Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

Paroko Msaidizi wa Parokia ya Parokia ya Mtakatifu Yosefu Allamano, Kibada, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Steven Nyilawila, akimpongeza Padri Ambrose Mosha OFMCap, kwa kutimiza Jubilei ya Miaka 50 ya Upadri, wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Jubilei ya Miaka 25 na 50 ya Upadri, iliyoadhimishwa katika Parokia ya Bikira Maria wa Fatima – Msimbazi, jimboni humo.

VATICAN CITY, Vatican

Baba Mtakatifu Fransisko ametaka kuwepo kwa hatua za kusitisha  mapigano mara moja huko Lebanon, Gaza, Palestina, Israel na maeneo mengine kama Ukraine, Sudan na Myanmar.
Katika Siku ya Wahamiaji na Wakimbizi, Papa alisema kwamba hali ya uhamaji ni fursa ya kukua kwa udugu, akitoa tangazo la ufunguzi wa mchakato wa kumtangaza Mfalme Baudouin kuwa mwenyeheri.
Baada ya Misa hiyo Takatifu iliyoongozwa na Papa Fransisko katika Uwanja wa Mfalme Baudouin huko Bruxelles, alitoa shukrani kwa Maaskofu nchini Ubelgiji kwa maneno mazuri, akisema “Ninatoa shukrani za dhati kwa Wakuu, Mfalme na Malkia, na vile vile Wakuu wa Kifalme, Mtawala Mkuu na Malkia wa Luxembourg, kwa uwepo wao na ukarimu wao katika siku hizi.
Vile vile, ninatoa shukrani zangu kwa wote ambao, kwa njia nyingi, mmefanya kazi pamoja kuandaa Ziara hii. Kwa namna ya pekee, ninawashukuru wazee na wagonjwa ambao wamesali sala zao.”
“Leo tunaadhimisha Siku ya Wahamiaji na Wakimbizi Duniani yenye mada “Mungu anatembea na watu wake”. Kutoka nchi hii ya Ubelgiji, ambayo imekuwa, na bado ni kivutio cha wahamiaji wengi, ninarudia wito wangu kwa Ulaya na Jumuiya ya Kimataifa kuzingatia hali ya uhamiaji kama fursa ya kukua pamoja katika udugu, na ninakaribisha kila mtu kuona katika kila jambo kaka na dada mhamiaji uso wa Yesu, ambaye alifanyika mgeni na msafiri kati yetu,” alisema Baba Mtakatifu.
Papa alibainisha kwamba anaendelea kufuatilia kwa uchungu na wasiwasi mkubwa upanuzi na kuimarika kwa mzozo nchini Lebanon, akisema kwamba Lebanon ni ujumbe, lakini kwa sasa ni ujumbe wa kuteswa na vita, hivyo ambavyo vina madhara makubwa kwa idadi ya watu, kwani wengi wanaendelea kufa, siku baada ya siku, katika Mashariki ya Kati.
Aliongeza kwamba wanawaombea wahanga pamoja na familia zao, akitoa wito kwa pande zote kukomesha moto mara moja huko Lebanon na Gaza, pamoja na maeneo mengine ya Palestina na Israeli.
“Pia, ninawashukuru wengi wenu mliokuja kutoka Uholanzi, Ujerumani, Ufaransa kushiriki siku hii, asanteni.
Kwa wakati huu, pia ningependa kukupatia habari fulani. Nikirudi Roma nitaanza mchakato wa kutangazwa Mwenyeheri kwa Mfalme Baudouin, mfano wake kama mtu wa imani uwaangazie watawala. Ninaomba Maaskofu wa Ubelgiji wajitolee katika kuendeleza jambo hili,” alisema Papa.
Sambamba na hayo, aliomba kumgeukia Bikira Maria wakati wa kusali Sala ya Malaika wa Bwana pamoja, akisema kuwa hayo yalikuwa maombi maarufu sana katika vizazi vilivyopita, na hivyo napaswa kuhuishwa kwa kuwa ni muunganisho wa fumbo la Kikristo, na Kanisa linatufundisha kulijumuisha katika shughuli za kila siku.
Baada ya Adhimisho hilo la Misa Takatifu, Askofu Mkuu Luc Terlinden wa Jimbo Kuu Katoliki la Malines -Bruxelles, alishukuru kwa niaba ya Maaskofu wenzake, pamoja na Waamini wa Kanisa nchini Ubelgiji kwa ziara yake nchini.
Alimshukuru Baba Mtakatifu Fransisko kwa kwenda kukutana na wazalendo na wahusika, na kwa namna ya pekee wale walioko kwenye matatizo, pamoja na wenye majeraha ya kina yanayotokana na manyanyaso.
Aidha, alimshukuru Baba Mtakatifu kwa kuingia katika mazungumza na wanafunzi, watafiti na wanafunzi katika fursa ya miaka 600 ya Chuo Kikuu dada cha KULeuven na UCLouvain, na kwamba Papa anawafundisha wasitengenishe utafutaji wa ukweli, hekima na haki kijamii.
“Hekima inaweza kusaidia hadhi ya mtu binadamu, na kwa namna ya pekee katika Siku ya 110 ya Dunia ambayo imewekwa kwa ajili ya Wahamiaji na Wakimbizi, na inasaidia hata kulinda sayari yetu, “nyumba yetu ya pamoja,” alisisitiza, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Bruxelles.
Alisema kwamba wanaamini katika salamu za Baba Mtakatifu za wema, na kubainisha kwamba katika sala zao kwa ajili yake na kwa huduma yake, wanaikabidhi kwa Mama, Kikao cha Hekima na Mwenyeheri Anna wa Yesu.

