Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

Paroko wa Parokia ya Yohane wa Mungu – Yombo Vituka, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Patrick Bwakila akibariki matoleo wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Dominika, iliyokwenda sanjari na kuwapatia watoto Sakramenti ya Ekaristi Takatifu.

DAR ES SALAAM

Na Joyce Sudi

Kitunguu saumu ni moja ya kiungo chenye ufanisi  mkubwa mwilini katika kuboresha afya ya mwili, Kiungo hiki huwa ni sehemu ya vyakula mbalimbali tunavyokula kila siku, vikiwemo vile vinavyoliwa vibichi kama vile kachumbari na saladi, pamoja na vyakula vilivyookwa au kuchemshwa.
Kwa mujibu wa Taasisi ya Chakula na Lishe Nchini Tanazania {TFN}, kitunguu saumu kina viondoa sumu {antioxidant} ambazo huondoa alkali huru {freeradicals} katika mwili, na hivyo kusaidia kuzuia uharibifu wa sumu hizo mwilini, na pia kina vitamini na madini mengi kwa afya ya mwili, ambayo ni madini ya manganese, calcium, phosphorus, selenium na vitamin B6 na C.
Kitunguu saumu ni moja wapo ya viungo ambavyo mara nyingi hutumika kuongeza ladha katika chakula, ambapo vipo vitunguu saumu vya rangi nyeupe ambavyo huwa na tumba kubwa chache, lakini vipo vyenye rangi ya zambarau au pinki, ambavyo huwa na tumba ndogo na nyingi, ingawa vitunguu hivyo vyote vina ubora sawa.
Licha ya kitunguu saumu kuwa maarufu kutumika kama kiungo, lakini pia hufaa kutumika kusaidia katika matatizo mbalimbali ya kiafya, kama vile kuzuia maambukizi yatokanayo na bakteria, baadhi ya virusi na fangasi, hasa katika utumbo, mapafu na sehemu za ukeni.
Vilevile husaidia katika uyeyushaji wa chakula, kuzuia kuhara na maambukizi yatokanayo na fangasi kwenye kinywa kutokana na viambata vinavyopatikana kwenye vitunguu saumu ambavyo ni; Allicin, Vitamini C, Vitamin B6 na Manganese.
Nini husababisha harufu kali mdomoni baada ya kula kitunguu saumu?
Watu wengi wamekuwa wakisumbuliwa na swali hili, kwamba pamoja na virutubisho na madini muhimu yaliyopo kwenye kitunguu saumu, lakini inakuwa ngumu kutafuna kwa kuhofia harufu kali.
Ukweli ni kwamba pale unapotafuna kitunguu saumu,kemikali za kibaiolojia zilizopo kwenye mfumo wa chakula kwa ajili ya kuvunjwa vunjwa kwa chakula kiweze  kufyonzwa vizuri, hubadilisha kiambata kilichopo kwenye kiungo hicho kiitwacho Allin kuwa Allicin na kisha kuvunjwa zaidi kuwa Ally Methyl sulfide, na hivyo kusababisha harufu kali  ambapo njia  rahisi ya kuepusha harufu hii, ni kunywa maziwa (fresh)yasiyoganda ya ng’ombe.
Taasisi ya Chakula na Lishe Nchini Tanzania {TFN}, imetuandalia  namna ya  kuandaa kitunguu saumu kwa ajili ya kusaidia kutuliza vidonda vya kooni kwa watu wenye maambukizi ya  Virusi vya Ukimwi {H.I.V}.
Mahitaji:
Kitunguu saumu tumba 4, maji kikombe kimoja, na sukari au asali.
Namna ya kuandaa:
i.Menya  maganda kwa kisu na katakata kitunguu saumu.
ii. Tia  kwenye maji yanayochemka, acha kichemke kwa dakika 10.
iii. Ipua, funika na acha ipoe, Kisha ongeza asali au sukari kwa ajili ya ladha.
Matumizi:
Kunywa kikombe kimoja kutwa mara tatu.
Pia kitunguu saumu kinaweza kutumika kama dawa ya kikohozi
Namna ya kuandaa:
i. Ponda kitunguu saumu kilichomenywa maganda .
ii. Weka kwenye kijiko cha chai, chukua kijiko cha chai cha asali au sukari.
Tumia mara mbili kwa siku kwa kikohozi.
Angalizo:
Matumizi ya vitunguu saumu yanaweza kuingiliana na ufanyaji kazi wa dawa mbalimbali za hospital, hivyo hakikisha unamuuliza daktari wako kama hujaanza kutumia kitunguu saumu kama dawa. Pia kwa wale wenye presha usitumie, kwanza pata ushauri wa daktari.
Dawa hizo ni kama Isoniazid ambazo zinatumika kutibu maradhi ya kifua kikuu, cyclosporine, dawa hizi hutumika kwa waliopandikizwa kiungo mfano figo, Dawa za H.I.V. ambapo  kitunguu saumu kinaingiliana na ufyonzaji wa dawa hizi, na hivyo kupelekea dawa kutokufanya kazi.
Pia, Nonsteroidal anti-inflamatory drugs {NSAIDs], dawa hizi ni kama ibrufen, na Naproxen ambazo zikitumiwa pamoja na kitunguu saumu, huongeza kuvuja kwa damu.

