Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, amawasihi Wakatoliki kuacha woga kumtangaza Yesu Kristo, kwa sababu imani ndiyo inayowasaidia maishani.
Kardinali Pengo alitoa wito huo wakati akihubiri katika Adhimisho la Misa Takatifu ya kutoa Sakrameti ya Kipaimara kwa vijana 25, wa Parokia ya Mtakatifu Andrea Mtume, Bahari Beach.
“Ndugu zangu Waamini nawaomba sana, huyu Kristo tuko naye, kwa hiyo kama yupo anayejifichaficha, aache tabia hiyo, tumtangaze Kristo, ili na yeye atusaidie katika maisha yetu:
“Utakuta watu wengine ni Wakristo wazuri sana, lakini wanapenda kuwa na tabia ya kujificha,” alisema Kardinali Pengo.
Alisema kuwa hata wakati wa kula chakula, hawapigi ishara ya msalaba, hawasali kabisa kwa sababu ya woga.
Kardinali Pengo alibainisha kuwa tabia ya Mkristo kuwaogopa watu wakati wa kuombea chakula, haifai, kwani Mkristo kamili hatakiwi kumwogopa mtu, bali anatakiwa kumtangaza Bwana Yesu Kristo mahali popote pale.
Aidha, Kardinali Pengo aliwataka vijana waliompokea Roho Mtakatifu kupitia Sakramenti hiyo kutokuwa na woga, wakamtangaze Yesu katika maisha yao.
Aliwakumbusha vijana hao kufahamu kwamba kupitia Sakramenti hiyo, wamekuwa Askari imara wa Kristo, hivyo wanatumwa kwenda kumtangaza yeye.
Kardinali Pengo alisema kuwa imani ndiyo msingi wa maisha ya kila mmoja, akiwasihi Waimarishwa hao kusali kila wakati, kwani kwa kufanya hivyo, Ufalme wa Mungu utakuwa wokovu kwao.
Kardinali aliwashukuru Waamini wa Parokia ya Bahari Beach kwa zawadi walizompatia, huku akiwapongeza kwa hatua kubwa waliyopiga parokiani hapo, ikiwemo ujenzi wa kanisa, akisema kuwa anatamani kuona ujenzi huo ukimalizika mapema, ili na yeye afike tena kwa ajili ya kusali pamoja na Waamini hao parokiani hapo.
Kwa upande wake Paroko wa Parokia hiyo, Padri Marko Loth alimshukuru Kardinali Pengo kwa kuwapatia Sakramenti vijana hao.
Naye Mwenyekiti wa Parokia hiyo, Balozi Dk. James Msekela alisema kuwa hiyo ni siku kubwa kwao kwa kutembelewa na Kardinali Pengo, akiwaomba
Waamini wa Parokia hiyo kuongeza ushirikiano ili wamalize ujenzi wa kanisa lao kwa wakati uliokusudiwa.

Dar es Salaam

Na Mathayo Kijazi

Wazazi nchini wametakiwa kutambua kwamba namna wanavyoishi, na watoto wao pia wataishi kama wao.
Ili waweze kufuata maisha mema, wazazi hao wametakiwa kuishi maisha ya unyenyekevu na yenye kumpendeza Mungu, kwani watoto huiga mambo wanayofanya wazazi wao.
Hayo yalisemwa hivi karibuni na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Stephano Musomba wakati akitoa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya kutoa Sakramenti ya Kipaimara kwa vijana 158, wa Parokia ya Mtakatifu Monica, Matosa, jijini Dar es Salaam.
“Kwa hiyo, jinsi mnavyoishi ninyi wazazi, ndivyo watoto wenu watakavyoishi, kwa sababu hatua ya kwanza ya watoto, ni kuiga yale yanayofanywa na wazazi wao,” alisema Askofu Musomba.
Katika homilia yake Askofu huyo, aliwataka wazazi kuwaonyesha njia watoto wao, ili wafahamu namna ya kuwasiliana na Mungu katika maisha yao.
Aidha, Askofu Musomba aliwasisitiza wazazi hao kuwategemeza na kuwalinda watoto wao dhidi ya mashambulizi mbalimbali yaliyopo, ili wasiharibike katika ulimwengu huu.
Aliwasihi Waimarishwa wa Sakramenti Takatifu ya Kipaimara kutokuwa na hofu wala woga, kwani Roho Mtakatifu waliyempokea kupitia Sakramenti hiyo, atawapa nguvu ya kuyashinda majaribu wanayokutana nayo kila wakati.
Askofu Musomba aliwataka vijana hao kutosikiliza kelele zilizopo katikati yao, bali waisikilize sauti ya Kristo pekee.
Wakati huo huo, Askofu Musomba aliwaasa vijana hao kuwa wanyenyekevu katika maisha yao, kwani ndio utakaowasaidia kuisikia sauti ya Kristo katika maisha yao.

