Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

LONDON, England
Bingwa wa masumbwi mara mbili kwa upande wa wanawake Natasha Jonas, anatarajiwa kupanda ulingoni kupigania taji lake la nne la dunia mnamo Julai 1 mwaka huu.
Natasha atapambana na Kandi Wyatt raia wa Canada kuwania taji lililo wazi la IBF uzito wa welter kwenye pambano la linguini likiwakutanisha wakinadada Franchon Crews-Dezurn dhidi ya Savannah Marshall.
Jonas, ambaye tayari amejumuishwa katika orodha ya WBC, IBF na WBO uzito wa super-welterweight, atashuka kwenye uzani wa welter kupigana na Kandi Wyatt kuwania ubingwa wa IBF ulio wazi wa pauni 147.
Pambano hili la ubingwa ni pambano la kwanza kwa Natasha mwaka huu, kufuatia kupambana sana mwaka 2022 alipopanda daraja mara tatu na kunyakua mataji matatu ya dunia, akiwa na uzito wa pauni (ratili) 154.
Mchezo huo ulimfanya awe mwanamke wa kwanza kutwaa taji la Bondia Bora wa Mwaka wa Uingereza katika tuzo za kila mwaka za Bodi ya Ndondi ya Uingereza.

Dar es Salaam

Na Arone Mpanduka

Arsenal ilianza kama utani hivi pale kikundi cha wafanyakazi katika kiwanda cha kuzalisha zana za kivita cha Woolwich, walipoamua kuunda klabu ya soka mwishoni mwa mwaka 1886.
Klabu ikawa ikishiriki michezo huku ikijulikana kama Dial Square. Mchezo wao wa kwanza waliifunga timu ya Eastern Wanderers 6-0, tarehe Desemba 11 mwaka 1886.
Baada ya muda mfupi, jina likabadilishwa na kuwa Royal Arsenal, huku timu ikiendelea kushiriki katika michezo ya kirafiki na mashindano ya nyumbani kwa kipindi cha miaka michache iliyofuata.
Mwaka 1891 klabu ikawa ya kulipwa na kubadilisha jina na kuitwa Woolwich Arsenal, na hatimaye kujiunga na ligi ya soka mwaka 1893.
Baadae jina lilibadilika kutoka Woolwich Arsenal na kubaki Arsenal, ambalo jina lake la umaarufu ni ‘The Gunners’ (washika bunduki), wanaitwa washika bunduki kwa sababu ya kutokea kwenye kiwanda cha kuzalisha silaha.
‘Washika bunduki’ hao wakahamia Highbury mwaka 1913 kama timu ya Ligi Daraja la Pili. Baada ya Vita ya Kwanza ya Dunia (1914-1918), Arsenal wakapigiwa kura na kuingizwa katika ligi daraja la kwanza, iliyokuwa imeongezwa ukubwa, ambako wameendelea kudumu hadi leo.
Herbert Chapman (pichani) alichukua nafasi ya kuiongoza Arsenal mwaka 1925, na mwaka 1930 akaiwezesha kupata taji lao la kwanza kabisa pale walipoifunga Huddersield katika fainali ya kombe la FA.
Mwaka uliofuata Arsenal wakawa mabingwa kwa mara ya kwanza. Kati ya mwaka 1933 na 1935 timu ikaweza kunyakua ubingwa mara tatu mfululizo (hali ambayo imeweza kufikiwa tu na timu nne vigogo). Chapman alifariki katikati ya safari hiyo ya mafanikio akiwa tayari ni mtu wa historia kubwa klabuni.
Vita ya Pili ya Dunia ilikata mwendo kasi wa Arsenal. Lakini baada ya vita hivyo, Tom Whittaker akawa meneja na mafanikio zaidi yakafuata. Arsenal wakawa mabingwa 1947/48 na 1952/53; washindi wa kombe la FA 1950 na washindi wa pili 1952.
Mwaka 1986, George Graham aliyekuwa mchezaji katika kikosi kilichochukua ubingwa 1971, akawa meneja akichukua nafasi ya Don Howe. Siku njema zaidi zikafuata. Akaiongoza Arsenal kunyakua kwa mara ya kwanza kombe la ligi mwaka 1986/87 kwa kuifunga Liverpool katika fainali.
Miaka miwili baadae washika bunduki wakanyakua ubingwa wa ligi na goli maarufu la dakika ya mwisho kutoka kwa Michael Thomas na matokeo kuwa 2-0 ndani ya Anfield. Taji jingine ikawa mwaka 1990/91 wakiwa na kikosi kilichopoteza mchezo mmoja tu, wakijivunia ukuta imara wa mabeki wanne.
Vikombe zaidi vikafuata. Mwaka 1992/93 Arsenal ikawa klabu ya kwanza kuchukua vikombe vyote vya ligi ya England katika msimu mmoja.
Msimu kamili wa kwanza wa Arsene Wenger 1997/98 katika uwanja wa Highbury, ulishuhudia Arsenal kwa mara ya pili katika historia yake ikifanikiwa kunyakua vikombe vyote viwili; cha Ligi Kuu na FA, na kumwezesha kocha huyo Mfaransa huyo kuchukua tuzo ya Carling ya meneja bora wa mwaka.
Dennis Bergkamp akawa mwanasoka bora wa mwaka wa Chama cha Waandishi wa Habari za Soka (FWA) na mwanasoka bora wa mwaka wa Chama Cha Wanasoka wa Kulipwa (PFA). Msimu huo uling’ara zaidi kwa wanasoka wa Arsenal kutoka Ufaransa Emmanuel Petit na Patrick Vieira, baada ya kutoa mchango wao mkubwa katika ushindi wa timu yao ya taifa katika fainali za Kombe la Dunia mwaka 1998.
Msimu wa 2003/04 Arsenal wakamaliza michezo yote bila ya kufungwa na kuchukua taji la ubingwa wa Ligi. Pia walimaliza michezo yote wakiwa pointi 11 mbele ya mshindi wa pili Chelsea na kubeba taji kwa mara ya 13.
Tangu hapo Arsenal hawakupata mafanikio yoyote makubwa, na msimu wa 2022/2023 almanusura watwae taji la EPL, lakini walizidiwa kete na Manchester City.