Katika safu hii ya Chimba Chimba Historia ya Kanisa wiki iliyopita, tuliwaletea historia ya kuanza kwa Uinjilishaji nchini Zambia.  Leo tunaendelea na Uinjilishaji nchini humo, hususan Kanisa katika Zambia huru na kuanza kwa uinjilishaji nchini Malawi. Sasa endelea…

Mwaka 1923, Kampuni ya Cecil Rhodes iliachia utawala wake Zimbabwe na Zambia na Nchi hizi zikawekwa moja kwa moja chini ya ulinzi wa Serikali ya Uingereza. Mwaka 1953 Zimbabwe, Zambia na Malawi ziliunganishwa katika ‘Muungano wa Rhodesia na Nyasaland’.

Muungano huu ulipingwa sana na Waafrika wa Zambia na Malawi. Upinzani ulizidi sana mwaka 1960 na 1961 ukiongozwa na Harry Mwaanga Nkumbula wa African National Congress (ANC), na baadaye Kenneth Kaunda aambaye aliunda chama chake cha United National Independent Party (UNIP).

Kama sehemu nyingine, Waprotestanti wa Presbiteri na Methodisti ndio waliongoza katika kuchochea siasa ya kudai Uhuru. Kwa namna ya pekee, Kanisa la Methodisti la Kiafrika la Kiaskofu lililotokea Afrika ya Kusini na Zimbawe na mhubiri wake mkuu akiwa John Lester Membe, liliongoza.

Membe alihubiri hata katika mikutano ya chama cha siasa cha ANC cha Zambia. Hata Kenneth Kaunda kabla ya kuingia siasa, alijiunga na Kanisa hilo na kusaidia kama mhubiri na kiongozi wa Kwaya.

Baada ya uchaguzi wa mwaka 1962, vyama hivyo viwili vya ANC na UNIP viliungana katika Bunge, na kwa wingi wao wa kura, vikapinga muungano na kuuvunja. Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1963, chama cha Kenneth Kaunda cha UNIP kilishinda na kuunda Serikali ya Zambia huru (1963-1991).

Katika miaka iliyofuata, Kaunda alishirikiana sana na Mwalimu Nyerere wa Tanzania kupigania Uhuru wa Afrika, hasa sehemu ya Kusini mwa Afrika, yaani Rhodesia, Afrika ya Kusini na Namibia, zikiwa chini ya ubaguzi wa rangi wa Makaburu; na Angola na Msumbiji zikiwa chini ya ukoloni wa Wareno.

Katika uhuru wa kuabudu na shughuli za kidini, Serikali zote baada ya Uhuru, hazikuwa na shida. Dosari ilikuwa mwaka 1962 ambapo Kaunda ilibidi apigane vita na dhehebu la Lenshina lililohubiri watu wasishiriki katika siasa na Serikali, na wakataka kufanya serikali yao ndani ya Nchi.

Katika vita hivyo, zaidi ya watu elfu moja waliuawa. Baadaye hata wafuasi wa dhehebu la Mashahidi wa Yehova wa Watchtower, walishambuliwa lakini siyo rasmi. Serikali ya Frederick Chiluba (1991-2001) aliyemshinda Kaunda katika uchaguzi wa mwaka 1991, akiwa mlokole, kidini alijaribu kuifanya Zambia iwe rasmi nchi ya Kikristo, lakini alipingwa na Viongozi wa Dini.

Vile vile Chiluba alifadhili na kuhamasisha madhehebu ya kilokole ya Kipentekoste. Chiluba alirithiwa na Levy Mwanawasa. Wakati huu, Kanisa Zambia liko msitari wa mbele katika kupigania haki za binadamu, na kuhamasisha watu katika siasa ya demokrasia shirikishi.

Waamini wengi wa Kanisa Katoliki mwanzoni walikuwa Kaskazini, katika sehemu ya Wamisionari wa Afrika (zamani White Fathers) au kabila la Wabemba. Mwaka 1950, walikuwa zaidi ya laki mbli wakati Kusini kwa Wajezuiti na Wafransiskani, Waamini walikuwa hawafiki elfu sitini.

Mwaka 1990, Kaskazini ilikuwa na Waamini kama laki tisa, ambapo Kusini walikaribia milioni moja na nusu. Hivyo uwingi wa Waamini ulikuwa umehamia Kusini, lakini hata hivyo, kati yao wengi walikuwa Wabemba waliohamia Kusini, hasa katika machimbo.

Mwaka 2005 kati ya wakazi 11,600,000, Wakristo walikuwa asilimia 75, ingawa kati ya hao Madhehebu mengi yalikuwa ya Kipentekoste yaliyoshamiri hasa wakati wa Chiluba, ambayo huchanganya Ukristo na tamaduni za Kiafrika.

Wakatoliki walikuwa asilimia 26 ya wakazi wote nchini humo, ingawa Wakatoliki si wengi sana kwa hesabu, nguvu zao za ushawishi wa watu ni kubwa sana.