DAR ES SALAAM

Na Happiness Mthathia-TUDARCO

Serikali imesema kwamba imejipanga kupunguza kero ya usafiri kwa wanafunzi jijini Dar es Salaam, kwa kutekeleza mikakati iliyojiwekea, ikiwemo kutumia usafiri wa mabasi yaendayo haraka (Dar es Salaam Rapid Transit: DART) na Treni.
Hayo yalisemwa na Alhaji Maulidi, Afisa Elimu wa Mkoa wa Dar es Salaam wakati akizungumza na gazeti Tumaini Letu katika mahojiano maalum yaliyofanyika ofisini kwake jijini Dar es Salaam, kuhusu kero ya usafiri kwa wanafunzi. 
“Serikali inaendeleza ujenzi wa barabara za mabasi yaendayo haraka, ikiwemo barabara iendayo Gongo la Mboto kutoka mwanzo wa Barabara ya Nyerere, Msimbazi, Kariakoo. Pia, ina mkakati wa kujenga barabara kutoka Morocco (Kinondoni) kwenda Tegeta, na itafika mpaka Bunju ili kuwasaidia wanafunzi,” alisema Maulidi.
Alisema pia kuwa mpango wao ni kushirikisha sekta binafsi katika kutatua changamoto ya usafiri kwa wanafunzi jijini Dar es Salaam, kwani kwa sasa hali ni nzuri ikilinganishwa na ilivyokuwa katika miaka ya nyuma.
Maulidi alisema kuwa jukumu la Serikali kwa wanafunzi ni kuwapatia elimu bora, na kuongeza kuwa wazazi wana jukumu la kuhakikisha watoto wanafika shuleni na kurudi nyumbani kwa kuwapatia nauli kwa ajili ya usafiri.
Afisa huyo aliwataka makondakta kuwahudumia wanafunzi waweze kusafiri kwa wakati ili kupunguza changamoto wanayokumbana nayo, na kuwakanya wanafunzi nao ili wajiheshimu.
Baadhi ya wanafunzi wameliambia gazeti hili kwamba wamekuwa wakikabiliwa na changamoto kubwa ya usafiri nyakati za asubuhi na jioni kwa kukataliwa na makondakta wa daladala, na hivyo kuchelewa kwenda shule na kurejea nyumbani.
Mmmoja wa wanafunzi hao, John Elias wa Shule ya Sekondari Kawe Ukwamani jijini Dar es Salaam, alisema kuwa wanakumbana na changamoto hiyo mara kwa mara.
“Tumekua tukikataliwa na makonda kuingia kwenye daladala kitu ambacho kinasababisha tuchelewe kufika shule pia kurudi nyumbani nyakati za jioni,’’ alisema John.
Kwa upande wao baadhi ya wazazi akiwemo Mama Jordan, Mkazi wa Mtaa wa Goba jijini Dar es Salaam, alithibitisha kuwepo kwa changamoto hiyo kwa wanafunzi, akisema kuwa sababu ya makondakta kuwakwepa wanafunzi ni kiasi cha nauli wanacholipa cha Shilingi 200/=, hivyo wanaona bora wanafunzi waachwe.

