Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

DAR ES SALAAM

Na Arone Mpanduka

Mashindano maalum ya FIFA Series yamekuwa yakiwaacha njia panda Watanzania wengi ambao wamekuwa na maswali mengi hasa pale walipoiona Taifa Stars ikishiriki kule Azerbaijan.
Michuano ya FIFA Series ya 2024 ni msururu wa mechi zinazotambuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa FIFA, zinazohusisha timu za taifa kutoka mashirikisho tofauti ya mabara mbalimbali duniani.
Tayari uzinduzi wa mashindano hayo umefanyika mwezi huu ambao umehusisha mechi za makundi matano tofauti, iliyofanyika katika nchi tano mwenyeji kuanzia Machi 21 hadi 26 mwaka huu.
Mashindano hayo ya kirafiki yalitangazwa kwa mara ya kwanza kama mpango wa FIFA mnamo Desemba 2022 yakiwa najina la ‘FIFA World Series’, na baadaye kuthibitishwa na Rais wa FIFA Gianni Infantino mnamo Machi 16,2023 kufuatia kuchaguliwa tena kwa wadhifa huo wakati wa Kongamano la 73 la FIFA. mjini Kigali, Rwanda.
Shindano hili litaleta pamoja timu za taifa za wanaume kutoka mashirikisho yake sita katika msururu wa mashindano ya kirafiki wakati wa dirisha la mechi za FIFA na kufanyika Machi kila mwaka.
Mashindano hayo yananuiwa kuvipa vyama wanachama wa FIFA nafasi muhimu za kucheza kwa kuwaruhusu kucheza mara kwa mara timu kutoka mashirikisho mengine ambayo vinginevyo hawatakabiliana nayo, na hivyo kuruhusu fursa zaidi za maendeleo ya kiufundi.
Kwa mfano kumekuwa na ugumu kwa timu za barani Afrika kukutana na timu za Ulaya hasa kwa kukosa nafasi ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia mara kwa mara, hivyo FIFA Series hutoa faida kwa timu hizo kukutana.
Inakusudiwa pia kutoa vyama vya wanachama na fursa za ziada za kibiashara na mengine mengi.
Fainali hizo za mwaka 2024 zinafanyikakama hatua ya awali ya majaribio ya shindano hilo.
FIFA Series imegawanywa katika vituo vikuu sita ambavyo ni Algeria, Azerbaijan, Misri, Saudi Arabia A, Saudi Arabia B na Sri Lanka.
Kituo cha Algeria kinahusisha timu kama Algeria, Andorra, Bolivia na South Africa huku cha Azerbaijan kikiwa na timu za  Azerbaijan, Bulgaria, Mongolia na Tanzania.
Kituo cha Misri kina mwenyeji Misri, Croatia, New Zealand naTunisia wakati kituo cha Saudi Arabia A kina timu za Cambodia, Cape Verde, Equatorial Guinea na Guyana.
Saudi Arabia B ina timu za Bermuda, Brunei, Guinea na Vanuatu wakati Sri Lanka ina Bhutan, Central African Republic, Papua New Guinea na wenyeji Sri Lanka.
Mabara sita yaliyounganishwa kupitia FIFA Series ni Afrika(timu tisa), Asia(timu tano), Amerika Kusini(timu moja), Amerika Kaskazini(timu mbili), Oceania(timu tatu) na Ulaya(timu nne).
Katika FIFA Series ya mwaka huu. Misri pekee ndiyo ilikuwa na muundo wa mtoano, huku washindi wakiamuliwa kwa mikwaju ya penalti baada ya sare ndani ya muda wa kawaida.
FIFA Series ya Misri ni tofauti kidogo ambapo yenyewe inajulikana kama Kombe la Soka la Kimataifa la ACUD, ikiwa imefanyika Cairo na Mji Mkuu Mpya wa Utawala mnamo Machi 22, 23 na 26, na imehusisha wenyeji Misri (CAF), Croatia (UEFA), New Zealand (OFC) na Tunisia (CAF).

