DAR ES SALAAM
Na Mathayo Kijazi
Parokia Teule tatu za Mbweni Teta, Mbopo, na Nyakasangwe Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam zimepandishwa hadhi kuwa Parokia Kamili na kulifanya jimbo kufikisha Parokia162, kutoka 159.
Aidha, Vigango vitatu vya Nyantila, Yongwe, na Minazini, navyo vimepandishwa hadhi kuwa Parokia Teule.
Mabadiliko hayo yalitangazwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi katika Adhimisho la Misa takatifu ya kupadiri Mafuta Matakatifu iliyoadhimishwa katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu, jijini Dar es Salaam.
Katika mabadiliko hayo, Askofu Mkuu Ruwa’ichi alimteua Padri Cosmas Kangwele kuwa Paroko wa Parokia mpya ya Mbweni Teta, Padri Joseph Luena kuwa Paroko wa Parokia mpya ya Mbopo, na Padri Joseph Nkusi kuwa Paroko wa Parokia mpya ya Nyakasangwe.
Aidha, Askofu Mkuu alimhamisha kituo cha kazi Padri John Bosco Mligo aliyekwua akihudumu Parokia ya Mbagala Zakhem, kwenda kufanya Utume Parokia ya Pande Msakuzi, kama Paroko Msaidizi.
Wengine ni Padri Thomas Njuwe aliyeteuliwa kuwa Paroko wa Parokia ya Mikoroshoni, na kumhamisha Padri Canisius Hall aliyekuwa Paroko wa Parokia ya Mikoroshoni, kwenda kuwa Paroko Msaidizi Parokia ya Makongo Juu.
Askofu Ruwa’ichi pia alimteua Padri Israel Slaa anakwenda kuwa Paroko Msaidizi wa Parokia ya Mtakatifu Don Bosco, Kibaha, mkoani Pwani.
Aenzi mpango wa Papa kutunza mazingira:
Katika Adhimisho hilo la Misa Takatifu ya kubariki Mafuta Matakatifu, Askofu Mkuu Ruwa’ichi alitumia nafasi hiyo kuenzi mpango wa Baba Mtakatifu wa kutunza mazingira kwa kupanda miti wa ‘Laudato Si’.
Akizungumzia mpango huo wa utunzaji wa mazingira kwa kuwakabidhi Madekano miche ya miti ili wakaioteshe kwenye Dekania zao, kwani kwa kufanya hivyo, mazingira yatakuwa bora.
‘Mapadri teteeni waamini ‘wasitekwe’
Awali katika homilia yake, Askofu Mkuu Ruwa’ichi aliwasihi Mapadri kuwapatia Waamini mafundisho sahihi, ili wasirubuniwe na wababaishaji, hasa wanaojiita wapakwa mafuta.
“Naomba hapo mnivumilie kidogo niweke msisitizo, hizi ni zama zenye utata, hizi ni zama za wababaishaji. Wapo watu mbalimbali, wanajitokeza na kujitangaza kwamba wao ni wapakwa mafuta, kwa hiyo wanajipanga kugawia na kupaka watu mafuta. Naomba niseme kwa Wakristo wote, muwe macho na watu wa namna hiyo, maana wanawarubuni tu, hawana mafuta ya kuwapaka,”
Alibainisha kuwa licha ya kutoa mafundisho sahihi, pia Mapadri hao wanatakiwa kuhakikisha maisha yao inakuwa vielelezo bayana kwa Wakristo ili wafuate nyayo zao, wamjue, wamfuate na kumshuhudia kwa dhati Kristo.
Ataka Mapadri kuepa kuburuzwa:
Askofu Mkuu Ruwa’ichi alisema kuwa Mapadri nao wanatakiwa kuepa kishawishi cha kuburuzwa na wababaishaji, akiwasihi kutambua kwamba wanapotoa kitu chochote cha baraka, kitolewe kwa msingi na uwelewa wa mafundisho sahihi.
Kwa mujibu wa Askofu Ruwa’ichi kitendo cha baadhi ya watu wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu, kuunga mstari kwenda kukomunika wakati wao si Wakristo, ni cha kusikitisha.
Akumbusha matumizi ya Mafuta:
Askofu Mkuu Ruwa’ichi alisema kuwa Mafuta ya Krisma kwa uelewa sahihi wa Kikatoliki, yanatumika katika Sakramenti ya Kipaimara na katika Sakramenti ya Daraja Takatifu, akionya kwamba hayo si mafuta yanayowekwa kiholela, bali hutumika kwa malengo sahihi na kwa uelewa sahihi.
Aliwashukuru Mapadri wote wa Jimbo hilo walioshiriki katika Adhimisho la Misa Takatifu, akisema kwamba kuwepo kwao kunadhihirisha ushirikiano wao na Askofu katika kulihudumia, kuliongoza na kulitakatifuza Kanisa la Mungu.
Kwa upande wake Askofu Msaidizi wa Jimbo hilo, Mhashamu Stephano Musomba, alisema kuwa Mei 16 mwaka huu, ni Jubilei ya Miaka 25 ya Uaskofu wa Askofu Mkuu Ruwa’ichi, hivyo akizitaka Parokia zote kuwasilisha michango yao ifikapo Aprili 30 mwaka huu, ili mipango ifanyike mapema.
Hata hivyo, alisema kwamba kutakuwa na Kongamano la Ekaristi Takatifu Kitaifa ambalo litafanyika katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, ambalo safari hii ni mwenyeji.