DAR ES SALAAM

Na Deus Kamanga

Waamini wametakiwa kuendelea kuunga mkono jitihada za Kanisa katika kufanikisha maendeleo kwa vyombo vya Habari vya Kanisa ili viweze kufikisha ujumbe wa Mwenyezi Mungu kwa watu wote Ulimwenguni, kwani kwa kufanya hivyo watajipatia neema na baraka kwa Mungu.
Wito huo ulitolewa hivi karibuni na Padri Vitalis Kassembo, Mkurugenzi wa Walei Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam wakati akitoa homilia katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Shukrani ya Umoja wa Marafiki wa Tumaini Media (UMTUME), kuadhimisha Siku ya Mawasiliano Duniani iliyofanyika Parokia ya Bikira Maria Mama wa Fatima – Msimbazi, jijini Dar es Salaam.
Padri Kassembo ambaye pia ni Paroko wa Parokia ya Familia Takatifu - Mburahati, jimboni humo, alisema kuwa Kituo cha Tumaini Media jimboni Dar es Salaam, ni miongoni mwa vyombo vya Habari ndani ya Kanisa kinachofikisha ujumbe wa Mungu kwa watu, kikielimisha na kuhabarisha masuala mbalimbali ya kijamii yanayostawisha maelewano mazuri yenye kuleta mshikamano unaompendeza Mungu.
Padri Kassembo alisema kuwa jitihada zinazofanywa na Utume kwa ajili ya maendeleo ya Tumaini Media ni mfano dhahiri kwa waamini na watu wenye mapenzi mema na Kituo hicho cha Kanisa, hivyo akawataka waamini na watu wengine kuiga mfano huo kwa kuendelea kumshukuru Mungu, sanjari na kukichangia ili kisonge mbele.
Aliongeza pia kuwa ni jambo la msingi kwa kila mbatizwa kushirikiana na Kanisa na Taasisi zingine zenye nia njema ya kuviwezesha vyombo hivyo, wakiwemo UMTUME, kwa hali na mali kwa kuwa kufanya hivyo ni kujiwekea hazina mbinguni.
Awali Mkufunzi wa semina ya Umtume, Maalim Jeran Mushi aliwaasa Wanaumtume kudumisha upendo na umoja katika kutekeleza utume wao, kwa kutawaliwa na upole, unyenyekevu, hekima na amani.
Maalim Mushi alibainisha kuwa Wanaumtume wanapaswa kuwafikia watu wote katika hali ya unyenyekevu kwa kuwashirikisha lengo la kuisadia Tumaini Media kiuchumi, na kuacha tabia ya kukata tamaa kwa sababu Mungu Mwenyezi anaziona nia zao, na hawezi kuwaacha katika magumu yoyote.
Alifafanua kuwa kiasi hicho cha fedha kitaelekezwa kufanyia maboresho eneo la mapokezi katika ofisi za Tumaini Media, na wataendelea na maboresho kulingana na uhitaji wa maeneo mengine.