PARIS, Ufaransa
Bondia wa Ireland Amy Broadhurst anafikiri nafasi yake ya kushiriki katika Michezo ya Olimpiki ya Paris imekwisha.
Bingwa huyo wa Dunia, Ulaya na Jumuiya ya Madola amesema Chama cha Ndondi cha Riadha cha Ireland [IABA] kimemjulisha kwamba hatafanyiwa tathmini ya mashindano ya pili ya kufuzu kwa Dunia, yanayotarajiwa kufanyika mwishoni mwa Mei huko Bangkok.
Kwa mujibu wa Broadhurst, Kitengo cha Utendaji wa Juu kinataka kumtathmini mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 na bingwa mwingine wa dunia, Lisa O’Rourke, kwa ajili ya mashindano yajayo ya Ulaya badala ya kuwapeleka Thailand.
Anasema hilo halitafanyika.
“Nimemjulisha mwanasaikolojia wangu ili kuwafahamisha kuwa sitakuwa katika kituo cha utendakazi wa hali ya juu kwa siku zijazo, na nitakuwa nikifikiria sana kutorudi nyuma hata kidogo.”
Ilipowasiliana na BBC Sport (Northern Ireland Sport: NI), IABA haikuwa na maoni ya kutoa kujibu matamshi ya Broadhurst, kwani uteuzi katika vizito vyote, bado haujafanywa.
Inaonekana kuwa bingwa wa Ireland Grainne Walsh atachaguliwa kwenda Thailand, ingawa uteuzi wa kufuzu kwa Olimpiki bado haujafanywa.
Bondia huyo wa Offaly alikosa kushiriki Olimpiki ya Paris mapema mwezi huu alipopata kipigo cha kushtukiza cha uamuzi katika pambano la upendeleo.

MADRID, Hispania
Watu sita wamekamatwa baada ya ofisi za Shirikisho la Soka la Hispania pamoja na nyumba ya Rais wa zamani wa Shirikisho hilo, Luis Rubiales kuvamiwa na maafisa wa upelelezi kama sehemu ya uchunguzi.
Uchunguzi huo unahusu utakatishaji fedha na rushwa katika kashfa ya kuhamishwa kwa mashindano ya Super Cup ya Hispania kwenda Saudi Arabia.
Hadi sasa nyumba 11 zimepekuliwa juu ya kashfa hiyo inayokadiriwa kuwa na thamani ya pauni milioni 30.
Mamlaka nchini Hispania zimethibitisha kuwa Rubiales ni mmoja kati ya watu wengine watano ambao wameanza rasmi kuchunguzwa.
Maafisa hao hawakufanikiwa kumkuta Rubiales, kwani taarifa zinaeleza kuwa yupo nje ya nchi hiyo.
Ofisi ya waendesha mashtaka wa Serikali ya Hispania imesema kuwa polisi wakishirikiana na wapelelezi wa Europol walikuwa wakitafuta nyaraka fulani.
Ikumbukwe kuwa Rubiales ana kesi nyingine ya kumbusu mchezaji wa timu ya soka ya taifa ya wanawake ya Hispania baada ya fainali za Kombe la Dunia la wanawake zilizofanyika mwaka jana.

GEITA

Na Joel Maduka-Geita

Kufuatia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan kuendelea kusaidia kuinua michezo kwa kununua magoli, mdau mmoja wa michezo mkoani Geita, Hussen Makubi amejitokeza na kuongeza dau kwa Simba na Yanga kwa kila goli watakalolifunga kwenye mechi zao za Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Yanga inapambana kuhakikisha inaitoa Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini katika hatua ya Robo Fainali huku Simba ikitaka kuondokana na mazoea ya kuishia robo fainali kwa kutaka kuiondosha mashindanoni Al Ahly ya Misri.
Makubi maarufu kama Mwananyanzara ambaye tangu awali alikuwa na utaratibu wa kutoa shilingi laki tano kwa kila goli, sasa amepandisha dau kwa kuahidi kutoa shilingi milioni moja kwa kila goli.
Akizungumza na Tumaini Letu Makubi alisema amesikia Rais Samia amepandisha dau kutoka shilingi milioni tano hadi 10 kwa kila goli kwa timu hizo, hivyo na yeye kwa uwezo wake ameamua kutoka kwenye kiwango cha shilingi laki tano hadi milioni moja.
“Nimepandisha dau kwa kila goli litakalofungwa na Yanga na hata watani zetu Simba nao nitafanya hivyo hivyo.Lengo langu ni kuona timu hizo zinafanya vizuri kimataifa,”alisema Makubi ambaye ni shabiki mkubwa wa Yanga mkoani Geita.
Makubi aliahidi kuchinja ng’ombe na kuwanywesha supu wakazi wa Geita mjini kama ikitokea timu yake ya Yanga ikapata fursa ya kusonga mbele kwenda nusu fainali.
“Tutafunga mitaa Geita yote hii na kushangilia kama Yanga itafanikiwa kuwatoa Mamelodi na kwenda nusu fainali, na nitachinja ng’ombe na kuwanywesha supu mashabiki wote.Ninaamini hata mikoa mingine itaiga kwa hiki ninachokifanya,”alisema Makubi.
Baadhi ya wadau wa soka mkoani Geita akiwemo Emmanuel Ikolongo Otto na Emily Kimamba, wamempongeza Makubi kwa kujitoa kuzipa hamasa timu hizo.
“Mwananyanzala anafanya vizuri kwa sababu anaonyesha kwamba Geita ina wadau wa michezo wanaopenda maendeleo,” alisema Otto.

