mbinguni, cha mwaka 2022.
Kigango kipya cha Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Mvwagamale, Mtaa wa Magufuli kilizinduliwa Dominika ya Juni 11, 2023 sanjari na Adhimisho la Sherehe ya Mwili na Damu Takatifu ya Bwana Yesu Kristo.
Katika mahubiri yake wakati wa Misa hiyo Takatifu, Padri Kazikunema aliwataka waamini kuishi Kauli Mbiu inayohamasisha majitoleo kwa Sakramenti Kuu ambayo ni “Yesu wa Ekaristi Takatifu; Sadaka yangu; Chakula changu na Rafiki yangu”.
Parokia hiyo ni ya Kibalozi ikiwa chini ya Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma. Kichungaji na Kiutawala iko chini ya Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, baada ya Askofu Mkuu Kinyaiya, OFMCap, kukubaliana na Askofu Mkuu Jude Thaddaeus Ruwa’Ichi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.
Vivyo hivyo kwa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Parokia ya Kibalozi ni ya Mtakatifu Yuda Thadei, Stakishari, ambayo Paroko wake wa kwanza ni Padri Laurent Lelo kutoka Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma, ikiwa chini ya utawala wa Jimbo Kuu hilo, na uchungaji wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.
Parokia ya Watakatifu Wote, Nzuguni inaundwa na Vigango vinne vilivyozinduliwa rasmi katika kipindi cha miaka miwili na miezi sita ya Utume wa Paroko wa kwanza, Padri Joseph Mkonde “Kazikunema”.
Padri Mkonde ni miongoni mwa Mapadri watatu Wakurugenzi wenza wa miito ya Upadri, Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma, na pia ni mlezi wa Utume wa Mtakatifu Rita wa Kashia wa Jimbo hilo, ambapo Makao Makuu yake yapo katika Parokia ya Nzuguni.
“Nilifika Dodoma wakati huo ikiwa Parokia Teule, na ilituchukua miezi minne tu kufanikisha kufanya uzinduzi wa kuwa Parokia, ambapo kanisa lilifanyiwa maboresho pamoja na nyumba ya Padri, na baadaye tukajenga nyumba inayotarajiwa kuwa ya Masista, ambayo timu ya Tumaini Media ikiongozwa na Gaudence Hyera, ilifikia humo kwa muda wote walipokuwa Nzuguni kuanzia Juni 8 hadi 12; 2023” alieleza Padri Mkonde.
Alivitaja Vigango hivyo kuwa ni Kigango cha Mtakatifu Yohane Mbatizaji, Sokoine, ambacho kilianzishwa mwaka 1967; Kigango cha Roho Mtakatifu, Nharawanda, kilichozinduliwa mwaka 2022; na Kigango cha Bikira Maria Mpalizwa Mbinguni-Chamelo.
Kingine ni Kigango kipya cha Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Mvwagamale, Mtaa wa Magufuli kilichozinduliwa na Padri Joseph Mkonde Kazikunema, Dominika ya Juni 11 mwaka 2023, sanjari na Sherehe ya Mwili na Damu Takatifu ya Bwana Yesu Kristo.
Katika mahubiri yake wakati wa adhimisho la Misa Takatifu, Padri Kazikunema aliwataka waamini kuishi kauli mbiu inayohamasisha majitoleo (Totus Tuus)kwa Sakramenti Kuu, ambayo ni “Yesu wa Ekaristi Takatifu; Sadaka yangu; Chakula changu na Rafiki yangu.”
Jambo ambalo si jepesi na siyo kawaida, licha ya kutokea katika baadhi ya Parokia, ni andamo la Ekaristi ambalo lilichukua umbali wa zaidi ya kilomita 15, huku Paroko Padri Mkonde aliyekuwa peke yake, alibeba Monstrance yenye Hostia Takatifu, mpaka mwisho.
Andamo hilo lilianzia Mvwagamale, kupitia katika vigango na vituo vya sala vya Nanenane-Mtakatifu Faustina(Mtume wa Huruma ya Mungu), na Nhunduru-Mtakatifu Rita wa Kashia (muombezi wa mambo yaliyoshindikana), na kumalizikia Parokiani Nzuguni.
Akizungumzia shughuli za kichungaji, Padri Mkonde alieleza kuwa Misa Takatifu inaadhimishwa kila Dominika katika vigango vyote, akisaidiwa na mapadri na wengine wakiwemo Wamisionari wa Shirika la Ndugu Wafransisko Wakapuchin-OFMCap, na Ibada katika vituo vya Sala.