NEKEMTE, Ethiopia

Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Ethiopia (Catholic Bishops’ Conference of Ethiopia: CBCE), Mwadhama Abune Kardinali Berhaneyesus, amesema kuwa wajibu mtakatifu wa kupitisha cheo cha ukuhani kutoka kizazi hadi kizazi, ni utamaduni unaowezeshwa na Roho Mtakatifu uliopokelewa kutoka kwa Yesu Kristo.
Kardinali Berhaneyesus aliyasema hayo katika mahubiri yake wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu na kuwekwa wakfu na kusimikwa kwa Askofu Getahun Fanta Shikune, aliyeteuliwa kuwa Askofu wa Vicariate ya Nekemte, nchini Ethiopia.
Aidha, katika mwendelezo muhimu wa baraka za kuadhimisha Mwaka Mpya wa Ethiopia, Kanisa Katoliki nchini humo lilisherehekea kuwekwa wakfu kwa Askofu huyo Mteule.
Miongoni mwa waliohudhuria katika Adhimisho hilo, ni Askofu wa zamani Varghese Thottamkara, C.M., Askofu wa sasa wa Balasore, India, pamoja na Maaskofu mbalimbali, Mapadri, waalikwa maalum, vikundi vya kidini, familia, na Waamini waliojitolea kutoka kote nchini.
Kardinali Berhaneyesus alimkabidhi Askofu huyo jukumu la kuongoza huduma hiyo mpya iliyowekwa na Mungu, akiwahimiza Wakatoliki wote kumuunga mkono mchungaji wao mpya kwa subira pamoja na sala.
Ikumbukwe kwamba Baba Mtakatifu Fransisko alifanya uamuzi wa kihistoria kwa kuwateua Maaskofu watatu wapya wa Kanisa Katoliki nchini Ethiopia, ili kutimiza sala na matarajio ya muda mrefu ya Waamini katika majimbo matatu nchini humo.
Maendeleo hayo yaliyosubiriwa kwa muda mrefu yanaashiria hatua kubwa kwa Kanisa Katoliki la Ethiopia, ambalo lilikuwa likitafuta kwa dhati uongozi wa mtaa kwa ajili ya utume wake wa kiroho na kichungaji.
Matukio hayo yalihudhuriwa na idadi kubwa ya Waamini kutoka kote Ethiopia na nchi jirani, wakiwemo Maaskofu, Mapadre, Masista wa Kidini, na Walei kutoka Eritrea, Association of Member Episcopla Cenference in Eastern Africa: AMECEA (Chama cha Mabaraza ya Maaskofu Wanachama Afrika Mashariki), na Symposium of Episcopal Conference of Africa and Madagascar: SECAM (Kongamano la Mabaraza ya Maaskofu wa Afrika na Madagaska).
Pia, Mkutano huo uliakisi umoja mpana wa Kanisa Katoliki Barani Afrika na nafasi yake katika Ukatoliki wa Kimataifa, na kwamba Sherehe za kuwekwa wakfu hazikuwa za kiroho tu, bali pia za kijumuiya, zilisherehekewa kwa furaha na ushiriki mkubwa kutoka sekta zote za jamii, zikiwemo jumuiya za mitaa, vikundi vya vijana, viongozi wa serikali, na wawakilishi kutoka mashirika mbalimbali ya kidini.
Kardinali Berhaneyesus alisema kwamba ushiriki huo mkubwa na wa aina mbalimbali, ulionyesha uhusiano thabiti kati ya Kanisa na watu wa Ethiopia, pamoja na nafasi muhimu ya Kanisa katika maisha ya kiroho na kijamii ya taifa.
Aliongeza kwamba uwepo wa Wawakilishi wa Kiekumene na Serikali pia ulionyesha dhamira ya Kanisa Katoliki katika ushirikiano wa dini na majadiliano kati ya dini mbalimbali, jambo ambalo ni la muhimu ambalo Maaskofu wapya wanatarajiwa kuendeleza na kuimarisha zaidi.
Alibainisha pia kuwa kuzingatia mizozo ya sasa ya Ethiopia, machafuko ya kijamii, na kuongezeka kwa mahitaji ya kibinadamu, Kanisa Katoliki linaonekana kama mhusika mkuu katika juhudi zinazoendelea za nchi kuelekea ujenzi wa amani na upatanisho.
Alisema kwamba mchanganyiko huo wa desturi za Kikatoliki na za kimaeneo uliashiria dhamira ya Kanisa ya kuishi pamoja na mshikamano kati ya jumuiya mbalimbali za kikabila na kidini nchini Ethiopia.