DAR ES SALAAM

Na Mathayo Kijazi

Waamini wametakiwa kuendelea kujitolea damu bila kuogopa, ili kuokoa maisha ya wengi wenye uhitaji.
Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu alitoa rai hiyo alipokuwa akizungumza na Walezi wa Shirika la Kipapa la Utoto Mtakatifu, walipofanya matendo ya huruma katika Hospitali ya Kardinali Rugambwa, Ukonga, jijini Dar es Salaam.
“Wanaotoa damu kwa kweli tunawashukuru sana, kwani wanaokoa maisha ya watu wengi. Pengine kuna wengine wanaogopa kutoa damu. Kwa hiyo, naomba msiogope, unapotoa damu ujue kwamba unaokoa maisha ya mtu.
“Siyo kwamba ni wakinamama wanaojifungua ndio tu wanaohitaji kuongezewa damu, lakini kuna wengine pia ambao pengine wamekutwa na upungufu wa damu, wapo wengine waliopata ajali ambayo imesababisha damu nyingi kumwagika, kwa hiyo unapotoa damu, unaokoa maisha ya watu hao,” alisema Askofu Mchamungu.
Askofu Mchamungu aliwahimiza Walezi hao kuendelea kuwalea watoto katika malezi bora, ili liweze kupatikana Taifa lenye kujaliana.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mashirika ya Kipapa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Timothy Nyasulu Maganga, aliwashukuru Walezi hao kwa kufanya matendo ya upendo, huku akiwapongeza kwa majitoleo yenye thamani ya Shilingi 10,150,000/=, kwani mwaka jana ilikuwa Shilingi milioni tisa.
Naye Mganga Mkuu wa Hospitali ya Kardinali Rugambwa, Dk. Jane Manyahi, aliwashukuru Walezi hao kwa kufanya matendo ya upendo hospitalini hapo, huku akiwaomba kuwa hayo waliyoyafanya yasiwe mwisho, bali yawe endelevu.
Aliwaomba wale wote wenye vigezo vya kuchangia damu kwenda kufanya hivyo, kwani wakichangia, watapewa kadi maalum za kuwatambulisha kwamba ni wachangiaji, ili na wao au ndugu zao watakapohitaji kuchagiwa damu, waweze kuchangiwa.
Akisoma historia fupi ya Hospitali ya Kardinali Rugambwa, Katibu wa Hospitali hiyo, Honest Antony alisema kuwa Hospitali hiyo ilianza Mei 22 mwaka 1986 kama Zahanati, wakati huo Kanisa lilikuwa na zahanati nzuri katika maeneo ya Pugu kwenye shule ya Mtakatifu Fransisko, iliyotaifishwa mwaka 1970.
Alisema kuwa Serikali ilitaka pia kuchukua Zahanati hiyo iliyoendeshwa na Masista wa Baldeg. Kardinali Laurean Rugambwa aliyependa kuwa na hospitali ya Jimbo akishauriana na viongozi jimboni, alisisitiza wabadilishane na Zahanati ya Serikali iliyokuwa hapo Ukonga.
“Ukonga palikuwepo tayari Parokia, na Paroko wake Padri Zakeo, Mfransiskani Mkapuchini, alifanya kazi kubwa katika mchakato mzima wa makabidhiano. Bahati nzuri Waamini wa Ukonga walimpenda sana Padri Zakeo, nao wote kupitia Halmashauri ya Walei ya Parokia ya Ukonga, walikuwa nyuma yake katika shughuli nzima, hasa kazi ya kukabidhi umiliki wa viwanja,” alisema Katibu, na kuongeza,
“Mwadhama Laurean Kardinali Rugambwa aliwaomba Masista wa Shirika la Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu wa Bukoba waje kusimamia zahanati hii ya Ukonga, na Viongozi wao wakakubaliana Septemba 17 mwaka 1984 Shirika liliwatuma Masista wawili wauguzi na wakunga, Sista Ariadina Bijuka na Sista Mechtilda Lwakalema, ambao bado wako hai mpaka leo.”