Kanisa nchini Malawi
Nchi ya Malawi au Nyasaland, kama ilivyoitwa na wakoloni, wakifuatia jina ambalo Livingstone alilipa Ziwa la Nyasa, inakaliwa na makabila matatu. Wakazi asilia ni Wachewa, na hadi sasa ndilo kabila lenye watu wengi, na lugha yao ni lugha ya taifa, pamoja na Kiingereza.

Wachewa katika karne ya 15, waliongoza ufalme wa Maravi. Wakiwa na Makao yao Makuu Kusini ya Ziwa Nyasa, walishamiri na walitanuka hadi sehemu za Msumbiji na Zambia.
 
Ufalme huu uliangushwa na makundi mawili, la kwanza ni lile la Wangoni waliokimbia kutokana na mashambulizi ya Wazulu, wakiongozwa na Shaka. Wangoni kwa ukatili, waliteka falme walizokutana nazo njiani.

Kundi la pili lilikuwa la Wayao, ambao walishirikiana na Waarabu kwa kuteka watu na kuwauza utumwani. Wayao kwa sababu ya kushirikiana na Waarabu walishashika dini ya Kiislamu kama dini yao ya jadi.

Walianzisha vituo vya watumwa kwenye mwambao wa Ziwa Nyasa, kituo kikubwa kikiwa Nkhotakota, ambacho kiliweza kusafirisha watumwa kati ya 5,000 hadi 20,000 kwa mwaka. Huu ndio unyama aliouona Livingstone na kuomba msaada wa ulimwengu kwa wenye mapenzi mema. Ni juhudi za Dkt. David Livingstone, Wamisionari wengi walimiminika Afrika ya Mashariki na Kati.