Dar es Salaam

Na Mwandishi wetu

Waimarishwa wameelezwa kwamba kumpokea Roho Mtakatifu kupitia Sakramenti Takatifu ya Kipaimara, ni kupewa jukumu la kuisimamia, kuilinda na kuitetea imani, pamoja na kuitangaza Habari Njema kwa maneno na matendo.
Fundisho hilo limetolewa hivi karibuni na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Stephano Musomba wakati wa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Sakramenti ya Kipaimara katika Parokia ya Bikira Maria Malkia - Kilimahewa, jimboni humo.
“Kwa upande wetu pia ni siku muhimu ya kukumbuka Vipaimara vyetu. Tulipompokea Roho Mtakatifu katika Kipaimara, tukapewa kazi ya kusimamia imani, kulinda imani na kuitetea, tukapewa kazi hiyo ya kutangaza Habari Njema, kumshuhudia Kristu kwa maneno yetu na matendo yetu,” alisema Askofu Musomba.
Aliongeza kwamba kupitia kumbukumbu hiyo, ni vizuri pia kutathmini na kuona ni kwa kiasi gani Wakristu wamefanikiwa, na kwamba ikiwa hawajafanikiwa, waache nafasi ili Kristu aweze kupenya na kutawala katika maisha yao.
Vile vile, Askofu Musomba aliwasihi Waamini kuondoa hali yoyote ya ukaidi, woga, ubaguzi, ubinafsi pamoja na roho zozote ambazo haziendani na mambo muhimu katika kuitangaza Habari Njema katika maisha yao.
“…maana yake tunaambiwa alama ya kwanza katika ujio wa Roho Mtakatifu, ni uvumi kama upepo mkali kutoka mbinguni, ukajaza chumba kile. Tunaona kwamba upepo ukiwa mkali, mtu anaweza akachukuliwa akashangaa anapeperushwa…
“Lakini lengo la upepo mkali ni kuondoa yote ya zamani, kuondoa ukaidi, kuondoa woga, kuondoa roho zozote zile ambazo haziendani na yale ambayo ni muhimu katika kutangaza Habari Njema, kuondoa ubaguzi, kuondoa ubinafsi, walitikiswa, na haya yote yakaondoka,” alisema Askofu Musomba.
Aliongeza kwamba upendo wa Mungu ndio unaowafanya watu wasiwe na ubaguzi, huku akiwasisitiza kuepuka kuwa na roho za usengenyaji pamoja na kuwachafua wengine katika jamii walipo, kwani kufanya hivyo siyo upendo wa Mungu unavyoelekeza.
Aliwataka Wakristo kuweka pembeni mambo yote yasiyompendeza Mungu katika maisha, badala yake wawe kitu kimoja, huku wakizungumza lugha moja.