Katibu alisema kuwa wakati mchakato wa makubaliano na Serikali ukiendelea, Kardinali Laurean Rugambwa alianza kujenga Konventi ya Masista katika kiwanja cha Kanisa Parokiani Ukonga. Baadaye Jimbo Kuu lilipata kiwanja cha zahanati na kujenga nyumba nyingine ya Masista mwaka1995, na konventi ya kwanza ilibadilishwa na kuwa nyumba ya Mapandri.
Alibainisha kuwa mazungumzo juu ya makabidhiano yalikuwa magumu kwa sababu ya uwepo wa wengine ambao walitaka kuchukua zahanti hiyo. Mwadhama Kardinali Laurean Rugambwa ilibidi atie nguvu na ushawishi sana, akisaidiwa na Padre Zakeo na waamini, hasa wa Parokia ya Ukonga.
Alisema kuwa Mei 22 mwaka 1986, Sista Ariadina Bijuka alikabidhiwa uongozi wa zahanati ya Ukonga, akiwa bado mwajiriwa wa Serikali, na wafanyakazi wote wakiwa wa Serikali na Zahanati ikiwa bado serikalini. Wakati huo Zahanati haikuwa na madawa zaidi ya makopo kidogo ya Panadol. Hivyo, Masitsa waliamua kuwalipisha kidogo wateja na kununua dawa pole pole, watu wakaipenda zahanati, na wakaja wingi kutibiwa.
Aliongeza kuwa Machi 14 mwaka 1989, Serikali ilikabidhi jengo la zahanati, vifaa vyote na wafanyakazi kwa Kanisa.  Mwadhama Kardinali Rugambwa alimtuma Monsinyori Deogratius Mbiku (hayati), kupokea makabidhiano kwa niaba ya Jimbo.
Kwa mujibu wa Katibu huyo, mwaka 1997 ilitambuliwa rasmi kama Zahanati ya Huduma ya Uzazi ya Ukonga. Kwa upendo na heshima kwa Mwadhama Kardinali Rugambwa, mashirika ya Ulaya kwa namna ya pekee Misereor, waliendelea kusaidia zahanati hata baada ya Kardinali kuustaafu, kwa mfano mwaka 1996 Padri Stanislaus Kutajwaha alimsindikiza Kardinali Rugambwa kwenda Roma na Aachen Ujerumani, kule alishuhudia jitihada zake katika uzee wake alivyoendelea kupigania Hospitali ya Rugambwa, pale Ukonga.
Anasema, “Shughuli zake huko Aachen zilionyesha wazi kwamba hata katika uzee, tamaa yake Mwadhama ilikuwa bado ni kujaribu kwa uwezo wake wote, kuinua hali ya watu wake kiroho na kimwili.
Wakati huo pia ndoto yake ilikuwa kuboresha makao ya masista wa Shirika Jipya la Masista wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, na kupanua Hospitali ya Ukonga kwa ajili ya hudma za afya kwa wananchi.
Alisema pia kuwa mwaka 2001 kituo cha Ukonga kiliweza kutoa huduma za upasuaji, hasa kwa akinamama wajawazito na watoto. Kutoka mwaka 1999 hadi 2008, Shirika la Kiitaliani ola CUAMM likiongozwa na Dkt. Flavio Bobbio lilileta misaada mingi katika Mradi wa Uzazi Salama wakitoa vifaa, dawa, mafunzo, hata na usafiri wa gari ya wagonjwa.
Katibu huyo alisema kuwa kwa sasa wanamshukuru Mungu kwa kuweza kupata cheti rasmi cha kupandishwa ngazi ya Hospitali hiyo hadi kuwa Hospitali ya Mkoa kuanzia Januari 27 mwaka 2022.
“Tunaendelea taratibu katika maboresho mbalimbali ya kukidhi huduma zinazopaswa kutolewa katika Hospitali ya Mkoa. Basi ninyi kama wadau wakubwa wa Kanisa letu Jimboni Dar es Salaam, tunaendelea kuwaomba mtushike mkono ili tuweze kuikamilisha hii kazi iliyopo mbele yetu ya upanuzi wa Hospitali, ili wananchi wote waweze kupata huduma bora kutoka katika hospitali yetu hii,” alisema Katibu.
Aliwashukuru Walezi hao kwa kufika katika hospitali hiyo, huku akiendelea kuwaomba zaidi ufadhili wao ili waendelee kusonga mbele.