DAR ES SALAAAM

Na Dk. Felician B. Kilahama

Mungu Mwenyezi alituumba binadamu kwa ‘sura na mfano wake’ (Kitabu cha Mwanzo, 1:26); akatuweka duniani na kutupa madaraka ya kumiliki na kutawala vyote alivyoviumba.
Akisema: binadamu “wakatawale samaki baharini, ndege angani, wanyama, nchi yote vile vile, kila kiumbe kitambaacho juu ya nchi.” Vile vile, Mungu akahitimisha uumbaji akiwaagiza mwanamume na mwanamke: “zaeni mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuimiliki”.
Tangu kuumbwa Adamu na Eva/Hawa, ni miaka mingi imepita. Hata hivyo, takwimu zinaashiria kuongezeka idadi ya watu duniani, ikiwa takriban bilioni nane (8), hii leo.
Hiyo ni ishara kuwa dunia inazidi kujaa watu wakati mataifa kama ‘China’ na ‘India’ yakiongoza kwa takriban asilimia 40 ya idadi ya watu wote. Tanzania yenye ardhi kubwa (hekta 94.55 milioni), kwa takwimu za 2022, kuna watu 61,741,120.
Kwa uwiano wa ukubwa wa nchi, bado tunatakiwa kuzaa na kuijaza nchi. Tunatumiaje ‘vipawa’ tulivyopewa na Mungu Mwenyezi? Vijana vipaumbele vyenu ni nini kama siyo kwanza kuwa baba hodari wa familia bora na yenye kumcha Mungu. Je, vijana wetu wamekengeushwa na nini: utandawazi, mifumo-dijitali na kuiga yasiyofaa, au ni mifumo kijamii na kiutawala?
Hakuna shaka mataifa yaliyoendelea hayajali chochote wanafanya kulingana na matakwa yao, kwenda kinyume na agizo la Mungu wakichochea maovu, mfano, kuhamasisha ndoa kati ya mwanaume na mwanaume (ushoga); mwanamke na mwanamke (ulezibiani), ikiwemo kutunga Sheria ‘kuharibu na/au kutoa mimba, na kuchochea wanawake wasipate ujauzito’.
Masuala hayo ni machukizo kwa Mungu aliyetuumba, akatujalia neema tuzae na kuongezeka. Wakati nikiwa mdogo, nilikuwa nasikia watu vijijini wakisema, “kuzaa watoto wengi ni baraka” familia zilikuwa zinafurahia kuzaa watoto na kuishi kwa uelewano mkubwa kama jamii moja. Nyakati hizi hali imekuwa tofauti kiasi cha ‘vijana’ kuoa na kuzaa watoto ni dhiki kubwa au kama ni laana, wakati ni baraka/zawadi kwa familia.
Maisha ya babu/bibi zetu yalikuwa yameegamia kwenye misingi/mifumo ya kijadi, kiutamaduni wakiabudu miungu mingine (ingawa walifahamu yupo Mungu Muumbaji. Mtazamo huo hautofautiani na ilivyoandikwa katika Matendo ya Mitume kwamba Mtume Paulo wakati akipita huku na huko akiwa ‘Athene’ akaona ‘Madhabahu’ iliyoandikwa: “Kwa Mungu Asiyejulikana”.
Ikawa baada ya kuyaona hayo, akawahubiria habari njema kuhusu huyo Mungu wanayemwabudu bila kumjua (Mdo, 17:23). Hivyo na wahenga wengi wa kale yalifanya hivyo hadi Injili ilipowafikia, takribani miaka 100 iliyopita.
Tukumbuke kuwa maisha yetu yamejengwa kwenye misingi ya mifumo ya kiroho ,ambayo Mungu aliiweka kimpangilio. Hivyo vijana wetu wanapaswa kufahamu kuwa kukiuka kuyatekeleza maagizo ya Mungu; mafanikio yatakuwa haba kwa kukosa maarifa yatokayo kwa Mungu.
Kilichonisukuma kuyasema hayo ni hali ya vijana wetu hususan wa kiume; kujisahau kuwa wao ni wanaume wanaotegemewa kujenga familia zilizo bora na endelevu. Nimekuwa nikisia msemo “dunia inawayawaya” ukimaanisha binadamu kukosa utulivu/umakini kwa kuhangaika huku na huko mpaka kupayapaya bila kujua mustakabali wa maisha kwa ujumla.
Ukitafakari hali hiyo kwa umakini mkubwa, utagundua kuwa hali ya sasa tunayoishuhudia kwa vijana wetu wa kiume, hakika ni matokeo ya kuhangaika kidunia zaidi, kuliko kusimama imara kwa msingi na maagizo ya Mungu Mwenyezi.
Moja ya athari kubwa kwa vijana Tanzania; ni ‘unywaji pombe’ uliokithiri. Kawaida Watanzania wengi vijijini/mijini wapo wanaokunywa pombe aina mbalimbali. Wakati nikiwa kijana kabla na baada ya kuanza shule; nilikuwa naona wanaokunywa pombe walikuwa watu wazima (wenye familia), hakuna kijana aliyekuwa hajaoa angeweza kuruhusiwa kujumuika nao.
Hata kama angekuwa ameoa, lakini bado hajawa na uzoefu wa kutosha kimaisha, haikuwa rahisi ajumuike na watu wazima. Mifumo kijadi au kimila ilikuwa imezuia vijana kutojitosa kwenye unywaji pombe bila ya kujijengea msingi imara wa kuweza kuyamudu maisha yake na familia.
Nyakati hizi maisha ni kidijitali, kisiasa, kisaikolojia, kiteknolojia, kimaendeleo hadi kusema kila mtu yuko huru kufanya anavyotaka ili mradi amefikisha umri wa miaka 18 au zaidi. Hali hiyo inakinzana na Sheria, Kanuni pamoja na Mifumo ya Kiroho aliyoiweka Mungu. Kadhalika, Serikali kwa dhamira ya kupata mapato zaidi, ikapunguza bei ya pombe.