AMSTERDAM, Uholanzi
Mshambulizi wa zamani wa Uholanzi Quincy Promes amehukumiwa kifungo cha miezi 18 jela kwa kumdunga kisu binamu yake kwenye goti.
Tukio hilo lilitokea kwenye karamu ya familia mnamo Julai 2020 na fowadi huyo wa Spartak Moscow alipatikana na hatia ya kuhukumiwa na mahakama ya Uholanzi.
Wakili wake alisema kuwa atakata rufaa, kulingana na mtangazaji wa Uholanzi RTL.
Promes, ambaye pia amewahi kuzichezea Sevilla na Ajax, anaishi Urusi na hakuhudhuria kikao cha mahakama.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 31 pia alishtakiwa na waendesha mashtaka wa Uholanzi mwezi uliopita, kwa madai ya kuhusika na ulanguzi wa dawa za kulevya.

Dar es Salaam

Na Mwandishi wetu

Imeelezwa kuwa timu za soka za Simba, Yanga na Azam FC zipo kwenye hekaheka za kuchomoleana wachezaji wenyewe kwa wenyewe ili kuzipa uimara timu zao kuelekea msimu ujao.
Tumaini Letu limebaini kwamba Azam FC baada ya kumchukua ‘kimafia’ Feisal Salum, wana mpango wa kumchukua beki wa Yanga Joyce Lomalisa pamoja na Djuma Shaban ambao hawaonyeshi nia ya kuendelea kubaki Jangwani.
Mbali na kutaka kuibomoa Yanga, Azam FC imeelezwa kutaka kufanya ‘vurugu’ kwa Simba kwa kuweka pesa ndefu kwa kiungo tegemeo Clatous Chama ili akaimarishe kikosi chao.
Chama amekuwa na msaada mkubwa kwa Simba, hasa kutokana na uwezo wake wa kutengeneza nafasi za kufunga katika mazingira magumu ya mchezo.
Yanga nao kwa kuonyesha kwamba si wanyonge, wanaendelea kumfukuzia kiungo James Akaminko ambaye miezi michache iliyopita, walithibitisha kupeleka barua ya maombi ya kufanya nae mazungumzo, ingawa mabosi wa Azam walikataa.
Kwa upande wao Simba SC, duru zinaeleza kwamba wanamfukuzia mchezaji wa Azam FC Sospeter Bajana ambaye msimu uliomalizika alionyesha uwezo mkubwa.
Sambamba na hilo, wekundu hao wanataka saini ya kiungo mkabaji wa Yanga, Mkongomani Yanick Bangala, ambaye naye taarifa za sasa zinadai hana nia ya kuendelea kubaki Jangwani.
Hata hivyo Afisa Habari wa Azam FC Hashim Ibwe na Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba Ahmed Ally, kwa nyakati tofauti wamenukuliwa wakisema kwamba hawana mpango wowote na wachezaji wanaohusishwa nao, huku wakiwataka mashabiki wao kusubiri mambo mazuri yajayo kuhusiana na usajili watakaofanya.
Ahmed Ally alisema kwamba wamechoka kuonewa na kufanywa wanyonge, hivyo msimu ujao watahakikisha wanarejesha heshima yao dimbani kwa kusajili wachezaji hatari wa kimataifa.
Kwa upande wake Afisa Habari wa Yanga Ali Kamwe alisema kwamba mipango ya kuwanasa wachezaji wakubwa wa Kimataifa inaendelea, na kwamba hata ikitokea hao wanaotajwa kuondoka wakafanikiwa kuondoka, bado kikosi chao hakitotetereka, kwa sababu Yanga ina viongozi makini na wenye weledi.