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya limepata Askofu mpya Msaidizi Mhashamu Askofu Mteule Godfrey Jackson Mwasekaga.
Baba Mtakatifu Fransisko alifanya uteuzi huo hivi karibuni ambapo kabla ya uteuzi huo, Askofu Msaidizi Mteule Godfrey Jackson Mwasekaga, alikuwa Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Fransisko wa Assisi, Mwanjelwa, Jimboni Mbeya, na pia alikuwa Makamu Askofu wa jimbo hilo.
Alisoma katika Seminari Kuu ya Mtakatifu Augustino, Peramiho, Jimbo kuu Katoliki la Songea, na hatimaye akapewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 14 Julai, 2005 kwa ajili ya Jimbo kuu la Mbeya. Hadi kuteuliwa kwake alikuwa ni Makamu Askofu Jimbo Kuu la Mbeya, Mkurugenzi wa Idara ya Katekesi Jimbo, na Mkurugenzi wa Kituo cha Katekesi na Paroko wa Mwanjelwa.
Askofu Msaidizi Mteule Godfrey Jackson Mwasekaga (pichani) alizaliwa Machi 17 mwaka 1976 huko Kyela, Mbeya. Alisoma katika Seminari Kuu ya Mtakatifu Augustino, Peramiho, Jimbo Kuu Katoliki la Songea, na hatimaye alipewa Daraja Takatifu ya Upadri Julai 14 mwaka 2005 kwa ajili ya Jimbo Kuu la Mbeya.
Tangu wakati huo kama Padri, aliteuliwa kuwa Paroko-usu Parokia ya Mtakatifu Claver, Mlowo, kati ya Mwaka 2005 hadi Mwaka 2008. Mkurugenzi wa Idara ya Katekesi Jimbo, na Mkurugenzi wa Kituo cha Katekesi kati ya Mwaka 2006 hadi mwaka 2008.
Alitumwa na Jimbo Kuu la Mbeya kujiendeleza kwa masomo katika Taalimungu katika Taasisi ya “Salesiano San Tommaso Messina” nchini Italia.
Baadaye akazama zaidi katika Taalimungu na kujipatia Shahada ya Uzamivu katika Taalimungu kutoka katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Wasalesian, kilichoko Roma, kati ya Mwaka 2008 hadi mwaka 2017.
Baada ya masomo yake, alirejea Jimboni Mbeya na kuteuliwa kuwa Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Petro Claver, Mlowo, kati ya Mwaka 2018-2019.
Kuanzia mwaka 2017 ni Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Katekesi Jimbo Kuu la Mbeya, Mkurugenzi wa Kituo cha Katekesi na Mratibu wa Liturujia ya Kanisa. Na pia kuanzia mwaka 2019, akateuliwa kuwa Makamu Askofu Jimbo Kuu la Mbeya, na Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Fransisko wa Assisi, Mwanjelwa, Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya.