Kimsingi, mapato ya Serikali yanapoongezeka, kwa namna moja au nyingine, tunatarajia huduma za kijamii kuboreshwa na kuimarisha miundombinu kwa maendeleo endelevu. Kuna pombe ambazo vijana wanachangamkia, mfano, “sungura” na “konyagi.” kadhalika, usambazaji pombe kwa kutumia vifungashio vyenye ujazo mdogo mdogo, unahamasisha vijana wengi wanywe pombe zaidi kwa bei poa.
Kuwepo vyanzo vya mapato kwa Serikali hasa ambavyo haviumizi walipa kodi na wananchi kwa ujumla ni jambo jema; lakini tunapotafakari suala la unywaji pombe ee-vijana wengi wanaathirika sana kwa kiwango cha taifa kuelekea pabaya.  Mbali na pombe, changamoto nyingine ni “dawa za kulevya”; zikiwa kama ‘pacha’ wa pombe, kwa kutumiwa na vijana wengi.
Uzoefu unaonyesha kuwa kijana akishazoea dawa zinazolewesha, kuacha inakuwa kizaazaa. Kuna wakati Serikali ilijitahidi kudhibiti kwa kiasi kukubwa, matumizi ya dawa zinazolewesha kwa kuhakikisha haziingizwi nchi hovyo.
Hata hivyo, “operesheni iliyofanywa na Mamlaka ya Kuzuia na Kudhibiti Dawa za kulevya; iliyofanyika kati ya Agosti 24 na Septemba 2, 2024”; imedhihirisha kuwa sasa-upo udhaifu mkubwa katika mifumo husika ya kudhibiti uagizaji na uingizaji dawa zinazolewesha. Ripoti iliyotolewa na Mamlaka Septemba 10, ilionyesha kuwa kiasi kikubwa cha dawa hizo zilizoingizwa nchini, zikamatiwa Manispaa za Kinondoni na Ubungo kwa kuwanasa watuhumiwa kadhaa.
Swali linabaki. Je, dawa hizo zimepitia wapi bila kugundulika mpaka zikawa mitaani kiasi-hicho? Kadhalika, matumizi ya “bangi” (Cannabis sativa) pia yamekuwa yakiongezeka kila kukicha. Je, tunakwama wapi hadi taifa kushindwa kudhibiti matumizi ya dawa zinazolevya?
Tujitathimini kwa kina miaka michache ijayo nguvukazi nchini itakuwa ya namna gani Iwapo vijana wengi wa umri kati ya miaka 20 hadi 40 inakuwa katika hali hii isiyoridhisha, na huenda vijana wanaoinukia nao wakatumbukia kwenye janga hili. Nini hatima ya Tanzania? Kwanza, viongozi wajao watakuwa wa namna gani, wenye mwelekeo gani je, watakuwa na maarifa gani?
Je, Vijana wataishi maisha ya namna gani kama mwelekeo wao kwa sasa ni kunywa/kulewa kupindukia? Agosti, 2024 mtaa mmoja Jijini-Kati Dar-es-Salaam, karibu na Posta ya Zamani, niliona vijana wanne wamejibanza mahali akiwepo binti mmoja.
Kwa kuwa nilikwa nikitembea kwa miguu, nikapunguza mwenda taratibu kuona nini kinachoendelea. Nilichokishuhudia walikuwa wakinywa, lakini kwa kutunia chupa moja wakipokezana. Vile vile, walikuwa wanavuta kitu kama sigara pia kwa kupokezana: niliduwaa kwa hali niliyoiona bila kuwakaribia.
Mbele yangu alikuwa mama, mtu-mzima akielekea nilikokuwa natoka; baada ya kusalimiana. Nikamuuliza hiyo ni ishara gani kwa vijana wetu. Mama alisema hiyo ndiyo ‘hali halisi’ kwa vijana wa Tanzania. Tukaishia kusema: “Mwenyezi Mungu uwarehemu vijana hawa na wengine wa aina hiyo, maana wanaangamia kwa kukosa maarifa (akili zao zimepinda)”.
Tutamwomba Mungu, lakini kwa utashi aliotupa kuweza kufanya uchaguzi sahihi, mathalani, ufanye nini, ule nini, unywe nini, uvaeje au uishi maisha gani! Hivyo, inabidi tuwajibike kwa maisha tunayoishi. Dunia moja, ‘binadamu wote sawa’ lakini tunatofautiana katika uwezo wa kufanya maamuzi sahihi kuishi, vizuri bila kukengeuka hadi kupoteza ‘afya ya akili’ zetu.
Vijana kutumbukia kwenye unvwaji pombe na matumizi dawa zinazolevya, Mungu hahusiki hata kidogo, maana Mungu anatupenda na anatuwazia mema, pia huzibariki kazi za mikono yetu. Kadhalika, ili tubarikiwe, lazima ‘vigezo na masharti’kuzingatiwa ipasvyo. Kinyume cha hapo, ni laana mpaka huruma ya Mungu ipatikane kupitia toba ya kweli; pia kwa kufunga vile vile kuomba bila kukata-tamaa.
Ombi langu kwa Serikali, unywaji ‘pombe kupindukia’ ikiwemo ‘dawa-zinazolevya,’ hatua madhubuti zichukuliwe kwa kupandisha bei za ‘vileo’ vyote, pia kuhakikisha dawa-zinazolevya, zinadhibitiwa kwa hali ya juu sana kwa dhamira njema ili kuokoa nguvukazi ya taifa.
Vile vile, atakaye thibitishwa Kisheria kufanya biashara haramu, adhabukali zichukue mkondo wake bila kuoneana haya wala huruma, ili tusiendelee kuliangamiza taifa kwa maslahi binafsi. Taifa bora linahitaji ‘vijana’ imara, wenye nguvu, afya na akili timamu pamoja na maarifa ya kimbingu.
Kumbuka ‘kumcha Mungu’ ndiyo chanzo cha maarifa, na taifa lenye hofu ya Mungu hutenda haki kwa wote na kuuchukia ‘uovu’ kwa sababu ‘uovu’ ni janga kwa taifa, husababisha watu walaaniwe. Hivyo, tuwe makini tujiepushe na hali hiyo.

Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam (katikati), akiwa katika picha ya pamoja na Maaskofu Wasaidizi wa Jimbo hilo, Mapadri Wanajubilei wa Miaka 25 na 50, pamoja na Mapadri wengine, baada ya Adhimisho la Misa Takatifu ya Jubilei hiyo, iliyoadhimishwa katika Parokia ya Bikira Maria wa Fatima – Msimbazi, jimboni humo. (Picha zote na Yohana Kasosi)

Paroko Msaidizi wa Parokia ya Parokia ya Mtakatifu Yosefu Allamano, Kibada, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Steven Nyilawila, akimpongeza Padri Ambrose Mosha OFMCap, kwa kutimiza Jubilei ya Miaka 50 ya Upadri, wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Jubilei ya Miaka 25 na 50 ya Upadri, iliyoadhimishwa katika Parokia ya Bikira Maria wa Fatima – Msimbazi, jimboni humo.

VATICAN CITY, Vatican

Baba Mtakatifu Fransisko ametaka kuwepo kwa hatua za kusitisha  mapigano mara moja huko Lebanon, Gaza, Palestina, Israel na maeneo mengine kama Ukraine, Sudan na Myanmar.
Katika Siku ya Wahamiaji na Wakimbizi, Papa alisema kwamba hali ya uhamaji ni fursa ya kukua kwa udugu, akitoa tangazo la ufunguzi wa mchakato wa kumtangaza Mfalme Baudouin kuwa mwenyeheri.
Baada ya Misa hiyo Takatifu iliyoongozwa na Papa Fransisko katika Uwanja wa Mfalme Baudouin huko Bruxelles, alitoa shukrani kwa Maaskofu nchini Ubelgiji kwa maneno mazuri, akisema “Ninatoa shukrani za dhati kwa Wakuu, Mfalme na Malkia, na vile vile Wakuu wa Kifalme, Mtawala Mkuu na Malkia wa Luxembourg, kwa uwepo wao na ukarimu wao katika siku hizi.
Vile vile, ninatoa shukrani zangu kwa wote ambao, kwa njia nyingi, mmefanya kazi pamoja kuandaa Ziara hii. Kwa namna ya pekee, ninawashukuru wazee na wagonjwa ambao wamesali sala zao.”
“Leo tunaadhimisha Siku ya Wahamiaji na Wakimbizi Duniani yenye mada “Mungu anatembea na watu wake”. Kutoka nchi hii ya Ubelgiji, ambayo imekuwa, na bado ni kivutio cha wahamiaji wengi, ninarudia wito wangu kwa Ulaya na Jumuiya ya Kimataifa kuzingatia hali ya uhamiaji kama fursa ya kukua pamoja katika udugu, na ninakaribisha kila mtu kuona katika kila jambo kaka na dada mhamiaji uso wa Yesu, ambaye alifanyika mgeni na msafiri kati yetu,” alisema Baba Mtakatifu.
Papa alibainisha kwamba anaendelea kufuatilia kwa uchungu na wasiwasi mkubwa upanuzi na kuimarika kwa mzozo nchini Lebanon, akisema kwamba Lebanon ni ujumbe, lakini kwa sasa ni ujumbe wa kuteswa na vita, hivyo ambavyo vina madhara makubwa kwa idadi ya watu, kwani wengi wanaendelea kufa, siku baada ya siku, katika Mashariki ya Kati.
Aliongeza kwamba wanawaombea wahanga pamoja na familia zao, akitoa wito kwa pande zote kukomesha moto mara moja huko Lebanon na Gaza, pamoja na maeneo mengine ya Palestina na Israeli.
“Pia, ninawashukuru wengi wenu mliokuja kutoka Uholanzi, Ujerumani, Ufaransa kushiriki siku hii, asanteni.
Kwa wakati huu, pia ningependa kukupatia habari fulani. Nikirudi Roma nitaanza mchakato wa kutangazwa Mwenyeheri kwa Mfalme Baudouin, mfano wake kama mtu wa imani uwaangazie watawala. Ninaomba Maaskofu wa Ubelgiji wajitolee katika kuendeleza jambo hili,” alisema Papa.
Sambamba na hayo, aliomba kumgeukia Bikira Maria wakati wa kusali Sala ya Malaika wa Bwana pamoja, akisema kuwa hayo yalikuwa maombi maarufu sana katika vizazi vilivyopita, na hivyo napaswa kuhuishwa kwa kuwa ni muunganisho wa fumbo la Kikristo, na Kanisa linatufundisha kulijumuisha katika shughuli za kila siku.
Baada ya Adhimisho hilo la Misa Takatifu, Askofu Mkuu Luc Terlinden wa Jimbo Kuu Katoliki la Malines -Bruxelles, alishukuru kwa niaba ya Maaskofu wenzake, pamoja na Waamini wa Kanisa nchini Ubelgiji kwa ziara yake nchini.
Alimshukuru Baba Mtakatifu Fransisko kwa kwenda kukutana na wazalendo na wahusika, na kwa namna ya pekee wale walioko kwenye matatizo, pamoja na wenye majeraha ya kina yanayotokana na manyanyaso.
Aidha, alimshukuru Baba Mtakatifu kwa kuingia katika mazungumza na wanafunzi, watafiti na wanafunzi katika fursa ya miaka 600 ya Chuo Kikuu dada cha KULeuven na UCLouvain, na kwamba Papa anawafundisha wasitengenishe utafutaji wa ukweli, hekima na haki kijamii.
“Hekima inaweza kusaidia hadhi ya mtu binadamu, na kwa namna ya pekee katika Siku ya 110 ya Dunia ambayo imewekwa kwa ajili ya Wahamiaji na Wakimbizi, na inasaidia hata kulinda sayari yetu, “nyumba yetu ya pamoja,” alisisitiza, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Bruxelles.
Alisema kwamba wanaamini katika salamu za Baba Mtakatifu za wema, na kubainisha kwamba katika sala zao kwa ajili yake na kwa huduma yake, wanaikabidhi kwa Mama, Kikao cha Hekima na Mwenyeheri Anna wa Yesu.

