Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

Na Arone Mpanduka

Chimbuko la bendi ya Maquis du Zaire kwa nchi ya Tanzania lilianzia mwaka 1973, wakati Franco Luambo Luanzo Makiadi akiwa na bendi yake ya T.P. OK. Jazz alikuja hapa nchini na akafanya onyesho kamambe katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam(sasa uwanja wa Uhuru).
Mwaka mmoja baadae wa 1972, bendi ya Maquis du Zaire, nayo ikaingia kwa mbwembwe na kuweka makazi yake ya kudumu katika jiji la Dar es Salaam.
Bendi hiyo Maquis du Zaire iliyotokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ikafia humu nchini miaka ya 1990.
Ilikuwa kivutio kikubwa kwa Watanzania na kuwapa hekaheka wanamuziki wa Tanzania katika miaka hiyo.
Kwa nchini Congo, bendi hiyo ilianza mwaka 1960, vijana wa wakati huo katika mji wa Kamina huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), waliungana na kuunda bendi yao, wakaiita Super Theo.
Bendi hiyo ilikuwa ikitoa burudani tosha kwa wapenzi wa muziki wa mji huo wa Kamina na vitongoji vinavyouzunguka mji huo. Baadae wakaibadilisha majina na bendi ikawa Super Gabby. Lakini uongozi wa Super Gabby ulitaka kuleta mageuzi katika muziki mwaka 1972, walipobadilisha majina rasmi na kuwa Maquis du Zaire.
Mwaka huo huo bendi hiyo iliingia hapa Tanzania wakipitia nchini Uganda.
Walipofika katika jiji la Dar es Salaam, walipata mkataba wa kupiga muziki katika ukumbi wa Mikumi Tours, uliokuwa maeneo la Tazara Buguruni, jijini Dar es Salaam.
Baada ya kumaliza mkataba wao, waliondoka wakaenda kupiga muziki katika Klabu ya Hunters kwa kipindi kifupi.
Kisha viongozi wa bendi hiyo wakafanya mazungumzo na mfanyabiashara Hugo Kisima, aliyekuwa akimiliki ukumbi wa Safari Resort, maeneo ya Kimara, jijini Dar es Salaam. Wakaanza kupiga muziki kwa mkataba na mfanyabiashara huyo.
Februari 1977 viongozi wa bendi hiyo ya Maquis du Zaire, waliamua kukiongezea nguvu kikosi chao. Hivyo walimtuma Tchibangu Katayi ‘Mzee Paul’ aliyekuwa mwanamuziki wa bendi ya Maquis du Zaire.
Pia alikuwa mmoja kati ya viongozi wa bendi hiyo.Mzee Paul aliwachukua baadhi ya wanamuziki ili kuja nao Tanzania kuongeza nguvu katika bendi ya Maquis du Zaire.
‘Mzee Paul’ alibahatika kuwachukua wanamuziki akina Kikumbi Mwanza Mpango, au ‘King Kiki’, mtunzi na mwimbaji, Kanku Kelly kwa upande wa tarumbeta., Ilunga Banza ‘Mchafu’, aliyekuwa akiungurumisha gitaa la besi, Mutombo Sozy aliyekuwa akizicharanga ‘drums’, na mnenguaji Ngalula Tshiandanda.
Wakati huo Maquis du Zaire walikuwa wakicheza muziki wakitumia mtindo wa ‘Chakula Kapombe’, ambao kwa Watanzania ulikuwa mpya, na ukapendwa mno na mashabiki.