Na Mwandishi wetu

Mfuko wa Self (Self-Microfinance Fund) unaomilikiwa na Serikali chini ya Wizara ya Fedha na Mipango, umefanikiwa kuikuza Sekta Ndogo ya Fedha na Wajasirimali kwa kutoa mikopo yenye thamaini ya Shilingi bilioni 324 katika kipidi cha kufikia Desemba 31 mwaka 2023.
Aidha, Self imejipanga kuhakikisha inasogeza zaidi huduma zake kwa kuongeza matawi nchi nzima kutoka 12 ya sasa hadi kufikia 20 ifikapo mwaka 2026, kwa kutengeneza mifumo mizuri ya ufuatiliaji na usimamizi wa fedha ili kuwafikia watu wengi, wakiwemo wakulima katika maeneo ya vijijini.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Self, Mudith Cheyo alisema hayo hivi karibuni katika Mkutano wake na Wahariri na Waandishi wa Vyombo yya Habari nchini, akielezea mafanikio, mipango mikakati na changamoto katika Taasisi hiyo ya fedha.
“Sisi kama Self, tangu tulipokabidhiwa mamlaka hii mwaka 2015 kuiinua sekta ndogo ya fedha, tumeweza kufanya kazi kubwa katika utoaji wa mikopo kwa wajasiriamali na Taasisi 200 nchi nzima …na katika hilo tumesaidia sana katika kuikuza na kuiendeeleza Sekta Ndogo ya Fedha nchini,” alisema Cheyo.
Cheyo alisema kuwa pamoja na mambo mengine, kwa sasa Self inaendelea na mikakati yake ya kujiimarisha zaidi, kwani tangu ilipopewa mtaji na serikali ili kuikuza na kiendeleza Sekta Ndogo ya Fedha kwa njia ya mikopo, wameiwezesha taasisi hiyo kujitegemea, na haijawahi kurudi serikalini kuomba tena mtaji.
Cheyo alifafanua kwamba Serikali iliwapatia mtaji wa Shilingi bilioni 56, na kwa usimamizi mzuri wa Taasisi hiyo, wameweza kutengeneza faida na sasa wamefikisha Shilingi bilioni 62, na imekuwa ikitoa gawio la Shilingi milioni 240 hadi milioni 250 kwa Serikali.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Biashara na Masoko wa Mfuko wa Self, Petro Mataba, alibainisha kuwa katika kutekeleza majukumu yake, Self ilitoa elimu ya fedha kwa wajasiriamali 1517, kuhusu namna ya kusimamia fedha na uendeshaji biashara.
Akizungumzia changamoto zinazoikabili Self, Mataba alisema kuwa wakopaji wengi wamekuwa wakishindwa kurejesha mikopo yao, lakini uongozi wa Taasisi hiyo umejipanga na kufanikisha kudhibiti mikopo chechefu kwa asilimia 10.
Aidha, alisema kuwa changamoto nyingine ni wakopaji kushindwa kutekeleza mipango waliyojiwekea, na hivyo kuelekeza fedha za mikopo katika mambo ambayo hawajakusudia, matokeo yake wanakwama kulipa madeni yao.
Kwa upande wa mipango ya baadaye ya Taasisi hiyo, Mataba alisema kuwa mfuko huo umejipanga kupanua wigo wake kwa kuwafikia watu wengine hadi maeneo ya vijijini, ili kuwawezesha watu wengi katika sekta ndogo ya fedha kupata mikopo ili kujikwamua kiuchumi.
Mpango mwingine ni kuongeza ufanisi kwa kutumia njia ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), ili kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi, na kutoa huduma endelevu kwa watu.

Na Mwandishi wetu

Mbunge wa Jimbo la Segerea Wilayani Ilala, Jijini Dar es Salaam, Bonnah Kamoli, amesema kuwa dhamira yake ni kuhakikisha barabara za Jimbo hilo zinapitika wakati wote, ikiwa ni pamoja na kujengwa kwa kiwango cha lami, zege au changarawe.
Kamoli alisema hayo katika hafla ya Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (Tanzania Rural and Urban Roads Agency: TARURA) Wilaya ya Ilala, kukabidhi mradi wa ujenzi wa barabara ya Zimbili-Kichangani ya kilomita 0.5 kwa Mkandarasi Kampuni ya SERC Constructions Co.Ltd, katika Kata ya Kinyerezi.