Jubilei hii ya Miaka 50 ya Wawata nchini, itafunguliwa na Misa Takatifu na kufuatiwa na Mashangilio ya Sherehe hii kubwa kwa WAWATA | Picha hizi zinatengenezwa na TUMAINI MEDIA. Matumizi yoyote ya picha hizi ni marufuku bila idhini kutoka TUMAINI MEDIA Hakimiliki © Tumaini Television - Haki zote zimehifadhiwa.Tafadhali Endelea Ku- Subscribe akaunti hii na bonyeza alama ya Kengele ili kupata taarifa zetu kwa wakati sahihi.

DAR ES SALAAM

Na John Kimweri

Askofu wa Jimbo Katoliki la Zanzibar Mhashamu Augustine Shao, amesema kuwa mafuta Matakatifu ya Krisma yanamsaidia mtu kuwa shuhuda na mfano mwema wa imani, ndani na nje ya Kanisa.
Askofu Shao aliyasema hayo hivi karibuni wakati akitoa homilia yake kwenye Adhimisho la Misa ya kutoa Sakramenti Takatifu ya Kipaimara, iliyofanyika Parokia ya Mtakatifu Paulo Mtume, Ubungo Msewe, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.
Alisema kwamba miongoni mwa alama za nje za Roho Mtakatifu ni mpako wa Krisma Takatifu, ambayo humsaidia mtu aliyeimarishwa kuwa kuhani na shuhuda mwaminifu wa imani ya Kristo.
“Miongoni mwa alama za nje za Roho Mtakatifu ni Krisma Takatifu. Haya mafuta ya Krisma yanakufanya wewe uwe shuhuda na mfano mwema wa Neno, na pia uwe Kuhani wa imani yake Kristo,”alisema Askofu Shao.
Alitaja alama nyingine kuwa ni kofi la upendo, ambalo si kwa ajili ya kumuumiza mtu anayeimarishwa, bali ni kumkomaza kiimani.
Aidha, Askofu Shao alisema kuwa Roho Mtakatifu pia anaweza kuwashukia waimarishwa kwa njia ya kuwekewa mikono.
Kwa mujibu wa Askofu Shao, Roho Mtakatifu anaweza kumshukia mtu yeyote na kumpa maelekezo ya kufanya jambo fulani, kwa manufaa ya watu wengine.
Askofu Shao aliwahimiza vijana walioimarishwa kuisimamia, kuitetea na kuishuhudia imani yao kwa matendo mema, huku akiwasihi wazazi na walezi kuwaombea watoto wao ili wazidi kuimarika.
“Mafundisho ya Kanisa ni kila wakati haya huwa ni endelevu, bado mna safari ya mafundisho zaidi, hasa ya kuilinda na kuitetea imani yenu. Hivyo basi, vijana mnaombwa kuwa mashuhuda wa Injili na matendo mema,”alisema Askofu Shao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Walei Parokia ya Mtakatifu Paulo Mtume, Ubungo Msewe, Bosco Bugali, alisema kuwa Parokia hiyo ilianzishwa mwaka 1973, na imetoa zaidi ya Parokia sita, ila kwa sasa ina Kigango kimoja.
Parokia hiyo ina waamini 2488, Jumuita 39, Kanda Tano na Vyama vya Kitume, vikiwemo Chama cha Vijana Wakatoliki Wafanyakazi (VIWAWA); Shirika la Kipapa la Utoto Mtakatifu;Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA); na Lejio Maria.