Kufika kwa wanamuziki hao, kulileta changamoto kubwa katika muziki. Tungo nzuri za Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kiki’, zilikuwa chachu masikioni mwa wapenzi wa muziki wa dansi. Kiki pia yaelezwa kuwa ndiye aliyeleta Mapinduzi makubwa ya muziki hapa nchini Tanzania.
Maquis du Zaire wakaazisha mtindo mwingine wa ‘Kamanyola’, uliowapagaisha wapenzi na wadau toka pembe zote za jiji la Dar es Salaam.
Mwishoni mwa 1977, Marquis du Zaire walimaliza mkataba kwa Hugo Kisima, wakaondoka.Bahati nyingine ikawadondokea tena baada ya kuingia mkataba mwingine wa kupiga muziki kwa mzee Makao, aliyekuwa akimiliki ukumbi wa Savannah, maeneo ya Ubungo.Wakiwa Savannah, walianzisha mitindo ya ‘Sanifu’, na ‘Ogelea piga mbizi’.
Lakini ukumbi huo ukabadilishwa jina ukaitwa White House. Ikumbukwe kwamba Maquis pia ilikuwa ikipiga kwenye ukumbi wa Mpakani, maeneo ya Mwenge.Mwishoni mwa mwaka 1978, Maquis du Zaire  waliamua kuimarisha tena kikosi chao kwa kuwaleta wanamuziki wengine wapya kutoka DRC.Iliwaleta akina Kabeya Badu, Kalala Mbwebwe, Ngoyi Mubenga na Khatibu Iteyi Iteyi.
Bendi hiyo ilikuwa ikiongozwa na wanahisa akina Chinyama Chiyaza ‘Chichi’, Chibangu Katayi ‘Mzee Paul’, Chimbwiza Mbangu Nguza au ‘Nguza Vicking’, Mutombo Lufungula ‘Audax’ na Mbuya Makonga ‘Adios’.
Chini ya uongozi huo, katika miaka ya 1980 mafanikio makubwa yalionekana, mojawapo ni lile la kuanzisha Kampuni iliyofahamika kama Orchestra Maquis Company (OMACO).
Kampuni hiyo iliweza kumiliki shamba la matunda, wakalima kwa kutumia trekta zao maeneo ya Mbezi nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam. Mazao yao walikuwa wakiyapeleka na kuuza katika Soko Kuu la Kariakoo jijini Dar es Salaam.OMACO pia ilimiliki mradi mwingine wa viwanja tisa na nyumba kadhaa, maeneo ya Sinza, jijini Dar es Salaam.
Kwa wakati huo, watu wengi hawakuwa na haja ya kuchukua teksi kurudi nyumbani, kwani muziki wa Maquis du Zaire ulikuwa unarindima hadi alfajiri. Muda ambao mabasi ya UDA ya Ikarus yalikuwa yameanza kazi. Wakati huo hazikuwepo ‘Dala dala’, Bajaji wala Pikipiki kwa maana ya Bodaboda.
Hata hivyo, baadae bendi hiyo ilianza kufa taratibu kufuatia baadhi ya wanamuziki kuondoka kwenda kutafuta maisha sehemu nyingine, na wengine kusahindwa kufanya kazi hiyo kutokana na umri kuwa mkubwa, na magonjwa ya hapa na pale.
Mwanzoni mwa miaka ya 1990, bendi ilipotea kabisa na kuacha historia ya kipekee.
Baadhi ya nyimbo za Marquis du Zaire zilizovuma kwa uzuri na utamu wake ni ‘Ni Wewe Pekee; Makumbele; Kalubandika; na Promotion’.
This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.