DAR ES SALAAM

Na Mathayo Kijazi

Waliokuwa wanafunzi katika Shule za Seminari nchini, wamekutana na kutafakari Neno la Mungu katika mafungo yaliyoandaliwa na Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, huku wakiaswa kutambua kwamba hata Mtu anapojiona ni Mtakatifu kiasi gani, lakini bado mbele za Mungu, ni mdhambi, kwani Mungu ndiye Mtakatifu pekee.
Kauli hiyo ilitolewa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi katika Mafungo ya ‘Former Seminarians’, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, yaliyofanyika katika Kituo cha Hija – Pugu, jimboni humo.
“Mbele ya Mungu hata kama uko Mtakatifu kiasi gani, mbele ya Mungu ambaye ndiye utakatifu wote, ndiye ukamilifu wote, ni lazima ujitambue kwamba uko mdhambi, kwa kuwa Mungu tu ndiye peke yake Mtakatifu, Mungu tu ndiye peke yake mwenye haki, na Mungu tu ndiye peke yake asiye na lawama yoyote. Sisi wote tumeshaguswa na dhambi,” alisema Askofu Mkuu Ruwa’ichi.
Aidha, Askofu Mkuu aliwasihi Waseminari hao kutokuona haya kumwomba Mungu toba, au kujikabidha mbele za Mungu na kuomba huruma yake, kwani yeye ndiye anayewastahilisha, anayewatakasa na kuwawezesha.
Aliwataka kutokuogopa kufuata mfano wa mtoza ushuru, ambaye kwa kujitazama mapungufu yake, alisimama mbali na kujipiga kifua, huku akiomba toba.
Aliwaonya kuacha kujitokeza mbele za Mungu na kumkumbusha kwamba wao ni wenye haki kutokana na mambo wanayoyafanya katika maisha yao.
“Yaani mtego wa kufanya mazoezi fulani ya kiroho au ya kidini, na kujidhani sasa wamemuweka Mungu sawa, na kujidhani kwamba sasa sisi ni wenye haki, ndivyo alivyofanya yule Mfarisayo aliyeenda mbele ya Altare akaanza kumkumbusha Mungu jinsi yeye Farisayo alivyo na fadhila.
“Niwakumbushe tu kidogo, alimwambia Mungu, tazama mimi nilivyo mwenye haki, nafanya kadha wa kadha. Siko mzinzi, siko mwizi, siko mwongo, siko mvivu…… Yaani ni kama Mungu anatangaziwa hizo fadhila kusudi iweje. Kusudi mategemeo ni kwamba Mungu atampigapiga mabegani, na kumwambia ‘well done’. Lakini Mungu siyo wa hivyo, Mungu harubuniwi,” alisema Askofu Ruwa’ichi.
Alisema kuwa malezi waliyoyapata Waseminari hao pindi wakiwa Seminarini, yamewaunda na kuwapa fursa ya kupambanua na kuitikia wito wa Mungu.
Askofu Mkuu alisema kuwa kijana mdogo katika kukua kwake anapojitambua, asaidiwe ili akue katika mtindo ambao unamjenga kiutu, kiroho, na unamsababisha afanye maamuzi sahihi.
Aliwataka wale walioondolewa Seminarini ambao bado wana majeraha, kuondoa majeraha hayo, ili waamue kujikabidhi kwa Mungu na kuomba neema ya kukua katika njia zake, pamoja na kusamehe.
Pia, alisema kuwa mtu asiyesamehe, anaendelea kubeba mizigo, hivyo akawataka walioondolewa Seminarini, kuacha kujibebesha mizigo ya hasira, na ya kutaka kulipiza kisasi.
Kwa upande wake Mkuu wa Majeshi Mstaafu (CDF), Venance Mabeyo, akizungumza kwa niaba ya Waseminari wa zamani, alisema kuwa hiyo ni fursa kubwa kukutana katika Adhimisho hilo, kwani wengine hawafahamiani kutokana na wingi wao.
Mabeyo aliwasihi Waseminari wenzake wa zamani kuwa watu wa kusameheana pale wanapokoseana, huku wakiepuka kuwa na jazba, akisema kwamba yeyote mwenye jazba, neno ‘msamaha’ halikai katika msamiati wake.
Alisema pia kuwa kila mmoja anatakiwa kujitafakari na kujiuliza, je, anafanya mara ngapi matendo ya huruma? Huku akisisitiza kuishi vizuri na watu wa hulka tofauti tofauti katika jamii zao.