DAR ES SALAAM

Na Alex Kachelewa

Uongozi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), umesema hatua ya kuboresha huduma zake kumesaidia mfuko huko kupiga hatua kubwa kimaendeleo kwa kuwa na ongezeko kubwa la mapato hadi kufikia Shilingi trilioni 8.5/- ikiwa ni ongezeko la asilimia 70% ya waajiri wapya.
Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba, alisema hayo hivi karibuni wakati akizungumza katika Mkutano kati ya NSSF na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), uliofanyika jijini Dar es Salaam.
“NSSF imepiga hatua kubwa sana mwaka hadi mwaka na hasa wakati huu ambapo huduma zetu tumeziboresha zaidi na kumaliza kero mbalimbali kwa wanachama wetu hasa wazee ambao walikuwa wakijipanga mstari katika ofisi zetu kwa muda mrefu kusubiria huduma ya madai yao…
“Lakini kwa sasa mtu anaweza kukaa hata sebuleni kwake kwa kutumia simu yake ya mkononi anahakiki michango yake na anaweza kufanya mchakato wote wa malipo na akafanikisha akiwa huko alipo na hiyo pia hata kuomba kadi endapo itapotea,”alisema Mshomba.
Mshomba alisema kuwa mpango wa NSSF kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano TEHAMA, imeufanya mfuko huo kupiga hatua kubwa na kuondoa usumbufu wote uliokuwa ukijitokeza miaka iliyopita na sasa mambo ni mazuri kwa wastaafu kwani kila kitu kinafanyika kwa wakati kwa njia ya mtandao.
Mshomba alibainisha kuwa kwa sasa uongozi wake unaendelea na mikakati mbalimbali, ili hadi kufikia Desemba mwaka 2025, huduma zote zifanyike kwa kutumia TEHAMA.
“Tayari sisi NSSF tumezindua huduma ya Mwanachama wetu kuproces mafao yake kwa njia ya mtandao mfumo huu utakwenda kuondoa usumbufu wote kufika ofisini atamaliza yeye mwenyewe huko huko,”alisema Mshomba.
Kuhusu sekta Binafsi, Mshomba alisema kwamba tayari mchakato umekamilika kwa lengo la kuhakikisha watu waliojiajiri katika sekta zisizo rasmi ikiwemo, kilimo, ufugaji, uvuvi, uchimbaji madini wadogo na kadhalika watafikiwa kwa huduma ya NSSF ili nao waweze kupata mafao wakiwa wazee.
Alifafanua kuwa Wanachama wa sekta hizo wao wamewekewa utaratibu mzuri wa kuchangia kiasi cha Shilingi 30,000/- kwa mwezi au kulipa kidogo kidogo kwa kila siku, wiki ama mwezi ili nao waweze kunufaika na akiba za uzeeni.
Aidha, Mshomba alisema mpango huo unakwenda sanjari na wafanyakazi wa Sekta binafsi ambao wanapenda kujiwekea akiba zaidi wao wewenye kwa njia ya uchangiaji binafsi ili waweze kutunisha zaidi akiba zao za mafao.
Kwa mujibu wa Mshomba, kwa sasa baada ya Sheria mpya kupitishwa na Bunge Wanachama pia wanaweza kufanya kazi sehemu mbili hata tatu na waajiri hao wote wakawachangia fedha katika akiba zao za mafao, isipokuwa mwajiri moja anapaswa kuthibitisha wazi kwamba ndiye atakayehusika moja kwa moja na NSSF, kwa kukumbushwa kuwasilisha michango hiyo kisheria.
Hata hivyo, Mshomba alitumia nafasi hiyo kuwasihi wanachama kuacha tabia ya kukimbilia kuchukua mafao yao kabla ya kutimiza umri wa kustaafu, kwani kufanya hivyo ni kujinyima fursa hasa manufaa ya mafao uzeeni.