DAR ES SALAAM

Na Esther Ngubes-TURDACO

Kamishna Msaidizi wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Michael Stephen Deleli, amesema kuwa ajali nyingi za bodaboda, zinatokana na usimamizi mbovu wa wamiliki wa vyombo hivyo, kutokana na baadhi yao kuwapa madereva wasio na weledi.
Akizungumza na gazeti Tumaini Letu katika mahojiano maalumu yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, Kamishna Deleli alisema kuwa wamiliki wengi wa bodaboda hawawasimamii vema watu wanaowapa pikipiki hizo ikiwemo kutozingatia kama wana leseni ama laa.
Aidha, alisema kuwa jambo lingine ni woga wa abiria kushindwa kuwaonya madereva pindi wanapotumia usafiri huo, hasa wanapokwenda mwendo kasi, na uwezekano wa kusababisha ajali.
“Katika tathmini yetu, tumegundua kuwa ajali nyingi hususan za bodaboda, zinasababishwa na ukosefu wa usimamizi wa vyombo hivyo vya usafiri kutoka kwa wamiliki wakuu…
“Pia, woga wa abiria pindi wanapotumia usafiri huo kwa kushindwa kuwaonya madereva wanapoendesha kwa mwendo kasi, hii ni kutokujua wajibu na haki zao za kimsingi wanapokuwa barabarani,” alisema Kamishna Deleli.
Alibainisha pia kuwa takwimu zinaonyesha kwamba ajali nyingi zinatokana na miundombinu mibovu ya barabara, ubovu wa vyombo vyenyewe vya usafiri, pamoja na makosa ya kibinadamu yanayosababishwa na ukosefu wa elimu kuhusu matumizi sahihi ya barabara kwa kuzingatia Sheria za Usalama Barabarani.
Aidha, Deleli alisema kuwa kulingana na makosa hayo, baadhi ya madereva huvunja sheria kwa makusudi kutokana na sababu za kumchelewesha abiria, na sababu nyingine binafsi.
Alisema kuwa Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani kimeweka mikakati madhubuti ili kuhakikisha ajali za barabarani zinapungua kwa kiasi kikubwa, hususani ajali za pikipiki, ikiwemo kutoa elimu kwa madereva wa pikipiki kwa kuweka sheria kali zitakazosaidia kupungua kwa ajali hizo.
Kamishina Deleli alisema kuwa miongoni mwa adhabu hizo ni kifungo au faini kwa yeyote atakayejihusisha na uvunjifu wa sheria hizo.
“Natoa rai kwa wananchi wote, madereva, na wamiliki wakuu wa vyombo hivyo vya usafiri, hususani pikipiki, wahakikishe kuwa vyombo hivyo vya usafiri vipo katika mikono salama ya madereva hao.
“Nasisitiza sana kwa madereva wa pikipiki kujiepusha na uendeshaji wa mwendokasi, kuvaa kofia ngumu (helmet), kujiepusha na upakiaji hatarishi wa abiria zaidi ya mmoja, na uendeshaji wa pikipiki ukiwa umetumia kilevi au afya ya mwili ikiwa haipo vizuri,” alisema Kamishna Deleli.
Akizungumza na Tumaini Letu, mmoja wa madereva wa pikipiki aliyejitambulisha kwa jina la Temu, alisema kuwa Sheria za Usalama barabarani wanazifuata, lakini kutokana na makosa ya kibinadam na baadhi ya changamoto zinakuwa nje ya uwezo wao, hujikuta wakisababisha ajali hizo.