DAR ES SALAAM

Na Mathayo Kijazi

Utoaji wa huduma za Kijamii zikiwemo Elimu, Afya, na huduma zingine katika kustawisha ustawi na maendeleo ya mwanadamu, ni njia mojawapo za uinjilishaji katika kumtangaza Yesu Kristo.
Hayo yalisemwa hivi karibuni na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Dominika ya Nne ya Kwaresma, iliyokwenda sanjari na kuweka jiwe la msingi katika Shule ya Parokia ya Bikira Maria Mama wa Rozari Takatifu - Makongo Juu, jijini Dar es Salaam.
“Hamkuishia hapo, mmepania kujikita katika huduma za kijamii. Huduma za Kijamii ni namna mojawapo ya uinjilishaji. Tunainjilisha kwa kutoa elimu, tunainjilisha kwa kutoa huduma za afya, tunainjilisha kwa kutoa huduma nyingine zozote zinazochangia ustawi na maendeleo ya mwanadamu;
“Basi, kwa kuwa na mikakati hiyo, nawatambua kama Parokia hai. Muendelee kuwa na umoja, muendelee kuwa na mwamko wa kichungaji, muendelee kuinjilisha na kumtangaza Kristo kwa hali na mali. Leo mnapoweka jiwe la msingi la shule ya Parokia hii, nawaombea shughuli hii iendelee vizuri ili ipate kufikia upeo unaotakiwa,” alisema Askofu Ruwa’ichi.
Awali katika homilia yake, Askofu Mkuu Ruwa’ichi aliwataka Wakristo kusikia furaha kutambulika kama watoto wa Mungu, na kama watu waliokombolewa katika maisha yao.
Aliwasihi kuendelea kumwomba Mungu awazidshie neema yake ili wazidi kukua katika fadhila, katika imani, na katika ushuhuda wa Kikristo.
Aidha, aliwaalika Waamini kutambua kwamba wao siyo Wakristo kwa sababu ya mastahili yao wala kutokana na wema wao, bali wako Wakristo kwa sababu Mungu anawapenda na kuwahurumia.
“Mungu alilichagua Taifa la Israel liwe Taifa lake Takatifu, siyo kwa sababu walikuwa Taifa kubwa kuliko Mataifa yote, na wala siyo kwa sababu walikuwa wazuri kuliko watu wote, bali Mungu aliwateua kutokana na huruma na upendo wake,” alisema Askofu Mkuu, na kuongeza,
“Na ukweli huo unaweza kuusema pia kuhusu sisi Wakristo. Sisi tuko Wakristo, siyo kwa sababu ya mastahili yetu, tuko Wakristo, siyo kwa sababu ya wema wetu, tuko Wakristo kwa sababu Mungu anatupenda.”
Kwa upande wake Paroko wa Parokia hiyo, Padri Joseph Massenge, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Tumaini Media, alimshukuru Askofu Mkuu Ruwa’ichi kwa kufika parokiani hapo na kudhimisha Misa hiyo Takatifu, pamoja na kuweka jiwe la msingi la shule ya Parokia hiyo.
Padri Massenge alisema kuwa lengo la kujenga shule hiyo, ni kuwapunguzia changamoto wazazi na walezi ambao mara kwa mara hutumia muda wao kuwapeleka watoto wao katika shule za mbali na eneo hilo.
“Shule hii tungependa iwe na mtindo wa shule kama ile ya St. Joseph kule mjini, kwa sababu watu wengi kutoka huku Makongo wanaamka usiku usiku kuwapeleka watoto wao kule St. Joseph,” alisema Padri Massenge.
Aidha, Padri Massenge alitumia nafasi hiyo kuwaomba Waamini kuchangia ujenzi wa shule hiyo, ili baadaye wapewe kipaumbele pindi wanapokwenda kuandikisha watoto wao kujiunga na shule hiyo.
“Lakini niwakumbushe ninyi vijana mnaozaa, nawaambia tena, hata kama Baba Askofu atanihamisha, nitarudi kuja kukagua siku ya kuandikisha watoto, kama majina yako hayapo kwenye vitabu vya kuchangia shule, kupata nafasi utapata tabu sana. Kwa hiyo mjitahidi mchangie,” alisema Padri Massenge.
Vile vile, Padri huyo alithibitisha kwamba shule hiyo haitakuwa na gharama kubwa katika utoaji wa huduma ya elimu, bali itakwenda katika mfumo wa kawaida, kwani ni Waamini wenyewe ndio wamechangia ujenzi huo.