DAR ES SALAAM

Na Mathayo Kijazi

Imeelezwa kuwa kazi ya Msimamizi katika Sakramenti Takatifu ya Kipaimara, ni kuwasaidia wazazi wa mtoto anayemsimamia, ikiwemo kujua maendeleo ya kiroho ya mtoto huyo, na kwamba siyo tu kumuwekea mkono begani wakati wa kupokea.
Ufafanuzi huo ulibainishwa na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu wakati wa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya kutoa Sakramenti ya Kipaimara kwa Vijana 49 katika Parokia ya Mtakatifu Simon Stock – Mbezi Mageti, jimboni humo.
“Pengine watu wanaweza kujiuliza kwamba nini majukumu ya msimamizi wa mtoto wakati wa kupokea Sakramenti Takatifu ya Kipaimara. Msimamizi ni mzazi wa mtoto huyo kiroho, na anatakiwa kujua maisha ya mtoto huyo baada ya kupokea Kipaimara.”
“Kwa hiyo, wewe msimamizi jitahidi kuulizia maendeleo ya mtoto uliyemsimamia. Tambueni kwamba mna kazi ya kuwalea watoto hawa, siyo tu kuwabandikia mikono begani wakati wa kupokea Sakramenti hii ya Kipaimara,” alisema Askofu Mchamungu.
Askofu huyo aliwasihi Waamini kuchangia katika shughuli za kimungu, ikiwemo ujenzi wa kanisa, kwani kufanya hivyo si kama kuchangia katika sherehe za harusi, bali ni kufanya jambo litakalowapatia baraka.
Hata hivyo Askofu Mchamungu aliwaasa Waamini kutokuoneana wivu katika maisha yao, bali waweke kipaumbele suala la kusaidiana, huku wakiwa katika misingi ya kumpendeza Mungu.
‘Kwa hiyo ndugu zangu, hakuna sababu ya kuoneana wivu. Tunaona katika maeneo mbalimbali watu wanaoneana sana wivu. Kwa Mkristu, hiyo siyo tabia nzuri kabisa,” alisema Askofu Mchamungu.
Vile vile, Askofu Mchamungu aliwapongeza Wanaparokia hiyo kwa hatua nzuri waliyofikia ya ujenzi wa kanisa, akiwaomba kuongeza umoja na mshikamano ili waweze kukamilisha.
Kwa upande wake Paroko wa Parokia hiyo, Padri Nelson Osmond alimshukuru Askofu Mchamungu kwa kufika parokiani hapo, na kuwaimarisha Vijana 49 kwa Sakramenti Takatifu ya Kipaimara.
Padri Nelson aliwapongeza Waimarishwa kwa kupokea Sakramenti hiyo, akiwasihi kuendelea kuyaishi yale yote waliyofundishwa ili yaendelee kuwasaidia katika maisha yao.
Akizungumza kwa niaba ya Halmashauri ya Walei Parokia, Mwenyekiti wa Parokia hiyo, Dk. Felix Sukuma   alimshukuru Askofu Mchamungu, akisema kwamba wamefarijika kutembelewa na Askofu aliyewaongoza katika Adhimisho hilo la Misa Takatifu.