Na Arone Mpanduka

Hivi karibuni tumeshuhudia Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) likimtimua kocha wa timu ya taifa (Taifa Stars), Kim Poulsen, baada ya kutoridhishwa na mwenendo wake ikiwemo Taifa Stars kupoteza kwenye mchezo wa nyumbani wa kuwania tiketi ya kufuzu fainali za Afrika kwa wachezaji wa ndani.
Wapo watu walioshangaa, na wapo walioona kuwa maamuzi yaliyofanywa ni sahihi kwa sababu kocha haajiriwi ili afukuzwe hasa kama ikitokea kushindwa jukumu alilopewa.
Kwa miaka mingi sasa tumekuwa tukiajiri makocha kwa timu ya taifa na kisha kuwatimua, huku tukiwashushia lawama nzito kwamba wao ndiyo sababu kuu ya timu zetu kushindwa. Mwaka 2006 Rais Jakaya Kikwete kwa wakati ule, alituonyesha njia kwa kumleta kocha wa kigeni Marcio Maximo kutoka nchini Brazil, na hapo ndipo tukawa tunaamini moja kwa moja kwamba suluhisho kuu la timu zetu za taifa kufanya vizuri ni kuajiri makocha wa kigeni.
Ninadhani kuna mahali tunakwama, na pengine hatufahamu suluhisho lake, na hata kama tunalifahamu, tunaamua kujifanya hatufahamu. Unapofanya jambo ambalo hujui, unakwenda wapi na ukaendelee kulilazimisha, itakuwa sawa na kufukuza kuku gizani, ukidhani utamkamata.
Ukweli ni kwamba mafanikio ya timu zetu za taifa yamekuwa yanapatikana kwa kubahatisha, na si katika mifumo sahihi. Bado tunaogopa kuanza na sifuri ili twende mbele, na badala yake tunataka kulazimisha, tukiamini kwamba tutafika tunapopataka.
Kuna vitu havipo sawa, na inabidi turekebishe ili soka letu lifike tunapopataka.Na vitu hivyo vinaanzia katika ngazi ya familia, Serikali na vyombo vinavyohusika na mchezo wa soka.
Tatizo kubwa tulilonalo ni kutokuwa na mfumo bora wa kufikia mafanikio ya mpira wa miguu, vinginevyo tutaishia kuilaumu TFF na makocha wanaokuja kufundisha timu zetu.
Tukianzia ngazi ya familia, wachezaji wote waliopo wana wazazi au walezi wao. Je, nini mchango wao katika malezi ya kimwili na kisaikolojia kwa watoto wao? Kwa sababu leo hii tunaweza kuwa na wachezaji wazuri wazawa lakini hawana nidhamu.
Kitu ambacho ni muhimu kwa maisha ya mchezaji kinachoweza kumpeleka nje ya nchi kucheza soka la kulipwa, na hatimaye kuongeza ubora kwenye timu za taifa, ni ufundi au umahiri wa kucheza soka.
Jambo lingine katika familia ni suala la lishe bora. Je, umewahi kujiuliza ni kwa nini wachezaji wa kizazi hiki wana maumbo madogo madogo, ikilinganisha na wale wa miaka 30 iliyopita? Wazazi katika hilo wanahusikaje?
Ukija katika ngazi ya klabu, je, vilabu vyetu vinaendeshwa kwa weledi, kwa maana ya kuandaa timu zetu za wakubwa? Kuna uwekezaji wa kiwango gani katika miundo mbinu ya soka?
Kwa sababu ukichunguza kwa makini utabaini, kwamba klabu chache za Ligi Kuu zina mifumo mizuri ya kutengeneza vijana, lakini zingine hazina, na hata yakitokea mashindano ya vijana, wanachofanya ni kuokota vijana wa mitaani ili kuiridhisha TFF.
Tukija kwa Serikali, je, kuna viwanja vingapi vya wazi ambavyo vilikuwa vinatumika kwa michezo zamani, lakini sasa hivi vimegeuzwa kuwa ofisi za watu binafsi, gereji, shule ama baa? Na katika hilo hilo la viwanja, ni shule ngapi za umma za Msingi na Sekondari zina viwanja vye michezo? Watoto watacheza wapi? Vipaji tutaviibua wapi? Na hapo ndipo msingi wa soka wa nchi yoyote unapoanzia.
Je, kuna waalimu wangapi wa michezo waliofuzu kwenye eneo hilo katika shule zetu za umma za msingi na sekondari, na je, kuna shule ngapi zenye vipindi na ratiba za michezo kama ilivyokuwa zaidi ya miaka 40 iliyopita?
Majibu ya jumla ni kwamba kwa sasa hakuna maeneo mengi ya wazi, na hata shule nyingi za umma ninazoziona mitaani hazina viwanja vya kuchezea. Mfano mzuri ni Shule ya Msingi Tabata Liwiti, ambayo ipo jirani kabisa na ofisi za Tumaini Media ambayo uwanja wake wa soka linajengwa jengo la Shule ya Sekondari. Pongezi kwa kuweka jengo hilo, lakini watoto watachezea wapi?
Hapo Wizara husika na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) wanapaswa kutengeneza na kusimamia mfumo ulio bora ambao ndio utakuwa muongozo wa nchi. Nilisikia sera ya michezo inakamilishwa, lakini bado sifahamu ilipofikia.
Itaendelea wiki ijayo.