DAR ES SALAAM

Na Angela Msele

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi amewausia Waamini na watoto kuacha dhambi ya wivu, kwani itawasababishia kupata ukoma wa kiroho.
Amewakumbusha Waamini kufahamu kwamba Agosti 8 kila mwaka, ni siku ya kumuenzi Mtakatifu Dominiko aliyeishi karne ya 13, ambaye ndiye mwanzilishi wa Shirika la Dominiko.
Askofu Mkuu Ruwa’ichi aliyasema hayo hivi karibuni wakati akihubiri katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Shukrani kwa Mungu kwa safari za Kitume za Watoto wa Shirika la Kipapa la Utoto Mtakatifu Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam walizozifanya katika Jimbo Katoliki la Kondoa mkoani Dodoma na Utete mkoani Pwani, iliyofanyika Parokia ya Bikira Maria wa Fatima – Msimbazi, jimboni Dar es Salaam.
“Tunakuwa wakoma wa kiroho pale tunapochukiana na kuoneana wivu, na tunapofanya mambo mabaya yanayowaumiza wenzetu,”alisema Askofu Rua’ichi na kuongeza;
“Yesu anatufundisha Neno la Mungu, yeye ambaye ni Neno wa Mungu, kwa upendo wake alifufua wafu, aliwaponya wagonjwa na kulisha wenye njaa…daima tunatakiwa kuwa watu wa sala, kwa sababu hata Yesu ambaye ni mwana wa Mungu, alisali.”
Askofu Mkuu Ruwa’ichi alibainisha kuwa sala ni mahusiano kati ya binadamu na Mungu, inayowaunganisha wanadamu na Mwenyezi.
Naye aliyekuwa Mkurugenzi wa Mashirika ya Kipapa Taifa (PMS), Padri Jivitus Kaijage, alimshukuru Mungu kwa kumaliza salama muda wake wa utume katika nafasi hiyo, akimshukuru Askofu Mkuu Ruwa’ichi kwa ushirikiano wake katika kipindi chote cha miaka 12 ya kuwa Mkurugenzi wa mashirika hayo.
Kwa upande wake Padri Alfred Gwene, Mkurugenzi mpya wa PMS,Taifa, aliwataka walezi kuwafundisha sala watoto hao na kuwafanya washiriki shughuli zote za kimisionari.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Walezi wa Utoto Mtakatifu Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Cletus Majani, alimshukuru Askofu Mkuu Ruwa’ichi kwa kuwapa ruhusa ya kushiriki Makongamano yote yaliyofanyika katika Majimbo hayo.
Aliongeza kuwa Kongamano la Utoto Mtakatifu lililofanyika Utete mkoani Pwani, lilizaa matunda kwa kupata kijana wa Kidato cha Pili kutoka Dini nyingine, ambaye aliomba kubatizwa ili awe Mkatoliki, ambaye tayari ameanza mafundisho, kwa ruhusa ya wazazi wake.
Katika misa hiyo parokia 10 bora zilizotoa idadi kubwa ya watoto katika Makongamano hayo, zilipoongezwa na kuzawadiwa vyeti.

DAR ES SALAAM

Na Mathayo Kijazi

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi, amesema kuwa jamii isipobadilika na kuwekeza katika maadili mema kwa watoto wao, Ulimwengu utawateka.
Askofu Mkuu Ruwa’ichi alisema hayo katika Adhimisho la Misa Takatifu ya kutoa Sakramenti ya Kipaimara iliyokwenda sanjari na Kutabaruku Kanisa la Parokia ya Kung’ara kwa Yesu Kristo, Mbezi Mshikamano, iliyokuwa ikifahamika awali kama Parokia ya Mtakatifu Yohane Paul II, Mbezi Mshikamano.
Aidha, Askofu Mkuu Ruwa’ichi alimwagiza Paroko wa Parokia hiyo kuhakikisha watoto wote walioimarishwa wanatengenezewa utaratibu mzuri wa kuendelea na mafunzo ya Imani Katoliki, ili waweze kuimarika zaidi katika Imani hiyo.
Wazazi na walezi walikumbushwa pia kufahamu kwamba kwa sasa Dunia imekengeuka, hivyo ni wajibu wao kuhakikisha kwamba wanawekeza Imani kwa watoto wao, kwani kwa kushindwa kufanya hivyo, Ulimwengu utawekeza kwa watoto hao, na hivyo watapotezwa.
“Wekezeni maadili mema kwa Watoto wenu, hasa katika wakati huu ambapo dunia hii imemezwa na mambo mabaya kwa sababu msipowekeza sasa, dunia itawekeza kwako,” alisema Askofu Mkuu Ruwa’ichi.
Askofu Mkuu aliongeza kuwa hali ya maisha ya Dunia hasa katika suala la maadili, limekuwa baya akiisihi jamii kuwalea watoto katika misingi thabiti ya kiimani, ili watoto hao wasije kutekwa na Ulimwengu.
Awali katika homilia yake Askofu Mkuu Ruwa’ichi, aliwasisitiza Waamini hao kuwa kama walivyojenga kanisa zuri, wanatakiwa pia kuwa wazuri na wenye kujaa neema kutoka ndani ya mioyo yao.
“Wewe ni kanisa, wewe ni hekalu, wewe ni makao ya Roho Mtakatifu. Sasa kama mmejenga kanisa zuri, hebu kwanza muanze ninyi wenyewe kuwa wazuri. Muanze kujifunza kuwa watu mliojaa neema. Msiruhusu Mioyo yenu, akili zenu, dhamiri zenu, na nafsi zenu zijae masizi ya dhambi,” alisema Askofu Ruwa’ichi.
Aidha, aliwakumbusha Waamini wa parokia hiyo kufahamu kwamba kanisa na altare vinapopakwa mafuta ya Krisma, vinakabidhiwa mikononi mwa Mungu ili aviweke rasmi kwa ajili ya mambo yanayomhusu Yeye na watu wake.
Askofu Mkuu aliwataka Wakristo hao kulitumia kanisa hilo kwa ibada stahiki na kwa heshima inayostahili, akiwaonya wale wasioelewa kwamba wako wapi, watambue wako mahali patakatifu.