DAR ES SALAAM

Na Mathayo Kijazi

Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Stephano Musomba amewataka Waamini kuwa wanyenyekevu, kwani utawasaidia kuuona ukuu wa Mungu.
Askofu Musomba alisema hayo wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Jubilei ya Miaka 25 na 50 ya Upadri, iliyoadhimishwa katika viwanja vya Kituo cha Msimbazi, jimboni Dar es Salaam.
“Katika hilo ni kwamba sifa zimwendee Mungu kwa makuu aliyowatendea ndugu zetu Wajubilanti kwa miaka 25 na miaka 50. Si rahisi hivyo, na ndiyo maana haya yote yanahitaji sana unyenyekevu. Katika unyenyekevu, ndipo tunapotambua ukuu huu wa Mungu katika maisha yetu,” alisema Askofu Musomba.
Musomba aliwaasa Wakristo kumshukuru Mungu kwa zawadi ya Makuhani, akiwasihi kutambua kwamba Makuhani hao ni Kristu mwingine.
“Tunapoadhimisha haya yote, tunathamini sana wito huu mkubwa wa Ukuhani. Kwa maneno mengine hawa Makuhani ambao ni Yesu mwingine. Na katika kumshukuru huyu Kristo, tumshukuru Mungu tumeona makuu anayotutendea kwenye maisha yetu. Na katika kuyaona hayo makuu, siyo kwamba tunajivunia kwamba tumeweza, ila tunamshukuru Mungu, na tunamsifu yeye peke yake,” alisema Askofu huyo.
Sambamba na hayo, alikumbusha kile kilichoendelea katika Kongamano la 5 la Kitaifa la Ekaristi Takatifu juu ya Ukuu wa Adhimisho la Misa Takatifu, na kwamba wanaojongea mbele za Mungu, Mungu hawezi kuwaacha.
Wakati huo huo, Askofu Musomba aliwapongeza Mapadri hao kwa Jubilei yao ya Miaka 25 na 50 ya Upadri, akisema kwamba wamefanya kazi kubwa kwa kuweza kukaa katika utume wao, pamoja na kudumisha utambulisho wao kama Makuhani.
Askofu huyo aliongeza kwamba kama Wanajimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, wameziona kazi pamoja na utume kwa ujumla uliofanywa na Mapadri hao katika Parokia pamoja na Taasisi mbalimbali jimboni humo, hasa katika malezi yao ya kuwapeleka watu kwa Mungu.
Naye Askofu Msaidizi wa Jimbo hilo, Mhashamu Henry Mchamungu, akiwasilisha salamu za Askofu Mkuu, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi, aliwapongeza Mapadri hao kwa Jubilei yao ya Miaka 25 na 50, huku akiwapongeza kwa kazi kubwa wanazozifanya katika utume wao.
Askofu Mchamungu alibainisha kwamba hakuna mtu yeyote duniani mwenye mamlaka au uwezo wa kumwondolea mtu Daraja Takatifu la Upadri, bali binadamu anao uwezo wa kumwondolea mtu hadhi ya Uklero.
“Nadhani itabidi siku moja tuboreshe lugha. Kusema miaka 25 au 50 ya Upadri kwa tukio kama hili, je utawezaje kutofautisha na tukio ambalo ni Padri ambaye hayupo katika utumishi, lakini na yeye anakumbuka kwamba ametimiza miaka 25 au miaka 50 ya Upadri?
‘Kama mnavyojua, kuna Sakrementi tatu ambazo zinaweka alama isiyofutika, ambazo ni Ubatizo, Kipaimara, na Daraja Takatifu la Upadri. Tunapoongelea kuhusu Daraja Takatifu la Upadri, ni kwamba hakuna binadamu yeyote duniani ambaye anao uwezo wa kumwondolea mtu Daraja Takatifu la Upadri, ila binadamu anao uwezo wa kukuondolea ile hadhi ya Uklero. Lakini anayekuwa Padri, anakuwa Padri milele.
Askofu huyo alibainisha kwamba neno Utumishi ni muhimu sana, na ndilo neno linalofaa kutumika kwa Mapadri, kwani linaonyesha kwamba wanapongezwa kwa miaka hiyo wakiwa katika utumishi wao, na si nje ya utumishi kama ilivyo kwa wengine.

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimesema kuwa hali ya uwekezaji nchini imeongezeka katika kipindi cha Aprili hadi Juni mwaka huu.
Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Gilead Teri alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na kueleza kwamba TIC ilisajili miradi 198 yenye thamani ya dola za Kimarekani bilioni 1.69 sawa na zaidi ya Shilingi trilioni tatu, itakayoajiri watu 9600 kote nchini.

Dar es Salaam

Na Israel Mapunda

Meneja wa Maabara Kuu ya Veterinari kutoka Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Dk. Geofrey Omarch amefanya ukaguzi wa vyakula vya Mifugo kwa wazalishaji, wauzaji na watumiaji wa vyakula hivuo Wilaya ya Kinondoni Mkoa wa Dar Es Salaam ili kufuatilia ubora wa vyakula hivyo.
Dk. Omarch aliongeza kuwa TVLA kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi inalenga kuwalinda watumiaji wa vyakula hivyo ili kulinda ubora wa vyakula vinavyozalishwa vitokanavyo na zao la Mifugo pamoja na kuongeza soko la Mifugo kimataifa.
“Tumekuwa tukifanya ukaguzi huu mara kwa mara kwa wasindikaji, wauzaji na watumiaji wa vyakula vya Mifugo ili watumiaji wa mazao hayo wawe salama wakati wote. TVLA imedhamilia kuwapitia wazalishaji wote Tanzania nzima kwa nyakati tofauti ili kujiridhisha kile kinachozalishwa kama kinakidhi ubora, kukagua marighafi za uzalishaji, hatua za uzalishaji pamoja na kukagua vibali vya uzalishaji,” alisema Dk. Omarch.
Baadhi ya wazalishaji wa vyakula vya Mifugo Wilaya ya Kinondoni waliishukuru Serikali kwa kuendelea kuwafanyia ukaguzi wa mara kwa mara kwani ukaguzi huo unaowaongezea umakini kwenye uzalishaji wa vyakula.
Wameiomba Serikali kutochoka kwenda kuwakagua na kuwapa ushauri na kuendelea kuwadhibiti baadhi ya wazalishaji ambao sio waaminifu wanaowaharibia soko la vyakula kwa kuzalisha vyakula vyenye mapungufu na kuvipiga chapa za kampuni zingine.
Wakala ya Maabara ya Veterinali Tanzania (TVLA) imekuwa ikifanya ukaguzi wa vyakula vya mifugo mara kwa mara kwa wazalishaji, wauzaji na pamoja na wanunuzi wa vyakula vya Mifugo kwa kushirikiana na wakaguzi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Ofisi za Wakuu wa Mikoa pamoja na Halmashauri.