Na Arone Mpanduka

Chimbuko la bendi ya Maquis du Zaire kwa nchi ya Tanzania lilianzia mwaka 1973, wakati Franco Luambo Luanzo Makiadi akiwa na bendi yake ya T.P. OK. Jazz alikuja hapa nchini na akafanya onyesho kamambe katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam(sasa uwanja wa Uhuru).
Mwaka mmoja baadae wa 1972, bendi ya Maquis du Zaire, nayo ikaingia kwa mbwembwe na kuweka makazi yake ya kudumu katika jiji la Dar es Salaam.
Bendi hiyo Maquis du Zaire iliyotokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ikafia humu nchini miaka ya 1990.
Ilikuwa kivutio kikubwa kwa Watanzania na kuwapa hekaheka wanamuziki wa Tanzania katika miaka hiyo.
Kwa nchini Congo, bendi hiyo ilianza mwaka 1960, vijana wa wakati huo katika mji wa Kamina huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), waliungana na kuunda bendi yao, wakaiita Super Theo.
Bendi hiyo ilikuwa ikitoa burudani tosha kwa wapenzi wa muziki wa mji huo wa Kamina na vitongoji vinavyouzunguka mji huo. Baadae wakaibadilisha majina na bendi ikawa Super Gabby. Lakini uongozi wa Super Gabby ulitaka kuleta mageuzi katika muziki mwaka 1972, walipobadilisha majina rasmi na kuwa Maquis du Zaire.
Mwaka huo huo bendi hiyo iliingia hapa Tanzania wakipitia nchini Uganda.
Walipofika katika jiji la Dar es Salaam, walipata mkataba wa kupiga muziki katika ukumbi wa Mikumi Tours, uliokuwa maeneo la Tazara Buguruni, jijini Dar es Salaam.
Baada ya kumaliza mkataba wao, waliondoka wakaenda kupiga muziki katika Klabu ya Hunters kwa kipindi kifupi.
Kisha viongozi wa bendi hiyo wakafanya mazungumzo na mfanyabiashara Hugo Kisima, aliyekuwa akimiliki ukumbi wa Safari Resort, maeneo ya Kimara, jijini Dar es Salaam. Wakaanza kupiga muziki kwa mkataba na mfanyabiashara huyo.
Februari 1977 viongozi wa bendi hiyo ya Maquis du Zaire, waliamua kukiongezea nguvu kikosi chao. Hivyo walimtuma Tchibangu Katayi ‘Mzee Paul’ aliyekuwa mwanamuziki wa bendi ya Maquis du Zaire.
Pia alikuwa mmoja kati ya viongozi wa bendi hiyo.Mzee Paul aliwachukua baadhi ya wanamuziki ili kuja nao Tanzania kuongeza nguvu katika bendi ya Maquis du Zaire.
‘Mzee Paul’ alibahatika kuwachukua wanamuziki akina Kikumbi Mwanza Mpango, au ‘King Kiki’, mtunzi na mwimbaji, Kanku Kelly kwa upande wa tarumbeta., Ilunga Banza ‘Mchafu’, aliyekuwa akiungurumisha gitaa la besi, Mutombo Sozy aliyekuwa akizicharanga ‘drums’, na mnenguaji Ngalula Tshiandanda.
Wakati huo Maquis du Zaire walikuwa wakicheza muziki wakitumia mtindo wa ‘Chakula Kapombe’, ambao kwa Watanzania ulikuwa mpya, na ukapendwa mno na mashabiki.
