DAR ES SALAAM
Na Edvesta Tarimo
Machi 24 kila mwaka, Dunia huadhimisha Siku ya Kifua Kikuu au TB (Tuberculosis), ambapo huweka kauli mbalimbali zenye lengo la kukuza uelewa na kupambana na ugonjwa huo unaozidi kupoteza maisha ya watu ulimwenguni.
Takwimu za Shirika la Afya Duniani (World Health Organisation: WHO), mwaka 2023 zinaonyesha kuwa, ugonjwa wa kifua kikuu bado ni tatizo kubwa, kwani kati ya wagonjwa wanaokisiwa kuwa na ugonjwa huo nchini 128,000, ni asilimia 78 tu ndio waliogundulika.
Kwa mujibu wa (World Health Organisations – WHO) taarifa zilizochapishwa katika tovuti yake ya mwaka 2023, zinaonesha kuwa watu milioni 1.6 (ikiwa ni pamoja na watu 187,000 wenye maambukizi ya ukimwi), walikufa kwa ugonjwa wa kifua kikuu duniani.
Kifua kikuu au (TB Tuberculosis), ni ugonjwa wa kuambukiza ambao huathiri mapafu na husababishwa na bakteria, ugonjwa huu husambazwa kwa njia ya hewa wakati mtu aliyeambukizwa anapokohoa, kupiga chafya au kutema mate.
Nchini Tanzania, mwaka huu Shirika la PASADA (Pastoral Activities and Services for People with AIDS Dar es Salaam Archdiocese - PASADA) kwa kushirikiana na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kutoa miradi, (United Nations Office for Project Services – UNOPS) kupitia mradi wa “STOP TB” kwa kipindi cha mwaka 2018 hadi 2023, limeweza kufikia watu wapatao 24, 801 wa kifua kikuu.
Dk. Jackline Mwaipaja, Meneja wa Mradi PASADA, anasema kuwa kupitia mradi wa “STOP TB” umewezesha PASADA kutoa huduma zinazowezesha jamii kufuatilia huduma za kifua kikuu.
Mwaipaja anaongeza kuwa mradi umewezesha PASADA kutoa huduma hizo zinafanyika kupitia mfumo wa “One Impact Tb Kiganjani”, kutoa huduma ambayo zinazingatia haki na usawa wa kijinsia.
Kupitia mradi huo waliweza kufikia watu 622 kupata huduma za kiugundizi na matibabu kifua kikuu. Kuanzia mwezi wa 4 hadi mwezi 12 mwaka 2023, waliibua wagonjwa 919 wa kifua kikuu. kati yao wagonjwa 111 ni watoto chini ya miaka 15 sawa na asilimia 12 ya wagonjwa wote waliogundulika.
Dk. Mwaipaja anasema kuwa wagonjwa 256 waligundulika wana maambukizi ya pamoja, yaani kifua kikuu na maambukizi ya virusi vya ukimwi. Wote wameunganishwa kwenye huduma na wanaendelea na huduma ya matibabu.
PASADA kupitia wahudumu wa afya ngazi ya jamii, (community health workers - CHWs), wameweza kwenda mtaani kuwaibua wagonjwa wahudumu wa ngazi ya jamii ambapo kwa kipindi cha wiki mbili, yaani kuanzia tarehe 1 mwezi wa 3 hadi 15 mwezi wa 3 mwaka huu, wagonjwa 1626 walifikiwa na kupewa elimu kuhusu kifua kikuu.
Dk. Mwaipaja anaongeza, mbali na elimu, walipewa dodoso ili kuona kwamba kama wana viashiri vya kifua kikuu, na kati ya 161 walionekana wana viashiria vya kifua kikuu walifanyiwa vipimo, huku wateja 27 waliogundulika wana kifua kikuu waliunganishwa katika matibabu.
Uelewa wa Jamii kuhusu Kifua Kikuu:
Kimsingi, linapokuja suala la Afya jamii haijazingatia kwenda kupimwa afya zao kutokana na uelewa mdogo wa masuala ya afya, kwani baadhi ya watu katika jamii, husubiri kwenda hospitali pindi wanapohisi homa.
Katibu wa Afya Jimbo Katoliki la Dar es Salaam, Pauline Archard, anahimiza waliofikiwa na PASADA kuwa mabalozi kwa kuwasaidia wenzeo kwa kuwapeleka kwa mtoa huduma, na kumwambia amsaidie kama alivyosaidiwa yeye.
Archard anasema kwamba katika kuhakikisha jamii inapata uelewa wa ugonjwa wa kifua kikuu, serikali kuweka mikakati madhubuti wa kuwasaidia watu hawa baada ya kugunduliwa, kwa kushirikiana na PASADA hasa katika suala la vipimo, na kwamba walitarajia kupungua kwa ugonjwa lakini kwa mujibu wa takwimu mbalimbali unaonekana kama unakuja tena, yaani unaongezeka.
Gharama za x – ray kikwazo kwa wagonjwa:
Changamoto ya gharama ya kipimo cha mionzi (x – ray), wagonjwa wengi hawana uwezo wa kugharamia vipimo vya x-ray hivyo Watanzania walio wengine wanashidwa kumudu gharama za kufanyiwa vipimo ili kujua afya zao.