DAR ES SALAAM

Na Mathayo Kijazi

Imeelezwa kuwa Mungu ameumba uoto wa asili, maji, na viumbe malimbalimbali duniani ili visiharibiwe, kwani chanzo cha kutoka kwa mabadiliko ya tabianchi ni kuharibiwa kwa mazingira.
Hayo yalisemwa hivi karibuni na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddeus Ruwa’ichi wakati akihubiri katika Adhimisho la Misa Takatifu ya kutoa Sakramenti Takatifu ya Kipaimara kwa vijana 42 wa Parokia ya Mtakatifu Yohane Mbatizaji – Msongola ‘B’, jimboni humo.
“Mnaposikiliza taariba ya habari, au mnaposoma kwenye magazeti, na kwenye vilongalonga vyenu, mnaona mahali pengi kuna habari juu ya Tabianchi. Hayo mabadiliko ya tabianchi yanamuumiza mwanadamu, yanaviumiza viumbe, yanatusambaratisha,” alisema Askofu Mkuu Ruwa’ichi:
“Sasa hayo mabadiliko ya tabianchi hayakutokea hivi hivi, kuna mkono wa mtu. Sasa msiseme kwamba Askofu anashabikia uchawi, ninaposema kuna mkono wa mtu, sina maana kwamba kuna mchawi, kama kuna mchawi ni sisi, yaani mimi na wewe. Mkono unaovuruga nchi na kufanya kuwe na mabadiliko holela, ni mkono wa mwanadamu mvurugaji, mwanadamu mchafuaji.”
Askofu Ruwa’ichi aliwasisitiza kuwa Wakristo wanatakiwa kutodhoofisha uoto wa asili ulioumbwa na Mungu, akisema, “Mnatambua kwamba pale mlipofyeka mkaondoa uoto wa asili, pamedhoofika. Kwa hiyo Mungu aliyeumba uoto wa asili, aliyeumba miti, aliyeumba maji, aliyeumba majani, aliyeumba wanyama na ndege, ametaka vitu hivi vitumiwe kwa utaratibu kusudi vimhifadhi mwanadamu kwa vizazi vyote.”
Aliongeza kuwa sehemu yoyote yenye joto kali lililopitiliza, hakuna mwanadamu anayeweza kuishi wala kustahimili hapo, hivyo yeyote anayevuruga na kuharibu mpangilio huo wa asili, anajitakia maangamizi.
Wakati huo huo Askofu Mkuu Ruwa’ichi aliwasisitiza Waamini kujenga urafiki na maumbile, akiwataka kuyaratibu, kuyatumia kwa uangalifu na staha kama Mwenyezi Mungu alivyoagiza.
Kwa mujibu wa Askofu Mkuu, Waamini wanapaswa kuwa na mahusiano mazuri kati yao na Mungu, akiwasihi wapende kujenga mahusiano safi, hai, na yenye tija na Mungu wao, kwani wakitenda hivyo, watakuwa wanajitahidi kuzingatia anayotaka Mungu.
Wakati huo huo, Askofu Mkuu huyo aliwaasa waamini daima kuwa watu wa amani, wakiwa viumbe wenye kupendana na kusaidiana, badala ya kusakamana.
Awapa darasa Waimarishwa
Akizungumzia kuhusu Waimarishwa hao, Askofu Mkuu Ruwa’ichi aliwataka vijana hao kufahamu kwamba wanapompokea Roho Mtakatifu, wanakamilishwa, na hivyo wanatumwa kuifanya kazi ya kuitangaza Habari Njema kwa watu wote.
Paroko na Paroko Msaidizi, kwa kushirikiana na wazazi parokiani hapo, waliagizwa na Askofu Mkuu Ruwa’ichi kuendelea kuwapatia mafunzo ya kiimani vijana hao ili wakue katika misingi yenye maadili mema.