Kufika kwa wanamuziki hao, kulileta changamoto kubwa katika muziki. Tungo nzuri za Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kiki’, zilikuwa chachu masikioni mwa wapenzi wa muziki wa dansi. Kiki pia yaelezwa kuwa ndiye aliyeleta Mapinduzi makubwa ya muziki hapa nchini Tanzania.
Maquis du Zaire wakaazisha mtindo mwingine wa ‘Kamanyola’, uliowapagaisha wapenzi na wadau toka pembe zote za jiji la Dar es Salaam.
Mwishoni mwa 1977, Marquis du Zaire walimaliza mkataba kwa Hugo Kisima, wakaondoka.Bahati nyingine ikawadondokea tena baada ya kuingia mkataba mwingine wa kupiga muziki kwa mzee Makao, aliyekuwa akimiliki ukumbi wa Savannah, maeneo ya Ubungo.Wakiwa Savannah, walianzisha mitindo ya ‘Sanifu’, na ‘Ogelea piga mbizi’.
Lakini ukumbi huo ukabadilishwa jina ukaitwa White House. Ikumbukwe kwamba Maquis pia ilikuwa ikipiga kwenye ukumbi wa Mpakani, maeneo ya Mwenge.Mwishoni mwa mwaka 1978, Maquis du Zaire  waliamua kuimarisha tena kikosi chao kwa kuwaleta wanamuziki wengine wapya kutoka DRC.Iliwaleta akina Kabeya Badu, Kalala Mbwebwe, Ngoyi Mubenga na Khatibu Iteyi Iteyi.
Bendi hiyo ilikuwa ikiongozwa na wanahisa akina Chinyama Chiyaza ‘Chichi’, Chibangu Katayi ‘Mzee Paul’, Chimbwiza Mbangu Nguza au ‘Nguza Vicking’, Mutombo Lufungula ‘Audax’ na Mbuya Makonga ‘Adios’.
Chini ya uongozi huo, katika miaka ya 1980 mafanikio makubwa yalionekana, mojawapo ni lile la kuanzisha Kampuni iliyofahamika kama Orchestra Maquis Company (OMACO).
Kampuni hiyo iliweza kumiliki shamba la matunda, wakalima kwa kutumia trekta zao maeneo ya Mbezi nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam. Mazao yao walikuwa wakiyapeleka na kuuza katika Soko Kuu la Kariakoo jijini Dar es Salaam.OMACO pia ilimiliki mradi mwingine wa viwanja tisa na nyumba kadhaa, maeneo ya Sinza, jijini Dar es Salaam.
Kwa wakati huo, watu wengi hawakuwa na haja ya kuchukua teksi kurudi nyumbani, kwani muziki wa Maquis du Zaire ulikuwa unarindima hadi alfajiri. Muda ambao mabasi ya UDA ya Ikarus yalikuwa yameanza kazi. Wakati huo hazikuwepo ‘Dala dala’, Bajaji wala Pikipiki kwa maana ya Bodaboda.
Hata hivyo, baadae bendi hiyo ilianza kufa taratibu kufuatia baadhi ya wanamuziki kuondoka kwenda kutafuta maisha sehemu nyingine, na wengine kusahindwa kufanya kazi hiyo kutokana na umri kuwa mkubwa, na magonjwa ya hapa na pale.
Mwanzoni mwa miaka ya 1990, bendi ilipotea kabisa na kuacha historia ya kipekee.
Baadhi ya nyimbo za Marquis du Zaire zilizovuma kwa uzuri na utamu wake ni ‘Ni Wewe Pekee; Makumbele; Kalubandika; na Promotion’.
This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.