NEKEMTE, Ethiopia

Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Ethiopia (Catholic Bishops’ Conference of Ethiopia: CBCE), Mwadhama Abune Kardinali Berhaneyesus, amesema kuwa wajibu mtakatifu wa kupitisha cheo cha ukuhani kutoka kizazi hadi kizazi, ni utamaduni unaowezeshwa na Roho Mtakatifu uliopokelewa kutoka kwa Yesu Kristo.
Kardinali Berhaneyesus aliyasema hayo katika mahubiri yake wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu na kuwekwa wakfu na kusimikwa kwa Askofu Getahun Fanta Shikune, aliyeteuliwa kuwa Askofu wa Vicariate ya Nekemte, nchini Ethiopia.
Aidha, katika mwendelezo muhimu wa baraka za kuadhimisha Mwaka Mpya wa Ethiopia, Kanisa Katoliki nchini humo lilisherehekea kuwekwa wakfu kwa Askofu huyo Mteule.
Miongoni mwa waliohudhuria katika Adhimisho hilo, ni Askofu wa zamani Varghese Thottamkara, C.M., Askofu wa sasa wa Balasore, India, pamoja na Maaskofu mbalimbali, Mapadri, waalikwa maalum, vikundi vya kidini, familia, na Waamini waliojitolea kutoka kote nchini.
Kardinali Berhaneyesus alimkabidhi Askofu huyo jukumu la kuongoza huduma hiyo mpya iliyowekwa na Mungu, akiwahimiza Wakatoliki wote kumuunga mkono mchungaji wao mpya kwa subira pamoja na sala.
Ikumbukwe kwamba Baba Mtakatifu Fransisko alifanya uamuzi wa kihistoria kwa kuwateua Maaskofu watatu wapya wa Kanisa Katoliki nchini Ethiopia, ili kutimiza sala na matarajio ya muda mrefu ya Waamini katika majimbo matatu nchini humo.
Maendeleo hayo yaliyosubiriwa kwa muda mrefu yanaashiria hatua kubwa kwa Kanisa Katoliki la Ethiopia, ambalo lilikuwa likitafuta kwa dhati uongozi wa mtaa kwa ajili ya utume wake wa kiroho na kichungaji.
Matukio hayo yalihudhuriwa na idadi kubwa ya Waamini kutoka kote Ethiopia na nchi jirani, wakiwemo Maaskofu, Mapadre, Masista wa Kidini, na Walei kutoka Eritrea, Association of Member Episcopla Cenference in Eastern Africa: AMECEA (Chama cha Mabaraza ya Maaskofu Wanachama Afrika Mashariki), na Symposium of Episcopal Conference of Africa and Madagascar: SECAM (Kongamano la Mabaraza ya Maaskofu wa Afrika na Madagaska).
Pia, Mkutano huo uliakisi umoja mpana wa Kanisa Katoliki Barani Afrika na nafasi yake katika Ukatoliki wa Kimataifa, na kwamba Sherehe za kuwekwa wakfu hazikuwa za kiroho tu, bali pia za kijumuiya, zilisherehekewa kwa furaha na ushiriki mkubwa kutoka sekta zote za jamii, zikiwemo jumuiya za mitaa, vikundi vya vijana, viongozi wa serikali, na wawakilishi kutoka mashirika mbalimbali ya kidini.
Kardinali Berhaneyesus alisema kwamba ushiriki huo mkubwa na wa aina mbalimbali, ulionyesha uhusiano thabiti kati ya Kanisa na watu wa Ethiopia, pamoja na nafasi muhimu ya Kanisa katika maisha ya kiroho na kijamii ya taifa.
Aliongeza kwamba uwepo wa Wawakilishi wa Kiekumene na Serikali pia ulionyesha dhamira ya Kanisa Katoliki katika ushirikiano wa dini na majadiliano kati ya dini mbalimbali, jambo ambalo ni la muhimu ambalo Maaskofu wapya wanatarajiwa kuendeleza na kuimarisha zaidi.
Alibainisha pia kuwa kuzingatia mizozo ya sasa ya Ethiopia, machafuko ya kijamii, na kuongezeka kwa mahitaji ya kibinadamu, Kanisa Katoliki linaonekana kama mhusika mkuu katika juhudi zinazoendelea za nchi kuelekea ujenzi wa amani na upatanisho.
Alisema kwamba mchanganyiko huo wa desturi za Kikatoliki na za kimaeneo uliashiria dhamira ya Kanisa ya kuishi pamoja na mshikamano kati ya jumuiya mbalimbali za kikabila na kidini nchini Ethiopia.

Dar es Salaam

Na Mwandishi wetu

Waimarishwa wameelezwa kwamba kumpokea Roho Mtakatifu kupitia Sakramenti Takatifu ya Kipaimara, ni kupewa jukumu la kuisimamia, kuilinda na kuitetea imani, pamoja na kuitangaza Habari Njema kwa maneno na matendo.
Fundisho hilo limetolewa hivi karibuni na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Stephano Musomba wakati wa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Sakramenti ya Kipaimara katika Parokia ya Bikira Maria Malkia - Kilimahewa, jimboni humo.
“Kwa upande wetu pia ni siku muhimu ya kukumbuka Vipaimara vyetu. Tulipompokea Roho Mtakatifu katika Kipaimara, tukapewa kazi ya kusimamia imani, kulinda imani na kuitetea, tukapewa kazi hiyo ya kutangaza Habari Njema, kumshuhudia Kristu kwa maneno yetu na matendo yetu,” alisema Askofu Musomba.
Aliongeza kwamba kupitia kumbukumbu hiyo, ni vizuri pia kutathmini na kuona ni kwa kiasi gani Wakristu wamefanikiwa, na kwamba ikiwa hawajafanikiwa, waache nafasi ili Kristu aweze kupenya na kutawala katika maisha yao.
Vile vile, Askofu Musomba aliwasihi Waamini kuondoa hali yoyote ya ukaidi, woga, ubaguzi, ubinafsi pamoja na roho zozote ambazo haziendani na mambo muhimu katika kuitangaza Habari Njema katika maisha yao.
“…maana yake tunaambiwa alama ya kwanza katika ujio wa Roho Mtakatifu, ni uvumi kama upepo mkali kutoka mbinguni, ukajaza chumba kile. Tunaona kwamba upepo ukiwa mkali, mtu anaweza akachukuliwa akashangaa anapeperushwa…
“Lakini lengo la upepo mkali ni kuondoa yote ya zamani, kuondoa ukaidi, kuondoa woga, kuondoa roho zozote zile ambazo haziendani na yale ambayo ni muhimu katika kutangaza Habari Njema, kuondoa ubaguzi, kuondoa ubinafsi, walitikiswa, na haya yote yakaondoka,” alisema Askofu Musomba.
Aliongeza kwamba upendo wa Mungu ndio unaowafanya watu wasiwe na ubaguzi, huku akiwasisitiza kuepuka kuwa na roho za usengenyaji pamoja na kuwachafua wengine katika jamii walipo, kwani kufanya hivyo siyo upendo wa Mungu unavyoelekeza.
Aliwataka Wakristo kuweka pembeni mambo yote yasiyompendeza Mungu katika maisha, badala yake wawe kitu kimoja, huku wakizungumza lugha moja.