Dar es Salaam

Na Salum Mgweno-SJMC

Soko la Kilamba katika Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam, limegeuka gofu baada ya kutelekezwa na wafanyabiashara kwa takriban miaka miwili.
Moja ya sababu za kulikacha soko hilo ni ubovu wa barabara, hali inayowalazimu wananchi wa maeneo hayo kutembea umbali mrefu kufuata mahitaji yao katika masoko ya mbali.
Akizungumza na Tumaini Letu, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kilamba Nzasa B, Hassan Ugando alisema kuwa soko hilo lenye vizimba takribani, 72, lilianzishwa tangu mwaka 2005 kwa gharama ya Shilingi milioni 100, ambapo Shilingi milioni 80 ni kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, huku Shilingi milioni 20 zikiwa ni nguvu za wananchi, limekuwa likitumika msimu kwa msimu na kisha kutelekezwa, ambapo kwa mara ya mwisho kutumiwa na wafanyabiashara ilikuwa mwaka 2021.
“Mwaka 2020 kwenda 2021, bado kulikuwa na wafanyabiashara kadhaa ambao pia waliondoka. Kwa hiyo kama unavyoona, wamebaki wale wachache wenye vibanda pembeni mwa soko na yule wa buchani tu,” alisema Ugando.
Ugando alisema kuwa miongoni mwa sababu za soko hilo kukosa ustawi wa kibiashara baada ya kukamilika ujenzi wake, ni kwamba waliokabidhiwa vizimba vya biashara hawakuwa wafanyabiashara.
Kwa mujibu wa Ugando, pia ugawaji wa vizimba hivyo, ulitoa kipaumbele kwa wananchi walioshiriki bega kwa bega ujenzi wa soko hilo. Hivyo licha ya wengi wao kuwa siyo wafanyabiashara, walichukua kwa lengo la kukodisha ili wapate pesa.
Ugando alisema kuwa ubovu wa barabara pia umechangia watu kulikimbia soko hilo, na hivyo kuendeelea kusalia kuwa gofu na mapango ya ndege.
Ugando amelieleza Tumaini Letu kuwa kitendo cha wafanyabiashara kukimbilia maeneo ya barabarani wakiamini kuwa ndiyo sehemu yenye mzunguko mzuri wa biashara kutokana na idadi kubwa ya watu, imedhoosha soko hilo.
Naye Emmanuel Pascal, mfanyabiashara wa nyama pembezoni mwa soko hilo, aliiomba Serikali kukarabati vyoo na huduma ya maji, ili kuweka sawa mazingira ya soko hilo.

LUSAKA, Zambia
Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Zambia, Zambia Conference of Catholic Bishops (ZCCB), Askofu Mkuu Mhashamu Ignatius Chama amewataka vijana waliohitimu Chuo Kikuu cha Kikatoliki Zambia, kuwa mabalozi wa uadilifu katika maisha binafsi na kitaaluma.
Askofu Mkuu Chama alisema hayo wakati wa mahafali ya 12 ya Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Zambia, na kueleza kwamba ubora wa kitaaluma, siyo tu kupata alama za juu, bali ni kukuza kiu ya maarifa, kukuza ujuzi wa kufikiri kwa kina, na kukuza shauku kubwa ya kujifunza.