KIBAHA

Na Mathayo Kijazi

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi amewataka Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA), na waamini wote kutambua kwamba wanapomsifu Mtakatifu Agustino, wanapaswa pia kumshukuru Mama yake mzazi Mtakatifu Monica.
Askofu Ruwa’ichi aliyasema hayo wakati akitoa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Kilele cha Jubilei ya Miaka 50 ya Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) Kijimbo, katika Kumbukumbu ya Mtakatifu Monica, iliyofanyika katika Seminari Ndogo ya Mtakatifu Maria, Visiga, jimboni humo.
“Tunaadhimisha mambo kadhaa, kwanza kabisa tunawamkumbuka WAWATA, na hususan Mtakatifu Monica, mama yake Mtakatifu Agustino. Huyu ni mama wa mfano, mama aliyetukuka, mama wa kuigwa. Mama huyu alizaliwa mwaka 331 katika Bara la Afrika, huko Afrika ya Kaskazini,” alisema Askofu Mkuu, na kuongeza,
“Alizaliwa na kulelewa vizuri katika familia ya Kikristo, akajenga na kustawisha fadhila zilizo njema; fadhila ya Imani; fadhila ya mapendo; fadhila ya huruma na fadhila za kimama. Tumtukuze Mungu kwa zawadi ya Mama huyu kutoka Bara la Afrika,” alisema Askofu Mkuu Ruwa’ichi.
Askofu Ruwa’ichi aliwapongeza WAWATA kwa kuendelea kusimama imara na kwa kujitolea kwao katika shughuli mbalimbali za Kanisa, huku akiwasihi kufahamu kwamba wao ni zawadi ya Mungu kwa Kanisa na Ulimwengu.
Askofu Mkuu Ruwa’ichi alimshukuru Mungu kwa utume unaofanywa na akinamama hao, hasa kuwalea Vijana wa Seminari ya Visiga, akimwomba Mungu awazidishie neema na baraka zake, ili utume wao uendelee kustawi, na kuutukuza ukuu wa Mungu.
Askofu Ruwa’ichi aliwasihi WAWATA kutafakari kwamba wao ni baraka kutoka kwa Mungu, kwa uwepo wao wa Miaka 50 sasa, kwani Utume wa Wanaume Wakatoliki (UWAKA), hata miaka 30 bado hawajafikisha, huku akiwasihi akinamama hao kumshukuru Mungu kwa mema yote anayowajalia.
Aidha, aliwaasa WAWATA kuendelea kubaki kuwa Wakristo Wakatoliki wazuri, hata katika Kanisa la nyumbani, kwa kusimama imara na kuwa mama bora, hata katika familia zao.
Kwa upande wao, Maaskofu Wasaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu na Mhashamu Stephano Musomba, waliwapongeza WAWATA kwa kuadhimisha Jubilei yao ya Miaka 50, na kwa kazi nzuri ya utume wanaoendelea nao kuufanya jimboni humo.
Naye, Mwenyekiti wa Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA), Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Stella Rwegasira aliwashukuru waamini wote walioshiriki Adhimisho hilo.
Aidha, Catherine Mwingira, Katibu wa WAWATA Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam alisema kuwa wanamshukuru Mungu kwa kufikisha Miaka 50 tangu chama hicho cha Kitume kuanzishwe na waasisi wao, huku akisema kuwa yamefanyika mengi mazuri tangu kuanzishwa kwa chama hicho hadi sasa.
Chama cha Kitume cha Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA), kilianzishwa rasmi mwaka 1972.