“Tunaendelea na miradi ya ujenzi parokiani na katika vigango vyote, ambapo ujenzi wa nyumba ya mapadri ya ghorofa tano, kwa matumizi mbalimbali ya kichungaji, inajengwa katika eneo la Parokia, pamoja na Grotto ya Familia Takatifu na ya Mtakatifu Rita wa Kashia,” alieleza Padri Mkonde.
Alieleza pia kuwa nyumba hiyo ya ghorofa tano kwa sasa inaonekana kama ni kubwa mno, lakini miaka ijayo itakuwa ndogo kwa kuwa wanatarajia mapadri, watawa na viongozi walei na waamini wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, watakuwa wanapata mahali pa kufikia wakiwa katika uinjilishaji Dodoma.
Aligusia pia katika Kigango cha Sokoine, ujenzi wa nyumba ya mapadri umeanza na pia mkakati wa kuongeza eneo lao kwa kununua baadhi ya nyumba za jirani, ili kufanya upanuzi wa kanisa na kujenga nyumba ya Masista.
Kigango cha Roho Mtakatifu kipo katika hatua ya kumalizia ujenzi wa kanisa na kupaka rangi, pamoja na kuanza ujenzi wa nyumba ya Mapadri, kwani wanayo matarajio makubwa ya kutangazwa kuwa Parokia Teule wakati wowote mwaka 2023 au 2024.
Akizungumza na Tumaini Letu, Mwenyekiti wa Halmashauri Walei wa Kigango hicho, Isaya Ntalugila alisema kuwa ni kigango cha pili kuzinduliwa katika Parokia ya Nzuguni, mbali na kuwa ni kigango cha pili, lakini kinasifika kwa waamini wake kujitoa kwa hali na mali katika kufanikisha maendeleo ya kiroho, kimwili na kijamii.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Kigango hicho, Jeremiah Msangi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Liturjia Kigango cha Roho Mtakatifu, alikazia kwamba hawana hofu kwamba kila jambo lililopangwa, ikiwemo miundombinu bora na taratibu za liturjia, ziko vizuri.
Msangi alieleza kuwa walipata ruhusa ya Paroko kuadhimisha Sherehe ya Mwili na Damu peke yao kutokana na utaratibu waliojipangia wa kufanya Andamo la sakramenti kuu kwa kupita katika kila nyumba ya mwamini kigangoni hapo na kuhamasisha Imani na majitoleo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kigango cha Bikira Maria Mpalizwa Mbinguni, Francis Mwakasege alisema kuwa kilizinduliwa rasmi Mei 28 mwaka 2023 na Paroko wa Parokia hiyo, Padri Joseph Mkonde Kazikunema.
Alibainisha pia kuwa matarajio ya waamini wa kigango hicho ndani ya miaka miwili, ni kuijenga ili iwe Parokia Teule.
Nao Viongozi wa Vyama vya Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA), Anecia Longino, na wa Utume wa Wanaume Katoliki (UWAKA), Acley Mushi, waliunga mkono kile ambacho alieleza Mwenyekit Mwakasege.
“Tumejipanga ili kuhakikisha tunapiga hatua za haraka kuyafikia malengo tuliyojiwekea, ikiwemo kuimarisha Utume wa Walei kuanzia ngazi ya Familia, Jumuiya na Vyama vya kitume,” walisema viongozi hao.
Nacho Kigango cha Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili kinaendelea kujiongeza kwa ujenzi wa kanisa, na kujiandaa kuanza ujenzi wa nyumba za mapadri, masista na huduma nyingine.
Parokia ya Nzuguni pia inazo Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo ambazo zinathibitisha uhai wa imani kwa waamini wake kiroho na kimwili, kutokana na kujitoa kwa moyo kushiriki kazi za uinjilishaji kuanzia mwamini binafsi, katika familia, hadi Parokiani.
Upande wa Vyama vya Kitume, Parokia hiyo inajumuisha Utoto Mtakatifu, Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA), Utume wa Wanaume Katoliki (UWAKA), Vijana Wakatoliki Wafanyakazi (VIWAWA), Utume wa Rita wa Kashia, Lejio Maria, na Utume wa Kwaya Katoliki Tanzania (UKWAKATA).
Kauli Mbiu ya Parokia ya Watakatifu Wote, Nzuguni, ni: “Watamtazama yule waliyemtoboa,” andiko linalopatikana katika Injili kama ilivyoandikwa na Mtakatifu Yohane, Sura ya 19, Aya ya 37.
Andiko hilo linasomeka chini ya msalaba kwenye Mnara wa Msalaba Mtakatifu uliosimikwa mbele ya lango kuu la Kanisa la Parokia ya Watakatifu Wote, Nzuguni.