MTWARA

Na Mwandishi wetu

Serikali imesema kuwa itajenga Kongani ya Viwanda vya kuchakata mazao ya Mikoa ya Kusini kwa gharama ya zaidi ya Shilingi bilioni 300.
Akizungumza katika mwendelezo wa ziara yake mkoani Mtwara, Waziri wa Kilimo Hussein Bashe, kuwa alisema iwe jua ama mvua itajenga Kongani ya Viwanda vya kuchakata mazao ya Mikoa ya Kusini eneo la Maranje Mkoani Mtwara yenye gharama ya zaidi ya sh. Bilioni 300.
Kongani ya Viwanda (Industrial Park) inajengwa katika kijiji cha Maranje na Tulia, Kata ya Mtiniko, Nanyamba Mji, Mkoani Mtwara
Alisema eneo la mradi lina jumla ya ekari 1,572, ambapo eneo linaloendelezwa kwa sasa ni ekari 354, na ekari 1,218 zilizobaki zitasafishwa na kuwekewa uzio mwezi ujao.
Waziri Bashe alieleza kuwa, Kongani hiyo ya Viwanda ndilo suluhisho la changamoto walizonazo wakulima wa mikoa hiyo.
“Wapo watu walisema ni ndoto, haitawezekana leo, nawaambia Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan ni msikivu na mtendaji, ameamua iwe jua iwe mvua, Kongani itajengwa hapa na itahusisha viwanda mbali mbali vya kuchakata korosho, ufuta, mbaazi na mengine,”alisema Waziri Bashe.
Alisema, Serikali imeanza hatua za awali za ujenzi wa Kongani hiyo, na zaidi ya sh. Bilioni 7 zimewekezwa.
“Mradi huu mkubwa unaoitwa Dkt Samia Suluhu Hassan, unalenga kujenga viwanda vya kubangua korosho visivyopungua 30 kwa awamu, na tayari zaidi ya shilingi bilioni saba zimetumika kujenga maghala mawili na kisima kimoja,”allisema Bashe.
Aliongeza pia kuwa maghala hayo mawili ya awali, yenye uwezo wa kuhifadhi tani 20,000 za korosho, yanatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba mwaka huu, ili msimu wa korosho wa mwaka kesho uanze kwa ufanisi.
alisema huo pia utatoa fursa za ajira kati ya watu 33,000 mpaka 35,000 ambapo ajira za kwanza zitanufaisha wananchi wenyeji .
“Mradi huu unatarajiwa kuajiri kati ya watu 33,000 mpaka watu 35,000 na utakuwa suluhisho la changamoto ya muda mrefu juu ya bei ya korosho kwa mikoa yote inayolima korosho, ikiwemo Mtwara, Ruvuma, na Lindi. Serikali yenu ni sikivu haitarudi nyuma, hiki kiwanda kitajengwa kwa maslahi ya wananchi wa kusini,”alisisitiza Bashe.
Aidha, Waziri Bashe alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kurejeshwa kwa agenda ya ushuru wa mauzo ya nje, lengo ni kuwezesha upatikanaji wa ruzuku na pembejeo, ili kumuinua mkulima.
Bashe alisema kuwa fedha hizo za ushuru huo zikikusanywa, zinarudi Bodi ya Korosho ili kusimamia mahitaji ya korosho.
“Faida zake ni kubwa kwa kuwa ushuru huu sasa unarudi bodi ya Korosho ili kuwezesha wakulima wa zao hilo. Sasa tumetoka kuzalisha tani 180,000 hadi tani 310,000 na tunatarajia kufikia tani 500,000”, alisema.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Nanyamba Abdallah Chikota alimpongeza Waziri Bashe kwa mapambano ya kutetea maslahi ya wakulima wadogo nchini.