DAR ES SALAAM
Na Mathayo Kijazi
Waliokuwa wanafunzi katika Shule za Seminari nchini, wamekutana na kutafakari Neno la Mungu katika mafungo yaliyoandaliwa na Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, huku wakiaswa kutambua kwamba hata Mtu anapojiona ni Mtakatifu kiasi gani, lakini bado mbele za Mungu, ni mdhambi, kwani Mungu ndiye Mtakatifu pekee.
Kauli hiyo ilitolewa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi katika Mafungo ya ‘Former Seminarians’, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, yaliyofanyika katika Kituo cha Hija – Pugu, jimboni humo.
“Mbele ya Mungu hata kama uko Mtakatifu kiasi gani, mbele ya Mungu ambaye ndiye utakatifu wote, ndiye ukamilifu wote, ni lazima ujitambue kwamba uko mdhambi, kwa kuwa Mungu tu ndiye peke yake Mtakatifu, Mungu tu ndiye peke yake mwenye haki, na Mungu tu ndiye peke yake asiye na lawama yoyote. Sisi wote tumeshaguswa na dhambi,” alisema Askofu Mkuu Ruwa’ichi.
Aidha, Askofu Mkuu aliwasihi Waseminari hao kutokuona haya kumwomba Mungu toba, au kujikabidha mbele za Mungu na kuomba huruma yake, kwani yeye ndiye anayewastahilisha, anayewatakasa na kuwawezesha.
Aliwataka kutokuogopa kufuata mfano wa mtoza ushuru, ambaye kwa kujitazama mapungufu yake, alisimama mbali na kujipiga kifua, huku akiomba toba.
Aliwaonya kuacha kujitokeza mbele za Mungu na kumkumbusha kwamba wao ni wenye haki kutokana na mambo wanayoyafanya katika maisha yao.
“Yaani mtego wa kufanya mazoezi fulani ya kiroho au ya kidini, na kujidhani sasa wamemuweka Mungu sawa, na kujidhani kwamba sasa sisi ni wenye haki, ndivyo alivyofanya yule Mfarisayo aliyeenda mbele ya Altare akaanza kumkumbusha Mungu jinsi yeye Farisayo alivyo na fadhila.
“Niwakumbushe tu kidogo, alimwambia Mungu, tazama mimi nilivyo mwenye haki, nafanya kadha wa kadha. Siko mzinzi, siko mwizi, siko mwongo, siko mvivu…… Yaani ni kama Mungu anatangaziwa hizo fadhila kusudi iweje. Kusudi mategemeo ni kwamba Mungu atampigapiga mabegani, na kumwambia ‘well done’. Lakini Mungu siyo wa hivyo, Mungu harubuniwi,” alisema Askofu Ruwa’ichi.
Alisema kuwa malezi waliyoyapata Waseminari hao pindi wakiwa Seminarini, yamewaunda na kuwapa fursa ya kupambanua na kuitikia wito wa Mungu.
Askofu Mkuu alisema kuwa kijana mdogo katika kukua kwake anapojitambua, asaidiwe ili akue katika mtindo ambao unamjenga kiutu, kiroho, na unamsababisha afanye maamuzi sahihi.
Aliwataka wale walioondolewa Seminarini ambao bado wana majeraha, kuondoa majeraha hayo, ili waamue kujikabidhi kwa Mungu na kuomba neema ya kukua katika njia zake, pamoja na kusamehe.
Pia, alisema kuwa mtu asiyesamehe, anaendelea kubeba mizigo, hivyo akawataka walioondolewa Seminarini, kuacha kujibebesha mizigo ya hasira, na ya kutaka kulipiza kisasi.
Kwa upande wake Mkuu wa Majeshi Mstaafu (CDF), Venance Mabeyo, akizungumza kwa niaba ya Waseminari wa zamani, alisema kuwa hiyo ni fursa kubwa kukutana katika Adhimisho hilo, kwani wengine hawafahamiani kutokana na wingi wao.
Mabeyo aliwasihi Waseminari wenzake wa zamani kuwa watu wa kusameheana pale wanapokoseana, huku wakiepuka kuwa na jazba, akisema kwamba yeyote mwenye jazba, neno ‘msamaha’ halikai katika msamiati wake.
Alisema pia kuwa kila mmoja anatakiwa kujitafakari na kujiuliza, je, anafanya mara ngapi matendo ya huruma? Huku akisisitiza kuishi vizuri na watu wa hulka tofauti tofauti katika jamii zao.