Baba Mtakatifu Fransisko (kushoto) akisalimiana na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI wakati Papa alipomtembelea Mstaafu huyo katika makazi yake, akiambatana na Makardinali wapya.

Vatican City

Makardinali Wapya wamemtembelea na kumsalimia Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, katika makazi yake.

Makardinali hao 20 walifanya ziara hiyo ya Kitume, baada ya Ibada ya kutangazwa na kusimikwa, ambapo walikwenda kumsalimia na kumtakia heri Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI.

Mababa Watakatifu hao wawili kwa pamoja baada ya kusalimiana na kuteta na Makardinali hao wapya, waliwabariki ili wakawashe moto wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.

Baba Mtakatifu Fransisko aliwatangaza na kuwasimika Makardinali wapya na kuwapigia kura Wenyeheri wapya wanaotarajiwa kuingizwa kwenye orodha ya Watakatifu wa Kanisa.

Wenyeheri hao ni Mwenyeheri Padri Giovanni Battista Scalabrini aliyetangazwa na Mtakatifu Yohane Paulo II, kuwa Mwenyeheri, Novemba 9, mwaka 1997.
Padre Giovanni Battista alizaliwa Julai 8, mwaka 1839 na kufariki dunia Juni Mosi mwaka 1905.

Alikuwa ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Piacenza-Bobbio, Italia na Mwanzilishi wa Mashirika ya Wamisionari wa Mtakatifu Carlo Borromeo, maarufu kama Wascalabrini, na pia ni Muasisi wa Taasisi ya Waamini Walei Wascalabrini, iliyoanzishwa kunako mwaka 1961.

Wa pili ni Mwenyeheri Artemide Zatti, Bruda wa Shirika la Wasalesian wa Don Bosco, aliyezaliwa tarehe 12 Oktoba 1880, nchini Italia.
Akafariki dunia Machi 15, mwaka 1951 huko Viedma nchini Argentina.

Utakatifu wake unapata chimbuko lake katika huduma kwa maskini kwa kuongoza hospitali na duka la dawa kwa ajili ya maskini, kwa muda wa miaka 40.
Aprili 14 mwaka 2002, alitangzwa na Baba Mtakatifu Yohane Paulo II, sasa ni Mtakatifu, kuwa ni Mwenyeheri.

Ujenzi wa Kituo cha Afya cha kisasa katika Kata ya Lukobe, Mkoani Morogoro ukiendelea.