DAR ES SALAAM

Na Alex Kachelewa

Uongozi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), umesema hatua ya kuboresha huduma zake kumesaidia mfuko huko kupiga hatua kubwa kimaendeleo kwa kuwa na ongezeko kubwa la mapato hadi kufikia Shilingi trilioni 8.5/- ikiwa ni ongezeko la asilimia 70% ya waajiri wapya.
Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba, alisema hayo hivi karibuni wakati akizungumza katika Mkutano kati ya NSSF na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), uliofanyika jijini Dar es Salaam.
“NSSF imepiga hatua kubwa sana mwaka hadi mwaka na hasa wakati huu ambapo huduma zetu tumeziboresha zaidi na kumaliza kero mbalimbali kwa wanachama wetu hasa wazee ambao walikuwa wakijipanga mstari katika ofisi zetu kwa muda mrefu kusubiria huduma ya madai yao…
“Lakini kwa sasa mtu anaweza kukaa hata sebuleni kwake kwa kutumia simu yake ya mkononi anahakiki michango yake na anaweza kufanya mchakato wote wa malipo na akafanikisha akiwa huko alipo na hiyo pia hata kuomba kadi endapo itapotea,”alisema Mshomba.
Mshomba alisema kuwa mpango wa NSSF kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano TEHAMA, imeufanya mfuko huo kupiga hatua kubwa na kuondoa usumbufu wote uliokuwa ukijitokeza miaka iliyopita na sasa mambo ni mazuri kwa wastaafu kwani kila kitu kinafanyika kwa wakati kwa njia ya mtandao.
Mshomba alibainisha kuwa kwa sasa uongozi wake unaendelea na mikakati mbalimbali, ili hadi kufikia Desemba mwaka 2025, huduma zote zifanyike kwa kutumia TEHAMA.
“Tayari sisi NSSF tumezindua huduma ya Mwanachama wetu kuproces mafao yake kwa njia ya mtandao mfumo huu utakwenda kuondoa usumbufu wote kufika ofisini atamaliza yeye mwenyewe huko huko,”alisema Mshomba.
Kuhusu sekta Binafsi, Mshomba alisema kwamba tayari mchakato umekamilika kwa lengo la kuhakikisha watu waliojiajiri katika sekta zisizo rasmi ikiwemo, kilimo, ufugaji, uvuvi, uchimbaji madini wadogo na kadhalika watafikiwa kwa huduma ya NSSF ili nao waweze kupata mafao wakiwa wazee.
Alifafanua kuwa Wanachama wa sekta hizo wao wamewekewa utaratibu mzuri wa kuchangia kiasi cha Shilingi 30,000/- kwa mwezi au kulipa kidogo kidogo kwa kila siku, wiki ama mwezi ili nao waweze kunufaika na akiba za uzeeni.
Aidha, Mshomba alisema mpango huo unakwenda sanjari na wafanyakazi wa Sekta binafsi ambao wanapenda kujiwekea akiba zaidi wao wewenye kwa njia ya uchangiaji binafsi ili waweze kutunisha zaidi akiba zao za mafao.
Kwa mujibu wa Mshomba, kwa sasa baada ya Sheria mpya kupitishwa na Bunge Wanachama pia wanaweza kufanya kazi sehemu mbili hata tatu na waajiri hao wote wakawachangia fedha katika akiba zao za mafao, isipokuwa mwajiri moja anapaswa kuthibitisha wazi kwamba ndiye atakayehusika moja kwa moja na NSSF, kwa kukumbushwa kuwasilisha michango hiyo kisheria.
Hata hivyo, Mshomba alitumia nafasi hiyo kuwasihi wanachama kuacha tabia ya kukimbilia kuchukua mafao yao kabla ya kutimiza umri wa kustaafu, kwani kufanya hivyo ni kujinyima fursa hasa manufaa ya mafao uzeeni.