Katika safu hii ya Chimba Chimba Historia ya Kanisa wiki iliyopita, tuliwaletea Historia ya Dini ilivyokuwa wakati wa Mapinduzi ya Viwanda (Industrial Revolution) barani Ulaya. Leo tunawaletea Misingi na Haki ya Mafundisho ya Kijamii ya Kanisa. Sasa endelea…

Mwaka 1967 Papa Paulo VI (1963-1978: wa 262) alitoa barua yake ya Kichungaji “Populorum Progressio,” yaani ‘Maendeleo ya Binadamu’. Licha ya mengine, alisisitiza kwamba hakuna maendeleo ya kweli, kama siyo ya binadamu wote.
Anasisitiza juu ya wajibu wa mataifa tajiri kusaidia yale maskini. Wakati wa kuadhimisha miaka 80 tangu itolewe barua ya Rerum Novarum Mei mwaka 1891, Papa Paulo VI alitoa barua ya Kitume mwezi Mei 1971 “Octogesima Adveniens”, yaani ”Ujio wa Miaka Themanini”.
Katika barua hiyo, aliongelea hasa hali duni katika miji. Tarehe 26 Oktoba 1975 alitoa barua nyingine ya “Evangelii Nuntiandi”, yaani “Utangazaji wa Injili”, ikiadhimisha miaka 10 ya Mtaguso wa Pili wa Vatikano (1962-1965), alisisitiza kwamba kazi ya Kanisa ni kupigana dhidi ya uonevu na udhalilishaji.
Papa Yohana Paulo II (1978-2005: wa 264) alitoa barua mbili kukazia mafundisho hayo ya Kanisa juu ya jamii. Mwaka 1981 ikiwa miaka 90 tangu barua ya Rerum Novarum, aliandika barua ya kitume ya “Laborem Exercens” akisisitiza kwamba haki binafsi ya kuwa na mali haipashwi kuathiri umma, yaani haki ya wote kuwa na mali au kukiuka haki za jamii.
Papa Yohana Paulo II alirudia mawazo hayo kwa mkazo zaidi, hasa akikosoa ubepari uliopindukia, na ujamaa hasi katika barua yake nyingine ya kitume “Centesimus Annus” ya mwaka 1991, akiadhimisha miaka 100 ya Rerum Novarum.
Kwa namna hii, unaonekana umuhimu wa barua ya Papa Leo XIII (1878-1903: 256) iliyolitoa Kanisa katika makucha ya mabepari bila kuiingiza katika utumwa wa wajamaa hasi, au ukomunisti. Kabla Papa Yohana Paulo II hajafariki mwaka 2005. ulitolewa muhtasari (Compendium) ya Mafundisho ya Kanisa juu ya jamii.
Papa Benedikto XVI (2005 -2013: wa 265) akifuata katika nyayo za watangulizi wake, mwaka 2009 alitoa barua ya Kitume “Caritas in Veritate”, yaani “Upendo katika Ukweli”.
Licha ya kusisitiza yale yaliyosemwa na watangulizi wake, pia aliisifu hasa barua ya kitume ya Papa Paulo VI ya mwaka 1967” Populorum Progressio” kwa kuongelea, siyo tu juu ya maslahi ya wafanyakazi, bali pia juu ya maendeleo ya binadamu mzima (Integral Developoment).
Papa Benedikto XVI alikosoa sana ubepari, akiuona kukosa utu na kuwa na ubinafsi wa kujitafutia faida kutoka kwa wengine bila kuona wajibu wa kurudisha vilevile kwa jamii. Alisisitiza juu ya haki za jamii kuzidi haki za mtu binafsi kupata faida. Alilaumu ubepari kwa madhara ya siki hizi, yakiwemo vilevile balaa la madawa ya kulevya.
Papa Fransisko (wa sasa: 2013: wa 266), mafundisho yake yote ni juu ya upendo na kujali. Mwaka 2016 alitangaza mwaka wa Huruma ya Mungu na Upatanisho. Mafundisho yote ya wakati huo yalikuwa Mungu atakuhurumia, nawe ukiwahurumia wengine.
“Kuweni na Huruma kama Baba yenu wa Mbunguni alivyo na Huruma.” Katika barua yake ya Kitume “Evangelium Gauduim” au “Furaha ya Injili” ya mwaka 2013, anasihi serikali mbalimbali na vyombo vya kimataifa vya fedha kuhakikisha kuwa watu wanapata haki za msingi, yaani kazi, afya na elimu.
Anakubali haki ya serikali kuingilia uchumi kwa wema wa umma. Anapinga utamaduni wa kuabudu fedha na kuacha soko huria kwa faida ya wachache, wakati wengi wanakuwa fukara. Analaami utofauti unaoongezeka kati ya walionacho na wasionacho.
Katika barua nyingine ya Kitume ya mwaka 2015 “Laudato Si”, ambayo ilipokelewa vizuri sana na watu wa rika na Imani mbalimbali, anaongelea siyo tu juu ya haki ya wanyonge, bali na ulazima wa kutunza mazingira, na kulaani matumizi mabaya ya nyenzo za dunia kwa sababu ya ulafi.
Aliongeza barua nyingine mbili akisisitiza juu ya upendo na kujali; “Gaudete et Exultate” yaani “Furahini na Kushangilia” ya mwaka 2018 na “Fratelli Tutti”, yaani “Sote ni Ndugu”, ya mwaka 2020.
Kanisa katika mafundisho yake ya kijamii katika miaka hii yote, imesisitiza juu ya mambo yafuatayo:

1.    Haki ya Uhai:
    Maisha ya binadamu ni matakatifu tangu kutungwa mimba hadi kifo. Kila binadamu siyo tu ana haki ya kuishi, bali pia ana haki ya kupata heshima. Katika mafundisho yake yote, Kanisa linasisitiza kwamba kila binadamu ameumbwa katika sura ya Mungu, na watu wote wana haki sawa mbele ya Mungu, na hivyo wanastahili heshima.

2.    Auni (Subsidiarity):
    Hii ilisisitizwa hasa kuanzia na barua ya Papa Pio XI ya Quadragesimo Anno mwaka 1931. Madaraka ya juu yasichukue kile ambacho madaraka ya chini yanaweza, na yana haki nacho. Mkubwa asaidie kile ambacho mdogo hawezi peke yake kufanya, la sivyo unamnyang’anya heshima na juhudi zake.

3.    Mshikamamno na kufanya juhudi kwa wema wa wote (Common Good):
    Watu hatuko kisiwa, hivyo lazima kusaidiana kama binafsi, kama junuiya, na kama mataifa.

4.    Upendo ndio upeo wa yote:
    Hapa siyo upendo wa kihisia, bali ni upendo wa kweli wa kujitoa kwa ajili ya wengine.
    Hayo maagizo manne yanakuwa msingi wa haki na wajibu katika Mafundisho ya Kanisa juu ya jamii kama haki ya kupata kazi; haki ya familia; haki ya uhuru wa kuabudu na kuwasiliana; utunzaji wa mazingira; haki ya kuwa na mali binafsi; kujali maskini; na wasiojiweza.

Masista na Waamini wa Parokia ya Mtakatifu Ambrose Tagaste, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, wakiwa katika Adhimisho la Misa Takatifu ya kutoa Sakramenti Takatifu ya Kipaimara, iliyofanyika parokiani hapo.