DAR ES SALAAM
Na Mathayo Kijazi
Mkuu wa Idara ya Walei Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Delphinus Ngaiza, amewasihi Viongozi wa Utume wa Wanaume Katoliki (UWAKA) Taifa, kuiga mfano wa Mtakatifu Yosefu kwa kuwa wanyenyekevu, na wenye kumtanguliza Mungu katika mambo yao.
Padri Nagiza alisema hayo hivi karibuni katika homilia yake, wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu, katika Mkutano wa Viongozi hao wa UWAKA, walipokutana kwa lengo la kujadili mambo mbalimbali, yatakayokiendeleza chama hicho cha kitume ngazi ya Taifa, uliofanyika katika Kiwanda cha Woiso Original Products, kilichopo Salasala jijini Dar es Salaam.
DAR ES SALAAM
Na Mwandishi wetu
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Sana Jude Thaddaeus Ruwa’ichi, amewataka walezi kuwapuuza vijana wanaojiita Wakatoliki, na kulipinga Kanisa Katoliki kuwa ni ‘fake’, na Ukristo wao hauna mizizi.
Askofu Mkuu Ruwa’ichi alitoa wito huo hivi karibuni wakati akitoa homilia yake, katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Shukrani ya Walezi wa Shirika la Kipapa la Utoto Mtakatifu Jimbo, iliyofanyika katika Parokia ya Mtakatifu Gaspar –Mbezi Beach.
DAR ES SALAAM
Na Mathayo Kijazi
Abate Christian Temu –OSB wa Abasia ya Ndanda, Jimbo Katoliki la Mtwara, amesema kuwa maisha ya Mkristo ni kama Hija, kwani kila wakati anakuwa safarini kuelekea mbinguni kwa Mwenyezi Mungu.
Aidha, Abate Temu amewasihi Wakristo kutoogopa jambo lolote, akiwasihi kuwa majasiri kwani Mungu yupo nao, na masuala ya amani na haki ni matunda ya Kimungu.
Abate Temu alitoboa siri hiyo hivi karibuni katika homilia yake, katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Kufunga Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, iliyoadhimishwa katika Kituo cha Hija - Pugu, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.
DAR ES SALAAM
Na Angela Kibwana
Zaidi ya shilingi milioni 200, zinatarajiwa kutumika katika ujenzi wa nyumba ya Padri, katika Parokia mpya ya Bikira Maria wa Rozari-Msomwero, jimboni Morogoro, ambayo itakuwa ni hatua muhimu ya kukamilisha makazi ya Padri, anayefanya utume parokiani hapo, kwa lengo la kusogeza huduma za kiroho kwa Waamini.
Akizungumza kwa mahojiano maalumu, Paroko wa Parokia hiyo Padri Chediel Mloka, amebainisha kuwa parokia hiyo mpya ilitangazwa miaka mitatu iliyopita, na Askofu Lazarus Vitalis Msimbe SDS, wa Jimbo Katoliki Morogoro, ili kunusuru imani za Waamini ambao walikuwa wanapata huduma za kiroho, katika Parokia ya Ilonga.
Alisema kuwa kwa sasa wakati anaendelea kusubiri kukamilika kwa nyumba hiyo, anaishi nyumba ya kupanga umbali wa Kilomita nne toka yalipo makazi hayo, hadi kufika kanisani hapo.
DAR ES SALAAM
Na Mathayo Kijazi
Wakristo wamesisitizwa kuwa wanakanisa halisi, hasa katika zama hizi zenye ugeugeu na ubabaishaji mwingi, ili waendelee kuwa na roho zenye uadilifu na uungwana.
Kauli hiyo ilitolewa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Sana Jude Thaddaeus Ruwa’ichi, wakati wa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Jubilei ya Miaka 25, ya Parokia ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili - Mavurunza, jimboni humo.
Na Mwandishi Wetu
Katika makala haya kuhusu Ubatizo wa Bwana, Mwadhama Protace Kardinali Rugambwa katika mahubiri yake, ametumia fursa hii kufafanua alama muhimu, zilizojionesha wakati Kristo Yesu alipobatizwa mtoni Yordani.
Anasema kwamba alama ya kwanza ni Maji: Alama ya kifo na uhai; Mbingu zikamfunukia, Roho Mtakatifu akashuka juu yake kama hua; Alama ya pili ni kufunguka kwa mbingu; Alama ya mabadiliko ya ndani ya mwanadamu, mbele ya Mwenyezi Mungu; Alama ya tatu ni Roho Mtakatifu aliyemshukia Kristo Yesu na sauti ya Baba wa milele ikasikika: Huyu ni mwanangu, mpendwa wangu.
Ubatizo ni sakramenti inayotuingiza katika Ukristo, ni sakramenti inayotuondolea dhambi ya asili na adhabu zake zote. Ni kwa njia ya Ubatizo tunazaliwa upya kwa maji na Roho Mtakatifu, na hivyo tunakuwa ni watoto wa Mungu na wa Kanisa.
DAR ES SALAAM
Arone Mpanduka
Michel Kuka Mboladinga, ambaye pia anajulikana kama Michel Kuka, Michel Nkuka, au kwa jina la utani “Lumumba” na “Lumumba Vea”, ni shabiki wa soka wa timu ya taifa ya DR Congo, anayejulikana kwa tabia yake ya kipekee, wakati wa mechi za timu ya taifa ya kandanda ya DR Congo.
Amekuwa shabiki kindakindaki wa taifa la Congo tangu mwaka 2013, ambapo amekuwa akisimama jukwaani bila kutikisika katika michezo yote. Amekuwa akiiga mkao wa sanamu ya mwanasiasa wa zamani na mkombozi wa taifa hilo, Patrice Lumumba mjini Kinshasa.