MOROGORO

Na Angela Kibwana

Serikari ya Tanzania imetoa Shilingi milioni 500/- zilizotokana na tozo za miamala ya simu, kukamilisha mradi mkubwa wa ujenzi wa Kituo cha Afya cha kisasa katika Kata ya Lukobe, Mkoani Morogoro.
Kukamliki kwa mradi huo kutawanufaisha zaidi ya wananchi 35,000 watakaopata shida za kiafya kutoka Kata ya Lukobe na Kata jirani, Mkoani humo.
Akizungumza wakati wa kukagua mradi huo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Ally Machela alisema kuwa tayari Serikali imetoa shilingi milioni 500/= zilizopokelewa na Manispaa ya Morogoro kukamilisha ujenzi wa kituo hicho.
“Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro inatekeleza mradi mkubwa wa ujenzi wa Kituo cha Afya katika Kata ya Lukobe kitakachohudumia wananchi 35,000 baada ya kukamilika kwake,”alisema Machela.
Alifafanua kuwa fedha zilizotolewa katika awamu ya kwanza ambazo ni kiasi cha Shilingi milioni 250/=, zilitumika kujenga maabara,jengo la wagonjwa wa nje, na kibanda cha kuchomea taka.
Aidha, alifahamisha kuwa katika awamu ya pili, Serikali ilitoa Shilingi milioni 250/- kwa ajili ya majengo mawili ambayo ni jengo la wazazi, jengo la kufulia nguo, na jengo la upasuaji.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Manispaa ya Morogoro Dk. Charles Mkombachepa, alisema kuwa kituo hicho cha afya kitaongeza tija kwa wananchi kwa sababu kina uwezo wa kuhudumia watu 35,000 kutoka Kata ya Lukobe, Mkundi, Kihonda na Kata nyingine jirani.
Aliongeza kuwa kituo hicho kina majengo mbalimbali ya kutolea huduma kwa wagonjwa, kati yao kuna jengo la wanawake; jengo la wagonjwa wa nje; jengo la wazazi; jengo maalum kwa ajili ya upasuaji wajawazito; na huduma nyingine za afya ya mwanamke.
Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini, Abdulaziz Abood, baada ya kuridhishwa na ujenzi wa kituo hicho, aliahidi kutoa magari mawili yenye thamani ya Shilingi milioni 172/- kubebea wagonjwa  katika Kituo cha Afya Lukobe, na Kituo cha Afya Tungi kinachojengwa  kwa mapato ya ndani ya Manispaa.
Nao baadhi ya wakazi wa Kata ya Lukobe walisema kuwa wanamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kutenga fedha ili kukamilisha ujenzi huo.
Naye Mwandishi Victor Wambura anaripoti kuwa, wasomi nchini wameiomba Serikali kutimiza ahadi yake kwa wananchi kwa kuzielekeza tozo ili kuboresha miradi ya maendeleo ya jamii, hivyo kuondoa malalamiko ya wananchi kuhusu tozo hizo.
Akizungumza na gazeti la Tumaini Letu, Mchumi na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar salaam (UDSM) Dk. Martin Chegere, alisema kuwa hakuna tozo yoyote itakayomfurahisha mtu, na hakuna mtu anaependa kitu kinachomchukulia pesa yake, ikiwa hakipo kwenye matumizi yake.
“Tumeahidiwa kwamba vikichukuliwa basi vitarudi kwa mfumo utakaotusaidia kuweka mazingira mazuri ya afya, elimu na miundombinu, hizo ndizo ahadi tulizoahidiwa na viongozi wetu,” alisema Dk. Chegere.         
Alisema pia kuwa Serikali inatakiwa kuwatendea watu haki, kulingana na ahadi ya kuboresha miundombinu ya kijamii, kwa sababu wananchi wanaumia wakiona vitu hivyo havitendeki, hasa kwa kutumia kodi hiyo ya tozo.
Aidha, Dk. Chegere alisema kwamba usahihi wa tozo utakuwepo pale ambapo Serikali itarejesha kwa wananchi kwa namna bora zaidi ya kuwapatia huduma.
Aliwasihi wananchi kuiunga mkono Serikali, kwani hata kwenye Bibilia Takatifu, Yesu aliwaambia wanafunzi wake kuwa ya Kaisari mpe Kaisari na ya Mungu mpe Mungu, ikiwa na maana ya kwamba serikali nayo inahitaji mapato.
Naye Mchumi na Muhadhiri wa Chuo Kikuu Cha Dar esalaam Dk. Innocent Pantaleo, alisema kuwa Wananchi wanatakiwa kuiunga mkono Serikali kwa kukusanya mapato, na kudai kwamba kwa sasa wahisani hawaleti pesa za kutosha kama ilivyokuwa awali.
Aidha, Dk. Pantaleo aliiomba Serikali kuzingatia usawa kwa kumwangalia mwananchi mwenye kipato cha chini, ili kuondoa matabaka.
Hata hivyo, alisema Serikali izingatie kuboresha maeneo ambayo yanamgusa huyo mwananchi anaetozwa kodi kwa kuboresha miundombinu ya kijamii, kama vile ya afya, elimu na miundombinu, kwani hicho ndicho kilio cha wengi.