MOROGORO

Na Angela Kibwana

Mhashamu Askofu Lazarus Msimbe -SDS, wa Jimbo Katoliki la Morogoro, ametoa wito kwa Mapadri kutohubiri Injili ya mafanikio, kwa sababu kuna desturi ambayo inataka kuzuka hata ndani ya Kanisa Katoliki, kwa sababu baadhi ya waamini kutaka miujiza na mafanikio, hali inayosababisha baadhi yao kuhamia Makanisa mengine.
Askofu Msimbe alisema hayo katika mahubiri wakati wa kutoa Daraja la Upadre kwa Mashemasi wanne wa Shirika la Wasalvatorian, iliyofanyika Chuo Kikuu Kishiriki cha Jordan, Jimboni Morogoro.
Aidha, Askofu Msimbe alisema kuwa Mapadri wanapaswa kuhubiri Injili ya Yesu, ambayo si Injili ya kutaka mafanikio. Hivyo, ni kazi ya Mapadri kuwaeleza waamini ukweli, kwamba hakuna mafanikio yanayoweza kujitokeza bila kuvuja jasho, au kufanya kazi kwa bidii.
 Alisema kuwa kutokana na desturi iliyozuka kwa waamini wengi kutekwa na injili ya miujiza na mafanikio, Askofu Msimbe ametumia nafasi hiyo kuwatahadharisha Mapadre kutojihusisha na mitego ya kudanganya watu kukanyaga waamini wao, kukanyaga mafuta ya upako, kwa kigezo cha kujipatia utajiri.
Alibainisha kuwa Mapadri wanatakiwa kuwahubiria watu ukweli kwamba kuna mateso katika safari ya kutafuta mafanikio, waamini wanahitaji kufundishwa mbinu bora za kuwa na mipangilio mizuri, kwa sababu hakuna mtu anayeweza kupata mafanikio kwa njia rahisi.
Hata hivyo aliwaonya Mapadri, kutozigeuza Baraka zao kuwa biashara kwa sababu wamepewa bure ili kuwahudumia watu. Wasiuze baraka zao, jambo la msingi kwao ni kuhakikisha wanahubiri injili ya Yesu ambayo haitaki ulaini katika maisha.
Mapadri wanapaswa kutambua kuwa wao ni mbegu ambayo inapaswa kumea vizuri kwa kufanya mambo yampendezayo Mungu, kwani ni kielelezo katika kuyaenzi matakatifu, kwa kuwa kazi moja na muhimu ya mapadri ni kuhubiri Neno la Mungu, na wala siyo kujisifia wenyewe.
Alisema kuwa maadhimisho ya Sakramenti mbalimbali za Kanisa ndiyo dira inayoweza kumtambulisha Padre. Mapadre waepuke tabia ya kujisifia wenyewe, hivyo watu watatambua uzuri wa Padre kulingana na huduma makini kwa watu wake, hasa uadhimishaji wa Misa Takatifu.
Katika kuadhimisha Masakramenti, hasa Sakramenti ya Kitubio, Mapadri wanapaswa kuwa makini kuwatia moyo waamini wanapofanya kitubio ili kuwapatanisha na Mungu, na wala waamini wasikatishwe tamaa.
Sambamba na hayo, amewaomba mapadre hao wapya kushiriki maisha ya Jumuiya na kuziishi karama za Shirika la Wasalvatoariani, waishi kadri ya nadhiri zao kwa kuzingatia mambo ya msingi yanayowatambulisha kuwa WATAWA.
Wanapaswa kuzingatia maisha ya sala ambayo yatawasaidia kutimiza mapenzi ya Mungu na kufanya utume watakaopangiwa na wakubwa wao wa shirika, ili watekeleze kwa uaminifu na kwa uangalifu.
Aliwaomba waamini na watu wenye mapenzi mema kuwaombea Mapadri wapya na wengine waliotangulia katika utumishi huo kuwa wafuasi wema wa Kristo, ili kuwavuta vijana wengi wanaotamani kujiunga na wito huo Mtakatifu.
Mapadre wapya ni Padri Edward Lupaka, Padri Deogatius Silayo, Padri Erasmus Kayongo, na Padri Musa Ndelule.