Jamaa huyu amejizolea umaarufu zaidi kwa vyombo vya habari vya kimataifa, wakati wa Kombe la Mataifa ya Afrika la 2025, nchini Morocco.
London, Uingereza
Kiungo wa kati wa Tottenham, Rodrigo Bentancur, anahitaji upasuaji wa misuli ya paja, na anatarajiwa kukosa angalau miezi mitatu.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Uruguay, ambaye amekuwa mchezaji muhimu kwa timu ya Thomas Frank msimu huu, alipata jeraha hilo katika mchezo wa Ligi Kuu ya Spurs dhidi ya Bournemouth wiki iliyopita.
London, Uingereza
Mshindi wa fainali wa zamani wa Wimbledon, Milos Raonic, alisema kwamba amekuwa mtu mwenye bahati zaidi kutimiza ndoto zake, alipotangaza kustaafu kutoka tenisi.
Mkanada huyo mwenye umri wa miaka 35, alimshinda Roger Federer na kufikia shindano la Wimbledon mwaka wa 2016, ambapo alishindwa moja kwa moja na Andy Murray wa Uingereza.
Raonic, ambaye alishinda mataji nane ya ngazi ya ziara, alifikia kiwango cha juu cha dunia cha tatu mwaka huo huo, baada ya pia kufika nusu fainali ya Australian Open.
DAR ES SALAAM
Na Nicolaus Kilowoko
Kocha Mkuu wa klabu ya soka ya Simba, raia wa Afrika Kusini Steven Barker, baada ya kuiongoza klabu hiyo kwenye michezo mitatu ya michuano ya Mapinduzi Cup 2026, ametoa maagizo kwa uongozi wa klabu hiyo, kusajili wachezaji wanne kwenye dirisha dogo la mwezi Januari.
DAR ES SALAAM
Na Mwandishi wetu
Shirikisho la ngumi Tanzania (BFT), limeandaa mikakati ya kumleta bondia maarufu duniani, Manny Pacquiao, nchini Tanzania, kwa ajili ya mashindano ya semi Pro fights ya BFT.
Lengo la BFT kumleta Pacquiao nchini Tanzania, ni kwa ajili ya uzinduzi wa mashindano hayo, pia atashiriki matukio ya kijamii ya kuinua mchezo wa ngumi hapa nchini.
DAR ES SALAAM
Na Arone Mpanduka
Klabu ya Singida Black Stars, imesema kuwa haina ukaribu wala urafiki wowote na klabu ya Yanga, hasa kwenye kupeana wachezaji na kupeana matokeo, kama watu wanavyodai.
Singida imeyasema hayo, wakati wimbi la kuuziana na kupeana wachezaji wa mkopo likishamiri, katika kila dirisha la usajili hapa nchini.
Katika dirisha dogo la sasa la usajili, Singida iliwatoa kwa mkopo wachezaji Mohammed Damaro na Marouf Tchakei kwenda Yanga, huku Yanga ikimtoa Mamadou Doumbia kwa mkopo kwenda Singida, jambo ambalo wadau wa soka wakalazimika kuweka hadharani shaka yao, kuhusiana na timu hizo mbili.
Na Dkt. Felician B. Kilahama
Namshukuru Mwenyezi Mungu aliye mwingi wa rehema, aliyeumba wanadamu kwa sura na mfano wake. Hili ni “wazo mbadala”, ikimaanisha kwamba kuna kinachotakiwa kufanyika, lakini katika harakati za utekelezaji likajitokeza ‘wazo mbadala’.
Uchaguzi Mkuu ulifanyika Oktoba 29, 2025, na aliyekuwa mgombea urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Mheshimiwa Dk. Samia Suluhu Hassan, akatangazwa mshindi na kuapishwa rasmi Jumatatu, Novemba 3, 2025.
Baada ya zoezi hilo kukamilika, Rais aliunda Baraza la Mawaziri, ambalo pamoja na Wakuu wa Mikoa, Wilaya, Viongozi wakuu wa Halmashauri husika, kwa pamoja inakuwa Serikali inayoongozwa na Rais.
Wakati wa kampeni za uchaguzi, kuna sehemu ambazo wananchi waliomba serikali itakayoundwa, kuanzisha wilaya na halmashauri mpya, ili kuwarahisishia wananchi kupata huduma wanazohitaji, ikiwemo kutatuliwa kero haraka iwapo ofisi husika zitakuwa karibu.
NA PAUL MABUGA
Ilikuwa ni usiku wa vilio, hasira, lakini pia fahari kubwa. Jumapili iliyopita nchini Morocco, dunia ilishuhudia vijana wa Taifa Stars wakiondolewa kwenye michuano ya AFCON 2025, kichwa cha juu dhidi ya wenyeji Morocco.
Kufungwa goli 1-0 na timu namba moja barani Afrika, huku mwamuzi Boubou Traoré, akionekana kuwa “mchezaji wa 12” wa wapinzani, ni jambo ambalo halitafutika haraka kwenye akili za Watanzania.
Dakika ya mwisho ya mchezo itabaki kuwa jeraha, mchezaji wa Stars anaangushwa ndani ya kumi na nane, dunia nzima inaona ni penati ya wazi, lakini filimbi ya mwamuzi inabaki kimya, na VAR inajiziba macho.
Tulitolewa kama “ndama” anayepelekwa machinjioni, lakini kabla kisu hakijagusa shingo, ndama huyu alionesha kuwa ana pembe za chuma.
Hata hivyo, kuna mambo matano ya Stars kujivunia katika AFCON hii: Moja ikiwa ni kuvunjwa kwa mwiko wa miaka 45, kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1980, Tanzania imeweza kuvuka hatua ya makundi, na kuingia hatua ya mtoano (Round of 16).