Shaaban Salum, mkazi wa jijini Dar es Salaam anawashukuru PASADA kwa kumfikia na kumpatia matibabu, kwani mara ya kwanza walimkuta yupo kijiweni wakamchukua na kumfanyia uchunguzi wa x-ray, na kugundulika ana maradhi ya kifua kikuu, wakampatia dawa, na sasa anaendelea vizuri na matibabu.
Salum anaomba PASADA waendelee kutoa huduma hiyo kwa kuwa watu wengi mtaani na hawana uwezo wa kujitibu katika jamii hawajiwezi na wanahitaji.
Shaaban Puga anasema kuwa alikuwa anaumwa na hajiwezi kutokana na hali duni ya maisha. Shirika la PASADA walifika mtaani kwake na kumchukua na kwenda nae ofisini kwao kumpatia huduma ya maradhi yanayomsumbua.
“Nilikuwa taabani, sasa hivi nashukuru nina afya njema nimepata huduma zao vizuri, nafanya kazi zangu kama kawaida. Nawashukuru sana na waendelee kufuatilia watu mtaani kwani wapo wengi wanaumwa,” anasema Puga.
PASADA inaungana na Shirika la Afya Duniani, Serikali kupitia Wizara ya Afya na wadau wote wa Afya katika mapambano mbalimbali katika kutokomeza kifua kikuu ifikapo mwaka 2030.
Serikali imeelekeza kwenda kufanya utafiti na kuwaibua, katika zoezi hilo, pasada kupitia wahudumu ngazi ya jamii, wamekwenda mtaani kutafuta na kuwaibua wagonjwa.
Tiba ya Kifua Kikuu:
Tiba ya kifua kikuu inajihusisha na matumizi ya dawa za kifua kikuu kwa muda wa miezi sita au tisa. Dawa hizi hutolewa chini ya uangalizi, yaani mgonjwa anakunywa chini ya uangalizi wa mhudumu wa afya.
Kwa mujibu wa wataalam wa Afya, tiba ya kifua kikuu inatolewa bure nchini kote Tanzania kama ilivyo dawa za kufubaza maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi (HIV)
Dokta Eugen Rutaisire, Mkurugenzi wa huduma za tiba shirika la PASADA, amesema kuwa wao kama wataalam, bado wana nafasi kubwa ya kuendelea kuwafuatilia wale ambao wameathirika katika jamii, kwani ni kuendelea kuwafuatilia kwa ukaribu.
Dokta Rutaisire anasema kwamba malengo ya kutokomeza kifua kikuu ifikapo mwaka 2030 inawezekana kwa kuongeza juhudi za kupambana na ugonjwa wa kifua kikuu bila kuchoka, na kwani kila kitu kinawezekana kama kikiwekewa nia na uthubutu wa kukabiliana nacho.
Mikakati ya Serikali kuitokomeza
Dk. Jonas Lulandala ni Mganga Mkuu wa Manispaa ya Temeke, anasema kwamba serikali imetengeneza mazingira wezeshi kiasi kwamba huduma za afya zitaweza kutolewa na serikali na mashirika.
Anaongeza kusema kuwa huduma za Afya hatuwezi kushikilia kama serikali peke yao, bali kwa kuzifanya kwa kushirikiana na mashirika, na wadau mbalimbali.
Kuhusu suala la upimaji kwa kutumia mionzi, yaani X – Ray, amesema atalifikisha kwa mganga mkuu wa mkoa kuona namna ya kulifanyia kazi ili kuweza kusaidia kuwahudumia wagonjwa wanaohitaji kufanyiwa kipimo hicho.
Dk. Lulandala anasema kwamba kipimo cha mionzi, yaani X- Ray kwa Hospitali ya Temeke katika vituo vyake vya kutolea huduma, tayari vipimo hivyo vipo, na kwamba lazima kuweka utaratibu wa kuona namna nzuri ya kuwapima wagonjwa.
Wakati ugonjwa huo unatibika na kuzuilika, wakuu wa nchi katika mkutano wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa kuhusu TB (TB Tuberculosis) wa mwaka 2023, walikadiria kuwa dola bilioni 13 zilihitajika kila mwaka kwa ajili ya kuzuia, utambuzi, matibabu, na matunzo, ili kukomesha janga hilo ifikapo mwaka 2030.
Pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika upambanaji wa kutokomeza kifua kikuu, bado kuna changamoto zinazojitokeza, hususani kuifikia jamii husika kwa ujumla wake; uelewa mdogo kwenye jamii kuhusu dalili za kifua kikuu na namna mbalimbali za kujikinga; unyanyapaa wa wagonjwa baada ya kugundulika kuwa na maambukizi ya kifua kikuu; na fedha kidogo za utekelezaji wa afua za kifua kikuu.
Maadhimisho ya Siku ya Kifua Kikuu Dunia mwaka huu yamebebwa na kauli mbiu ya mwaka huu, “Ndiyo! Tunaweza kukomesha TB,” ikikusudia kutuma ujumbe wa matumaini katika kukomesha janga hilo.