ARUSHA

Na Mwandishi wetu

Mkurugenzi wa Idara ya Ulinzi na Usalama wa Mtoto, Jimbo Kuu Katoliki la Arusha, Padri Dennis Ombeni amewataka Raia wa Jumuiya ya Afrika Mashariki popote walipo, kuwa mstari wa mbele kulinda uhai wa mtoto angali bado tumboni.
Mambo yanayojumuisha katika kumlinda na kumtetea mtoto, yakiwemo ya ukuaji, kumlinda katika nyanja zote kiuchumi, kiafya na kiakili, na ustawi wa Mtoto.
Padri Ombeni aliyasema hayo katika warsha kwa Vijana na wazazi iliyofanyika jijini Arusha iliyolenga kuwajengea uelewa kuhusu athari zilizopo kwenye muswada wa ujinsi na afya ya kizazi wa Jumuiya ya Afika Mashariki wa mwaka 2021.
Kupitia mkutano huo, Padri Ombeni alieleza kusikitishwa juu ya mauaji katika jamii kati ya wanandoa yanayotokea kwa kisingizio cha wivu wa mapenzi jambo alilosema ni ouvu na linapaswa kukemewa kwa nguvu zote kwani linaingilia Uhai ambao asili yake ni Mungu.
“Maandiko Matakatifu kupitia Bibilia yanaeleza kwa namna kuu mbili, juu ya thamani ya uhai katika Bibilia, Maandiko Matakatifu yanatetea uhai, hasa pale kwenye Agano la Kale, ambapo baada ya Mungu kumuumba Adamu na kumpatia msaidizi wake Eva, aliwabariki na kusema, enendeni mkazae na kuijaza dunia,”alisema Padri Ombeni.                          
Alisema pia kuwa uhai wa mwanadamu ni kitu kitakatifu, hivyo unapaswa kulindwa na kutunzwa tangu kutungwa mimba hadi kifo chake cha kawaida. Hivyo muswada huo wa Ujinsi na Afya ya kizazi haupaswi katika Mataifa ya Jumuiya Afrika Mashariki kwani unakwenda kinyume na Utu, Dini na tamaduni za watu hao.
Kwa mujibu wa Padri Ombeni Mswaada huo unatishia uwepo wa Dini na Imani za Watu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, pia unadhalilisha Mila na Desturi za watu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, kwani hautoi nafasi kwa wahudumu wa afya kutumia dhamiri zao katika kutoe elimu ya afya ya uzazi kwa wanaowahudumia.
Kutokana na hayo na mengine maovu yaliyoko katika Mswaada huo ambao umeakisiwa na kupigiwa debe na baadhi ya vikundi vyenye nia ovu na watu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Padri Ombeni amewataka watanzania wote kuungana na wananchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kuupinga Muswaada huo.
Mmoja wa Washiriki wa Mkutano huo, aliyejitambulisha kwa jina la Anna Anatoli alisema ulimwengu umekosa hofu ya Mungu  na ndiyo maana imefika hatua wanadamu wanaweka mikakati ya kutowesha Uhai bila kuwa na hofu ya kwamba kazi hiyo ni ya kwake Mungu Muumba ambaye yeye ni asili ya Uhai wenyewe.
“Hatuna sababu ya kushabikia mambo kutoka mataifa ya mbali ambayo kwao wamefika mahali wameona Uhai si zawadi kutoka kwa Mungu kwenda kwa mwanadamu, natamani kuona tunabaki na vyakwetu huku tukiendelea kuwajengea hofu ya Kimungu watoto wetu,”alisema Anna.
Kwa upande wake Betty Sammaye aliwataka wazazi kusimama na kuwapeleka watoto wao Kanisani kwani Mtoto akikuwa kwenye uwepo wa kumcha Mungu ataweza kusimama na kujitetea na Neema ya Mungu itakuwa ndani katika kumwongoza.
Betty amewataka wazazi kuchukua muda kuzungumza na watoto wao, kwani vitu vinabadilika mno kila siku, na kamwe wasikubali watoto wao kutoka nje ya himaya yao bila kufahamu kwa kina ni wapi hasa wanakwenda na wanakwenda kufanya nini.
Muswada huo wa Afya ya Kizazi na Ujinsi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wa Mwaka 2021 unaelezwa kukiuka maadili, Utu na Dini za watu wa Jumuiya ambao una vipengele vinavyochochoa ngono kwa watoto na Vijana, na pia utoaji mimba.
Na ikiwa muswada huo utaachwa upite, basi itazilazimu nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutunga Sheria kulingana na matakwa ya muswada huo.

Page 1 of 2